Yesu kwa Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - KITABU cha MBINGU - Juzuu Na. 25 - Desemba 21, 1928🖋📃📖📔

Yesu kwa Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - KITABU cha MBINGU - Juzuu Na. 25 - Desemba 21, 1928🖋📃📖📔


Novena yangu ya Noeli Takatifu inaendelea. Huku akiwa anaendelea kuonja na kusikia zile hatua tisa za Pendo la ziada la Umwilisho, Yesu Mpendwa Wangu alinivutia Kwake na kuanza kunionyesha jinsi kila hatua ya Pendo Lake la ziada lilivyokuwa ni bahari isiyokuwa na ukingo. Katika bahari hiyo, kulikuwa na mawimbi makubwa ambayo ndanimo niliweza kuwaona watu wote wakielea huku wakiwa wamemezwa na miali ile ya Pendo. Ni sawa kama vile samaki wanavyokuwa wakielea ndani ya maji ya bahari. Maji hayo huwa ndiyo uhai wa samaki, ni mwongozo wao, ni ramani yao ya majira, ni ulinzi, na kinga yao, chakula chao, kitanda chao na ikulu yao. Na huwa hivyo kiasi kwamba, ikitokea tu wanatolewa nje ya maji hayo ya bahari huwa ni lazima waseme:

uhai wetu umekwisha kwani tupo nje ya urithi wetu – yaani tupo nje ya yale makao yetu asilia tuliyokuwa tumepewa na Muumba Wetu’.

Ndivyo kadhalika haya mawimbi makuu ya miali yaliyokuwa yakipanda toka mabahari haya ya moto wa Pendo, mabahari yaliyowameza wanadamu. Mabahari ya Pendo yalitaka yawe daima ndiyo uhai wao, mwongozo wao wa majira na mwelekeo, kinga yao, chakula, kitanda, ikulu na makao asilia ya wanadamu. Lakini wanadamu hawa walipotoka tu nje ya mabahari hayo ya pendo walikabiliwa mara na kifo. Yesu Kichanga Mdogo, analia, analalamika, anaomboleza, anasali, anapiga kelele, anaguna na anahema na kutweta, kwa vile hapendi kabisa hata mtu mmoja wa hawa watu aende nje ya miali Yake hiyo inayomeza watu ndani yake. Hataki kuona yeyote wao akifa.

Oh! Laiti bahari ingekuwa na akili! Bahari hiyo, kupita zaidi ya mama mwenye moyo wa upendo, ingelia kwa uchungu sana kuomboleza samaki wake wanapotolewa nje ya maji yake na kufa, kwani bahari ingeonja inanyang’anywa bila huruma ule uhai, ambao huwa inaumiliki na kuuhifadhi kwa upendo mkubwa kabisa. Inapofikia hapo, bahari, kwa mawimbi yake makali, ingejitupa kuwamaliza wale wote waliodiriki kunyang’anya uhai wa samaki wake wengi hivi iliyokuwa ikiwamiliki, na ambao ndio utajiri wake na utukufu wake.

Yesu akaendelea kusema: “Na kama bahari haitalia, Mimi ninalia ninapoona kwamba, kwa utovu wa shukrani, wanadamu hawapendi kuuishi uhai wao ndani ya bahari Yangu ya Pendo, ingawa kama Pendo Langu hilo limekwisha kuwamezea wanadamu wote ndani Yake. Bali badala yake, wanadamu wanajirarua toka miali Yangu, wanayakimbia Makao Yangu ya asili, wanapoteza ikulu yao, wanapoteza mwongozo na dira yao, wanapoteza kinga yao, chakula chao, malazi yao na hata uhai wao. Iweje Mimi nisiweze kulia inapofikia hali hiyo? Hawa walitoka Kwangu – waliumbwa na Mimi. Hawa walikuwa wamemezwa tayari katika ile miali ya Pendo Langu, niliyokuja nayo katika tendo la kujimwilisha Mimi Mwenyewe kwa ajili ya kuwapenda wanadamu wote. Sasa ninaposikia nikisimuliwa nawe zile hatua tisa za Pendo-Kupindukia Langu, ile bahari ya Pendo Langu inavimba – kwa kweli inachemka. Inatengeneza mawimbi makuu, inaunguruma kweli, hata inamziwisha kila mtu, ili asiweze kusikia kitu chochote kingine isipokuwa wasikie tu malalamiko Yangu ya upendo, vilio Vyangu katika uchungu, machozi Yangu yanayoendelea kudondoka yakisema:

Acheni kunifanya Mimi niwe naendelea kulia zaidi, ebu basi tupeane busu la amani. Ebu tupendane na sote tufurahi – yaani, Muumba na ninyi wanadamu’ ”.

Hapo Yesu akakaa kimya, na katika dakika ile niliziona Mbingu zikifunguka. Mwonzi wa mwanga uliteremka toka juu, ukatua juu yangu, na ukawa unawaangaza wale wote waliokuwa wamenizunguka. Ndipo Yesu Mpendwa Wangu wa daima akaendelea kuniambia:

“Binti wa Utashi Wangu, huo mwonzi wa jua uliomulika ukikulenga wewe ndiyo Utashi Wangu wa Kimungu unaokuletea Uhai wa Mbinguni rohoni mwako.

