006 Al-An’aam

006 Al-An’aam

Khamis

  Next page 📄 2

 الأنْعَام

 

 Utangulizi Wa Suwrah

 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَجَعَلَ الظُّلُمَاتِ وَالنُّورَ ۖ ثُمَّ الَّذِينَ كَفَرُوا بِرَبِّهِمْ يَعْدِلُونَ ﴿١﴾

1. AlhamduliLLaah (Himdi Anastahiki Allaah), Ambaye Ameumba mbingu na ardhi na Akajaalia viza na nuru, kisha wale ambao wamekufuru wanawasawazisha wengine na Rabb wao.

 

 

 

هُوَ الَّذِي خَلَقَكُم مِّن طِينٍ ثُمَّ قَضَىٰ أَجَلًا ۖ وَأَجَلٌ مُّسَمًّى عِندَهُ ۖ ثُمَّ أَنتُمْ تَمْتَرُونَ ﴿٢﴾

2. Yeye Ndiye Ambaye Amekuumbeni kutokana na udongo kisha Akahukumu muda maalumu, na uko Kwake muda maalumu uliokadariwa, kisha nyinyi mnatilia shaka!

 

 

 

وَهُوَ اللَّـهُ فِي السَّمَاوَاتِ وَفِي الْأَرْضِ ۖ يَعْلَمُ سِرَّكُمْ وَجَهْرَكُمْ وَيَعْلَمُ مَا تَكْسِبُونَ ﴿٣﴾

3. Na Yeye Ndiye Allaah mbinguni na ardhini, Anajua ya siri yenu na ya dhahiri yenu, na Anajua yale mnayoyachuma.[1]

 

وَمَا تَأْتِيهِم مِّنْ آيَةٍ مِّنْ آيَاتِ رَبِّهِمْ إِلَّا كَانُوا عَنْهَا مُعْرِضِينَ ﴿٤﴾

4. Na haiwafikii Aayah (Ishara, Muujiza, Hoja bayana) yoyote ile katika Aayaat (Ishara, Miujiza, Hoja bayana) za Rabb wao isipokuwa huwa ni wenye kuipuuza.

 

 

فَقَدْ كَذَّبُوا بِالْحَقِّ لَمَّا جَاءَهُمْ ۖ فَسَوْفَ يَأْتِيهِمْ أَنبَاءُ مَا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ ﴿٥﴾

5. Kwa yakini wameikadhibisha haki ilipowajia, basi zitawafikia khabari muhimu za yale waliyokuwa wakiyafanyia istihzai.

 

 

 

أَلَمْ يَرَوْا كَمْ أَهْلَكْنَا مِن قَبْلِهِم مِّن قَرْنٍ مَّكَّنَّاهُمْ فِي الْأَرْضِ مَا لَمْ نُمَكِّن لَّكُمْ وَأَرْسَلْنَا السَّمَاءَ عَلَيْهِم مِّدْرَارًا وَجَعَلْنَا الْأَنْهَارَ تَجْرِي مِن تَحْتِهِمْ فَأَهْلَكْنَاهُم بِذُنُوبِهِمْ وَأَنشَأْنَا مِن بَعْدِهِمْ قَرْنًا آخَرِينَ ﴿٦﴾

6. Je, hawaoni ni karne ngapi za vizazi Tumeziangamiza kabla yao? Tuliwamakinisha katika ardhi kwa namna ambayo Hatujapata kuwamakinisha nyinyi, na Tukawapelekea mvua tele iendeleayo, na Tukajaalia mito ipitayo chini yao. Hatimaye Tukawaangamiza kwa dhambi zao na Tukaanzisha baada yao karne nyingine ya vizazi.

 

 

 

وَلَوْ نَزَّلْنَا عَلَيْكَ كِتَابًا فِي قِرْطَاسٍ فَلَمَسُوهُ بِأَيْدِيهِمْ لَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا إِنْ هَـٰذَا إِلَّا سِحْرٌ مُّبِينٌ ﴿٧﴾

7. Na lau Tungelikuteremshia (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) maneno yaliyoandikwa katika karatasi, kisha wakaigusa kwa mikono yao, bila shaka wale waliokufuru wangelisema: Hii si chochote isipokuwa ni sihiri (uchawi) bayana.

 

 

 

 

وَقَالُوا لَوْلَا أُنزِلَ عَلَيْهِ مَلَكٌ ۖ وَلَوْ أَنزَلْنَا مَلَكًا لَّقُضِيَ الْأَمْرُ ثُمَّ لَا يُنظَرُونَ ﴿٨﴾

8. Na wakasema: Mbona hakuteremshiwa Malaika? Na lau Tungeliteremsha Malaika, basi amri ingepitishwa kisha wasingelipewa muhula.

 

 

 

 

وَلَوْ جَعَلْنَاهُ مَلَكًا لَّجَعَلْنَاهُ رَجُلًا وَلَلَبَسْنَا عَلَيْهِم مَّا يَلْبِسُونَ ﴿٩﴾

9. Na lau Tungelimfanya Malaika, bila shaka Tungelimfanya binaadam mwanamume, na Tungeliwatatanishia yale wanayojitatanisha.

 

 

 

 

وَلَقَدِ اسْتُهْزِئَ بِرُسُلٍ مِّن قَبْلِكَ فَحَاقَ بِالَّذِينَ سَخِرُوا مِنْهُم مَّا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ ﴿١٠﴾

10. Na kwa yakini walifanyiwa istihzai Rusuli kabla yako, lakini wale waliowafanyia dhihaka, yaliwazunguka yale yale waliyokuwa wakiyafanyia istihzai.

 

 

 

قُلْ سِيرُوا فِي الْأَرْضِ ثُمَّ انظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُكَذِّبِينَ ﴿١١﴾

11. Sema: Nendeni katika ardhi, kisha mtazame vipi ilikuwa hatima ya wenye kukadhibisha.[2]

 

 

 

قُل لِّمَن مَّا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ قُل لِّلَّـهِ ۚ كَتَبَ عَلَىٰ نَفْسِهِ الرَّحْمَةَ ۚ لَيَجْمَعَنَّكُمْ إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ لَا رَيْبَ فِيهِ ۚ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنفُسَهُمْ فَهُمْ لَا يُؤْمِنُونَ ﴿١٢﴾

12. Sema: Ni vya nani vilivyomo mbinguni na ardhini? Sema: Ni vya Allaah. Amejiwajibishia Nafsi Yake[3] Rahmah. Bila shaka Atakukusanyeni Siku ya Qiyaamah, hapana shaka yoyote ndani yake. Wale ambao wamekhasiri nafsi zao basi wao hawaamini.

