006-Al-An’aam

006-Al-An’aam

Khamis

Next page 📄 4

 

 

قُلْ تَعَالَوْا أَتْلُ مَا حَرَّمَ رَبُّكُمْ عَلَيْكُمْ ۖ أَلَّا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا ۖ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا ۖ وَلَا تَقْتُلُوا أَوْلَادَكُم مِّنْ إِمْلَاقٍ ۖ نَّحْنُ نَرْزُقُكُمْ وَإِيَّاهُمْ ۖ وَلَا تَقْرَبُوا الْفَوَاحِشَ مَا ظَهَرَ مِنْهَا وَمَا بَطَنَ ۖ وَلَا تَقْتُلُوا النَّفْسَ الَّتِي حَرَّمَ اللَّـهُ إِلَّا بِالْحَقِّ ۚ ذَٰلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ ﴿١٥١﴾

151. Sema: Njooni nikusomeeni yale Aliyoyaharamisha Rabb wenu kwenu. Kwamba msimshirikishe na chochote, na muwafanyie ihsaan wazazi wawili, na wala msiwaue watoto wenu kutokana na umasikini. Sisi Tunakuruzukuni pamoja nao. Na wala msikaribie machafu yaliyo dhahiri na yaliyofichika. Na wala msiue nafsi ambayo Allaah Ameiharamisha (kuiua) isipokuwa kwa haki (ya sharia). Hivyo ndivyo Alivyokuusieni kwayo mpate kutia akilini.

 

 

 

 

وَلَا تَقْرَبُوا مَالَ الْيَتِيمِ إِلَّا بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ حَتَّىٰ يَبْلُغَ أَشُدَّهُ ۖ وَأَوْفُوا الْكَيْلَ وَالْمِيزَانَ بِالْقِسْطِ ۖ لَا نُكَلِّفُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا ۖ وَإِذَا قُلْتُمْ فَاعْدِلُوا وَلَوْ كَانَ ذَا قُرْبَىٰ ۖ وَبِعَهْدِ اللَّـهِ أَوْفُوا ۚ ذَٰلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ ﴿١٥٢﴾

152. Na wala msiikaribie mali ya yatima isipokuwa kwa njia njema ya manufaa mpaka afikie umri wa kupevuka. Na timizeni kipimo na mizani kwa uadilifu. Hatukalifishi nafsi isipokuwa kadiri ya uwezo wake. Na mnaposema basi fanyeni uadilifu japokuwa ni jamaa wa karibu. Na timizeni Ahadi ya Allaah. Hivyo ndivyo Alivyokuusieni (Allaah) kwayo mpate kukumbuka.

 

 

 

وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ ۚ ذَٰلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ ﴿١٥٣﴾

153. Na kwamba hii ndiyo njia Yangu iliyonyooka, basi ifuateni. Na wala msifuate njia nyinginezo zitakufarikisheni na Njia Yake.[26] Hivyo ndivyo Alivyokuusieni (Allaah) kwayo mpate kuwa na taqwa. 

 

 

 

ثُمَّ آتَيْنَا مُوسَى الْكِتَابَ تَمَامًا عَلَى الَّذِي أَحْسَنَ وَتَفْصِيلًا لِّكُلِّ شَيْءٍ وَهُدًى وَرَحْمَةً لَّعَلَّهُم بِلِقَاءِ رَبِّهِمْ يُؤْمِنُونَ ﴿١٥٤﴾

154. Tena Tulimpa Muwsaa Kitabu kutimiza (neema) juu ya yule aliyefanya vitendo vyema, na kiwe chenye kuchambua wazi kila kitu, na kiwe mwongozo na rahmah ili wapate kuamini kukutana na Rabb wao.

 

 

 

وَهَـٰذَا كِتَابٌ أَنزَلْنَاهُ مُبَارَكٌ فَاتَّبِعُوهُ وَاتَّقُوا لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ ﴿١٥٥﴾

155. Na hiki ni Kitabu (Qur-aan) Tumekiteremsha kilichobarikiwa, basi kifuateni na muwe na taqwa mpate kurehemewa.

 

 

 

أَن تَقُولُوا إِنَّمَا أُنزِلَ الْكِتَابُ عَلَىٰ طَائِفَتَيْنِ مِن قَبْلِنَا وَإِن كُنَّا عَن دِرَاسَتِهِمْ لَغَافِلِينَ ﴿١٥٦﴾

156. Msije kusema: Hakika Kitabu kimeteremshwa juu ya makundi mawili kabla yetu, lakini tulikuwa hatuna habari yoyote kuhusu waliyokuwa wakiyasoma.

 

 

أَوْ تَقُولُوا لَوْ أَنَّا أُنزِلَ عَلَيْنَا الْكِتَابُ لَكُنَّا أَهْدَىٰ مِنْهُمْ ۚ فَقَدْ جَاءَكُم بَيِّنَةٌ مِّن رَّبِّكُمْ وَهُدًى وَرَحْمَةٌ ۚ فَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّن كَذَّبَ بِآيَاتِ اللَّـهِ وَصَدَفَ عَنْهَا ۗ سَنَجْزِي الَّذِينَ يَصْدِفُونَ عَنْ آيَاتِنَا سُوءَ الْعَذَابِ بِمَا كَانُوا يَصْدِفُونَ ﴿١٥٧﴾

157. Au mkaseme: Lau tungeliteremshiwa Kitabu basi bila shaka tungelikuwa tumehidika zaidi kuliko wao. Kwa yakini imekwishakufikieni hoja bayana kutoka kwa Rabb wenu na mwongozo na rahmah. Hivyo basi nani ni dhalimu zaidi kuliko yule aliyekadhibisha Aayaat za Allaah na akajitenga nazo? Tutawalipa wale wanaojitenga na Aayaat Zetu adhabu ovu kwa sababu ya kujitenga kwao.

