@furqanbot

@furqanbot


وَقَالَ الْمَلِكُ ائْتُونِي بِهِ ۖ فَلَمَّا جَاءَهُ الرَّسُولُ قَالَ ارْجِعْ إِلَىٰ رَبِّكَ فَاسْأَلْهُ مَا بَالُ النِّسْوَةِ اللَّاتِي قَطَّعْنَ أَيْدِيَهُنَّ ۚإِنَّ رَبِّي بِكَيْدِهِنَّ عَلِيمٌ﴿٥٠﴾

50. Mfalme akasema: “Nileteeni (Yuwsuf).” Basi (Yuwsuf) alipojiwa na mjumbe alisema: “Rejea kwa bwana wako umuulize nini mkasa wa wanawake waliojikata mikono yao. Hakika Rabb wangu kwa vitimbi vyao ni Mjuzi.”

 

 

 

قَالَ مَا خَطْبُكُنَّ إِذْ رَاوَدتُّنَّ يُوسُفَ عَن نَّفْسِهِ ۚ قُلْنَ حَاشَ لِلَّـهِ مَا عَلِمْنَا عَلَيْهِ مِن سُوءٍ ۚ قَالَتِ امْرَأَتُ الْعَزِيزِ الْآنَ حَصْحَصَ الْحَقُّ أَنَا رَاوَدتُّهُ عَن نَّفْسِهِ وَإِنَّهُ لَمِنَ الصَّادِقِينَ﴿٥١﴾

51. (Mfalme) Akasema: “Nini jambo lenu lilikuwa mlipomtongoza Yuwsuf kinyume na nafsi yake?” Wakasema: “Utakasifu ni wa Allaah! (Au Allaah Asijaalie)! Hatukujua uovu wowote kwake.” Mke wa ‘Aziyz akasema: “Hivi sasa umefichuka ukweli! Mimi nilimtongoza kinyume na nafsi yake. Na hakika yeye bila shaka ni miongoni mwa wakweli.”

 

 

 

ذَٰلِكَ لِيَعْلَمَ أَنِّي لَمْ أَخُنْهُ بِالْغَيْبِ وَأَنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي كَيْدَ الْخَائِنِينَ﴿٥٢﴾

52. (Yuwusuf akasema:) “Hivyo ili (‘Aziyz) apate kujua kwamba mimi sikumfanyia khiyana kwa siri; na kwamba Allaah Haongozi vitimbi vya makhaini.”

 

 

 

وَمَا أُبَرِّئُ نَفْسِي ۚ إِنَّ النَّفْسَ لَأَمَّارَةٌ بِالسُّوءِ إِلَّا مَا رَحِمَ رَبِّي ۚ إِنَّ رَبِّي غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٥٣﴾

53. “Na siitoi hatiani nafsi yangu. Hakika nafsi ni yenye kuamrisha sana maovu isipokuwa ambayo Rabb wangu Ameirehemu. Hakika Rabb wangu ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu.”

 

 

 

وَقَالَ الْمَلِكُ ائْتُونِي بِهِ أَسْتَخْلِصْهُ لِنَفْسِي ۖ فَلَمَّا كَلَّمَهُ قَالَ إِنَّكَ الْيَوْمَ لَدَيْنَا مَكِينٌ أَمِينٌ ﴿٥٤﴾

54. Na mfalme akasema: “Nileteeni (Yuwsuf) nimteue makhsusi kwangu.” Basi aliposema naye, akasema: “Hakika wewe leo kwetu umetamakani kwa cheo na umekuwa muaminiwa.”

 

 

 

قَالَ اجْعَلْنِي عَلَىٰ خَزَائِنِ الْأَرْضِ ۖإِنِّي حَفِيظٌ عَلِيمٌ ﴿٥٥﴾

55. (Yuwsuf) Akasema: “Niweke katika kusimamia hazina ya nchi; hakika mimi ni mhifadhi mjuzi.”

 

 

 

وَكَذَٰلِكَ مَكَّنَّا لِيُوسُفَ فِي الْأَرْضِ يَتَبَوَّأُ مِنْهَا حَيْثُ يَشَاءُ ۚ نُصِيبُ بِرَحْمَتِنَا مَن نَّشَاءُ ۖ وَلَا نُضِيعُ أَجْرَ الْمُحْسِنِينَ ﴿٥٦﴾

56. Na hivyo ndivyo Tulivyommakinisha Yuwsuf katika ardhi; anakaa humo popote atakapo. Tunamfikishia rahmah Yetu Tumtakaye, na wala Hatupotezi ujira wa watendao ihsaan.