 

 

 

وَلَهُ مَا سَكَنَ فِي اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ ۚ وَهُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ ﴿١٣﴾

13. Na ni Vyake vyote vinavyotulia katika usiku na mchana. Naye Ni Mwenye Kusikia yote, Mjuzi wa yote.

 

 

 

 

قُلْ أَغَيْرَ اللَّـهِ أَتَّخِذُ وَلِيًّا فَاطِرِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَهُوَ يُطْعِمُ وَلَا يُطْعَمُ ۗ قُلْ إِنِّي أُمِرْتُ أَنْ أَكُونَ أَوَّلَ مَنْ أَسْلَمَ ۖ وَلَا تَكُونَنَّ مِنَ الْمُشْرِكِينَ ﴿١٤﴾

14. Sema: Je, nimfanye rafiki mlinzi asiyekuwa Allaah Muanzilishi wa mbingu na ardhi, Naye Ndiye Anayelisha na wala Halishwi? Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Hakika mimi nimeamrishwa niwe wa kwanza katika wenye kusilimu. Na wala usijekuwa kabisa miongoni mwa washirikina.

 

 

 

قُلْ إِنِّي أَخَافُ إِنْ عَصَيْتُ رَبِّي عَذَابَ يَوْمٍ عَظِيمٍ ﴿١٥﴾

15. Sema: Hakika mimi nakhofu, ikiwa nitamuasi Rabb wangu, adhabu ya Siku iliyo kuu kabisa.

 

 

 

مَّن يُصْرَفْ عَنْهُ يَوْمَئِذٍ فَقَدْ رَحِمَهُ ۚ وَذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْمُبِينُ ﴿١٦﴾

16. Atakayeepushwa nayo (adhabu) Siku hiyo, basi kwa yakini (Allaah) Amemrehemu. Na huko ndiko kufuzu kulio wazi.

 

 

 

 

وَإِن يَمْسَسْكَ اللَّـهُ بِضُرٍّ فَلَا كَاشِفَ لَهُ إِلَّا هُوَ ۖ وَإِن يَمْسَسْكَ بِخَيْرٍ فَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿١٧﴾

17. Na Allaah Akikugusisha kwa dhara, basi hakuna yeyote wa kuiondoa isipokuwa Yeye, na Akikugusisha kheri, basi Yeye juu ya kila kitu Ni Muweza.

 

 

 

 

وَهُوَ الْقَاهِرُ فَوْقَ عِبَادِهِ ۚ وَهُوَ الْحَكِيمُ الْخَبِيرُ ﴿١٨﴾

18. Naye Ndiye Aliyedhibiti vyote chini ya Mamlaka Yake Aliye juu ya Waja Wake. Naye Ndiye Mwenye Hikmah wa yote, Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri.

 

 

 

قُلْ أَيُّ شَيْءٍ أَكْبَرُ شَهَادَةً ۖ قُلِ اللَّـهُ ۖ شَهِيدٌ بَيْنِي وَبَيْنَكُمْ ۚ وَأُوحِيَ إِلَيَّ هَـٰذَا الْقُرْآنُ لِأُنذِرَكُم بِهِ وَمَن بَلَغَ ۚ أَئِنَّكُمْ لَتَشْهَدُونَ أَنَّ مَعَ اللَّـهِ آلِهَةً أُخْرَىٰ ۚ قُل لَّا أَشْهَدُ ۚ قُلْ إِنَّمَا هُوَ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ وَإِنَّنِي بَرِيءٌ مِّمَّا تُشْرِكُونَ ﴿١٩﴾

19. Sema: Kitu gani ushahidi wake ndio mkubwa zaidi? Sema: Allaah. Yeye Ni Shahidi baina yangu na baina yenu. Na nimefunuliwa Wahy hii Qur-aan ili nikuonyeni kwayo na kila itakayemfikia. Je, hivi kweli nyinyi mnashuhudia kwamba wako waabudiwa wengine pamoja na Allaah? Sema: Mimi sishuhudii (hayo). Sema: Hakika Yeye Ni Mwabudiwa wa haki Mmoja (Pekee), na hakika mimi sihusiki na mnavyomshirikisha navyo.

 

 

 

 

الَّذِينَ آتَيْنَاهُمُ الْكِتَابَ يَعْرِفُونَهُ كَمَا يَعْرِفُونَ أَبْنَاءَهُمُ ۘ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنفُسَهُمْ فَهُمْ لَا يُؤْمِنُونَ ﴿٢٠﴾

20. Wale Tuliowapa Kitabu wanamjua (Nabiy Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم)  au wanaijua Tawhiyd) kama wanavyowajua watoto wao. Wale ambao wamekhasiri nafsi zao basi wao hawaamini.

 

 

 

 

وَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّنِ افْتَرَىٰ عَلَى اللَّـهِ كَذِبًا أَوْ كَذَّبَ بِآيَاتِهِ ۗ إِنَّهُ لَا يُفْلِحُ الظَّالِمُونَ ﴿٢١﴾

21. Na nani mdhalimu zaidi kuliko yule anayemtungia Allaah uongo au anayekadhibisha Aayaat (na Ishara, Dalili bayana) Zake? Hakika madhalimu hawatofaulu.

 

 

 

 

وَيَوْمَ نَحْشُرُهُمْ جَمِيعًا ثُمَّ نَقُولُ لِلَّذِينَ أَشْرَكُوا أَيْنَ شُرَكَاؤُكُمُ الَّذِينَ كُنتُمْ تَزْعُمُونَ ﴿٢٢﴾

22. Na Siku Tutakayowakusanya wote pamoja, kisha Tutawaambia wale walioshirikisha: Wako wapi washirika wenu ambao mlikuwa mnadai (kuwa waungu wawaombeeni)?

