Yesu kwa Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - KITABU cha MBINGU - Juzuu na. 19 - Mei 31, 1926🖋📄📖📔

Yesu kwa Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - KITABU cha MBINGU - Juzuu na. 19 - Mei 31, 1926🖋📄📖📔


Ule mwanga wa Utashi wa Mungu unaendelea kunifunika mimi. Na akili yangu ndogo, wakati inapoogelea ndani ya bahari kuu ya mwanga huo, inaweza tu kutwaa dozi chache za mwanga huo, na kutwaa miali michache midogo ya zile kweli nyingi kabisa, miali ile midogo ya maarifa na ya heri mbalimbali ambayo ile bahari kuu isiyo na ukomo ya Utashi wa Milele inazibeba. Na mara nyingi sana huwa siwezi kupata msamiati ufaao kwa ajili ya kuweza kuandika hiyo dozi ndogo ya mwanga juu ya karatasi. Ninatumia neno ‘dozi ndogo’ ninapolinganisha na ile dozi kubwa ninayoiacha, kwa vile, hii akili yangu ndogo na duni, huwa inachukua kiwango kile cha kutosha kunijaza mimi - yote inayobaki huwa ni lazima niiache. Huwa inatokea kama kwa mtu anayejitosa kupiga mbizi baharini. Huyo hulowa popote, maji hutiririka popote mwilini mwake, na huenda hata tumboni mwake. Lakini, atakapotoka nje ya bahari, je atakuwa anatoka na kiwango gani cha maji yote ya bahari? Ni kidogo mno - na kwa kweli ni sawa na si kitu unapolinganisha na maji yale yanayobakia baharini. Na kwa kule kuwa ndani ya bahari, je labda ataweza akasema kulikuwa na maji kiasi gani, au je kulikuwa na aina ngapi za samaki na labda kuna idadi zao ni ngapi pale ndani ya bahari? Wala hataweza. Lakini ataweza bado kuzungumzia juu ya kile kidogo alichofanikiwa kukiona kuhusu bahari. Ndivyo ilivyo roho yangu duni. Halafu, pindi nikiwa katika mwanga huo, Yesu Wangu Mtamu alikuja kutoka ndani mwangu akaniambia hivi:

“Binti Yangu, huo ndio umoja wa mwanga wa Utashi Wangu. Ili wewe uweze kuupenda zaidi na zaidi, na ili uweze kuthibitika zaidi ndani yake, Mimi ninapenda kukufahamisha ile tofauti kubwa iliyopo kati ya yule anayeishi ndani ya Utashi Wangu, ndani ya umoja wa mwanga huo, na yule ambaye anajiachia na kujikabidhi ndani ya Utashi Wangu.

Ili kukusaidia uweze kulielewa jambo hilo vizuri, Mimi nitakupatia ulinganisho kutoka jua lile ambalo lipo kule kwenye upeo wa anga. Lile jua, wakati lipo pale chini ya dari ya anga, husambaza mionzi yake juu ya sura yote ya ardhi. Ebu angalia: Yaelekea, kati ya ardhi na jua kuna namna fulani ya mapatano - jua linaigusa ardhi, na ardhi nayo inaupokea mwanga na ule mguso wa jua. Sasa, kwa kuupokea ule mguso wa mwanga, na kwa kujikabidhi kwa jua, ardhi inapokea matokeo yaliyopo ndani ya mwanga, na hayo matokeo yanaibadili ile sura ya ardhi. Yale matokeo ya mwanga yanaifanya ardhi ibadilike kuwa ya kijani tena, yanaifanya itoe maua - mimea inakua, matunda yanaiva, na maajabu mengine mengi yanayoanza kuonekana juu ya sura ya ardhi, yote yakiwa yamezalishwa na yale matokeo yaliyopo ndani ya mwanga wa jua.

Lakini, kwa kuyatoa yale matokeo yake, jua halitoi mwanga wake. Kinyume chake, jua linaendelea kuhifadhi umoja wake kwa wivu mkubwa, na yale matokeo yake siyo ya kudumu, na ndiyo maana, mtu utaiona masikini ardhi mara hii inatoa mauamaua, halafu yote yanafifia - ardhi inabadilika karibu katika kila majira mpya, na huwa inakabiliwa na mabadiliko endelevu. Kama jua lingekuwa linatoa matokeo na mwanga kwa ardhi, ardhi yenyewe ingebadilika kuwa jua na wala isingekuwa na hitaji tena la ombaomba kupata matokeo mbalimbali, kwani, kwa kuubeba mwanga ndani yake yenyewe, ardhi yenyewe ingekuwa ni mmiliki wa lile chimbuko la matokeo, chimbuko ambalo lipo ndani ya jua.

