Yesu kwa Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - KITABU cha MBINGU - Juzuu na. 18 - Agosti 9, 1925 🖋📄📖📔

Yesu kwa Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - KITABU cha MBINGU - Juzuu na. 18 - Agosti 9, 1925 🖋📄📖📔


Ee Yesu Wangu, unipe nguvu Wewe unayeona wazi uzito wa moyo wangu unaositasita katika kazi hii ya kuandika ambayo kama isingekuwa ni suala la huu utii kwa wakubwa na hofu ya kukusikitisha Wewe mimi nisingeweza kuandika hata neno moja. Halafu kutoweka kwako pengine kwa muda mrefu kunanifanya nipoteze hamu kabisa na hunifanya nipoteze uwezo kabisa kabisa. Kwa hiyo ninahitaji msaada mkubwa ili niweze kuandika katika karatasi kweli kile ambacho Utashi Wako Mtakatifu unaniambia. Basi unipe Mkono Wako kunisaidia na Wewe uwe pamoja nami daima.

Pindi nikiwa ninajiyeyushia ndani ya Utashi Mtakatifu wa Mungu, nikiwa katika kubadilishana kwa upendo kwa ajili ya kila kitu ambacho Mungu alikuwa ametenda katika Uumbwa, ikiwa yote ni kwa ajili ya kuwapenda wanadamu, mawazo yangu yakawa yananiambia eti haikuwa ni lazima kwa mimi kusali, na hasa namna ile ya kusali haikuwa inampendeza Yesu. Fikra hizo na sala hizo ni mawenge ya kichwani mwangu tu. Hapo Yesu Wangu mpendevu, akaingia ndani mwangu akaniambia:

“Binti Yangu, ni budi ukaelewa kwamba mtindo huo wa kusali, yaani kukumbuka kumrudishia Mungu kwa upendo kwa ajili ya kila kitu alichokiumba Yeye, ni wajibu na haki ya kimungu na inaingia kama jukumu la kwanza la mwanadamu. Uumbwa ulifanyika kwa ajili ya Pendo kwa binadamu. Yaani, Pendo Letu lilikuwa kubwa hivi kiasi ingekuwa ni lazima, Sisi tungelikuwa tumeumba mbingu nyingi, majua mengi, nyota nyingi, mabahari mengi, ardhi nyingi, mimea mingi, na vyote vyote, tungeliviumba kulingana na idadi ya wanadamu ambao wangekuja kujitokeza katika dunia hii ili mradi kila mmoja wao angeweza kujipatia Uumbwa wake mwenyewe, yaani kujipatia ulimwengu wote wa kwake tu. Ni ndivyo kwa kweli ilivyotokea wakati kilipokuwa kimeumbwa kila kitu na pakatokea Adamu peke yake akawa ndiye mtazamaji, na ndiye kiumbe pekee aliyeweza kustaajabu Uumbwa wote, ndiye peke yake aliweza kuvifurahia viumbe vyote na ndiye peke yake aliweza kufaidi kila jema alilolitaka kutoka kwa viumbe hao. Iwapo Sisi hatukufanya kitu hicho kwa sababu tu tulitaka mwanadamu aweze kufaidi vitu vyote kama mali yake mwenyewe na kamwe isitokee kinyume chake kwamba viumbe vingine ndio vifaidi. Na kwa kweli ni kiumbe gani asiyeweza akasema: ‘Jua ni langu mimi’ na akafaidi mwanga wa jua kadiri anavyotaka? Ni nani asiyeweza kusema . Maji ni yangu’ na akayatumia kuzima kiu chake na akatumia kadiri anavyoyahitaji? Nani hataweza kusema ‘Bahari, ardhi, moto, hewa, yote ni yangu mimi’?. Na vitu vingine vingi tu vilivyoumbwa na Mimi. Na kama kuna kitu ambacho binadamu amekosea, kitu kinachositisha uhai wake, ni ile dhambi ambayo ilifunga njia ya kuyapata mema Yangu, dhambi inayozuia hata vitu vilivyoumbwa na Mimi visiweze kumfikia mwanadamu mwenye utovu wa shukrani.