 

 

 

ثُمَّ لَمْ تَكُن فِتْنَتُهُمْ إِلَّا أَن قَالُوا وَاللَّـهِ رَبِّنَا مَا كُنَّا مُشْرِكِينَ ﴿٢٣﴾

23. Kisha haitokuwa hoja yao ya kujitetea isipokuwa kusema: Wa-Allaahi Rabb wetu! Hatukuwa washirikina.

 

 

 

انظُرْ كَيْفَ كَذَبُوا عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ ۚ وَضَلَّ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَفْتَرُونَ ﴿٢٤﴾

24. Tazama vipi walivyojiongopea wenyewe na yamewapotea yale waliyokuwa wakiyatunga (ya uongo).

 

 

 

وَمِنْهُم مَّن يَسْتَمِعُ إِلَيْكَ ۖ وَجَعَلْنَا عَلَىٰ قُلُوبِهِمْ أَكِنَّةً أَن يَفْقَهُوهُ وَفِي آذَانِهِمْ وَقْرًا ۚ وَإِن يَرَوْا كُلَّ آيَةٍ لَّا يُؤْمِنُوا بِهَا ۚ حَتَّىٰ إِذَا جَاءُوكَ يُجَادِلُونَكَ يَقُولُ الَّذِينَ كَفَرُوا إِنْ هَـٰذَا إِلَّا أَسَاطِيرُ الْأَوَّلِينَ ﴿٢٥﴾

25. Na wako miongoni mwao wanaotega sikio kukusikiliza. Nasi Tumeweka vifuniko kwenye nyoyo zao wasipate kuyafahamu na katika masikio yao uziwi.[4] Na wanapoona Aayah (Ishara, Ushahidi, Dalili) yoyote (ya kuthibitisha ukweli wako) hawaiamini. Hata wanapokujia kukubishia husema wale waliokufuru: Hizi si chochote ila ni hekaya za watu wa kale.

 

 

 

 

وَهُمْ يَنْهَوْنَ عَنْهُ وَيَنْأَوْنَ عَنْهُ ۖ وَإِن يُهْلِكُونَ إِلَّا أَنفُسَهُمْ وَمَا يَشْعُرُونَ ﴿٢٦﴾

26. Wao wanazuia asifuatwe, na wenyewe wanajiweka mbali naye. Lakini hawaangamizi isipokuwa nafsi zao wala hawahisi. 

 

 

 

 

وَلَوْ تَرَىٰ إِذْ وُقِفُوا عَلَى النَّارِ فَقَالُوا يَا لَيْتَنَا نُرَدُّ وَلَا نُكَذِّبَ بِآيَاتِ رَبِّنَا وَنَكُونَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ ﴿٢٧﴾

27. Na lau ungeliona watakaposimamishwa kwenye moto kisha wakasema: Laiti tungelirudishwa (duniani) na wala hatutakadhibisha Aayaat (na Ishara) za Rabb wetu, na tutakuwa miongoni mwa waumini!

 

 

 

 

بَلْ بَدَا لَهُم مَّا كَانُوا يُخْفُونَ مِن قَبْلُ ۖ وَلَوْ رُدُّوا لَعَادُوا لِمَا نُهُوا عَنْهُ وَإِنَّهُمْ لَكَاذِبُونَ ﴿٢٨﴾

28. Bali yamewadhihirikia yale waliyokuwa wakiyaficha kabla. Na lau wangelirudishwa, kwa yakini wangeyarudia yale waliyokatazwa, na hakika wao ni waongo!

 

 

 

وَقَالُوا إِنْ هِيَ إِلَّا حَيَاتُنَا الدُّنْيَا وَمَا نَحْنُ بِمَبْعُوثِينَ ﴿٢٩﴾

29. Na walisema: Haya si chochote isipokuwa ni uhai wetu wa dunia tu, na wala sisi hatutofufuliwa.[5]

 

 

 

وَلَوْ تَرَىٰ إِذْ وُقِفُوا عَلَىٰ رَبِّهِمْ ۚ قَالَ أَلَيْسَ هَـٰذَا بِالْحَقِّ ۚ قَالُوا بَلَىٰ وَرَبِّنَا ۚ قَالَ فَذُوقُوا الْعَذَابَ بِمَا كُنتُمْ تَكْفُرُونَ ﴿٣٠﴾

30. Na lau ungeliona watakaposimamishwa mbele ya Rabb wao. Atasema: Je, haya si ya kweli? Watasema: Ndio (kweli kabisa), tunaapa kwa Rabb wetu! Atasema: Basi onjeni adhabu kwa sababu ya yale mliyokuwa mkikufuru.

 

 

 

 

قَدْ خَسِرَ الَّذِينَ كَذَّبُوا بِلِقَاءِ اللَّـهِ ۖ حَتَّىٰ إِذَا جَاءَتْهُمُ السَّاعَةُ بَغْتَةً قَالُوا يَا حَسْرَتَنَا عَلَىٰ مَا فَرَّطْنَا فِيهَا وَهُمْ يَحْمِلُونَ أَوْزَارَهُمْ عَلَىٰ ظُهُورِهِمْ ۚ أَلَا سَاءَ مَا يَزِرُونَ ﴿٣١﴾

31. Kwa yakini wamekhasirika wale waliokadhibisha kukutana na Allaah. Hata itakapowajia Saa (mauti) kwa ghafla watasema: Ee majuto yetu kwa yale tuliyokusuru humo! Na ilhali wao wanabeba mizigo yao (ya dhambi) migongoni mwao. Tanabahi! Uovu ulioje wanayobeba!

 

 

 

 

وَمَا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا إِلَّا لَعِبٌ وَلَهْوٌ ۖ وَلَلدَّارُ الْآخِرَةُ خَيْرٌ لِّلَّذِينَ يَتَّقُونَ ۗ أَفَلَا تَعْقِلُونَ ﴿٣٢﴾

32. Na uhai wa dunia si chochote isipokuwa ni mchezo na pumbao. Na bila shaka nyumba ya Aakhirah ni bora zaidi kwa wenye taqwa. Je, basi hamtii akilini?

 

 

 

 

قَدْ نَعْلَمُ إِنَّهُ لَيَحْزُنُكَ الَّذِي يَقُولُونَ ۖ فَإِنَّهُمْ لَا يُكَذِّبُونَكَ وَلَـٰكِنَّ الظَّالِمِينَ بِآيَاتِ اللَّـهِ يَجْحَدُونَ ﴿٣٣﴾

33. Kwa yakini Tunajua (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kwamba yanakuhuzunisha yale wanayoyasema. Basi hakika wao hawakukadhibishi wewe (kwa vile wanakujua ni mkweli) lakini wanachokanusha madhalimu ni Aayaat (na Ishara) za Allaah.