 

 

 

هَلْ يَنظُرُونَ إِلَّا أَن تَأْتِيَهُمُ الْمَلَائِكَةُ أَوْ يَأْتِيَ رَبُّكَ أَوْ يَأْتِيَ بَعْضُ آيَاتِ رَبِّكَ ۗ يَوْمَ يَأْتِي بَعْضُ آيَاتِ رَبِّكَ لَا يَنفَعُ نَفْسًا إِيمَانُهَا لَمْ تَكُنْ آمَنَتْ مِن قَبْلُ أَوْ كَسَبَتْ فِي إِيمَانِهَا خَيْرًا ۗ قُلِ انتَظِرُوا إِنَّا مُنتَظِرُونَ ﴿١٥٨﴾

158. Je, wanangojea nini isipokuwa Malaika wawafikie (kuwatoa roho), au Awafikie Rabb wako (kuwahukumu)[27], au ziwajie baadhi ya Aayaat (Ishara, Alama za Qiyaamah)[28] za Rabb wako? Siku zitakapokuja baadhi ya Aayaat za Rabb wako haitoifaa nafsi imaan yake, ikiwa haikuamini kabla au haikuchuma katika imaan yake kheri yoyote. Sema: Ngojeeni hakika nasi tunangojea.

 

 

 

إِنَّ الَّذِينَ فَرَّقُوا دِينَهُمْ وَكَانُوا شِيَعًا لَّسْتَ مِنْهُمْ فِي شَيْءٍ ۚ إِنَّمَا أَمْرُهُمْ إِلَى اللَّـهِ ثُمَّ يُنَبِّئُهُم بِمَا كَانُوا يَفْعَلُونَ ﴿١٥٩﴾

159. Hakika wale waliofarakisha dini yao na wakawa makundi makundi,[29] wewe huhusiki nao kwa lolote. Hakika kesi yao iko kwa Allaah, kisha Atawajulisha yale waliyokuwa wakiyatenda.

 

 

 

مَن جَاءَ بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ عَشْرُ أَمْثَالِهَا ۖ وَمَن جَاءَ بِالسَّيِّئَةِ فَلَا يُجْزَىٰ إِلَّا مِثْلَهَا وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ ﴿١٦٠﴾

160. Atakayekuja na amali njema basi atapata (thawabu) kumi mfano wake. Na Atakayekuja na ovu basi hatolipwa ila mfano wake,[30] nao hawatodhulumiwa.

 

 

 

قُلْ إِنَّنِي هَدَانِي رَبِّي إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ دِينًا قِيَمًا مِّلَّةَ إِبْرَاهِيمَ حَنِيفًا ۚ وَمَا كَانَ مِنَ الْمُشْرِكِينَ ﴿١٦١﴾

161. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Hakika mimi Ameniongoza Rabb wangu kuelekea njia iliyonyooka, Dini iliyosimama thabiti, mila ya Ibraahiym aliyejitenga na itikadi potofu na kuelemea haki na hakuwa miongoni mwa washirikina.

 

 

قُلْ إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿١٦٢﴾

162. Sema: Hakika Swalaah yangu, na ibaada yangu ya kuchinja, na uhai wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Allaah Pekee Rabb wa walimwengu.[31]

 

 

لَا شَرِيكَ لَهُ ۖ وَبِذَٰلِكَ أُمِرْتُ وَأَنَا أَوَّلُ الْمُسْلِمِينَ ﴿١٦٣﴾

163. Hana mshirika, na kwa hayo ndio nimeamrishwa, nami ni Muislamu wa kwanza (katika ummah huu). 

 

 

 

قُلْ أَغَيْرَ اللَّـهِ أَبْغِي رَبًّا وَهُوَ رَبُّ كُلِّ شَيْءٍ ۚ وَلَا تَكْسِبُ كُلُّ نَفْسٍ إِلَّا عَلَيْهَا ۚ وَلَا تَزِرُ وَازِرَةٌ وِزْرَ أُخْرَىٰ ۚ ثُمَّ إِلَىٰ رَبِّكُم مَّرْجِعُكُمْ فَيُنَبِّئُكُم بِمَا كُنتُمْ فِيهِ تَخْتَلِفُونَ ﴿١٦٤﴾

164. Sema Je, nitake ghairi ya Allaah kuwa ni Rabb ilhali Yeye Ndiye Rabb wa kila kitu? Na nafsi yoyote haichumi (kheri au shari) ila itabeba yenyewe. Na wala habebi mbebaji, mzigo (wa dhambi) wa mwengine. Kisha kwa Rabb wenu ndio marejeo yenu, Atakujulisheni yale mliyokuwa mkikhitilafiana.

 

 

 

 

وَهُوَ الَّذِي جَعَلَكُمْ خَلَائِفَ الْأَرْضِ وَرَفَعَ بَعْضَكُمْ فَوْقَ بَعْضٍ دَرَجَاتٍ لِّيَبْلُوَكُمْ فِي مَا آتَاكُمْ ۗ إِنَّ رَبَّكَ سَرِيعُ الْعِقَابِ وَإِنَّهُ لَغَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿١٦٥﴾

165. Naye (Allaah) Ndiye Aliyekufanyeni warithi waandamizi wa duniani na Akanyanyua baadhi yenu juu ya wengine kwa daraja mbali mbali ili Akujaribuni katika yale Aliyokupeni. Hakika Rabb wako Ni Mwepesi wa Kuakibu, na hakika Yeye bila shaka Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu.

 

 

 

 

 

[1]  Yeye Ndiye Allaah Mwabudiwa Wa Mbinguni Na Ardhini:

 

Wafasiri wa Qur-aan wamekhitilafiana katika kauli nne kuhusu Kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):

وَهُوَ اللَّـهُ فِي السَّمَاوَاتِ وَفِي الْأَرْضِ ۖ يَعْلَمُ سِرَّكُمْ وَجَهْرَكُمْ وَيَعْلَمُ مَا تَكْسِبُونَ ﴿٣﴾

“Na Yeye Ndiye Allaah mbinguni na ardhini, Anajua ya siri yenu na ya dhahiri yenu, na Anajua yale mnayoyachuma.” [Al-An'aam (6:3)]

 

Kauli Ya Kwanza:

Maana yake ni: Yeye Allaah (سبحانه وتعالى) ni Ilaah (Apasaye kuabudiwa kwa haki), Anayeabudiwa mbinguni na ardhini, kwa sababu Yeye Pekee Ndiye Mwabudiwa wa haki katika ardhi na mbingu, kwa ushahidi wa Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):