Basi, hivyo ndivvyo anavyokuwa mtu yule ambaye anajikabidhi kwa Utashi Wangu na kuutii: Huyo anayaishi yale matokeo yaliyopo ndani ya Utashi Wangu. Na kwa vile hana mwanga, huwa anakosa kuwa na chimbuko la hayo matokeo ambayo yapo ndani ya lile Jua la Utashi wa Milele. Kwa sababu hiyo, watu hao, huonekana kuwa karibu sawa na ile ardhi: muda fulani wanakuwa ni matajiri wa fadhila na muda mwingine wanakuwa fukara. Na huwa wanabadilikabadilika kwa kila aina ya mazingira. Na zaidi hasa, endapo hawakujikabidhi kwa Utashi Wangu na kuutii kwa daima, hapo, wanakuwa sawa na ardhi ambayo haitaki kuguswa na mwanga wa jua. Na kwa kweli, kama ardhi hiyo itayapokea matokeo basi, ni kwa sababu tu itakuwa imeweza kukubali kuguswa na mwanga wa jua. Vinginevyo ardhi hiyo ingebaki imechujuka na wala isingeweza kuzalisha hata jani moja la nyasi.

Ndivyo alivyokuwa Adamu baada ya ile dhambi. Alikuwa amepoteza ule umoja wa mwanga, na kwa hiyo, alikuwa amepoteza lile chimbuko la mema na matokeo yaliyopo ndani ya Jua la Utashi Wangu. Hakuwa tena na uwezo wa kuuonja ujazo wa lile Jua la Kimungu lililopo ndani yake mwenyewe. Ndani yake yeye mwenyewe hakuweza tena kuuona ule umoja wa mwanga ambao Muumba Wake alikuwa ameusimika kilindini mwa roho yake. Umoja huo wa mwanga ndio uliokuwa unawasilisha kwake ule ufanano wa Mungu, na ndio pia ulikuwa unamfanya awe ni nakala aminifu na halisia ya Muumba. Kabla ya kutenda dhambi, kwa vile, pamoja na Muumba Wake, alikuwa na chimbuko la ule umoja wake wa mwanga, kila tendo lake dogo lilikuwa ni mwonzi wa mwanga, ambao, unapoulenga na kuuchoma Uumbwa wote, ulikuwa unakwenda moja kwa moja na kutua katikati ya Muumba Wake, na hivyo ulikuwa unamfikishia lile pendo, na yale malipo kwa mambo yale yote, yaliyokuwa yameandaliwa kwa ajili yake ndani ya Uumbwa wote. Yeye Adamu alikuwa ndiye aliyekuwa akileta harmonia ya mambo yote, na aliyekuwa akitengeneza ile noti ya upatanisho kati ya Mbingu na dunia. Lakini, mara tu alipojiondoa toka katika Utashi Wangu, yale matendo yake hayakuweza tenda kuchomoza kama mionzi na kwenda kuzichoma Mbingu na dunia, bali, badala yake, yalijikunyata, karibu sawa na mimea au maua yanayonyauka, na kubaki ndani ya ule mduara mdogo wa uwanja wake. Kwa hiyo, kwa kupoteza harmonia na Uumbwa wote, Adamu akageuka na kuwa ni noti kinzani katika Uumbwa wote. Oh! Ni jinsi agani alivyoteremka na kudondokea chini. Alilalamika na kuulilia sana ule umoja wa mwanga uliopotea, ambao, kwa kumpandisha juu ya viumbe vingine vyote, ulikuwa umemfanya Adamu kuwa mungu mdogo wa duniani!

Basi, ewe Binti Yangu, kutokana na hayo niliyokueleza, unaweza sasa kuelewa kwamba, kuishi ndani ya Utashi Wangu, ni kuwa na lile chimbuko la umoja wa mwanga wa Utashi Wangu, pamoja na ujazo wote wa matokeo yaliyomo ndani yake. Kwa hiyo, mwanga, pendo, uabudu..... hujitokeza katika kila tendo la mwanadamu, ambalo, kwa lenyewe kujiweka kuwa ni tendo kwa ajili ya kila tendo, na kuwa ni pendo kwa ajili ya kila pendo, sawa kama ule mwanga wa jua, hilo tendo la mwanadamu, linashambulia na linachoma kila kitu, linaleta harmonia kwa kila kitu, na linaweka na linasimika kila kitu ndani yake lenyewe. Na kama mwonzi unaong’aa kabisa, linafikisha kwa Muumba Wake yale malipo kwa ajili ya mambo yale yote aliyokuwa ameyatenda kwa ajili ya wanadamu wote, na linaifikisha pia ile noti halisi ya uelewano kati ya Mbingu na dunia.