 

 

 

 

وَلَقَدْ كُذِّبَتْ رُسُلٌ مِّن قَبْلِكَ فَصَبَرُوا عَلَىٰ مَا كُذِّبُوا وَأُوذُوا حَتَّىٰ أَتَاهُمْ نَصْرُنَا ۚ وَلَا مُبَدِّلَ لِكَلِمَاتِ اللَّـهِ ۚ وَلَقَدْ جَاءَكَ مِن نَّبَإِ الْمُرْسَلِينَ ﴿٣٤﴾

34. Na kwa yakini walikadhibishwa Rusuli kabla yako, na wao walivuta subira kwa kukadhibishwa huko, na waliudhiwa na kusumbuliwa mpaka ilipowafikia Nusura Yetu. Na hakuna yeyote awezaye kubadilisha Maneno ya Allaah. Zimekwishakujia khabari za Rusuli (waliopita kukuliwaza).

 

 

 

 

وَإِن كَانَ كَبُرَ عَلَيْكَ إِعْرَاضُهُمْ فَإِنِ اسْتَطَعْتَ أَن تَبْتَغِيَ نَفَقًا فِي الْأَرْضِ أَوْ سُلَّمًا فِي السَّمَاءِ فَتَأْتِيَهُم بِآيَةٍ ۚ وَلَوْ شَاءَ اللَّـهُ لَجَمَعَهُمْ عَلَى الْهُدَىٰ ۚ فَلَا تَكُونَنَّ مِنَ الْجَاهِلِينَ ﴿٣٥﴾

35. Na kama kukengeuka kwao kumekuwa ni mashaka mno kwako, basi ukiweza kutafuta njia ya chini kwa chini katika ardhi au ngazi kwendea mbinguni ili uwaletee Aayah (Ishara, Dalili) yoyote (basi fanya). Na kama Allaah Angetaka Angeliwakusanya katika hidaaya. Basi chunga usiwe miongoni mwa majahili.

 

 

 

إِنَّمَا يَسْتَجِيبُ الَّذِينَ يَسْمَعُونَ ۘ وَالْمَوْتَىٰ يَبْعَثُهُمُ اللَّـهُ ثُمَّ إِلَيْهِ يُرْجَعُونَ ﴿٣٦﴾

36. Hakika wanaitikia wale wanaosikia (kwa nyoyo za imaan). Ama wafu (wa nyoyo) Allaah Atawafufua, kisha Kwake watarejeshwa.

 

 

 

 

وَقَالُوا لَوْلَا نُزِّلَ عَلَيْهِ آيَةٌ مِّن رَّبِّهِ ۚ قُلْ إِنَّ اللَّـهَ قَادِرٌ عَلَىٰ أَن يُنَزِّلَ آيَةً وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٣٧﴾

37. Na walisema: Kwa nini hakuteremshiwa Aayah (Muujiza) kutoka kwa Rabb wake? Sema: Hakika Allaah Ni Muweza wa Kuteremsha Aayah (Muujiza) lakini wengi wao hawajui. 

 

 

 

 

وَمَا مِن دَابَّةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا طَائِرٍ يَطِيرُ بِجَنَاحَيْهِ إِلَّا أُمَمٌ أَمْثَالُكُم ۚ مَّا فَرَّطْنَا فِي الْكِتَابِ مِن شَيْءٍ ۚ ثُمَّ إِلَىٰ رَبِّهِمْ يُحْشَرُونَ ﴿٣٨﴾

38. Na hakuna kiumbe chochote kinachotembea katika ardhi wala ndege anayeruka kwa mbawa zake mbili, isipokuwa ni nyumati mfano wenu. Hatujaacha wala kusahau chochote katika Kitabu[6]. Kisha watakusanywa kwa Rabb wao.

 

 

 

 

وَالَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا صُمٌّ وَبُكْمٌ فِي الظُّلُمَاتِ ۗ مَن يَشَإِ اللَّـهُ يُضْلِلْـهُ وَمَن يَشَأْ يَجْعَلْهُ عَلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ ﴿٣٩﴾

39. Na wale waliokadhibisha Aayaat (na Ishara, Dalili) Zetu ni viziwi na mabubu waliozama ndani ya viza. Allaah Humpotoa Amtakaye na Humweka Amtakaye juu ya njia iliyonyooka. 

 

 

 

 

قُلْ أَرَأَيْتَكُمْ إِنْ أَتَاكُمْ عَذَابُ اللَّـهِ أَوْ أَتَتْكُمُ السَّاعَةُ أَغَيْرَ اللَّـهِ تَدْعُونَ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿٤٠﴾

40. Sema: Je, mnaonaje ikikufikieni adhabu ya Allaah au ikakufikieni Saa (Qiyaamah), je, mtamwomba ghairi ya Allaah? (Jibuni) mkiwa ni wakweli!

 

 

 

 

بَلْ إِيَّاهُ تَدْعُونَ فَيَكْشِفُ مَا تَدْعُونَ إِلَيْهِ إِن شَاءَ وَتَنسَوْنَ مَا تُشْرِكُونَ ﴿٤١﴾

41. Bali Yeye Pekee Ndiye mtayemwomba, kisha Akitaka Ataondoa yale (ya dhiki) mliyomwomba na mtasahau mnayoyashirikisha (pamoja Naye).

 

 

 

 

وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا إِلَىٰ أُمَمٍ مِّن قَبْلِكَ فَأَخَذْنَاهُم بِالْبَأْسَاءِ وَالضَّرَّاءِ لَعَلَّهُمْ يَتَضَرَّعُونَ ﴿٤٢﴾

42. Na kwa yakini Tulipeleka (Rusuli) kwa nyumati nyingi kabla yako, Tukawatia katika dhiki za ufukara na madhara ya magonjwa na misiba ili wapate kunyenyekea.

