Yesu kwa Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - KITABU cha MBINGU - Juzuu Na. 20 - Septemba 20, 1926🖋📃📖📔

Yesu kwa Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - KITABU cha MBINGU - Juzuu Na. 20 - Septemba 20, 1926🖋📃📖📔


Kishakumaliza kuandika kitabu kimoja, na wakati nikijiandaa kuanza kuandika kingine, nikawa ninaonja ugumu wa kuendelea kuandika, huku nikiwa nimejaa masikitiko, nilitweta, na ndipo Yesu Wangu Mtamu alipoingia ndani mwangu, akajionyesha huku akiwa anatikisa kichwa Chake, na akawa akitweta huku akiniambia:

“Binti Yangu, ni nini hicho, nini hicho? Kweli hupendi kuandika?”.

Na mimi, nilishikwa na hofu karibu kutetemeka. Nilipomwona akitweta kwa sababu yangu mimi, nilisema: ‘Ewe Pendo Langu, mimi ninatamani kile unachotaka Wewe. Ni kweli kwamba ninaonja sana ugumu wa sadaka ya kuandika, hata hivyo, kwa ajili ya kukupenda Wewe, mimi nitatekeleza kila kitu’.

Na Yesu aliongeza kusema:

“Ewe Binti Yangu, wewe hujapata kuelewa vema bado maana ya kuishi ndani ya Utashi Wangu. Wakati wewe ulipokuwa umetweta, Uumbwa mzima na kila mtu, na hata Mimi Mwenyewe, tulikuwa tumetweta pamoja nawe, kwa vile, kwa wale wanaoishi ndani ya Utashi Wangu, uhai wao ni mmoja, tendo lao ni moja, ujimudu wao ni mmoja, na mwangwi wao ni mmoja. Hawana jinsi ya kufanya isipokuwa wote kutekeleza kitu kile kile pamoja kwa sababu Mungu ndiye ujimudu wao wa awali, na kwa vile, vyote vilivyoumbwa vimetokea kwenye ujimudu uliojaa uhai. Hamna kitu ambacho ndani yake hakibebi ujimudu Wake, na vyote huwa vinatembea kuuzunguka ule ujimudu wa awali wa Muumba Wao. Kwa minajili hiyo, Uumbwa mzima upo ndani ya Utashi Wangu, tendo la mzunguko wake huwa halikomi, ni la kasi sana na lenye utaratibu. Yule anayeishi ndani ya huo Utashi, naye huwa anayo nafasi yake katika mpangilio kati ya Uumbwa. Naye, pamoja na kila mtu, huwa anaendelea kuzunguka kwa kasi bila kusimama kamwe.

Binti Yangu, ule mtweto wako wa kutopenda kuandika umetengeneza mwangwi wake ndani ya kila mtu. Kwani wewe unajua kile walichokuwa wakionja ndani yao wenyewe? Ni kama vile kikosi Fulani cha nyota kingekuwa kinajiondoa toka mahali pale kilipokuwepo kati yao - yaani, kujiondoa nje ya mpangilio wa Uumbwa, nje ya ile kasi ya mbio zake za kumzunguka Muumba Wao. Na wanadamu, walipokiona hicho kikosi cha mbinguni kikiwa kama vile kinajiondoa toka kati yao, wote walitikisika kwa hofu, na wakawa wanajiona kana kwamba wanazuiliwa katika mbio zao za kuzunguka. Hata hivyo, wakawa wote wametulizwa mara kwa ule uamuzi wako wa haraka, wa kujiunga nao tena na kuendelea nao. Ndipo, kwa mpangilio, wakaweza kuendelea na mbio zao kasi za kumzunguka Muumba Wao, wakimtukuza Yeye anayewashikilia wakiwa wameshonana Naye, ili kuwawezesha kuendelea na zile mbio za kumzunguka Yeye.

Hivi wewe ungelisema nini kama ungeliiona nyota moja ikijiondoa kutoka kwa zile nyota nyingine na ikiteremkia kule chini? Je wewe usingejisemea: ‘Nyota hiyo imekwenda nje ya mahali pake, haiishi tena maisha ya jumuia na nyenzake. Ni nyota iliyopotea?’.

Hivyo ndivyo Yule anayeishi ndani ya Utashi Wangu alivyokuwa anataka kutenda mambo yake mwenyewe. Anajiondoa toka mahali pake. Anajidondosha toka kwenye kilele cha zile Mbingu. Anapoteza ushirika wa Familia ya Mbinguni. Anapotea kabisa, mbali na Utashi Wangu. Anapotea mbali kutoka kwenye mwanga, mbali na nguvu, mbali na utakatifu, mbali na ule ufanano wa kimungu. Anapotea mbali na mpangilio, mbali na harmonia, na hata anapoteza ile kasi ya mbio zake za kumzunguka Muumba Wake.

Kwa hiyo basi, uwe makini, kwa vile, katika Ufalme wa Utashi Wangu, hakuna suala la kutopenda au la machungu na masikitiko, bali pale kila kitu ni furaha tu. Katika Ufalme wa Utashi Wangu hamna mambo ya kulazimishana, bali pale kila kitu ni hiari tupu, kana kwamba mwanadamu angetamani kutenda kile tu anachotaka kutenda Mungu - kana kwamba yeye mwenyewe angependelea kutenda jambo hilo”.