 

 

 

وَلَأَجْرُ الْآخِرَةِ خَيْرٌ لِّلَّذِينَ آمَنُوا وَكَانُوا يَتَّقُونَ ﴿٥٧﴾

57. Na bila shaka ujira wa Aakhirah ni bora zaidi kwa wale walioamini na wakawa na taqwa.

 

 

 

وَجَاءَ إِخْوَةُ يُوسُفَ فَدَخَلُوا عَلَيْهِ فَعَرَفَهُمْ وَهُمْ لَهُ مُنكِرُونَ ﴿٥٨﴾

58. Wakaja kaka zake Yuwsuf; wakaingia kwake, basi yeye akawatambua, lakini wao hawakumtambua.

 

 

 

وَلَمَّا جَهَّزَهُم بِجَهَازِهِمْ قَالَ ائْتُونِي بِأَخٍ لَّكُم مِّنْ أَبِيكُمْ ۚ أَلَا تَرَوْنَ أَنِّي أُوفِي الْكَيْلَ وَأَنَا خَيْرُ الْمُنزِلِينَ﴿٥٩﴾

59. Na alipowatayarishia maandalizi yao akasema: “Njooni na ndugu yenu kutoka kwa baba yenu. Je, hamuoni kwamba hakika mimi natimiza kikamilifu kipimo nami ni mbora wa wenye kukirimu?”

 

 

 

فَإِن لَّمْ تَأْتُونِي بِهِ فَلَا كَيْلَ لَكُمْ عِندِي وَلَا تَقْرَبُونِ ﴿٦٠﴾

60. “Msiponijia naye, basi hamtokuwa na kipimo kwangu wala msinikurubie.”

 

 

 

قَالُوا سَنُرَاوِدُ عَنْهُ أَبَاهُ وَإِنَّا لَفَاعِلُونَ﴿٦١﴾

61. Wakasema: “Tutamrairai baba yake na bila shaka tutafanya.”

 

 

 

وَقَالَ لِفِتْيَانِهِ اجْعَلُوا بِضَاعَتَهُمْ فِي رِحَالِهِمْ لَعَلَّهُمْ يَعْرِفُونَهَا إِذَا انقَلَبُوا إِلَىٰ أَهْلِهِمْ لَعَلَّهُمْ يَرْجِعُونَ ﴿٦٢﴾

62. (Yuwsuf) Akawaambia watumishi wake: “Wekeni bidhaa zao katika mizigo yao, huenda wakazitambua watakaporudi kwa ahli zao, huenda wakarejea.”

 

 

 

فَلَمَّا رَجَعُوا إِلَىٰ أَبِيهِمْ قَالُوا يَا أَبَانَا مُنِعَ مِنَّا الْكَيْلُ فَأَرْسِلْ مَعَنَا أَخَانَا نَكْتَلْ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ﴿٦٣﴾

63. Basi waliporejea kwa baba yao, walisema: “Ee baba yetu! Tumenyimwa kipimo basi mtume pamoja nasi ndugu yetu, tupate kupimiwa; na sisi bila shaka tutamhifadhi.”

 

 

 

قَالَ هَلْ آمَنُكُمْ عَلَيْهِ إِلَّا كَمَا أَمِنتُكُمْ عَلَىٰ أَخِيهِ مِن قَبْلُ ۖ فَاللَّـهُ خَيْرٌ حَافِظًا ۖ وَهُوَ أَرْحَمُ الرَّاحِمِينَ ﴿٦٤﴾

64. Akasema: “Je, nimwaminishe kwenu ila kama nilivyokuaminini juu ya kaka yake kabla? Basi Allaah ni Mbora wa wenye kuhifadhi. Naye ni Mbora zaidi wa kurehemu kuliko wengine wote wenye kurehemu.”

 

 

 

وَلَمَّا فَتَحُوا مَتَاعَهُمْ وَجَدُوا بِضَاعَتَهُمْ رُدَّتْ إِلَيْهِمْ ۖ قَالُوا يَا أَبَانَا مَا نَبْغِي ۖ هَـٰذِهِ بِضَاعَتُنَا رُدَّتْ إِلَيْنَا ۖوَنَمِيرُ أَهْلَنَا وَنَحْفَظُ أَخَانَا وَنَزْدَادُ كَيْلَ بَعِيرٍ ۖ ذَٰلِكَ كَيْلٌ يَسِيرٌ ﴿٦٥﴾

65. Walipofungua mizigo yao, wakakuta bidhaa zao zimerudishwa kwao. Wakasema: “Ee baba yetu! Tunataka nini zaidi? Hizi bidhaa zetu zimerudishwa kwetu, na tutawaletea chakula ahli zetu, na tutamhifadhi ndugu yetu, na tutapata ziada ya kipimo cha ngamia. Hicho ni kipimo chepesi.”