وَهُوَ الَّذِي فِي السَّمَاءِ إِلَـٰهٌ وَفِي الْأَرْضِ إِلَـٰهٌ ۚ  

“Na Yeye Ndiye Mwabudiwa wa haki mbinguni na ardhini pia (Ndiye Huyo Huyo) Ilaah.” [Az-Zukhruf (43:84)]

 

[Al-Qurtwubiy, Ibn Kathiyr, Ash-Shanqiytwiy, Ibn Al-Anbaariy na wengineo. Rejea Al-Jaami’u li-Ahkaamil-Qur-aan (6/390), Tafsiyr Al-Qur-aan Al-‘Adhwiym (3/240) na Adhwaau Al-Bayaan (7/4)]  

 

Kauli Ya Pili: 

Maana yake ni: Yeye Allaah Anajua siri zenu mbinguni na ardhini, na ushahidi ni Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):

قُلْ أَنزَلَهُ الَّذِي يَعْلَمُ السِّرَّ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ  

“Sema (ee Muhammad صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمَ): “Ameiteremsha Ambaye Anajua siri katika mbingu na ardhi.” [Al-Furqaan (25:6)]

 

Kwa kuzingatia kwamba Kauli Yake: 

 

“mbinguni na ardhini” [Al-An’aam (6:3)] inahusiana na: “Anajua siri zenu.”

 

Imaam Ad-Daaniyy amesema: Na imesemwa kuwa maana yake ni: Yeye Ndiye Mwabudiwa mbinguni na ardhini. Na Al-Ashmuwniyy kaunga mkono ufafanuzi huo.

 

Na amesema An-Nahhaas kuwa kauli hiyo ni bora katika yaliyoelezwa juu ya Aayah hiyo.

 

[Al-Muktafaa Fiy Al-Waqf Wal-Ibtidaa Fiy KitaabiLLaah ‘Azza Wa Jalla (273), Manaaru Al-Hudaa Fiy Bayaan Al-Waqf Wal-Ibtidaa (265). Adhwaau Al-Bayaan Fiy Iydhwaah Al-Qur-aan bil-Qur-aan (4/7)]   

 

Kauli Ya Tatu:

Ni kwamba Yeye Allaah, Ambaye Yuko mbinguni na katika ardhi, Anajua siri zenu na ya dhahiri yenu katika ardhi. Naye Yuko juu ya ‘Arsh Yake Akiwa juu ya Viumbe Vyake wote, Akiwa Anajua siri za watu wa ardhini na ya dhahiri yao, hakuna kinachofichika Kwake katika hayo. Na ushahidi ni Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):

أَأَمِنتُم مَّن فِي السَّمَاءِ أَن يَخْسِفَ بِكُمُ الْأَرْضَ فَإِذَا هِيَ تَمُورُ﴿١٦﴾

“Je, mnadhani mko katika amani na (Allaah) Aliyeko mbinguni kwamba Hatokudidimizeni ardhini, tahamaki hiyo inatikisika?”

 

أَمْ أَمِنتُم مَّن فِي السَّمَاءِ أَن يُرْسِلَ عَلَيْكُمْ حَاصِبًا ۖ فَسَتَعْلَمُونَ كَيْفَ نَذِيرِ﴿١٧﴾

“Au mnadhani mko katika amani na (Allaah) Aliyeko mbinguni kwamba Hatokutumieni tufani ya mawe? Basi mtajua vipi Maonyo Yangu!” [Al-Mulk (67:16-17)]

 

Na Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ ﴿٥﴾

“Ar-Rahmaan (Mwingi wa Rahmah), Yuko juu (Istawaa) ya ‘Arsh.” [Twaahaa (20:5)]

 

Kauli Ya Nne: 

Ina maana kutangulizwa na kuakhirishwa, yaani: Yeye Allaah Anajua siri zenu na ya dhahiri yenu mbinguni na ardhini. Na hii ni kauli ya Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما).

 

Kauli iliyo na nguvu kabisa katika kauli hizo nne ni:

 

Kauli ya kwanza ambayo ni kauli ya wengi katika Wafasiri wa Qur-aan, pamoja na kwamba kuna uwezekano wa kauli nyingine katika hizo, kwa sababu kila kauli ina ushahidi wake katika Qur-aan.

 

Shaykh Al-Islaam Ibn Taymiyyah (رحمه الله)     amesema: “Imaam wakubwa kama Imaam Ahmad na wengineo wameifasiri kwamba: “Kuwa Yeye Ni Mwabudiwa mbinguni na ardhini.” [Al-Furqaan Bayna Awliyaair-Rahmaan Wa-Awliyaa Ash-Shaytwaan (244)]

 

Ibn Kathiyr (رحمه الله)  amesema “Kauli iliyo sahihi kabisa ni kwamba: “Allaah Anaombwa mbinguni na ardhini, yaani Anaabudiwa, Anapwekeshwa, Anakiriwa kwa Uabudiwa na Anaitwa Allaah. Naye Anaombwa na wote kwa utashi na khofu isipokuwa wakanushaji katika majini na wanaadamu.” [Tafsiyr Al-Qur-aan Al-‘Adhwiym, (3/240)]

 

[2] Makafiri Wanatakiwa Watembee Maeneo Mbalimbali Wakatambue Hatima Za Waliokanusha Kabla Yao:

 

Allaah (سبحانه وتعالى) Anawatanabahisha makafiri, washirikina na wakanushaji wowote wale wa Tawhiyd Yake na Kuwakanusha Rusuli Wake kwa kuwataka waende nchi na maeneo mbalimbali ili wakajionee na watambue adhabu zilizowakumba wenzao wa kabla yao. Allaah (سبحانه وتعالى) Anataja hivyo katika Suwrah na Aayah mbalimbali. Kati ya Suwrah hizo ni pamoja na Aal-‘Imraan (3:137), Faatwir (35:43-44), Yuwsuf (12:109), An-Naml (37:69), Al-‘Ankabuwt (29:20), Ar-Ruwm (30:9) (30:42), Al-Hajj (22:46), Ghaafir (40:82) na Muhammad (47:10).

 

[3] Kuthibitisha Sifa Za Allaah (سبحانه وتعالى): Rejea Al-Fat-h (48:10), Huwd (11:37).