 

 

 

 فَلَوْلَا إِذْ جَاءَهُم بَأْسُنَا تَضَرَّعُوا وَلَـٰكِن قَسَتْ قُلُوبُهُمْ وَزَيَّنَ لَهُمُ الشَّيْطَانُ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٤٣﴾

43. Basi kwa nini ilipowafikia adhabu Yetu wasinyenyekee? Lakini nyoyo zao zimekuwa ngumu na shaytwaan akawapambia yale waliyokuwa wakiyatenda.

 

 

 

فَلَمَّا نَسُوا مَا ذُكِّرُوا بِهِ فَتَحْنَا عَلَيْهِمْ أَبْوَابَ كُلِّ شَيْءٍ حَتَّىٰ إِذَا فَرِحُوا بِمَا أُوتُوا أَخَذْنَاهُم بَغْتَةً فَإِذَا هُم مُّبْلِسُونَ ﴿٤٤﴾

44. Waliposahau yale waliyokumbushwa, Tuliwafungulia milango ya (neema za) kila kitu, mpaka walipofurahia kwa yale waliyopewa, Tukawachukua ghafla (kuwaadhibu), basi tahamaki wakawa wenye kukata tamaa.

 

 

 

 

فَقُطِعَ دَابِرُ الْقَوْمِ الَّذِينَ ظَلَمُوا ۚ وَالْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٤٥﴾

45. Basi ikakatwa mizizi ya watu waliodhulumu, na AlhamduliLLaah (Himdi Anastahiki Allaah) Rabb wa walimwengu.

 

 

 

قُلْ أَرَأَيْتُمْ إِنْ أَخَذَ اللَّـهُ سَمْعَكُمْ وَأَبْصَارَكُمْ وَخَتَمَ عَلَىٰ قُلُوبِكُم مَّنْ إِلَـٰهٌ غَيْرُ اللَّـهِ يَأْتِيكُم بِهِ ۗ انظُرْ كَيْفَ نُصَرِّفُ الْآيَاتِ ثُمَّ هُمْ يَصْدِفُونَ ﴿٤٦﴾

46. Sema: Mnaonaje ikiwa Allaah Atakuondoleeni kusikia kwenu (mkawa viziwi) na kuona kwenu (mkawa vipofu) na Akapiga mhuri juu ya nyoyo zenu (mkawa hamufahamu), je, ni mwabudiwa wa haki yupi ghairi ya Allaah Atakuleteeni hayo? Tazama jinsi Tunavyosarifu Aayaat (Hoja, Dalili) namna kwa namna kisha wao wanakengeuka.

 

 

 

قُلْ أَرَأَيْتَكُمْ إِنْ أَتَاكُمْ عَذَابُ اللَّـهِ بَغْتَةً أَوْ جَهْرَةً هَلْ يُهْلَكُ إِلَّا الْقَوْمُ الظَّالِمُونَ ﴿٤٧﴾

47. Sema: Mnaonaje ikikufikieni Adhabu ya Allaah ghafla au kwa kuiona inavyokujieni? Je, wataangamizwa isipokuwa watu madhalimu?  

 

 

 

 

وَمَا نُرْسِلُ الْمُرْسَلِينَ إِلَّا مُبَشِّرِينَ وَمُنذِرِينَ ۖ فَمَنْ آمَنَ وَأَصْلَحَ فَلَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ ﴿٤٨﴾

48. Na Hatupeleki Rusuli isipokuwa kuwa wabashiriaji na waonyaji tu. Na yeyote atakayeamini na akatengeneza (imaan yake na vitendo vyake), basi haitokuwa khofu juu yao na wala wao hawatohuzunika.

 

 

 

وَالَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا يَمَسُّهُمُ الْعَذَابُ بِمَا كَانُوا يَفْسُقُونَ ﴿٤٩﴾

49. Na wale waliokadhibisha Aayaat (na Miujiza, Ishara) Zetu, itawagusa adhabu kwa sababu ya ufasiki waliokuwa wanaufanya.

 

 

 

قُل لَّا أَقُولُ لَكُمْ عِندِي خَزَائِنُ اللَّـهِ وَلَا أَعْلَمُ الْغَيْبَ وَلَا أَقُولُ لَكُمْ إِنِّي مَلَكٌ ۖ إِنْ أَتَّبِعُ إِلَّا مَا يُوحَىٰ إِلَيَّ ۚ قُلْ هَلْ يَسْتَوِي الْأَعْمَىٰ وَالْبَصِيرُ ۚ أَفَلَا تَتَفَكَّرُونَ ﴿٥٠﴾

50. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Sikuambieni kuwa mimi nina hazina ya Allaah, na wala kwamba najua ya ghaibu, na wala sikuambieni kuwa mimi ni Malaika. Sifuati ila yale niliyofunuliwa Wahy. Sema: Je, analingana sawasawa kipofu na mwenye kuona? Basi hamtafakari?

 

 

 

 

وَأَنذِرْ بِهِ الَّذِينَ يَخَافُونَ أَن يُحْشَرُوا إِلَىٰ رَبِّهِمْ ۙ لَيْسَ لَهُم مِّن دُونِهِ وَلِيٌّ وَلَا شَفِيعٌ لَّعَلَّهُمْ يَتَّقُونَ ﴿٥١﴾

51. Na waonye kwayo (Qur-aan) wale wanaokhofu ya kwamba watakusanywa kwa Rabb wao, na hali ya kuwa hawana rafiki mlinzi wala mwombezi isipokuwa Yeye ili wapate kumcha Allaah (zaidi).

 

 

 

وَلَا تَطْرُدِ الَّذِينَ يَدْعُونَ رَبَّهُم بِالْغَدَاةِ وَالْعَشِيِّ يُرِيدُونَ وَجْهَهُ ۖ مَا عَلَيْكَ مِنْ حِسَابِهِم مِّن شَيْءٍ وَمَا مِنْ حِسَابِكَ عَلَيْهِم مِّن شَيْءٍ فَتَطْرُدَهُمْ فَتَكُونَ مِنَ الظَّالِمِينَ ﴿٥٢﴾

52. Na wala usiwafukuze wale wanaomwomba Rabb wao asubuhi na jioni wanataka Wajihi Wake. Si juu yako hisabu yao hata kidogo, na wala hisabu yako si juu yao hata kidogo, hata uwafukuze ukaja kuwa miongoni mwa madhalimu. 