 

 

 

قَالَ لَنْ أُرْسِلَهُ مَعَكُمْ حَتَّىٰ تُؤْتُونِ مَوْثِقًا مِّنَ اللَّـهِ لَتَأْتُنَّنِي بِهِ إِلَّا أَن يُحَاطَ بِكُمْ ۖ فَلَمَّا آتَوْهُ مَوْثِقَهُمْ قَالَ اللَّـهُ عَلَىٰ مَا نَقُولُ وَكِيلٌ ﴿٦٦﴾

66. Akasema: “Sitompeleka pamoja nanyi mpaka mnipe ahadi ya Allaah kwamba; bila shaka mtamrudisha kwangu isipokuwa ikiwa mmezungukwa.” Basi walipompa ahadi yao, akasema: “Allaah kwa tuyasemayo ni Mdhamini Anayetegemewa kwa yote.”

 

 

 

وَقَالَ يَا بَنِيَّ لَا تَدْخُلُوا مِن بَابٍ وَاحِدٍ وَادْخُلُوا مِنْ أَبْوَابٍ مُّتَفَرِّقَةٍ ۖوَمَا أُغْنِي عَنكُم مِّنَ اللَّـهِ مِن شَيْءٍ ۖإِنِ الْحُكْمُ إِلَّا لِلَّـهِ ۖ عَلَيْهِ تَوَكَّلْتُۖوَعَلَيْهِ فَلْيَتَوَكَّلِ الْمُتَوَكِّلُونَ ﴿٦٧﴾

67. Na akasema: “Enyi wanangu! Msiingie kupitia mlango mmoja, bali ingieni kupitia milango tofauti. Na wala siwezi kukufaeni chochote mbele ya Allaah. Hapana hukumu isipokuwa kwa Allaah. Kwake natawakali. Na Kwake watawakali wanaotawakali.”

 

 

 

وَلَمَّا دَخَلُوا مِنْ حَيْثُ أَمَرَهُمْ أَبُوهُم مَّا كَانَ يُغْنِي عَنْهُم مِّنَ اللَّـهِ مِن شَيْءٍ إِلَّا حَاجَةً فِي نَفْسِ يَعْقُوبَ قَضَاهَا ۚ وَإِنَّهُ لَذُو عِلْمٍ لِّمَا عَلَّمْنَاهُ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٦٨﴾

68. Na walipoingia kwa namna alivyowaamrisha baba yao, haikuwafaa kitu kwa Allaah isipokuwa haja iliyokuwa katika nafsi ya Ya’quwb aliyoitimiza. Na hakika yeye alikuwa mwenye elimu Tuliyomfunza, lakini watu wengi hawajui.

 

 

 

وَلَمَّا دَخَلُوا عَلَىٰ يُوسُفَ آوَىٰ إِلَيْهِ أَخَاهُ ۖ قَالَ إِنِّي أَنَا أَخُوكَ فَلَا تَبْتَئِسْ بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٦٩﴾

69. Na walipoingia kwa Yuwsuf, alimuweka ndugu yake karibu naye. Akasema: “Hakika mimi ni kaka yako, basi usisikitike kwa yale waliyokuwa wakiyafanya.”

 

 

 

فَلَمَّا جَهَّزَهُم بِجَهَازِهِمْ جَعَلَ السِّقَايَةَ فِي رَحْلِ أَخِيهِ ثُمَّ أَذَّنَ مُؤَذِّنٌ أَيَّتُهَا الْعِيرُ إِنَّكُمْ لَسَارِقُونَ﴿٧٠﴾

70. Na alipowatayarishia maandalizi yao alikitia kikopo cha kutekea katika mzigo wa ndugu yake, kisha mwenye kunadi akanadi: “Enyi wasafiri! Hakika nyinyi ni wezi!”

