006-Al-An’aam

006-Al-An’aam

Khamis

Washirikina wa Makkah walikuwa haweshi kuuliza lini Qiyaamah kitatokea. Rejea Al-A’raaf (7:187), Al-Ahzaab (33:63), An-Naazi’aat (79:42). Al-Mulk (67:25), Ash-Shuwraa (42:18), Ghaafir (40:59).

 

Aayah hii tukufu imetaja kuwa kutatokea Alama kuu kabla ya kufika Qiyaamah ambazo wale wasioamini kabla ya kutokea alama hizo, watakapotaka kuamini, basi imaan zao hazitawafaa lolote kwa kuwa hawatakubaliwa kuamini kwao.

 

‘Ulamaa wametaja alama hizo kubwa ingawa wamekhitilafiana katika mpangilio wake na kuzitaja kwake nazo ni:

 

(i) Kuja kwa Mahdi: Mja kutoka katika ahli wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) (ii) Kutokeza kwa Masiyh Ad-Dajjaal (iii) Kuteremka kwa Nabiy ‘Iysaa na (عليه السّلام)  na kumuua Masiyh Ad-Dajjaal na kuondosha misalaba, kuua nguruwe na kuondosha dini zote nyenginezo isipokuwa Uislamu (iv) Kuchomoza kwa Yaajuwj na Maajuwj (v) Kubomolewa Ka’bah na kutoka moshi (vi) Kuondoshwa Qur-aan nyoyoni mwa Waumini na Miswahafu (vii) Jua kuchomoza Magharibi (viii) Kutokeza mnyama mwitu mkubwa atakayewasemesha watu (ix) Mididimizo mitatu ya ardhi: Mdidimizo wa Mashariki, Magharibi na katika Jaziyrah ya Arabia (x) Moto utakaotoka kutoka Yemen utawapeleka watu kufika katika Ardhi ya Mkusanyiko.

 

Na Hadiyth ifuatayo imeorodhesha alama kumi: 

 

Amesimulia Hudhayfah Bin Asiyd (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa chumbani nasi tulikuwa chini yake, akachungulia na kutuuliza:  “Mnajadiliana nini?” Tukasema: (Tunajadili kuhusu) Saa (Qiyaamah). Hapo akasema: Saa (Qiyaamah) hakitatokea mpaka zionekane alama (au ishara) kumi: (i) Kudidimia kwa Mashariki (ii) Kudidimia kwa Magharibi. (iii) Kudidimia Bara la Arabu (iv) Moshi. (v) (Masiyh) Ad-Dajjaal. (vi) Mnyama mkubwa wa ardhi (atakayewasemesha watu) (vii) Ya-ajuwj na Ma-ajuwj (viii) Kuchomoza jua upande wa Magharibi (ix) Moto utakaotokea upande wa chini ya ‘Aden utakaowasukuma watu (kufikia Ardhi ya Mkusanyiko).” Shu'bah  amesema na amenihadithia  ‘Abdul-‘Aziyz bin Rufa’y kutoka kwa Abiy Atw-Twufayl kutoka kwa Abiy Sariyhah Hadiyth kama hiyo ila Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) hakuitaja (alama ya kumi) lakini alisema kuwa katika kumi, mojawapo ni kuteremka Nabiy ‘Iysaa bin Maryam (عليه السّلام) na katika riwaaya nyengine ni: Upepo mkali utakaowaendesha watu na kutupwa  baharini. [Muslim]

 

Rejea Al-Kahf (18:94) kulikotajwa kuhusu Yaajuwj na Maajuwj.

 

[29] Kugawanyika Watu Makundi Makundi:

 

Allaah (سبحانه وتعالى) Anawakemea wale wanaoigawa Dini yao, yaani, kuigawanya na kufarikiana ndani yake, na kila mmoja anajiwekea sehemu ya majina ambayo haimnufaishi mtu katika dini yake chochote, kama vile Uyahudi, Unaswara na Umajusi. Au (Majina hayo) hayamtimizii mtu imaan yake kwayo, kwa kuchukua kitu katika sharia na kukifanya kuwa ndio dini yake, na kuacha kitu mfano wake, au kinachostahiki zaidi yake. Hivyo ni kama ilivyo kwa watu wa makundi ya bid’ah na upotofu na wanao farakanisha ummah. Na Aayah tukufu ikaashiria kuwa Dini inaamrisha umoja na muungano, na inakataza mifarakano na khitilafu katika watu wa dini, na katika masuala yake yote ya msingi na matawi. Akamuamuru kuwatenga wale walioigawa dini yao. [Imaam As-Sa’diy katika Tafisyr yake]

 

Rejea pia Aayah (153) Suwrah hii ya Al-An’aam. 

 

[30]  Rahmah Ya Allaah (سبحانه وتعالى) Kwa Waumini Kuongezewa Thawabu Mara Kumi Kwa Amali Njema Moja Na Kuandikiwa Dhambi Moja Tu Kwa Tendo Ovu:

 

Ukitia niya kutenda amali moja lakini ukawa hukujaaliwa kuitenda utaandikiwa moja. Utakapoweza kuitenda utalipwa mara kumi yake.

Ukitia niya kutenda uovu haitoandikwa kwanza kwa kuwa Allaah (سبحانه وتعالى) Anampa mja muhula ajirudi ili asitende uovu au dhambi. Na atakapotenda basi ataandikiwa dhambi moja.

Amesimulia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Allaah Ameandika mema na mabaya, kisha Akayabainisha, basi atakayetia niya kutenda jema kisha asilifanye, ataandikiwa jema moja kamili. Atakapofanya hima na akalitenda, ataandikiwa mema kumi hadi kuzidi mia saba na ziada nyingi. Na atakayetia niya kufanya kitendo kibaya kisha asikifanye, ataandikiwa jema moja kamili. Atakapokifanya, ataandikiwa dhambi moja.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

[31] Dua Mojawapo Ya Kufungulia Swalaah:

 

Aayah (6:162-163) ni mojawapo ya Dua ya kufungulia Swalaah kama ilivyothibiti katika Sunnah kusema:

 

وَجَّهـتُ وَجْهِـيَ لِلَّذي فَطَرَ السَّمـواتِ وَالأَرْضَ حَنـيفَاً وَمـا أَنا مِنَ المشْرِكين، إِنَّ صَلاتـي، وَنُسُكي، وَمَحْـيايَ، وَمَماتـي للهِ رَبِّ العالَمين، لا شَريـكَ لَهُ وَبِذلكَ أُمِرْتُ وَأَنا مِنَ المسْلِـمين.

Nimeuelekeza uso wangu kwa yule Ambaye Ameanzisha mbingu na ardhi hali ya kuelemea katika haki, na sikuwa mimi ni katika washirikina, hakika Swalaah yangu na kuchinja kwangu na uhai wangu, na kufa kwangu ni kwa Allaah Rabb walimwengu, Hana mshirika, na kwa hilo nimeamrishwa nami ni katika Waislamu. 

 

Na katika riwaaya nyenginezo inaishia kwa:

وَأَنَا أَوَّلُ الْمُسْلِمِينَ

nami ni Muislamu wa kwanza.

(Kisha dua inaendelea)

 

Pia Aayah hii ni dalili mojawapo ya haramisho la kuchinja kwa kukusudia asiyekuwa Allaah.

 

 


Report Page