 

[4] Nyoyo Za Makafiri Zimefunikwa Na Masikio Yao Yana Uziwi:

 

Allaah (سبحانه وتعالى) Anafahamisha kuwa miongoni mwa washirikina ni wale wanaoisikiliza Qur-aan kutoka kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) lakini hawanufaiki na kusikiliza huku. Na kwa sababu hiyo, Allaah (سبحانه وتعالى) Anajaalia vifuniko juu ya nyoyo zao ili wasije wakaifahamu, na Anaweka uziwi masikioni mwao ili wasiisikie kwa sababu ya ukaidi wao na ukanushaji wao, na hata wangeona dalili gani na hoja zilizowazi vipi, wasingeliamini.

 

Na si kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Anawajaalia vifuniko nyoyoni mwao na uziwi masikioni bila ya sababu tu kama kwamba ni dhulma, Hasha! Allaah (سبحانه وتعالى) Hadhulumu chembe ya uzito wa atomu! Bali Allaah (سبحانه وتعالى) kwa Ujuzi Wake Ameshajua kuwa watu hawa kamwe hawataamini kama vile Alivyojua kuwa Abu Lahab ambaye ni ammi yake Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) hatoamini, Akateremsha Wahy wa Suwrat Al-Masad (111) wakati Abu Lahab yungali hai, kwani Allaah (سبحانه وتعالى) Angelijua kuwa atakuja kuamini angali yuhai, basi Asingeteremsha Suwrah ya Qur-aan inayomtaja jina Lake, ukanushaji wake, ukafiri wake na adhabu yake. Na hivyo ndivyo hali ya washirikina na makafiri hawa, kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Ameshajua kuwa hawataamini kamwe ndipo Anapojaalia vifuniko nyoyoni mwao na uziwi masikioni mwao.

 

Na maneno haya Ayasemayo Allaah katika Aayah hii, yalisemwa na wenyewe makafiri na washirikina wa Makkah: 

 

وَقَالُوا قُلُوبُنَا فِي أَكِنَّةٍ مِّمَّا تَدْعُونَا إِلَيْهِ وَفِي آذَانِنَا وَقْرٌ وَمِن بَيْنِنَا وَبَيْنِكَ حِجَابٌ فَاعْمَلْ إِنَّنَا عَامِلُونَ﴿٥﴾

“Na wakasema: Nyoyo zetu zimo katika vifuniko kwa yale unayotuitia, na masikioni mwetu mna uziwi, na baina yetu na baina yako kuna kizuizi, basi tenda nasi tunatenda.” [Fusw-Swilat (41:5)]

 

Na Allaah (سبحانه وتعالى)  Anataja kuweka vifuniko nyoyoni ili zisifahamu kitu kama Anavyosema:

فَإِنَّهَا لَا تَعْمَى الْأَبْصَارُ وَلَـٰكِن تَعْمَى الْقُلُوبُ الَّتِي فِي الصُّدُورِ ﴿٤٦﴾

“Kwani hakika hayapofuki macho, lakini zinazopofuka ni nyoyo zilizomo vifuani.” Rejea Al-Hajj (22:46) ambako kuna maelezo bayana kuhusu maana ya kupofuliwa nyoyo badala ya macho.

 

Kwa muktadha huu, mtu ambaye haamini Aakhirah, basi kamwe hatauona ujumbe wa Qur-aan kuwa una thamani kwake, wala hatokuwa na hisia ya imaan ya kuiamini Qur-aan, bali atahangaikia maisha na manufaa ya dunia na starehe za dunia anazoweza kuzihisi na kuzifurahikia. Ama Qur-aan, hiyo haitamfikia moyoni mwake kamwe!

 

Na hii inarejelea Qadar ya Allaah (سبحانه وتعالى) kwamba Anafanya hivyo kwa kuwa mtu ana uhuru wa kufuata njia mbili; ya hidaya na ya upotofu. Naye ni Mjuzi wa anayehidika na anayepotoka. Kwa ajili hiyo, wale wanaomkanusha Yeye na Ujumbe Wake na wakamshirikisha, Anawaachia wafanye watakavyo bila ya kuwaadhibu, lakini huko Aakhirah watakapofika ndipo watakapojuta na wakatamani kurudi duniani waamini.

 

[5] Makafiri Hawakuamini Kwamba Watafufuliwa: Rejea Al-Israa (17:49).

 

[6] Kitabu: Lawh Al-Mahfuwdhw (Ubao Uliohifadhiwa) Au Qur-aan [Tafsiyr Imaam As-Sa’diy] Rejea Al-Buruwj (85:22).       

 

[7] Kuthibitisha Sifa Za Allaah (سبحانه وتعالى): Rejea Aayah (12) ya Suwrah hii.

 

[8] Maana Ya Ghaibu: Rejea Al-Baqarah (2:3), Luqmaan (31:34) na An-Naml (27:65).

 

[9] Hakuna Kinachofichika Kwa Allaah (سبحانه وتعالى); Kiwe Cha Dhahiri Wala Cha Siri, Kikubwa Wala Kidogo Vipi:

 

Rejea Ghaafir (40:19) kwenye maelezo na rejea mbalimbali.

 

[10] Usingizi Ni Mauti Madogo. Rejea Az-Zumar (39:42).

 

[11] Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!: Rejea Luqmaan (31:13).

 

[12] Manabii Na Rusuli Kumi Na Nane Wametajwa Kuanzia Aayah Hii Na Zinazofuatia:

 

Kuanzia Aayah hii Al-An’aam (6:83) hadi (6:86) wametajwa Manabii kumi na nane, akijumuika na Nabiy Ibraahiym (عليه السّلام) ambaye ameelezewa katika Aayah zilizotangulia. Wengineo waliotajwa katika Suwrah nyenginezo ni: Aadam, Idriys, Huwd, Swaalih, Shu’ayb (عليهم السّلام) na Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم).

 

Suwrah nyenginezo zilotaja Manabii kwa wingi ni: Al-Anbiyaa (21), Maryam (19), Asw-Swaffaat (37), Swaad (38).

 

Rejea pia An-Nisaa (4:69) kupata maelezo kuhusu Manabii na tofauti ya Manabii na Rusuli.

 

Na Manabii na Rusuli, si wote waliosimuliwa katika Qur-aan kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى) katika Kauli Zake kwenye Suwrah An-Nisaa (4:164) na Ghaafir (40:78).