 

 

 

قَالُوا وَأَقْبَلُوا عَلَيْهِم مَّاذَا تَفْقِدُونَ﴿٧١﴾

71. Wakasema na huku wamewakabili: “Mmepoteza nini?”

 

 

 

قَالُوا نَفْقِدُ صُوَاعَ الْمَلِكِ وَلِمَن جَاءَ بِهِ حِمْلُ بَعِيرٍ وَأَنَا بِهِ زَعِيمٌ ﴿٧٢﴾

72. Wakasema: “Tumepoteza bika ya kupimia ya mfalme. Na atakayekuja nayo atapewa shehena ya ngamia; nami kwa hayo ni mdhamini.”‏

 

 

 

قَالُوا تَاللَّـهِ لَقَدْ عَلِمْتُم مَّا جِئْنَا لِنُفْسِدَ فِي الْأَرْضِ وَمَا كُنَّا سَارِقِينَ ﴿٧٣﴾

73. Wakasema: “Tunaapa kwa Allaah mmekwishajua hatukuja kufanya ufisadi katika ardhi, na hatukuwa wezi.”

 

 

 

قَالُوا فَمَا جَزَاؤُهُ إِن كُنتُمْ كَاذِبِينَ﴿٧٤﴾

74. Wakasema: “Basi nini jazaa yake, mkiwa ni waongo?” 

 

 

 

قَالُوا جَزَاؤُهُ مَن وُجِدَ فِي رَحْلِهِ فَهُوَ جَزَاؤُهُ ۚ كَذَٰلِكَ نَجْزِي الظَّالِمِينَ ﴿٧٥﴾

75. Wakasema: “Jazaa yake ni yule ambaye itapatikana (bika ya mfalme) kwenye mzigo wake; basi yeye ndiye jazaa yake. Hivyo ndivyo tunavyowalipa madhalimu.”

 

 

 

فَبَدَأَ بِأَوْعِيَتِهِمْ قَبْلَ وِعَاءِ أَخِيهِ ثُمَّ اسْتَخْرَجَهَا مِن وِعَاءِ أَخِيهِ ۚ كَذَٰلِكَ كِدْنَا لِيُوسُفَ ۖ مَا كَانَ لِيَأْخُذَ أَخَاهُ فِي دِينِ الْمَلِكِ إِلَّا أَن يَشَاءَ اللَّـهُ ۚ نَرْفَعُ دَرَجَاتٍ مَّن نَّشَاءُ ۗ وَفَوْقَ كُلِّ ذِي عِلْمٍ عَلِيمٌ ﴿٧٦﴾

76. Basi alianza (kutafuta) katika mizigo yao kabla ya mzigo wa ndugu yake. Kisha akaitoa kutoka katika mzigo wa ndugu yake. Hivyo ndivyo Tulivyompangia Yuwsuf. Hakuweza kumchukua ndugu yake katika sheria ya mfalme isipokuwa Atake Allaah. Tunampandisha vyeo Tumtakaye. Na juu ya kila mwenye elimu yuko mwenye elimu zaidi.

 

 

 

قَالُوا إِن يَسْرِقْ فَقَدْ سَرَقَ أَخٌ لَّهُ مِن قَبْلُ ۚ فَأَسَرَّهَا يُوسُفُ فِي نَفْسِهِ وَلَمْ يُبْدِهَا لَهُمْ ۚ قَالَ أَنتُمْ شَرٌّ مَّكَانًا ۖوَاللَّـهُ أَعْلَمُ بِمَا تَصِفُونَ ﴿٧٧﴾

77. Wakasema: “Ikiwa ameiba, basi amekwishaiba kaka yake kabla!” Yuwsuf aliyaweka siri katika nafsi yake na wala hakuwadhihirishia. Akasema: “Nyinyi mna hali mbaya; na Allaah Anajua zaidi yale mnayoyavumisha.”

 

 

 

قَالُوا يَا أَيُّهَا الْعَزِيزُ إِنَّ لَهُ أَبًا شَيْخًا كَبِيرًا فَخُذْ أَحَدَنَا مَكَانَهُ ۖ إِنَّا نَرَاكَ مِنَ الْمُحْسِنِينَ ﴿٧٨﴾

78. Wakasema: “Ee ‘Aziyz! Hakika yeye ana baba mkongwe, basi chukua mmoja wetu mahali pake. Hakika sisi tunakuona ni miongoni mwa wafanyao ihsaan.”

 

 

 

قَالَ مَعَاذَ اللَّـهِ أَن نَّأْخُذَ إِلَّا مَن وَجَدْنَا مَتَاعَنَا عِندَهُ إِنَّا إِذًا لَّظَالِمُونَ﴿٧٩﴾

79. Akasema: “Tunajikinga kwa Allaah kumchukua isipokuwa yule tuliyekuta kifaa chetu kwake (tukifanya), hakika sisi hapo bila shaka tutakuwa madhalimu.”