Ni tofauti kubwa ilioje kati ya mtu aliye na lile chimbuko la mema yaliyopo ndani ya Jua la Utashi Wangu, na mtu yule anayeyaishi tu matokeo yake! Ni tofauti ile iliyopo kati ya jua na ardhi. Jua huwa daima na ujazo wa mwanga wake na matokeo yake, huwa linaangaza daima na huwa ni tukufu katika ile dari ya zile anga, na wala huwa haliihitaji ardhi. Ingawa kama jua linagusa kila kitu, lenyewe huwa haliguswi, na wala huwa haliruhusu liguswe na mtu yeyote. Na hata kama mtu yeyote angethubutu kukazia macho yake ili kuliangalia, jua lingemtia kiza, lingempofusha na hata lingemwangusha chini kwa nguvu ya mwanga wake. Kwa upande mwingine lakini, ardhi huwa inahitaji kila kitu. Huwa inakubali na kuruhusu iwe inaguswa na iwe inavuliwa vazi lake. Na kama pasingekuwa na mwanga wa jua na pasingekuwa matokeo ya jua, ardhi ingekuwa ni gereza la giza totoro lililojaa na uchafu wa matatizo. Kwa hiyo, hakuna ulinganisho unaoweza kufaa kati ya yule anayeishi ndani ya Utashi Wangu na yeye anayejiweka chini ya utii kwa Utashi Wangu.

Kwa jinsi hiyo, Adamu alikuwa na ule umoja wa mwanga kabla ya kutenda dhambi. Baada ya hapo, katika kipindi chote cha uhai wake, hakuweza kuupata tena huo umoja. Kwake kilitokia kile kitokeacho kwa dunia ambayo inalizunguka jua. Kwa kutotulia mahali pamoja, wakati inapoendelea kuzunguka, inafikia mahali ambapo dunia hupingana na jua na kutengeneza giza la usiku. Ili kumsaidia Adamu kutulia tena mahali pamoja, ili aweze kuuzingatia tena umoja wa mwanga huo, palihitajika mtu atakayeweza kurekebisha, na huyo mrekebishaji alipasika awe ni mmoja aliye mkubwa zaidi kuliko yeye mwenyewe.

Palihitajika nguvu ya kimungu ambayo ingeweza kumwinua tena na kumnyosha. Hapo ndipo tunaona ulazima wa Ukombozi.

Mama Yangu wa Mbinguni naye alikuwa na huo umoja wa mwanga, na ndiyo maana, zaidi kupita hata jua, yeye anaweza kutoa mwanga kwa watu wote. Kati yake na ule Ukuu Mtukufu wa Juu hapajawahi kutokea kipindi cha usiku, na wala hapajawahi kuwa na kivuli chochote, bali pamekuwa daima na mwanga kamili wa mchana peke yake. Kwa sababu hiyo, katika kila dakika, huo umoja wa mwanga wa Utashi Wangu, uliufanya Uhai wote wa Kimungu uwe unatiririka ndani yake. Na huo umoja wa mwanga ukawa unamletea mabahari ya mwanga, mabahari ya furaha mbalimbali, ya heri mbalimbali, ya maarifa mbalimbali ya kimungu, mabahari ya uzuri, ya utukufu, na ya pendo. Na yeye, akiwa kama vile katika sherehe za ushindi, aliyafikisha mabahari hayo yote mbele ya Muumba Wake, yakiwa kama ni ya kwake mwenyewe. Aliyafikisha Kwake ili kumthibitishia pendo la kwake, uabudu wa kwake, na ili kumvutia kwake kwa nguvu ya uzuri wake mwenyewe. Na Umungu ukawa unamtiririshia mabahari mazuri mapya mengine mengi zaidi. Akabeba ndani yake pendo kubwa hivi kwamba, kama vile kwa nguvu ya asili yake mwenyewe, aliweza, kuwapenda watu wote, aliweza kuabudu na aliweza kulipa fidia kwa niaba ya watu wote.