 

 

 

وَكَذَٰلِكَ فَتَنَّا بَعْضَهُم بِبَعْضٍ لِّيَقُولُوا أَهَـٰؤُلَاءِ مَنَّ اللَّـهُ عَلَيْهِم مِّن بَيْنِنَا ۗ أَلَيْسَ اللَّـهُ بِأَعْلَمَ بِالشَّاكِرِينَ ﴿٥٣﴾

53. Na hivyo ndivyo Tulivyowafanyia mtihani baadhi yao kwa baadhi ili waseme: Je, hawa ndio wale Aliowafadhilisha Allaah baina yetu? Je, kwani Allaah Hajui wanaoshukuru?

 

 

 

وَإِذَا جَاءَكَ الَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِآيَاتِنَا فَقُلْ سَلَامٌ عَلَيْكُمْ ۖ كَتَبَ رَبُّكُمْ عَلَىٰ نَفْسِهِ الرَّحْمَةَ ۖ أَنَّهُ مَنْ عَمِلَ مِنكُمْ سُوءًا بِجَهَالَةٍ ثُمَّ تَابَ مِن بَعْدِهِ وَأَصْلَحَ فَأَنَّهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٥٤﴾

54. Na wanapokujia wale wanaoamini Aayaat (na Ishara) Zetu basi sema: Salaamun ‘alaykum! (Amani iwe juu yenu). Rabb wenu Amejiwajibishia Nafsi Yake[7] Rahmah; kwamba yeyote miongoni mwenu atakayetenda ovu kwa ujahili, kisha akatubia baada yake na akarekebisha (matendo yake), basi hakika Yeye Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu.

 

 

 

وَكَذَٰلِكَ نُفَصِّلُ الْآيَاتِ وَلِتَسْتَبِينَ سَبِيلُ الْمُجْرِمِينَ ﴿٥٥﴾

55. Na hivyo ndivyo Tunavyofasili waziwazi Aayaat (na Ishara) na ili idhihirike njia ya wahalifu.

 

 

 

قُلْ إِنِّي نُهِيتُ أَنْ أَعْبُدَ الَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ ۚ قُل لَّا أَتَّبِعُ أَهْوَاءَكُمْ ۙ قَدْ ضَلَلْتُ إِذًا وَمَا أَنَا مِنَ الْمُهْتَدِينَ ﴿٥٦﴾

56. Sema: Hakika mimi nimekatazwa kuabudu wale mnaowaomba badala ya Allaah. Sema: Sifuati hawaa zenu (kwani nikifuata,) kwa yakini nitakuwa nimepotoka, na hapo nami sitokuwa miongoni mwa waliohidika.

 

 

 

قُلْ إِنِّي عَلَىٰ بَيِّنَةٍ مِّن رَّبِّي وَكَذَّبْتُم بِهِ ۚ مَا عِندِي مَا تَسْتَعْجِلُونَ بِهِ ۚ إِنِ الْحُكْمُ إِلَّا لِلَّـهِ ۖ يَقُصُّ الْحَقَّ ۖ وَهُوَ خَيْرُ الْفَاصِلِينَ ﴿٥٧﴾

57. Sema: Hakika mimi niko juu ya hoja bayana kutoka kwa Rabb wangu nanyi mumeikadhibisha. Sina yale mnayoyahimiza. Hakuna hukumu isipokuwa ya Allaah Pekee. Anasimulia ya haki, Naye Ni Mbora wa Kuhukumu kuliko wote wenye kuhukumu.

 

 

 

قُل لَّوْ أَنَّ عِندِي مَا تَسْتَعْجِلُونَ بِهِ لَقُضِيَ الْأَمْرُ بَيْنِي وَبَيْنَكُمْ ۗ وَاللَّـهُ أَعْلَمُ بِالظَّالِمِينَ ﴿٥٨﴾

58. Sema: Lau ningelikuwa ninayo yale mnayoyaharakiza, basi bila shaka lingehukumiwa jambo baina yangu na baina yenu. Na Allaah Anawajua zaidi madhalimu.

 

 

 

وَعِندَهُ مَفَاتِحُ الْغَيْبِ لَا يَعْلَمُهَا إِلَّا هُوَ ۚ وَيَعْلَمُ مَا فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ ۚ وَمَا تَسْقُطُ مِن وَرَقَةٍ إِلَّا يَعْلَمُهَا وَلَا حَبَّةٍ فِي ظُلُمَاتِ الْأَرْضِ وَلَا رَطْبٍ وَلَا يَابِسٍ إِلَّا فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ ﴿٥٩﴾

59. Na Kwake (Allaah) zipo funguo za ghaibu, hakuna azijuaye ila Yeye tu.[8] Na Anajua yale yote yaliyomo barani na baharini. Na halianguki jani lolote ila Hulijua, wala punje katika viza vya ardhi, wala kinyevu na kikavu isipokuwa kimo katika Kitabu kinachobainisha wazi.[9]

 

 

 

وَهُوَ الَّذِي يَتَوَفَّاكُم بِاللَّيْلِ وَيَعْلَمُ مَا جَرَحْتُم بِالنَّهَارِ ثُمَّ يَبْعَثُكُمْ فِيهِ لِيُقْضَىٰ أَجَلٌ مُّسَمًّى ۖ ثُمَّ إِلَيْهِ مَرْجِعُكُمْ ثُمَّ يُنَبِّئُكُم بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿٦٠﴾

60. Naye Ndiye Anayekufisheni usiku (mnapolala)[10] na Anajua yale yote mnayoyafanya mchana, kisha Anakufufueni humo ili utimizwe muda maalumu uliokadariwa. Kisha Kwake Pekee ni marejeo yenu, kisha Atakujulisheni yale mliyokuwa mkiyatenda.

 

 

 

وَهُوَ الْقَاهِرُ فَوْقَ عِبَادِهِ ۖ وَيُرْسِلُ عَلَيْكُمْ حَفَظَةً حَتَّىٰ إِذَا جَاءَ أَحَدَكُمُ الْمَوْتُ تَوَفَّتْهُ رُسُلُنَا وَهُمْ لَا يُفَرِّطُونَ ﴿٦١﴾

61. Naye Ndiye Aliyedhibiti vyote chini ya Mamlaka Yake, Aliye juu ya Waja Wake. Na Anakutumieni Malaika wachungaji wadhibiti, hata yanapomfikia mmoja wenu mauti, Wajumbe Wetu humfisha, nao hawafanyi taksiri.