 

 

 

فَلَمَّا اسْتَيْأَسُوا مِنْهُ خَلَصُوا نَجِيًّا ۖقَالَ كَبِيرُهُمْ أَلَمْ تَعْلَمُوا أَنَّ أَبَاكُمْ قَدْ أَخَذَ عَلَيْكُم مَّوْثِقًا مِّنَ اللَّـهِ وَمِن قَبْلُ مَا فَرَّطتُمْ فِي يُوسُفَ ۖ فَلَنْ أَبْرَحَ الْأَرْضَ حَتَّىٰ يَأْذَنَ لِي أَبِي أَوْ يَحْكُمَ اللَّـهُ لِي ۖ وَهُوَ خَيْرُ الْحَاكِمِينَ ﴿٨٠﴾

80. Basi walipokata tamaa; wakajitenga kando kushauriana kisiri. Mkubwa wao akasema: “Je, hamjui kwamba baba yenu amekwishachukua kwenu ahadi kutoka kwa Allaah, na kabla hapo yale mlokusuru kuhusu Yuwsuf? Basi sitoondoka ardhi hii mpaka anipe idhini baba yangu, au Allaah Anihukumie. Naye ni Mbora wa wenye kuhukumu.”

 

 

 

ارْجِعُوا إِلَىٰ أَبِيكُمْ فَقُولُوا يَا أَبَانَا إِنَّ ابْنَكَ سَرَقَ وَمَا شَهِدْنَا إِلَّا بِمَا عَلِمْنَا وَمَا كُنَّا لِلْغَيْبِ حَافِظِينَ ﴿٨١﴾

81. “Rejeeni kwa baba yenu, na semeni: “Ee baba yetu! Hakika mwanao ameiba; nasi hatushuhudii isipokuwa kwa yale tunayoyajua; na hatukuwa wenye kuhifadhi ya ghayb.”

 

 

 

وَاسْأَلِ الْقَرْيَةَ الَّتِي كُنَّا فِيهَا وَالْعِيرَ الَّتِي أَقْبَلْنَا فِيهَا ۖ وَإِنَّا لَصَادِقُونَ﴿٨٢﴾

82. “Na uliza mji ambao tulikuwa humo, na msafara ambao tumekuja nao, na hakika sisi ni wakweli.”

 

 

 

قَالَ بَلْ سَوَّلَتْ لَكُمْ أَنفُسُكُمْ أَمْرًا ۖفَصَبْرٌ جَمِيلٌ ۖ عَسَى اللَّـهُ أَن يَأْتِيَنِي بِهِمْ جَمِيعًا ۚ إِنَّهُ هُوَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ﴿٨٣﴾

83. Akasema: “Bali nafsi zenu zimekushawishini jambo. Basi subira ni njema. Asaa Allaah Aniletee wote pamoja. Hakika Yeye Ndiye Mjuzi wa yote, Mwenye hikmah wa yote.”

 

 

 

وَتَوَلَّىٰ عَنْهُمْ وَقَالَ يَا أَسَفَىٰ عَلَىٰ يُوسُفَ وَابْيَضَّتْ عَيْنَاهُ مِنَ الْحُزْنِ فَهُوَ كَظِيمٌ ﴿٨٤﴾

84. Akajitenga nao, na akasema: “Ee majonzi yangu juu ya Yuwsuf.” Na macho yake yakageuka meupe kutokana na huzuni, naye huku akiwa amezuia ghaidhi za huzuni.

 

 

 

قَالُوا تَاللَّـهِ تَفْتَأُ تَذْكُرُ يُوسُفَ حَتَّىٰ تَكُونَ حَرَضًا أَوْ تَكُونَ مِنَ الْهَالِكِينَ﴿٨٥﴾

85. Wakasema: “Tunaapa kwa Allaah! Hutoacha kumkumbuka Yuwsuf mpaka uwe mgonjwa mahututi, au uwe miongoni mwa wenye kuhilaki.”

 

 

 

قَالَ إِنَّمَا أَشْكُو بَثِّي وَحُزْنِي إِلَى اللَّـهِ وَأَعْلَمُ مِنَ اللَّـهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ ﴿٨٦﴾

86. Akasema: “Hakika mimi nashitakia dhiki ya majonzi yangu na huzuni zangu kwa Allaah. Na najua kutoka kwa Allaah yale msiyoyajua.”

 

 

 

يَا بَنِيَّ اذْهَبُوا فَتَحَسَّسُوا مِن يُوسُفَ وَأَخِيهِ وَلَا تَيْأَسُوا مِن رَّوْحِ اللَّـهِ ۖ إِنَّهُ لَا يَيْأَسُ مِن رَّوْحِ اللَّـهِ إِلَّا الْقَوْمُ الْكَافِرُونَ ﴿٨٧﴾

87. “Ee wanangu! Nendeni mkauulizie kuhusu Yuwsuf na ndugu yake; na wala msikate tamaa na faraja ya Allaah; hakika hawakati tamaa na faraja ya Allaah isipokuwa watu makafiri.”