 

 

[13] Shirki Inabatilisha Amali: Rejea Az-Zumar (39:65) kwenye maelezo ya aina za shirki.

 

[14] Ummul-Quraa (Makkah): Sababu Za Kuitwa Ummul-Quraa (Mama Wa Miji), Umuhimu Na Fadhila Zake:

 

Mji wa Makkah unaitwa Ummul-Quraa (Mama wa miji) kwa sababu kadhaa. Miongoni mwazo ni:  

 

(i) Kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى): 

وَلِتُنذِرَ أُمَّ الْقُرَىٰ وَمَنْ حَوْلَهَا

“Na ili uonye (kwacho) Ummul-Quraa (Mama wa miji [Makkah]), na wale ambao wameuzunguka.”

 

Baadhi ya ‘Ulamaa wamesema: Mji wa Makkah umeitwa “Ummul Quraa” (Mama wa miji) kwa kuwa ndio asili ya miji yote ya ardhi, na kutokea hapo, ardhi ndipo ilipotandazwa. Na kwa sababu hiyo, mji wa Makkah uko katikati ya dunia.

 

Na ndio maana Makkah ukawa ni mji mkongwe kabisa uliojulikana kwa watu.

 

(ii) Mji wa Makkah una historia ya Nabiy Ismaa’iyl na baba yake Nabiy Ibraahiym (عليهما السلام). Pia Mama yake Nabiy Ismaa’iyl (Haajar) ambaye alisai baina ya Swafaa na Marwaa kusaka maji na kububujika kwa maji ya Zamzam. Pia Nabiy Ibraahiym (عليه السّلام) kujenga Al-Ka’bah, kisha akasimama kuomba duaa katika Maqaam Ibraahiym (Jiwe ambalo alisimama juu yake wakati wa ujenzi wa Al-Ka’bah) ambapo Waislamu wote wanaswali Rakaa mbili baada ya kutufu Al-Ka’bah. Rejea Al-Baqarah (2:125-129), Ibraahiym (14:35-42).

 

(iii) Nyumba ya kwanza ambayo imeasisiwa kwa ajili ya watu kufanya ibaada kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى) katika Suwrat Aal-‘Imraan (3:96).

 

(iv) Nabiy wa Mwisho kabisa Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) ambaye ametokana na kizazi cha Nabiy Ismaa’iyl (عليه السّلام), kuzaliwa humo na akaishi humo na ndipo alipoteremshiwa Wahy wa Qur-aan humo akaishi humo hadi kuhajiri Madiynah. 

 

(v) Masjid Al-Haraam iliyoko Makkah ni Msikiti wa kwanza kuanzishwa duniani kama ilivyothibiti katika Hadiyth: Abuu Dharr (رضي الله عنه) amehadithia kwamba: Nilisema: Ee Rasuli wa Allaah! Masjid gani ilijengwa ardhini mwanzo? Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Masjid Al-Haraam (Makkah).” Nikasema: Kisha upi? Akasema: “Masjid Al-Aqswaa (Palestina).” Nikasema: Kuna muda gani baina ya kuwepo Masjid mbili hizo? Akasema: “Miaka arubaini na popote itakapokudiriki Swalaah basi swali hapo pia ardhi ni mahala pa kuswali.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

(vi) Ni kivutio na kipenzi cha Waumini wa ulimwengu wote kwa sababu, baada ya Nabiy Ibraahim (عليه السّلام) [na mwanawe Nabiy Ismaa’iyl (عليه السّلام)] kujenga Al-Ka’bah, aliomba duaa kwamba nyoyo za watu zipendelee kuelekea huko. Rejea Ibraahiym (14:38).

 

(vii) Qibla cha Waislamu wote duniani kimo humo, kwa maana, Waislamu wote ulimwenguni wanaekelekea huko katika Swalaah zao, kitendo ambacho bila ya kuelekea Qiblah, Swalaah hitimii.

 

(viii) Swalaah inayoswaliwa humo ina thawabu maradufu: Amesimulia Jaabir (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)  amesema: “Swalaah katika Msikiti wangu ni bora kuliko Swalaah elfu kwengineko isipokuwa Al-Masjid Al-Haraam. Na Swalaah katika Al-Masjid Al-Haraam ni bora kuliko Swalaah elfu mia (laki moja) kwengineko.” [Ahmad, Ibn Maajah na imesahihishwa na Imaam Al-Albaaniy katika Swahiyh Ibn Maajah (1163), Swahiyh Al-Jaami’ (3838)]

 

(ix) Makkah ni mji Mtukufu kabisa na mambo kadhaa yameharamishwa ndani yake na ndio maana Makkah ikaitwa Haram Makkah. Hadiyth ifuatayo imetaja baadhi ya maharamisho: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Allaah Ameuharamisha Mji huu Siku Allaah Alipoumba mbingu na ardhi. Basi Mji huu ni hifadhi isiyoguswa kwa Haramisho la Allaah hadi Siku ya Qiyaamah, na hakuruhusiwa yeyote kabla yangu kupigana ndani yake, na haikuruhusiwa kwangu isipokuwa saa moja ya mchana. Basi ni hifadhi isiyoguswa kwa Haramisho la Allaah mpaka Siku ya Qiyaamah. Mwiba wake haukatwi, wala wanyama wake wa kuwindwa hawatimuliwi, wala haokoti chenye kupotezwa humo isipokuwa mwenye kukitangazia, na wala manyasi yake hayakatwi.” Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) akasema: Ee Rasuli wa Allaah! Isipokuwa “idh-khir” (aina ya mmea wenye harufu nzuri, [mchaichai]), kwani huo ni kwa mhunzi (kuwashia moto) na kwa (kuezekea paa za) nyumba zao. Akasema: “Isipokuwa idh-khir.” [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1834) na Muslim (1353)]

 

(x) Umrah na Hajj inatekelezwa huko Makkah na Hajj ni nguzo mojawapo katika nguzo tano za Uislamu.

 

Na mengineyo yametajwa kuhusu utukufu wa Makkah na Allaah Mjuzi zaidi.