 

    

 

ثُمَّ رُدُّوا إِلَى اللَّـهِ مَوْلَاهُمُ الْحَقِّ ۚ أَلَا لَهُ الْحُكْمُ وَهُوَ أَسْرَعُ الْحَاسِبِينَ ﴿٦٢﴾

62. Kisha watarudishwa (wote waliofishwa) kwa Allaah Rabb wao wa haki. Tanabahi! Hukumu ni Yake Pekee! Naye Ni Mwepesi zaidi wa Kuhisabu kuliko wote wanaohisabu.

 

 

 

قُلْ مَن يُنَجِّيكُم مِّن ظُلُمَاتِ الْبَرِّ وَالْبَحْرِ تَدْعُونَهُ تَضَرُّعًا وَخُفْيَةً لَّئِنْ أَنجَانَا مِنْ هَـٰذِهِ لَنَكُونَنَّ مِنَ الشَّاكِرِينَ ﴿٦٣﴾

63. Sema: Nani Anakuokoeni katika viza vya bara na bahari mnapomuomba kwa kunyenyekea na kwa siri (mkisema): Akituokoa kutokana na (janga) hili, bila shaka tutakuwa miongoni mwa wenye kushukuru.

 

 

 

قُلِ اللَّـهُ يُنَجِّيكُم مِّنْهَا وَمِن كُلِّ كَرْبٍ ثُمَّ أَنتُمْ تُشْرِكُونَ ﴿٦٤﴾

64. Sema: Allaah Anakuokoeni kutokana na hayo na katika kila janga kisha nyinyi mnamshirikisha.

 

 

 

قُلْ هُوَ الْقَادِرُ عَلَىٰ أَن يَبْعَثَ عَلَيْكُمْ عَذَابًا مِّن فَوْقِكُمْ أَوْ مِن تَحْتِ أَرْجُلِكُمْ أَوْ يَلْبِسَكُمْ شِيَعًا وَيُذِيقَ بَعْضَكُم بَأْسَ بَعْضٍ ۗ انظُرْ كَيْفَ نُصَرِّفُ الْآيَاتِ لَعَلَّهُمْ يَفْقَهُونَ ﴿٦٥﴾

65. Sema: Yeye ni Muweza wa kukuleteeni adhabu kutoka juu yenu, au kutoka chini ya miguu yenu, au Akutatanisheni mfarikiane kuwa makundi na Akuonjesheni baadhi yenu (vurugu la) nguvu za wengineo. Tazama jinsi Tunavyosarifu Aayaat (Ishara, Hoja, Dalili) namna kwa namna wapate kufahamu.

 

 

 

وَكَذَّبَ بِهِ قَوْمُكَ وَهُوَ الْحَقُّ ۚ قُل لَّسْتُ عَلَيْكُم بِوَكِيلٍ ﴿٦٦﴾

66. Na watu wako wameikadhibisha (Qur-aan) nayo ni haki. Sema: Mimi si mdhamini wenu.

 

 

 

 

لِّكُلِّ نَبَإٍ مُّسْتَقَرٌّ ۚ وَسَوْفَ تَعْلَمُونَ ﴿٦٧﴾

67. Kila khabari ina wakati maalumu, na mtakuja kujua.

 

 

 

 

وَإِذَا رَأَيْتَ الَّذِينَ يَخُوضُونَ فِي آيَاتِنَا فَأَعْرِضْ عَنْهُمْ حَتَّىٰ يَخُوضُوا فِي حَدِيثٍ غَيْرِهِ ۚ وَإِمَّا يُنسِيَنَّكَ الشَّيْطَانُ فَلَا تَقْعُدْ بَعْدَ الذِّكْرَىٰ مَعَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ ﴿٦٨﴾

68. Na unapowaona wale wanaoshughulika kuzisakama Aayaat Zetu, jitenge nao mpaka watumbukie kwenye mazungumzo mengineyo. Na kama shaytwaan akikusahaulisha, basi baada ya kukumbuka, usikae pamoja na watu madhalimu.

 

 

 

وَمَا عَلَى الَّذِينَ يَتَّقُونَ مِنْ حِسَابِهِم مِّن شَيْءٍ وَلَـٰكِن ذِكْرَىٰ لَعَلَّهُمْ يَتَّقُونَ ﴿٦٩﴾

69. Wenye taqwa, hawana jukumu la hisabu yao (kwa Allaah), lakini jukumu ni kuwakumbusha ili wapate kujirudi. 

 

 

 

 

وَذَرِ الَّذِينَ اتَّخَذُوا دِينَهُمْ لَعِبًا وَلَهْوًا وَغَرَّتْهُمُ الْحَيَاةُ الدُّنْيَا ۚ وَذَكِّرْ بِهِ أَن تُبْسَلَ نَفْسٌ بِمَا كَسَبَتْ لَيْسَ لَهَا مِن دُونِ اللَّـهِ وَلِيٌّ وَلَا شَفِيعٌ وَإِن تَعْدِلْ كُلَّ عَدْلٍ لَّا يُؤْخَذْ مِنْهَا ۗ أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ أُبْسِلُوا بِمَا كَسَبُوا ۖ لَهُمْ شَرَابٌ مِّنْ حَمِيمٍ وَعَذَابٌ أَلِيمٌ بِمَا كَانُوا يَكْفُرُونَ ﴿٧٠﴾

70. Na waachilie mbali wale walioifanya Dini yao mchezo na pumbao, na ukawaghuri uhai wa dunia. Basi wakumbushe kwayo (Qur-aan) isije kila nafsi ikaangamizwa kwa yale iliyoyachuma. Haina pasi na Allaah rafiki mlinzi wala mwombezi. Na hata ikitoa fidia ya kila aina haitopokelewa. Hao ndio wale walioangamizwa kwa sababu ya yale waliyoyachuma. Watapata kinywaji cha maji ya kutokota na adhabu iumizayo kwa sababu ya ukafiri wao.