 

 

 

فَلَمَّا دَخَلُوا عَلَيْهِ قَالُوا يَا أَيُّهَا الْعَزِيزُ مَسَّنَا وَأَهْلَنَا الضُّرُّ وَجِئْنَا بِبِضَاعَةٍ مُّزْجَاةٍ فَأَوْفِ لَنَا الْكَيْلَ وَتَصَدَّقْ عَلَيْنَا ۖ إِنَّ اللَّـهَ يَجْزِي الْمُتَصَدِّقِينَ﴿٨٨﴾

88. Walipoingia kwake wakasema: “Ee ‘Aziyz! Dhara imetugusa pamoja na ahli zetu, na tumekuja na bidhaa isiyo na thamani, basi tutimizie kipimo, na tupe swadaqah. Hakika Allaah Anawalipa watoao swadaqah.”

 

 

 

قَالَ هَلْ عَلِمْتُم مَّا فَعَلْتُم بِيُوسُفَ وَأَخِيهِ إِذْ أَنتُمْ جَاهِلُونَ ﴿٨٩﴾

89. Akasema: “Je, mmejua yale mliyomfanyia Yuwsuf na ndugu yake wakati nyinyi majahili?”

 

 

 

قَالُوا أَإِنَّكَ لَأَنتَ يُوسُفُ ۖ قَالَ أَنَا يُوسُفُ وَهَـٰذَا أَخِي ۖ قَدْ مَنَّ اللَّـهُ عَلَيْنَا ۖ إِنَّهُ مَن يَتَّقِ وَيَصْبِرْ فَإِنَّ اللَّـهَ لَا يُضِيعُ أَجْرَ الْمُحْسِنِينَ ﴿٩٠﴾

90. Wakasema: “Je, kwani wewe ndio Yuwsuf?” Akasema: “Mimi ni Yuwsuf, na huyu ni ndugu yangu. Kwa yakini Allaah Ametufanyia ihsaan. Hakika mwenye kuwa na taqwa na akasubiri, basi hakika Allaah Hapotezi ujira wa watendao ihsaan.”

 

 

 

قَالُوا تَاللَّـهِ لَقَدْ آثَرَكَ اللَّـهُ عَلَيْنَا وَإِن كُنَّا لَخَاطِئِينَ ﴿٩١﴾

91. Wakasema: “Tunaapa Allaah! Kwa yakini Allaah Amekustahabu kuliko sisi, nasi bila shaka tulikuwa wakosa.”

 

 

 

قَالَ لَا تَثْرِيبَ عَلَيْكُمُ الْيَوْمَ ۖ يَغْفِرُ اللَّـهُ لَكُمْ ۖ وَهُوَ أَرْحَمُ الرَّاحِمِينَ ﴿٩٢﴾

92. Akasema: “Hakuna lawama juu yenu leo. Allaah Atakughufurieni. Naye ni Mbora zaidi wa kurehemu kuliko wengine wote wenye kurehemu.”

 

 

 

اذْهَبُوا بِقَمِيصِي هَـٰذَا فَأَلْقُوهُ عَلَىٰ وَجْهِ أَبِي يَأْتِ بَصِيرًا وَأْتُونِي بِأَهْلِكُمْ أَجْمَعِينَ ﴿٩٣﴾

93. “Nendeni na kanzu yangu hii, na litupeni kwenye uso wa baba yangu, atakuwa mwenye kuona; na nijieni na ahli zenu nyote pamoja.”

 

 

 

وَلَمَّا فَصَلَتِ الْعِيرُ قَالَ أَبُوهُمْ إِنِّي لَأَجِدُ رِيحَ يُوسُفَ ۖ لَوْلَا أَن تُفَنِّدُونِ﴿٩٤﴾

94. Na ulipoondoka msafara baba yao alisema: “Hakika mimi nasikia harufu ya Yuwsuf, ikiwa hamkunidhania nachanganyikiwa akili.”

 

 

 

قَالُوا تَاللَّـهِ إِنَّكَ لَفِي ضَلَالِكَ الْقَدِيمِ﴿٩٥﴾

95. Wakasema: “Tunaapa kwa Allaah! Hakika wewe umo katika ukosefu wako wa zamani.”

 

 

 

فَلَمَّا أَن جَاءَ الْبَشِيرُ أَلْقَاهُ عَلَىٰ وَجْهِهِ فَارْتَدَّ بَصِيرًا ۖ قَالَ أَلَمْ أَقُل لَّكُمْ إِنِّي أَعْلَمُ مِنَ اللَّـهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ ﴿٩٦﴾

96. Basi alipokuja mtoaji bishara akaitupa (kanzu) juu ya uso wake akarudi kuona. Akasema: “Je, sikukuambieni kwamba hakika mimi najua zaidi kutoka kwa Allaah yale msiyoyajua?”