 

[15] Waongo Waliodai Unabii Baada Ya Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم):

 

Amesema ‘Ikrimah na Qataadah  (رضي الله عنهما): “Aayah hii imeteremshwa kumhusu Musaylamah Al-Kadh-dhaab Laana ya Allaah imfikie!” [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

Na Imaam As-Sa’adiy (رحمه الله)  amesema: “Waliojumuishwa katika Aayah hii ni wale wote wanaodai Unabii kama Musaylamah Al-Kadh-dhaab, Al-Aswad Al-‘Ansiyy, Mukhtaar na wengineo.” [Tafsiyr As-Sa’diy]. Wametajwa wawili hao katika Hadiyth ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم).  

 

Amesimulia Naafi’ Bin Jubayr (رضي الله عنه): Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) amesema: Musaylamah Al-Kadh-dhaab (yaani mrongo), alikuja na watu wake wengi Madiynah) katika zama za Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akawa anasema: “Lau Muhammad atanifanya mimi kuwa mrithi baada yake, basi nitamfuata.” Na watu wengi katika kaumu yake wakamfuata. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)        alimwendea akiwa na Thaabit bin Qays bin Sham-maas, na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa ameshika mkononi mwake kitagaa cha mtende (kipande cha jani la mtende). Akasimama mbele ya Musaylamah na watu wake, akasema: “Lau utaniomba kipande hiki (kitagaa), sitokupatia. Na wala huwezi kuikwepa Amri ya Allaah Aliyokuhukumia. Na ukiukanusha Uislamu, basi Allaah Atakuangamiza. Na wewe kwa hakika nakuona ni mtu mwenye sifa zile zile nilizoonyeshwa kwenye njozi.” Abu Hurayrah (رضي الله عنه) aliniambia kuwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)   amesema: “Nilipokuwa nimelala, niliona katika njozi vikuku viwili vya dhahabu mkononi mwangu, na hilo likanitia hamu mno. Kisha nikafunuliwa Wahy katika njozi hiyo nivipulize, nikavipuliza navyo vikaruka. Nikatafsiri njozi ya vikuku hivyo kuwa ni ishara ya waongo wawili watakaokuja baada yangu. Mmoja wao ni Al-‘Ansiyy, na mwengine ni Musaylamah Al-Kadh-dhaab kutoka Al-Yamaamah.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

[16] Viumbe Watafufuliwa Wakiwa Kama Walivyozaliwa: Rejea Al-Kahf (18:48), Al-Anbiyaa (21:104).

 

[17] Allaah (سبحانه وتعالى)  Mpasuaji Mbegu Na Anatoa Kilicho Hai Kutokana Na Kilicho Mfu, Na Mtoaji Wa Kilicho Mfu Kutokana Na Kilicho Hai.

 

Allaah (سبحانه وتعالى) Anaeleza kuwa Yeye huzifanya mbegu za nafaka na za matunda kupasuka na kuchipua ardhini, na kutoa aina mbalimbali ya nafaka, matunda, mboga na kadhaalika zikiwa katika rangi mbalimbali, umbo wa kila aina na ladha tofauti katika mazao hayo. Rejea Ar-Ra’d (13:3-4). Na kwamba Analeta mmea ulio hai kutoka mbegu ya nafaka na mbegu ya matunda, (mbegu) ambazo zisizokuwa na uhai na hii ni ishara na dalili mojawapo ya kuwa Yeye Ni Muumbaji wa kila kitu [Az-Zumar (39:62)] Na kama Anavyosema:

 

وَآيَةٌ لَّهُمُ الْأَرْضُ الْمَيْتَةُ أَحْيَيْنَاهَا وَأَخْرَجْنَا مِنْهَا حَبًّا فَمِنْهُ يَأْكُلُونَ ﴿٣٣﴾

“Na Aayah (Ishara, Dalili) kwao ni ardhi iliyokufa, Tukaihuisha, na Tukatoa humo nafaka, wakapata kuzila.” [Yaasiyn (36:33)]

 

Hali kadhalika Kauli Yake hii Allaah (سبحانه وتعالى):

  

يُخْرِجُ الْحَيَّ مِنَ الْمَيِّتِ وَمُخْرِجُ الْمَيِّتِ مِنَ الْحَيِّ

“Anatoa kilicho hai kutokana na kilicho mfu, na Mtoaji wa kilicho mfu kutokana na kilicho hai.” [Al-An’aam (6:95)]  

 

Ni mfano wa Yeye Allaah (سبحانه وتعالى) Kujaalia yai kutoka kwa kuku, kuzaliwa kuku kutokana na yai. [Tafsiyr Ibn Kathiyr]  

 

Rejea Aal-‘Imraan (3:26-27), Yuwnus (10:31), Ar-Ruwm (30:19), (30:50), na Yaasiyn (36:38) kwenye faida tele na maelezo bayana kuhusu Qudura, Takdiri ya Allaah (سبحانه وتعالى). 

 

[18] Takdiri (Qudura, Ukadariaji) Ya Allaah (سبحانه وتعالى): Rejea Aal-‘Imraan (3:190), (3:26-27) Yaasiyn (36:38), Al-Falaq (113:1).

 

[19] Nyota Zimeumbwa Kwa Ajili Ya Matatu:

 

Rejea pia An-Nahl (16:16).

 

Amesimulia Qataadah (رضي الله عنه) : “Allaah Ameumba hizi nyota kwa malengo matatu: (i) mapambo ya mbingu (ii) vimondo vya (kuwafukuza na kuwapiga) shaytwaan, (iii) alama za kuongoza njia (wasafiri wa majangwani na baharini). Basi atakayefasiri vingine amekosea na atakuta patupu Aakhirah (atakosa thawabu) kwani atakuwa amebeba asio na ilimu nayo kwa kuchupa mipaka ya ujuzi Wake.” [Al-Bukhaariy] 

 

Nyota zimeumbwa kwa ajili ya mambo matatu hayo tu! Basi Hadiyth hii inawakanusha wanajimu (watabiri wa nyota) jambo ambalo ni la kumshirikisha Allaah (سبحانه وتعالى) nayo ni shirki kubwa ambayo Allaah (سبحانه وتعالى) Haisamehe.

 

[20] Mustaqarr (Mahali pa kustakiri) ni tumboni mwa mama au duniani. Mustawda’ (Mahali pa kuhifadhiwa) ima migongoni mwa baba au kaburini.