Maadam mambo yote yalikuwa ndivyo hivyo, yaani kwamba katika vitu vyote vilivyoumbwa Mungu aliunganisha na upendo wake kwa kila mwanadamu, basi katika huyo mwanadamu uliingia wajibu wa kumlipa Mungu angalau kwa njia ya pendo lake dogo, yaani kwa shukrani yake, kwa kauli yake ya asante kwa Yule ambaye amemtendea mambo mengi namna ile. Kitendo hicho cha kutomlipa Mungu kwa njia ya upendo kwa ajili ya yale yote ambayo Mungu ameyatenda katika Uumbwa kwa manufaa ya binadamu, ndiyo dhambi ya kwanza ya udanganyifu anayotenda mwanadamu dhidi ya Mungu, ni sawa na kuiba au kupora mapaji ya Mungu bila hata kuyatambua na kukiri yanatoka wapi, na bila kumkiri na kumthamini Yule ambaye ndiye amempenda vikubwa namna ile. Kwa hiyo, huo ndio wajibu wa kwanza wa mwanadamu. Jukumu hili ni la lazima na muhimu hivi kiasi kwamba yule Binti Bikira aliyechukulia maanani kabisa suala la utukufu wetu, utetezi wetu, manufaa yetu, hakuweza kufanya namna nyingine isipokuwa kutembelea na kuzungukia makao yote ya viumbe vya Mungu, kuanzia makazi yale madogo kabisa hadi yale makubwa kabisa, ili akaingize na kupiga muhuri wa malipo yale ya Pendo, ya Utukufu, na ya Shukrani, kwa niaba ya wanadamu wote na kwa niaba ya vizazi vyote vya binadamu. Ah, ndiyo kwa kweli, alikuwa hasa ni Mama Yangu wa Mbinguni aliyeweza kujaza Mbingu na dunia kwa yale malipo kwa ajili ya chote alichotenda Mungu katika Uumbwa! Baada ya Mama, ulifuata Ubinadamu Wangu ambao ulitekeleza jukumu hilo takatifu sana ambalo mwanadamu alishindwa kabisa kabisa kulitekeleza. Baba yangu wa mbinguni alinitwaa Mimi na kuniweka niwe ndiyo sadaka ya fidia stahiki kwa ajili ya mwanadamu aliyekuwa amekosa. Hivyo, ndivyo zilivyokuwa hata sala Zangu na zile sala za Mama asiyeweza kamwe kutengana Nami. Je wewe basi hupendi kuwa unarudia zile sala Zangu? Kwa kweli hiyo ndiyo hoja iliyonifanya nikuite wewe katika Utashi Wangu, ili wewe ushirikiane Nasi na uwe unafuata na kurudia yale matendo yetu”.

Mimi nilikuwa najitahidi , kwa kadiri nilivyoweza, kuzungukia kwa vitu vyote vilivyoumbwa ili nikampe Mungu Wangu ile fidia ya Pendo, ya Utukufu, na ya Shukrani kwa ajili ya mambo yote aliyoyatenda ndani ya Uumbwa. Katika pita pita zangu niliweza kuona, ndani ya vitu vyote, zile fidia za upendo toka kwa Mama yangu Mtawala, na zile fidia za Mpendwa wangu Yesu. Mabadilishano hayo ya upendo yalileta harmonia nzuri sana kati ya Mbingu na dunia, na yalikuwa yakiunganisha Muumba na mwanadamu. Kila fidia ya Pendo ilikuwa ni kama noti ya musiki, musiki wa sonata ndogo ya Mbinguni, musiki ambao ulikuwa unateka watu. Yesu Wangu Mtamu akaongeza kuniambia:

“Binti Yangu, vitu vyote vilivyoumbwa havikuwa ni kitu kingine bali vilikuwa ni tendo la Utashi Wetu ambao ndio uliovileta duniani na wala vitu vyenyewe haviwezi kamwe kujiondoa mahali vilipo, haviwezi kubadili matokeo ya mwenendo wao, wala mahali vilipo, na wala haviwezi kuondoa au kubadili shughuli ambayo kila kimoja wao kilipata toka kwa Muumba. Vitu hivi vyote si kitu kingine isipokuwa ni vioo ambamo binadamu alipasika kutazama na kuangalia na kustaajabu sifa mbalimbali za Muumba Wake: Hapa aone Nguvu na Uweza, pale aone Uzuri upendezao, na pale katika vitu vingine aone Wema na Ukarimu, pale aone Ukuu, na pale aone Mwanga nk.. Ni kutaka kusema kuwa kila kitu kilichoumbwa humhubiria binadamu Sifa mbalimbali za Muumba Wake, na katika sauti yao bubu vitu hivyo vinasimulia jinsi gani Muumba anavyompenda binadamu. Kumbe lakini, katika kumwumba binadamu, haikuwa ni Utashi Wetu peke yake uliotoka ndani Mwetu, bali toka ndani Mwetu palitoka pia sehemu halisi ya Sisi Wenyewe, na sehemu hiyo tuliiyeyushia ndani ya binadamu, na kwayo hiyo sehemu, tukamuumba akiwa na uhuru wa utashi. Kutokana na hiyo sehemu Yetu, aliendelea kukua daima katika uzuri, katika hekima na katika fadhila na uwezo. Kutokana na ufanano na Sisi, yeye binadamu aliweza kuzalisha na kuongeza mema yake na neema zake.

Oh, laiti lile jua moja lingejaliwa kuwa na uhuru wa utashi na laiti lingekuwa na uwezo wa kutengeneza majua mawili kutokana na lile jua moja, na kutokana na majua mawili laiti lingekuwa na uwezo wa kutengeneza yakawa majua manne! Lo, ni Utukufu ulioje na Heshima ilioje ambayo hilo jua lingetoa kwa Muumba wake? Na Utukufu mwingi ulioje lingetoa na kuelekeza kwa nafsi yake yenyewe? Lakini kumbuka kuwa, jambo ambalo vitu vilivyoumbwa haviwezi vikatekeleza, kwa hoja ya kukosa kuwa na uhuru wa utashi, na kwa hoja kwamba hivyo vyote viliumbwa kwa ajili ya kupasika kumtumikia binadamu, jambo hilo hilo huweza kulitekeleza binadamu kwani ndiye kiumbe aliyepasika kumtumikia Mungu. Ni kwa hoja hiyo Pendo Letu Sisi lilielekezwa lote ndani ya binadamu, na kwa hiyo tuliweka viumbe vyote kuwa chini yake, vyote vilipangwa kumzunguka yeye binadamu ili mradi binadamu aweze kutumia kazi Zetu mbalimbali kama ngazi nyingi tu za kupandia na kama njia nyingi tu za kupitia ili kuja kwetu hata apate kutujua na aweze kutupenda. Lakini sasa, ebu fikiria, ni masikitiko na uchungu ulioje Kwetu, tunapomwona binadamu akiwa chini kabisa ya hivyo vitu Vyetu tulivyoviumba! Yaani, ni sikitiko gani kuona ile roho nzuri na ya kupendeza aliyopewa na Sisi ikiwa sasa imeharibika kwa dhambi na kuingia katika uchafu wa kupindukia. Huoni, ni mbaya mno kwani siyo tu amekosa kabisa kukua na kuongezeka katika kutenda mema, bali huoni kwamba amegeuka kuwa ovyo, mbaya na mchafu mno hata hatazamiki? Si hivyo tu. Kana kwamba vyote vilivyoumbwa kwa ajili yake binadamu havikutosha kuonyesha Pendo Letu kwake, Sisi tulimpatia zawadi nyingine kubwa zaidi na iliyopita zawadi nyingine zote, zawadi ambayo ingeulinda huo uhuru wa utashi wake. Yaani tulimpatia Utashi Wetu Sisi, kama kitu kitakachohifadhi, kama kitu kitakachomkinga, na kama chanjo na kama msaada kwake katika uhuru wa utashi wake. Ni kwa namna hiyo Utashi Wetu ulifanya kila kitu kiwezekanacho ili kumpatia binadamu misaada yote ile aliyoweza kuhitaji. Ndivyo pia Utashi Wetu ulivyotolewa kwake kama Uhai wake wa awali na kama kitendo cha awali kabisa katika matendo ya binadamu huyo. Kwa vile alipasika aendelee kukua katika neema na katika uzuri, huyu binadamu alihitaji Utashi Mkuu ambao siyo ungeusindikiza na kuambatana na utashi wake wa kibinadamu tu, bali alihitaji Utashi Mkuu pia kwa ajili ya kuja kuwa ni mbadala wa kazi zote na matendo yote yake mwanadamu. Lakini, kwa bahati mbaya, hata zawadi hii kubwa kabisa binadamu aliidharau, aliikataa na hakutaka kuitambua na kuijua.