Matendo yake madogo kabisa, ambayo kayatenda katika umoja wa mwanga huo, yakawa ni makuu kushinda matendo makuu kabisa na kushinda ile jumla ya matendo yote ya wanadamu tukiwaweka pamoja. Kwa hiyo basi, zile sadaka, zile kazi, na lile pendo la wanadamu wengine wote zaweza zikaitwa ni kama miali midogo midogo mbele ya jua, ni kama matone madogo madogo ya maji mbele ya bahari, unapoyalinganisha na matendo ya yule Malkia Mwenye Mamlaka. Ndiyo maana, kwa ile nguvu ya umoja wa mwanga huo wa Utashi Mkuu wa Juu, yeye Mama Yangu, alishangilia ushindi juu ya mambo yote, na aliweza kumteka hata Mwenyewe Muumba Wake kwa kumfanya Yeye awe Mfungwa Mahabusu ndani ya tumbo lake la umama. Ah! Ni peke yake huu umoja wa mwanga huo wa Utashi Wangu, ambao alikuwa nao yeye aliyekuwa anatawala juu ya kila kitu, ndio ulioweza kutenda muujiza huo ambao haujawahi kamwe kutokea hapo kabla. Umoja wa mwanga wa Utashi Wangu ulitekeleza hilo kwa kumjalia matendo yale yanayostahilika fika kwa huyo Mfungwa Mahabusu wa Kimungu.

Kwa kupoteza ule umoja wa mwanga, Adamu, alianguka kichwa chini miguu juu na akaingiza giza la usiku, madhaifu mbalimbali, matamaa, kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya vizazi vya binadamu.

Lakini, huyo Bikira mtukufu na adhimu, kwa kutotekeleza kamwe utashi wake mwenyewe, alibaki amesimama daima wima akiliangalia lile Jua la Milele, na kwa hiyo, kwake yeye kulikuwepo daima mwanga wa mchana na hata ndiye aliyefanya siku ya Jua la Haki ipambazuke kwa ajili ya vizazi vyote vya binadamu.

Kama huyu Malkia Bikira asingetenda kitu kingine cha ziada isipokuwa kuhifadhi ule umoja wa mwanga wa Utashi wa Milele ndani ya kina cha roho yake immakulata, hiyo ingetosha kabisa kuturejeshea Sisi ule utukufu wa wanadamu wote, yale matendo ya wote, na ile fidia kwa pendo lile la Uumbwa wote. Kwa njia yake huyu Bikira, kwa nguvu ya Utashi Wangu, Umungu ukawa unaonja mambo yafuatayo yakirejea Kwake: zile furaha mbalimbali, na zile heri mbalimbali ambazo ulikuwa umekwisha kupanga kuzipata kupitia Uumbwa.

Kwa sababu hiyo, anaweza akaitwa Malkia, akaitwa Mama, Mwasisi, anaweza akaitwa Msingi na Kioo cha kujitazamia cha Utashi Wangu, kioo ambamo watu wote wanaweza wakajiona wenyewe ili kuweza kuupata Uhai Wake”.

Baada ya hapo mimi nilijionja kulowana kwa mwanga huo, na nikawa ninauelewa ule muujiza mkuu wa kuishi ndani ya umoja wa mwanga huu wa Utashi Mkuu wa juu. Ndipo Yesu Wangu Mtamu, alirejea kwangu na kuongeza kusema:

“Binti Yangu, Adamu alipokuwa katika hali ile ya bila waa, na Mama yangu wa Mbinguni, wote walikuwa na ule umoja wa mwanga wa Utashi Wangu - siyo kwa nguvu yao wenyewe, bali kwa nguvu ile iliyowafikia kutoka kwa Mungu. Kwa upande mwingine, Ubinadamu Wangu Mimi ulikuwa na umoja huo kwa nguvu yake wenyewe kwa vile ndani yake kulikuweko siyo tu umoja wa mwanga wa Utashi Mkuu, bali kulikuwepo pia Neno wa Milele. Na kwa vile Mimi sitenganiki na Baba na Roho Mtakatifu, pale palitokea uwezekano, halisi na kamili, wa kuwepo mahali pengi kwa wakati mmoja - yaani, wakati nikiwa nimebaki pale Mbinguni juu, Mimi niliteremkia tumboni mwa Mama Yangu. Na kwa vile Baba na Roho Mtakatifu hawatenganiki toka Kwangu Mimi, Wao pia nao waliteremkia pale ndani ya tumbo, na kwa wakati ule ule walikuwa wamebakia kule juu kabisa mwa zile Mbingu”.