 

 

[21] Washirikina Wamempachikia Uongo Allaah Kuwa Ana Wana Wa Kike Na Wa Kiume: Rejea Asw-Swaffaat (37:149).

 

[22]  Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) Hakumuona Allaah (سبحانه وتعالى):

 

Masruwq (رضي الله عنه) amehadithia kwamba: Nilimwambia ‘Aaishah (رضي الله عنها): Ee Mama! Je Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) alimuona Rabb wake? Akasema: Hayo uliyoyasema yamefanya nywele zangu zisimame kunisisimka mwili! Tambua kwamba mtu akikutajia mambo matatu yafuatayo basi yeye ni muongo! Atakayesema kwamba Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) amemuona Rabb wake, kisha akasoma:

 

لَّا تُدْرِكُهُ الْأَبْصَارُ وَهُوَ يُدْرِكُ الْأَبْصَارَ ۖ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ ﴿١٠٣﴾

“Macho hayamzunguki bali Yeye Anayazunguka macho yote, Naye Ni Mwenye Kudabiri mambo kwa Ulatifu, Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri.” [Al-An'aam (6:103)]

 

Na akasoma pia:

 

وَمَا كَانَ لِبَشَرٍ أَن يُكَلِّمَهُ اللَّـهُ إِلَّا وَحْيًا أَوْ مِن وَرَاءِ حِجَابٍ أَوْ يُرْسِلَ رَسُولًا فَيُوحِيَ بِإِذْنِهِ مَا يَشَاءُ ۚ إِنَّهُ عَلِيٌّ حَكِيمٌ﴿٥١﴾

“Na wala haikuwa kwa mtu yeyote kwamba Allaah Amsemeze isipokuwa kwa Wahy au kutoka nyuma ya kizuizi, au Hutuma Mjumbe, kisha Anamfunulia Wahy Ayatakayo kwa Idhini Yake. Hakika Yeye Ni Mwenye ‘Uluwa, Mwenye Hikmah wa yote.” [Ash-Shuwraa (42:51)]

 

Kisha akaendelea kusema: Na atakayesema kwamba Nabiy anajua yatakayotokea kesho basi ni muongo. Kisha Akasoma:

وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ مَّاذَا تَكْسِبُ غَدًا ۖ

“Na nafsi yoyote haijui nini itachuma kesho, na nafsi yoyote haijui itafia katika ardhi gani.” [Luqmaan (31:34)]

 

Kisha akasema: Na atakayesema kuwa Nabiy ameficha aliyofunuliwa Wahyi (na maamrisho) basi ni muongo! Kisha akasoma:

 

يَا أَيُّهَا الرَّسُولُ بَلِّغْ مَا أُنزِلَ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ ۖ وَإِن لَّمْ تَفْعَلْ فَمَا بَلَّغْتَ رِسَالَتَهُ ۚ  

“Ee Rasuli! Balighisha yale yaliyoteremshwa kwako kutoka kwa Rabb wako. Na usipofanya, basi utakuwa hukubalighisha ujumbe Wake.” [Al-Maaidah (5:67)]

 

Kisha akasema: Lakini Nabiy alimuona Jibriyl katika umbile lake khalisi mara mbili. [Al-Bukhaariy]

 

Kwa upande mwengine Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما)  amesema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alimuona Allaah, na akasema kuwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alimuona Rabb wake mara mbili. [Tafsiyr Ibn Kathiyr]  

 

Al-Haafidhw, Ibn Hajar amesema: “Maelezo ya Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) yamekuja katika hali ya kutodhibitiwa (hayaelezi kama Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alimuona Rabb wake kwa macho yake au vipi) wakati kauli za Mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها) na wenziwe zimedhibitiwa kwa kusema Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) hakumuona Allaah “Kwa macho yake.” Tunaweza kuunganisha kauli hizo mbili kwa kusema Mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها)   alikataa muono “Kwa macho yake” na kauli ya Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما)  kuwa ni kamuona kiroho.” [Fat-hul-Baariy (8/608)]  

 

Na Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) kwa riwaaya nyingine alisema kuwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alimuona Rabb wake wakati akiwa katika usingizi, na hii ni njozi ya kweli. Na kauli ya Mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها) inakataa, na kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) hakumuona Rabb wake wakati yeye akiwa macho, lakini kauli hiyo haikatazi kuwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alimuona Rabb wake akiwa usingizini. Alichokana hapa ni kuwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) hakumuona Allaah kwa macho yake meupe, akiwa macho.  

 

Wale ambao wanao msimamo kuwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alimuona Rabb wake kwa macho yake meupe wanaleta Hadiyth dhaifu. Hakuna Hadiyth Swahiyh ambayo inaeleza ya kuwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alimuona Rabb wake kwa macho yake akiwa macho. Wenye msimamo huo wanaleta Hadiyth ya At-Tirmidhiy ambayo Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) anasema kuwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alimuona Rabb wake. ‘Ikrimah alimuuliza: “Vipi Aayah ambayo inasema:

 

لَّا تُدْرِكُهُ الْأَبْصَارُ وَهُوَ يُدْرِكُ الْأَبْصَارَ ۖ

“Macho hayamzunguki, bali Yeye Anayazunguka macho yote.” [Al-An’aam (6:103)]

 

Alijibu, kuwa ni wakati tu Allaah amezungukwa na Nuru, lakini Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alimuona Rabb wake mara mbili. “Hadiyth hii ni dhaifu.”

 

Kwa hali hiyo, hakuna mgongano wa kauli, na Allaah Anajua zaidi [Sharh ya Uswuwl Al-I’itiqaad cha Al-Laalika’iy, (93/512), As-Sunnah (1/181) na Swifaat Al-Maqdisiy ukurasa (109-111]   

 

Hapa kunathibitishwa kuwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) hakumuona Rabb wake wakati alipopelekwa Al-Israa Wal Mi’raaj, na dalili nyengine ni Hadiyth ifuatayo:

 

Amesimulia Abu Dharr (رضي الله عنه): Nilimuuliza Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم): Je ulimuona Rabb wako? Akasema: “(Yeye ni) Nuru; vipi niweze kumuona?” [Muslim]

 

Na hii ndio ‘Aqiydah ya Ahlus-Sunnah wal-Jamaa’ah kuwa Allaah Haonekani duniani, kinyume na ‘Aqiydah ya Masufi wanaoamini kuwa Allaah Anaonekana duniani kwa kuegemeza tukio hilo la Al-Israa Wal Mi’raaj.