Unaweza kuona basi, ni jinsi gani Utashi Wetu unavyoingia katika Uhai wa awali wa mwanadamu, na wakati ule wote ambapo Utashi Wetu huo unaendelea kushika kitendo cha awali cha mwanadamu na unapoendelea kushika Uhai wake mwanadamu, huyo mwanadamu anaendelea kukua daima katika neema, katika mwanga, katika uzuri, anaendelea kuhifadhi na kutunza kile kifungo cha kitendo cha kwanza cha uumbwa wake, na Sisi huwa tunaendelea kupokea Utukufu wa vitu vyote vilivyoumbwa kwani huwa vinaendelea kuutumikia Utashi Wetu unaotenda kazi ndani ya mwanadamu, ambaye ndiye kazi na lengo maalum na la pekee kabisa la Uumbwa wote. Kwa hiyo basi, ninakuagiza na kukuhimiza wewe uhakikishe kuwa Utashi Wetu Sisi uwe kwako ni muhimu kuliko hata uhai wako, na uwe ndio tendo la kwanza kati ya matendo yako yote”.

Juzuu na. 18 ku download - click here

Kila siku, hatua kwa hatua, jisomee hapa, ili upate kukua katika Paji la Uhai, ndani ya UTASHI WA MUNGU, kulingana na Mafundisho aliyoyatoa YESU kwake Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA

Swahili - Telegram Channel: Utashi Wa Mungu Na Upendo Wa Mungu

Swahili - Telegram Channel: Saa 24 Za Mateso Ya Bwana Weto Yesu Kristo

English - Telegram Channel: Divine Will Divine Love

English - Telegram Channel: The Virgin Mary in the Kingdom of the Divine Will

Français - Chaine de Telegram: Divine Volonte Divin Amour

Français - Chaîne de Telegram: Lettres de Luisa Piccarreta

Lingala - Chaine de Telegram: Mpo Elingi Nzambe Bolingi bwa Nzambe

Website all languages: www.divinewilldivinelove.com

Vitabu yote vilivyo katika faili za PDF vinaweza kupakuliwa bila gharama yoyote ile wakati wote ule. Pia, upo huru kabisa kuchapisha VITABU hivyo wewe mwenyewe binafsi au kuchapisha kwenye kiwanda chochote kile. Lakini vitabu hivyo ni kwa matumizi binafsi tu na siyo kwa ajili ya biashara! Hata hivyo una ruhusa ya kuwashirikisha na kuwapatia watu wengine vitabu hivyo kadiri unavyopenda!!

Swahili landing page: click here

English landing page: click here

Lingala landing page: click here

Kikongo landing page: click here

French landing page: click here

Italian landing page: click here

Report Page