Ni mzuri na wa kupendeza ilioje mwonzi huu wa jua! Siyo unakuangaza na kuleta Uhai wake kwa wewe tu, bali unaleta Uhai kwa kila mtu anayekusogelea wewe, na anayebaki kuwa karibu nawe, atakuwa anaonja huo Uhai wa mwanga; ni kwa vile, kama inavyotokea kwa jua, ndivyo mwanga wako utasambaa, na kuenea kukuzunguka, na hivyo utawapelekea wale wote wakuzungukao, lile busu la joto la mwanga, busu la pumzi yake na busu la Uhai wake.

Na Mimi, nikiwa ndani yako, ninafurahi kuona kuwa Utashi Wangu unaingia na kuenea, na unaanza kutekeleza shughuli Zake.

Ona sasa yale mabahari ya Pendo uliyokuwa unayaona. Siyo kitu kingine isipokuwa ni Utashi Wangu unaoanza kutenda kazi Yake.

Wakati Utashi Wangu unapotaka kuanza kutenda kazi, mabahari ya Pendo huvimba, huchemka, hutengeneza mawimbi yao makuu ambayo yanalia, yanalalamika, yanapiga kelele, yanasali, yanaunguruma hadi kuziwisha masikio.

Kwa upande mwingine lakini, wakati FIAT inapumzika na haitendi kazi, hapo bahari ya Pendo Langu huwa inatulia tu, inatoa mlio wa chinichini na kimya kimya, na wakati huo safari yake ya furaha na heri isiyoweza ikatengana nayo, huwa inaendelea kwa mtiririko wake kama kawaida.

Kwa hiyo, huwezi ukaijua furaha ninayoipata, heri ninayoionja, na hamu inayonifikia, ya kuangaza na ya kulitoa Neno Langu lenyewe, na kutoa Moyo Wangu wenyewe, kwa mtu yule anayejihusisha na shughuli yoyote ya kufanya Utashi wa Mungu uenee na kujulikana.

Hamu Yangu ni kubwa mno, hata ninamchukua mtu huyo na kumfungilia ndani Yangu Mimi Mwenyewe mithili ya ndani ya bahasha. Na Mimi Mwenyewe, nikifurikia nje yake, huwa najitokeza jukwaani na kuanza kuelezea juu ya Utashi Wangu unaotenda kazi katika Pendo Langu.

Hivi, je wewe, unadhani yule mtu, ambaye siku hizi, saa za jioni, huwa anazungumza hadharani juu ya hatua tisa za Pendo-Kupindukia Langu, kweli ni huyu Padre wako Mwungamishi? Hapana, mbona ni Mimi Mwenyewe, ambaye huwa natwaa moyo wake Mikononi Mwangu, na halafu namfanya awe anazungumza”.

Lakini wakati alipokuwa akiyasema hayo, ikawa ni wakati inapotolewa Baraka. Ndipo Yesu akaongeza kusema hivi:

“Binti, ninakubariki.

Kwangu Mimi, kila kitu hugeuka kuwa ni Baraka, pale ninapofikia kutekeleza kitendo Changu fulani juu ya mtu yule aliye na Utashi Wangu wa Kimungu, kama ninakubariki wewe, Baraka Yangu hiyo huwa inaiona mara ile nafasi na mahali pa kutua na kuhifadhi mema yote, na matokeo yote yanayobebwa na hiyo Baraka Yangu. Kama ninakupenda, Pendo Langu huona nafasi na mahali pa kutua na pa kuendeshea Uhai wake wa Pendo. Inaiona nafasi hiyo ndani ya ile FIAT Yangu iliyopo ndani mwako. Kwa sababu hiyo, chochote ninachotenda juu ya wewe, ndani ya wewe, na pamoja na wewe, huwa ni furaha na heri ninayoonja. Ni kwa vile ninajua kwamba, pale ndani yako, Utashi wa Mungu unayo daima nafasi na mahali pa kuweka kila kitu ninachotaka kukupatia wewe. Na tena hapo ndani yako, Utashi huo unayo pia nguvu ya kuzalisha zaidi hayo mema na mazuri ninayokupatia. Utashi huo ndani hapo ndio utendaji Wetu mkuu na ndio unaoshughulikia utengenezaji wa aina mbalimbali za Uhai kulingana na idadi ya matendo yote mengi tunayotekeleza pamoja na wanadamu ambao wanatawaliwa na Utashi huo”.