 

 

 

قَالُوا يَا أَبَانَا اسْتَغْفِرْ لَنَا ذُنُوبَنَا إِنَّا كُنَّا خَاطِئِينَ ﴿٩٧﴾

97. Wakasema: “Ee baba yetu! Tuombee maghfirah madhambi yetu; hakika sisi tulikuwa wakosa.”

 

 

 

قَالَ سَوْفَ أَسْتَغْفِرُ لَكُمْ رَبِّي ۖ إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ ﴿٩٨﴾

98. Akasema: “Nitakuombeeni maghfirah kwa Rabb wangu. Hakika Yeye Ndiye Mwingi wa kughufuria,Mwenye kurehemu.”

 

 

 

فَلَمَّا دَخَلُوا عَلَىٰ يُوسُفَ آوَىٰ إِلَيْهِ أَبَوَيْهِ وَقَالَ ادْخُلُوا مِصْرَ إِن شَاءَ اللَّـهُ آمِنِينَ ﴿٩٩﴾

99. Na walipoingia kwa Yuwsuf akawaweka karibu naye wazazi wake. Na akasema: “Ingieni Misri In Shaa Allaah mkiwa mmo katika amani.”‏

 

 

 

وَرَفَعَ أَبَوَيْهِ عَلَى الْعَرْشِ وَخَرُّوا لَهُ سُجَّدًا ۖ وَقَالَ يَا أَبَتِ هَـٰذَا تَأْوِيلُ رُؤْيَايَ مِن قَبْلُ قَدْ جَعَلَهَا رَبِّي حَقًّا ۖوَقَدْ أَحْسَنَ بِي إِذْ أَخْرَجَنِي مِنَ السِّجْنِ وَجَاءَ بِكُم مِّنَ الْبَدْوِ مِن بَعْدِ أَن نَّزَغَ الشَّيْطَانُ بَيْنِي وَبَيْنَ إِخْوَتِي ۚإِنَّ رَبِّي لَطِيفٌ لِّمَا يَشَاءُ ۚ إِنَّهُ هُوَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ ﴿١٠٠﴾

100. Akawapandisha wazazi wake wawili juu ya kiti cha ufalme; wakaporomoka wote kumsujudia. Na akasema: “Ee baba yangu! Hii ni tafsiri ya ndoto yangu hapo kabla, Rabb wangu Ameijaalia kweli. Na Akanifanyia ihsaan Aliponitoa kutoka jela, na Akakuleteni kutoka jangwani baada ya shaytwaan kuchochea baina yangu na baina ya kaka zangu. Hakika Rabb wangu ni Latifu kwa Atakayo. Hakika Yeye Ndiye Mjuzi wa yote, Mwenye hikmah wa yote.”

 

 

 

رَبِّ قَدْ آتَيْتَنِي مِنَ الْمُلْكِ وَعَلَّمْتَنِي مِن تَأْوِيلِ الْأَحَادِيثِ ۚ فَاطِرَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ أَنتَ وَلِيِّي فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ ۖ تَوَفَّنِي مُسْلِمًا وَأَلْحِقْنِي بِالصَّالِحِينَ ﴿١٠١﴾

101. “Rabb wangu kwa yakini Umenipa katika utawala, na Umenifunza katika tafsiri za masimulizi (ya ndoto na matukio). Muanzilishi wa mbingu na ardhi. Wewe ni Mlinzi, Msaidizi wangu duniani na Aakhirah. Nifishe hali ya kuwa Muislamu na Unikutanishe na Swalihina.”

 

 

 

ذَٰلِكَ مِنْ أَنبَاءِ الْغَيْبِ نُوحِيهِ إِلَيْكَ ۖوَمَا كُنتَ لَدَيْهِمْ إِذْ أَجْمَعُوا أَمْرَهُمْ وَهُمْ يَمْكُرُونَ ﴿١٠٢﴾

102. Hizo ni baadhi ya khabari za ghayb Tunakufunulia Wahy kwako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم). Na hukuwa pamoja nao pale walipokubaliana jambo lao, nao wakifanya mbinu.