 

Kadhaalika, Aayah hiyo vilevile haikanushi kuonekana Allaah Qiyaamah, bali Qiyaamah Allaah Ataonekana katika kisimamo cha Qiyaamah katika Jannah (Peponi) kwa dalili nyingi kutoka katika Qur-aan na Sunnah, kinyume na ‘Aqiydah ya makundi potofu yanayoamini kuwa Allaah Hatoonekana Aakhirah.

 

[23] Haramisho La Kuwatukana Watu Ili Tusi Lisimrudie Asiyestahiki Kutukanwa:

 

Tahadharisho kama hili la kutokuwatukana waabudiwa wa washirikina ili tusi lisimrudie Allaah (سبحانه وتعالى), limeharamishwa pia vile mtu kumtukana mzazi wa mwenziwe, ili tusi lisimrudie mzazi wake:

 

 

عَنْ عَبْدِ اَللَّهِ بْنِ عَمْرِو بْنِ الْعَاصِ ‏رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا‏ أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏قَالَ: {مِنْ اَلْكَبَائِرِ شَتْمُ اَلرَّجُلِ وَالِدَيْهِ.‏ قِيلَ: وَهَلْ يَسُبُّ اَلرَّجُلُ وَالِدَيْهِ؟ قَالَ: نَعَمْ.‏ يَسُبُّ أَبَا اَلرَّجُلِ، فَيَسُبُّ أَبَاهُ، وَيَسُبُّ أُمَّهُ، فَيَسُبُّ أُمَّهُ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Amesimulia ‘Abdullaah bin ‘Amr bin Al-‘Aasw (رضي الله عنهما): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Miongoni mwa madhambi makubwa ni mtu kutukana wazazi wake.” Swahaba wakasema: Mtu anaweza kutukana wazazi wake? Akasema: “Ndiyo, atamtukana baba wa mtu naye anamtukana baba yake, na atamtukana mama wa mtu naye atamtukana mama yake.” [Bukhaariy, Muslim]

 

Imaam As-Sa’diy (رحمه الله) amesema: Allaah (سبحانه وتعالى) Anawakataza Waumini kufanya jambo ambalo mwanzo waliruhusiwa na hata kuamrishwa kulifanya; nalo ni kudharau na kutukana masanamu ya washirikina ambao wamewafanya ni waabudiwa wao badala ya Allaah. Kuruhusika kwake ilikuwa ni kwa sababu kuwatukana waabudiwa wao ni kuwadhalilisha na ilikuwa ni njia ya kujikurubisha kwa Allaah. Lakini kwa sababu kufanya hivyo kungeweza kupelekea washirikina kumtukana Rabb wa ulimwengu, Ambaye Anatakasika na kila kosa na matukano au ovu lolote, Allaah Anakataza kuwatukana waabudiwa wa washirikina, kwa sababu watahamasika kulinda dini yao na watataka kujikurubisha kwa waabudiwa wao. Hivyo ni kwa kuwa Allaah Amewapambia kila umma matendo yake, wanafikiri kwamba njia zao ni nzuri, basi ikiwa Waislamu watatukana waabudiwa wao, wao washirikina watawalinda kwa njia zote, hata kama ni matusi kwa Allaah Rabb wa walimwengu. 

 

Lakini watu wote watarejea kwa Allaah Siku ya Qiyaamah kisha watahudhurishwa wao na vitendo vyao mbele Yake, na Awajulishe yale waliyokuwa wakiyafanya, mema na mabaya.

 

Aayah hii ni dalili kwamba njia za kutumika kufikisha jambo, zinapaswa kuzingatiwa kwa malengo, na kwamba njia ambazo zinaweza kusababisha kitu kuwa haramu- hata kama njia hizo zinaruhusiwa- basi zinapaswa kuzingatiwa kuwa ni haramu pia, ikiwa zitaongoza kwenye maovu. [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

[24] Mfano Wa Kafiri Aliyekuwa Maiti (Katika Viza) Na Muumini Aliyekuwa Hai (Katika Nuru):

 

Aliyekuwa maiti kabla ya hidaaya ya Allaah, yaani alikuwa mwanzo katika viza vya kufru, ujahili na uasi, kisha Allaah Akamhuisha katika nuru ya imaan, ilimu na utiifu, akatembea na nuru kati ya watu, akawa ni mtu ambaye ana utambuzi wa mambo yake, akiiongoza njia yake na akajua lililo jema na akajitahidi kulitekeleza mwenyewe na pia akalitekeleza katika uhusiano wake na wengineo. Hali kadhalika akatambua uovu na akauchukia na akijitahidi kuuepuka mwenyewe na kuwaepushia wenziwe. Je, huyu yuko sawa na aliye katika viza vya ujahili, upindukiaji mipaka, kufru na maasi, hawezi kutoka humo, kwa sababu amechanganyikiwa; hajui apitie njia gani, hivyo amefunikwa na wasiwasi, shaka, dhiki na huzuni.

 

Hapa Allaah Anabainisha watu wenye busara kwamba, wao tayari wanajua na kuelewa kwamba hawa wawili hawawezi kulingana sawa, kama vile hauwezi usiku na mchana kuwa sawa au mwanga na giza au walio hai na wafu... [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

Rejea pia Faatwir (35:19) kwenye maelezo na faida ziyada kuhusu mifano ya Allaah baina ya kafiri na Muumin. Rejea pia Huwd (11:24).

 

[25] Maana Ya Baghi Katika Qur-aan:

 

Rejea Ash-Shuwraa (42:14) kupata maana zake mbalimbali.

[26] Maana Ya Kutokufarikiana:

 

Rejea Al-Faatihah (1:6), Aal-‘Imraan (3:103).

 

[27] Kuteremka Allaah Na Malaika Siku Ya Qiyaamah:

 

Rejea Al-Fuqaan (25:25), Al-Haaqah (69:13-18), Al-Baqarah (2:210).

 

[28] Alama Kubwa Za Qiyaamah: Makafiri Hawakuamini Kuwa Qiyaamah Kitatokea:


 ☞ Ukurasa wa Nne




Report Page