Baada ya hapo, mimi nikawa naendelea kufanya ziara yangu ndani ya FIAT kutembelea matendo yake na kazi zake. Safari hii nilikwenda kwenye nyakati za awali za Uumbwa, ili nikajiunge na vitendo vile alivyofanya Baba yetu Adamu, wakati akiwa bado hana waa lolote la dhambi. Iikuwa kwa lengo kwamba niungane naye pale, na halafu mimi niweze kuendelea tangu pale alipoachia yeye. Ndipo Yesu Wangu Mpendwa akaingia ndani mwangu na kuniambia:

“Binti Yangu, nilipokuwa namwumba binadamu nilileta ulimwengu uliokuwa unaonekana, na ambamo mtu angekuwa huru kabisa kutembea na kuangalia kazi za Muumba Wake, zilizotendeka kwa utaratibu na mpangilio mkubwa, na katika upatano na ulinganifu; zilizotendeka kwa ajili ya kumpenda mwanadamu. Katika ulimwengu huo, uliokuwa hauna watu bado, yeye mwanadamu angeweza kutenda kazi zake pia.

Kama vile nilivyokuwa nimempa ulimwengu unaoonekana usio na watu, ndivyo papo hapo nilimpatia ulimwengu usio na watu, lakini usioonekana ambao ulikuwa mzuri zaidi kuliko ule unaoonekana. Huu usioonekana ulikuwa kwa ajili ya roho yake, na katika huu usioonekana mtu angeweza naye kutengeneza kazi zake, kutengeneza jua lake, mbingu zake, na nyota zake. Kwa kujifananisha na kumuiga Muumba Wake, mtu angeweza kuujaza ulimwengu huo usioonekana, kwa kazi zake zote.

Lakini, kwa vile mtu aliteremkia chini toka kwenye Utashi Wangu akijitenga na kwenda kuishi peke yake, hapo alipoteza ufanano wake na Muumba Wake, akapoteza na kielelezo cha kutazamia na kutumia katika kurudufu kazi Zetu.

Kwa hiyo basi, twaweza kusema kuwa katika ulimwengu huo wa roho usioonekana, hakuna kitu kinachoonekana pale ndani isipokuwa tu zile nyayo za awali za binadamu. Pengine pote ni tupu kabisa. Lakini kwa vyovyote, ulimwengu huo usioonekana ni budi ujazwe. Ni kwa hoja hiyo, Mimi ninawangojea kwa upendo kwelikweli wale wanaoishi na wanaopasika kuishi ndani ya Utashi Wangu. Watu hao, kwa kuonja ndani yao uwezo utokanao na ufanano Nasi, na huku wakiwa ndani yao na vile vielelezo vya kazi Zetu, wataharikisha kujaza ulimwengu huo usioonekana, ambao kwa upendo mno nilikuwa nimeutoa wakati ule wa Uumbaji.

Lakini je unajua huo ulimwengu usioonekana ni nini hasa?

Ulimwengu huo ni Utashi Wetu.

Kama vile nilivyokuwa nimetoa mbingu na jua kwa dunia ionekanayo ya binadamu, ndivyo nilitoa Mbingu na Jua la FIAT Yangu kwa dunia isiyoonekana ya roho ya mtu huyo. Kwa sababu hiyo, ninapokuona sasa unaanza kuweka nyayo zako kufuata nyayo zile za Adamu aliyekuwa bila waa lolote, ninaweza sasa kusema: 

‘Hatimaye sasa tunaona hapa ile ombwe ya ule ulimwengu tupu uliokuwa hauonekani, ulimwengu wa Utashi Wangu wa Kimungu ambao unaanza kupata ushindi wake kwa kupata kazi za kwanza za mwanadamu’.

Basi sasa uwe makini na uendelee daima kukimbilia ndani ya Utashi Wangu wa Kimungu”.

Juzuu na. 25 ku download - click here

Kila siku, hatua kwa hatua, jisomee hapa, ili upate kukua katika Paji la Uhai, ndani ya UTASHI WA MUNGU, kulingana na Mafundisho aliyoyatoa YESU kwake Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA

Swahili - Telegram Channel: Utashi Wa Mungu Na Upendo Wa Mungu

Swahili - Telegram Channel: Saa 24 Za Mateso Ya Bwana Weto Yesu Kristo

English - Telegram Channel: Divine Will Divine Love

English - Telegram Channel: The Virgin Mary in the Kingdom of the Divine Will

Français - Chaine de Telegram: Divine Volonte Divin Amour

Français - Chaîne de Telegram: Lettres de Luisa Piccarreta

Lingala - Chaine de Telegram: Mpo Elingi Nzambe Bolingi bwa Nzambe

Website all languages: www.divinewilldivinelove.com

Vitabu yote vilivyo katika faili za PDF vinaweza kupakuliwa bila gharama yoyote ile wakati wote ule. Pia, upo huru kabisa kuchapisha VITABU hivyo wewe mwenyewe binafsi au kuchapisha kwenye kiwanda chochote kile. Lakini vitabu hivyo ni kwa matumizi binafsi tu na siyo kwa ajili ya biashara! Hata hivyo una ruhusa ya kuwashirikisha na kuwapatia watu wengine vitabu hivyo kadiri unavyopenda!!

Swahili landing page: click here

English landing page: click here

Lingala landing page: click here

Kikongo landing page: click here

French landing page: click here

Italian landing page: click here

Report Page