 

 

 

وَمَا أَكْثَرُ النَّاسِ وَلَوْ حَرَصْتَ بِمُؤْمِنِينَ ﴿١٠٣﴾

103. Na wengi wa watu hawatoamini japokuwa utatilia hima.

 

 

 

وَمَا تَسْأَلُهُمْ عَلَيْهِ مِنْ أَجْرٍ ۚ إِنْ هُوَ إِلَّا ذِكْرٌ لِّلْعَالَمِينَ ﴿١٠٤﴾

104. Na huwaombi kwa haya ujira wowote (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم). Hii (Qur-aan) si chochote isipokuwa ni ukumbusho kwa walimwengu.

 

 

 

وَكَأَيِّن مِّنْ آيَةٍ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ يَمُرُّونَ عَلَيْهَا وَهُمْ عَنْهَا مُعْرِضُونَ ﴿١٠٥﴾

105. Na Aayah (ishara, dalili) ngapi katika mbingu na ardhi wanazipitia na huku wao wanazipuuza.

 

 

 

وَمَا يُؤْمِنُ أَكْثَرُهُم بِاللَّـهِ إِلَّا وَهُم مُّشْرِكُونَ ﴿١٠٦﴾

106. Na wengi kati yao hawamwamini Allaah isipokuwa wao ni wenye kufanya shirki

 

 

 

أَفَأَمِنُوا أَن تَأْتِيَهُمْ غَاشِيَةٌ مِّنْ عَذَابِ اللَّـهِ أَوْ تَأْتِيَهُمُ السَّاعَةُ بَغْتَةً وَهُمْ لَا يَشْعُرُونَ ﴿١٠٧﴾

107. Je, wanaaminisha kuwa haitowafikia adhabu ya Allaah ifunikizayo au itawafikia Saa kwa ghafla nao hawahisi?

 

 

 

قُلْ هَـٰذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّـهِ ۚ عَلَىٰ بَصِيرَةٍ أَنَا وَمَنِ اتَّبَعَنِي ۖ وَسُبْحَانَ اللَّـهِ وَمَا أَنَا مِنَ الْمُشْرِكِينَ ﴿١٠٨﴾

108. Sema: “Hii ndio njia yangu nalingania kwa Allaah, juu ya nuru za elimu na umaizi, mimi na anayenifuata. Na Utakasifu ni wa Allaah, nami si miongoni mwa washirikina.”

 

 

 

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ إِلَّا رِجَالًا نُّوحِي إِلَيْهِم مِّنْ أَهْلِ الْقُرَىٰ ۗ أَفَلَمْ يَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَيَنظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ ۗ وَلَدَارُ الْآخِرَةِ خَيْرٌ لِّلَّذِينَ اتَّقَوْا ۗ أَفَلَا تَعْقِلُونَ ﴿١٠٩﴾

109. Na Hatukutuma kabla yako (Rasuli) isipokuwa wanaume Tuliowafunulia Wahy katika watu wa miji; Je, basi hawatembei katika ardhi wakatazama vipi ilikuwa khatima ya wale kabla yao? Na bila shaka nyumba ya Aakhirah ni bora kwa wale waliokuwa na taqwa. Je, basi hawatii akilini?

 

 

 

حَتَّىٰ إِذَا اسْتَيْأَسَ الرُّسُلُ وَظَنُّوا أَنَّهُمْ قَدْ كُذِبُوا جَاءَهُمْ نَصْرُنَا فَنُجِّيَ مَن نَّشَاءُ ۖ وَلَا يُرَدُّ بَأْسُنَا عَنِ الْقَوْمِ الْمُجْرِمِينَ ﴿١١٠﴾

110. (Wakaendelea kulingania) Mpaka walipokata tamaa Rusuli na wakadhani kwamba wao wamekwishakadhibishwa ikawajia nusra Yetu; na Tukawaokoa Tuwatakao. Na wala hairudishwi nyuma adhabu Yetu kwa watu wakhalifu.

 

 

 

لَقَدْ كَانَ فِي قَصَصِهِمْ عِبْرَةٌ لِّأُولِي الْأَلْبَابِ ۗ مَا كَانَ حَدِيثًا يُفْتَرَىٰ وَلَـٰكِن تَصْدِيقَ الَّذِي بَيْنَ يَدَيْهِ وَتَفْصِيلَ كُلِّ شَيْءٍ وَهُدًى وَرَحْمَةً لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ﴿١١١﴾

111. Kwa yakini katika visa vyao kuna mafunzo kwa wenye akili. Haikuwa (Qur-aan) hadithi zinazotungwa, lakini ni sadikisho la (vitabu) vya kabla yake na tafsili ya kila kitu, na ni mwongozo na rahmah kwa watu wanaoamini.

 

 


Report Page