 

 

 

قُلْ أَنَدْعُو مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَنفَعُنَا وَلَا يَضُرُّنَا وَنُرَدُّ عَلَىٰ أَعْقَابِنَا بَعْدَ إِذْ هَدَانَا اللَّـهُ كَالَّذِي اسْتَهْوَتْهُ الشَّيَاطِينُ فِي الْأَرْضِ حَيْرَانَ لَهُ أَصْحَابٌ يَدْعُونَهُ إِلَى الْهُدَى ائْتِنَا ۗ قُلْ إِنَّ هُدَى اللَّـهِ هُوَ الْهُدَىٰ ۖ وَأُمِرْنَا لِنُسْلِمَ لِرَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٧١﴾

71. Sema: Je, badala ya Allaah tuviombe visivyoweza kutunufaisha wala kutudhuru tuje kurudishwa nyuma tulikotoka baada ya Allaah kutuhidi? Tuwe kama yule ambaye ameshawishiwa na mashaytwaan akikanganyika katika ardhi, anao marafiki wanamwita katika mwongozo: Njoo kwetu! Sema: Hakika Hidaya ya Allaah ndio Hidaya na tumeamrishwa tujisalimishe kwa Rabb wa walimwengu.

 

 

 

وَأَنْ أَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَاتَّقُوهُ ۚ وَهُوَ الَّذِي إِلَيْهِ تُحْشَرُونَ ﴿٧٢﴾

72. Na kuwa simamisheni Swalaah na mcheni Yeye, Naye Ndiye Ambaye Kwake mtakusanywa.

 

 

 

وَهُوَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ بِالْحَقِّ ۖ وَيَوْمَ يَقُولُ كُن فَيَكُونُ ۚ قَوْلُهُ الْحَقُّ ۚ وَلَهُ الْمُلْكُ يَوْمَ يُنفَخُ فِي الصُّورِ ۚ عَالِمُ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ ۚ وَهُوَ الْحَكِيمُ الْخَبِيرُ ﴿٧٣﴾

73. Naye Ndiye Ambaye Ameumba mbingu na ardhi kwa haki. Na Siku Atakaposema: Kun! Basi (jambo) huwa! Kauli Yake ni haki. Ni Wake Yeye tu ufalme Siku litakapopulizwa baragumu. Mjuzi wa ghaibu na dhahiri. Naye Ni Mwenye Hikmah wa yote, Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri.

 

 

 

وَإِذْ قَالَ إِبْرَاهِيمُ لِأَبِيهِ آزَرَ أَتَتَّخِذُ أَصْنَامًا آلِهَةً ۖ إِنِّي أَرَاكَ وَقَوْمَكَ فِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ ﴿٧٤﴾

74. Na pindi Ibraahiym alipomwambia baba yake Aazar: Je, unafanya masanamu kuwa ni waabudiwa? Hakika mimi nakuona wewe pamoja na watu wako katika upotofu bayana.

 

 

 

وَكَذَٰلِكَ نُرِي إِبْرَاهِيمَ مَلَكُوتَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَلِيَكُونَ مِنَ الْمُوقِنِينَ ﴿٧٥﴾

75. Na hivyo ndivyo Tunavyomwonyesha Ibraahiym ufalme mkubwa wa mbingu na ardhi na ili awe miongoni mwa wenye yakini.

 

 

 

فَلَمَّا جَنَّ عَلَيْهِ اللَّيْلُ رَأَىٰ كَوْكَبًا ۖ قَالَ هَـٰذَا رَبِّي ۖ فَلَمَّا أَفَلَ قَالَ لَا أُحِبُّ الْآفِلِينَ ﴿٧٦﴾

76. Na ulipomwingilia usiku akaona nyota. Akasema: Huyu ni Rabb wangu. Ilipotoweka akasema: Hakika mimi sipendi wanaotoweka. 

 

 

 

فَلَمَّا رَأَى الْقَمَرَ بَازِغًا قَالَ هَـٰذَا رَبِّي ۖ فَلَمَّا أَفَلَ قَالَ لَئِن لَّمْ يَهْدِنِي رَبِّي لَأَكُونَنَّ مِنَ الْقَوْمِ الضَّالِّينَ ﴿٧٧﴾

77. Kisha alipoona mwezi umechomoza akasema: Huyu ni Rabb wangu. Ulipotoweka akasema: Asiponiongoza Rabb wangu bila shaka nitakuwa miongoni mwa watu waliopotea.

 

 

 

فَلَمَّا رَأَى الشَّمْسَ بَازِغَةً قَالَ هَـٰذَا رَبِّي هَـٰذَا أَكْبَرُ ۖ فَلَمَّا أَفَلَتْ قَالَ يَا قَوْمِ إِنِّي بَرِيءٌ مِّمَّا تُشْرِكُونَ ﴿٧٨﴾

78. Kisha alipoliona jua limechomoza akasema: Huyu ni Rabb wangu, huyu ni mkubwa zaidi. Lilipotoweka akasema: Enyi watu wangu! Hakika mimi simo katika yale mnayoyashirikisha (na Allaah).

 

 

 

إِنِّي وَجَّهْتُ وَجْهِيَ لِلَّذِي فَطَرَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ حَنِيفًا ۖ وَمَا أَنَا مِنَ الْمُشْرِكِينَ ﴿٧٩﴾

79. Hakika mimi nimeelekeza uso wangu kwa Ambaye Ameanzisha mbingu na ardhi, nikijitenga na itikadi potofu na kuelemea haki, nami si katika washirikina.

 

 

 

وَحَاجَّهُ قَوْمُهُ ۚ قَالَ أَتُحَاجُّونِّي فِي اللَّـهِ وَقَدْ هَدَانِ ۚ وَلَا أَخَافُ مَا تُشْرِكُونَ بِهِ إِلَّا أَن يَشَاءَ رَبِّي شَيْئًا ۗ وَسِعَ رَبِّي كُلَّ شَيْءٍ عِلْمًا ۗ أَفَلَا تَتَذَكَّرُونَ ﴿٨٠﴾

80. Na watu wake wakamhoji. Akasema: Je, mnahojiana nami kuhusu Allaah na hali Amenihidi? Na wala sikhofu hayo mnayomshirikisha Naye (kwani sitodhurika) isipokuwa Rabb wangu Akitaka jambo. Rabb wangu Amezunguka kila kitu (kwa Ujuzi). Je, basi hamkumbuki?

 ☞ Ukurasa wa pili

 

Report Page