Basi, pindi Yesu alipokuwa akisema hilo, mimi nikawa nimeingiwa na shaka mintarafu Nafsi Tatu za Mungu, iwapo hizo Nafsi zote Tatu nazo zilikuwa zimeteswa au ilikuwa ni Neno peke yake aliyeteswa. Hapo Yesu alianza kurudia mazungumzo Yake akisema: 

“Binti Yangu, kwa vile Wao hawatenganiki na Mimi, Baba na Roho Mtakatifu waliteremka pamoja Nami, na Mimi nilikuwa nimebaki katika zile Mbingu pamoja Nao. Lakini jukumu la kulipa fidia, jukumu la kuteseka, na jukumu la kumkomboa binadamu lilichukuliwa na Mimi. Mimi, Mwana wa Baba, ndiye niliyebeba kazi ya kupatanisha Mungu na binadamu. Umungu Wetu ulikuwa haugusiki na mateso yaliyosababishwa na umivu lolote, hata lile dogo kabisa. Ilikuwa ni ule Ubinadamu Wangu, ambao, huku ukiwa umeunganika na Nafsi Tatu za Mungu kwa namna isiyotenganika, huku ukijitoa wenyewe na kujiweka kama mhanga wa huruma ya Umungu, ndio ulioteswa yale maumivu yasiyopata kusikika na ndio uliotoa fidia kwa mtindo wa kimungu. Na kwa vile Ubinadamu Wangu ulikuwa siyo tu na ule ujazo wa Utashi Wangu kama nguvu yake, bali, Neno Mwenyewe, kama vile pia Yeye Mwenyewe Baba, na Yeye Mwenyewe Roho Mtakatifu, kutokana na kutokutenganikana kwetu, uliweza, kwa ukamilifu zaidi, kuwapita na kuwashinda wote wawili, yule Adamu aliye bila waa na hata Mama Yangu Mwenyewe. Na kwa kweli, ndani yao hawa wawili ilikuwa ni neema, lakini ndani Yangu Mimi ilikuwa ni asilia Yangu. Wao walihitaji kuchota mwanga, kuchota neema, nguvu na uzuri wao toka kwa Mungu. Kumbe ndani ya Mimi kulikuwepo lile chimbuko linalochemka mwanga, uzuri, neema....... Kwa hiyo, tofauti iliyopo kati Yangu, kama asilia, na Mama Yangu Mwenyewe, kama neema, ilikuwa ni kubwa mno, kwamba, hata yeye alibaki ametiwa kiza mbele ya Ubinadamu Wangu.

Kwa sababu hiyo, Binti Yangu, angalia na uwe makini, huyu Yesu Wako analo lile chimbuko linalochemka, na Yeye daima anacho kitu cha kukupatia wewe, na wewe daima una kitu cha kuchukua. Hata ningekuelezea mambo mengi, mengi mangapi sijui, mintarafu Utashi Wangu, Mimi nitakuwa ninacho daima kitu cha ziada cha kukuambia. Na, iwe ni ufupi wa uhai wa hapa uhamishoni, au iwe ni ule umilele wote, vyote hivyo havitatosha kwa ajili ya kukufahamisha wewe habari yote ndefu ya Utashi Wangu Mkuu wa Juu, na havitatosha kuweza kuhesabia idadi ya yale makuu yaliyopo ndani yake”.

Juzuu na. 19 ku download - click here

Kila siku, hatua kwa hatua, jisomee hapa, ili upate kukua katika Paji la Uhai, ndani ya UTASHI WA MUNGU, kulingana na Mafundisho aliyoyatoa YESU kwake Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA

Swahili - Telegram Channel: Utashi Wa Mungu Na Upendo Wa Mungu

Swahili - Telegram Channel: Saa 24 Za Mateso Ya Bwana Weto Yesu Kristo

English - Telegram Channel: Divine Will Divine Love

English - Telegram Channel: The Virgin Mary in the Kingdom of the Divine Will

Français - Chaine de Telegram: Divine Volonte Divin Amour

Français - Chaîne de Telegram: Lettres de Luisa Piccarreta

Lingala - Chaine de Telegram: Mpo Elingi Nzambe Bolingi bwa Nzambe

Website all languages: www.divinewilldivinelove.com

Vitabu yote vilivyo katika faili za PDF vinaweza kupakuliwa bila gharama yoyote ile wakati wote ule. Pia, upo huru kabisa kuchapisha VITABU hivyo wewe mwenyewe binafsi au kuchapisha kwenye kiwanda chochote kile. Lakini vitabu hivyo ni kwa matumizi binafsi tu na siyo kwa ajili ya biashara! Hata hivyo una ruhusa ya kuwashirikisha na kuwapatia watu wengine vitabu hivyo kadiri unavyopenda!!

Swahili landing page: click here

English landing page: click here

Lingala landing page: click here

Kikongo landing page: click here

French landing page: click here

Italian landing page: click here

Report Page