Mimi nilitishika nilipokuwa ninayasikia hayo kutoka kwa Yesu Wangu Mtamu, na pale niliweza kuelewa ubaya mkubwa wa kutekeleza utashi wa mtu binafsi. Hapo nilimwomba Yeye, kutoka moyoni mwake, anipatie neema nyingi hivi hata nisiweze kuanguka katika kosa kubwa kama hilo. Lakini, pindi nikitenda hilo, yule Chema Changu Mpenzi, alikuja kwangu tena. Hata hivyo alijionyesha akiwa na viungo Vyake vyote vya mwili, vikiwa legelege kabisa, na kwa hiyo alikuwa akipata maumivu makali sana yasiyoelezeka. Alijitupa mikononi mwangu na kuniambia:

“Binti Yangu, hivi viungo Vyangu vya mwili vilivyolegea, vinavyoniletea maumivu makali mno, ni watu wale wote ambao hawatekelezi Utashi Wangu.

Kwa kuja Kwangu hapa duniani, nilijiweka Mwenyewe kuwa kichwa cha familia ya binadamu, na wao wamekuwa ni viungo vya mwili Wangu. Lakini, kwa njia ya hulka mbalimbali za uhai za Utashi Wangu, viungo hivi vyote vilikuwa vimeundwa, vimeunganishwa, na vikafungamanishwa pamoja. Na kadiri Utashi Wangu unavyotiririkia ndani yao hao binadamu, basi wao wanaingizwa katika mawasiliano na mwili Wangu, na wanaimarishwa kila mmoja awe, na abaki, mahali pake. Halafu, Utashi Wangu, mithili ya daktari tibabu mwenye huruma, siyo tu, huwa unatiririshia ndani yao zile hulka zake, zenye uhai na zilizo za kimungu, kwa ajili ya kuleta ule mzunguko wa lazima kati ya kichwa na viungo vyake vingine, bali huwa pia unaandaa bendeji za kuwafungilia binadamu, kikamilifu kabisa, kuhakikisha kuwa, kama viungo wawe wamebaki wamefungamana kithabiti kabisa kwenye kichwa chao. Lakini sasa, kwa kukosekana Utashi Wangu ndani ya hao binadamu, panakosekana kile ambacho ndicho budi kiwaletee joto, kiwaletee damu, na budi kiwaletee na nguvu. Panakosekana kile ambacho, kutoka kwenye kichwa, huwa kinawaletea amrisho linalowafanya waanze utendaji wao mbalimbali. Panakosekana kile ambacho huwa kinatoa huduma ya kuwafunga kwa bendeji thabiti wakati wanapolegea au wanapong’oka – kwa kweli panakosekana kila jambo.  Tunaweza tukasema, kwamba, mawasiliano yote kati ya viungo na kichwa chao yanakuwa yamekatika. Viungo hivyo hubaki mwilini Mwangu kwa ajili ya kuniletea Mimi maumivu tu.

Ni Utashi Wangu peke yake, ndio ambao, huwa unaleta uelewano na mahusiano kati ya Muumba na mwanadamu, kati ya Mkombozi na wakombolewa, kati ya Mtakasa na watakaswa. Bila Utashi Wangu, hali huwa kana kwamba Uumbaji na Ukombozi vilikuwa si kitu kabisa kwa wanadamu, kwa vile, kinakosekana kile ambacho huwa kinaleta na kutiririsha uhai na yale mema mbalimbali yanayobebwa ndani ya kazi hizo za Uumbaji na za Ukombozi. Hata Sakramenti zenyewe zitageuka kuwa laana kwao, kwa vile, kwa kukosekana Utashi Wangu ndani ya wanadamu, patakuwa panakosekana kile ambacho ndicho huwa kinalipasua lile pazia la Sakramenti mbalimbali, ili kuwaletea lile tunda, na ule uhai uliopo ndani ya Sakramenti husika. Kwa hiyo, Utashi Wangu ni kila kitu.

Bila Utashi Wangu, zile kazi Zetu nzuri kabisa na zipendezazo, na hata yale matendo Yetu makuu kabisa, vitabaki kama mambo ya nje nje tu kwa masikini wanadamu. Ni kwa vile, ni Utashi Wangu peke yake, ndio unaokuwa ni hifadhi ya kazi Zetu zote, na kwa hiyo, ni kwa njia ya Utashi Wangu peke yake, kazi hizo zaweza kuzalishwa kwa ajili ya wanadamu.

Oh! Kama watu wote wangetambua maana ya kutekeleza au kutotekeleza Utashi Wangu, ni wazi, wote wangekuwa wanakubaliana na huo Utashi Wangu, ili kusudi, wawe wanayapokea yale mema yote yanayowezekana na yanayofikiriwa, na ili wawe wanapokea ule mmiminisho wa ule Uhai wenyewe wa Kimungu”.

Halafu, baada ya hayo, mimi nikawa naendelea kutekeleza matendo yangu ya siku zote ndani ya Utashi Mkuu wa Juu, na kwa vile siku ilikaribia kupambazuka, nikawa ninasema:

‘Ewe Yesu Wangu, Pendo Langu, sasa siku inaanza, na mimi, ndani ya Utashi Wako, ninanuia kuanza ziara ya kuwatembelea wanadamu wote, ili kusudi, wanapoamka kutoka usingizini, wote wazindukie ndani ya Utashi Wako, na hivyo waweze kukutolea Wewe uabudu wa akili zote, wakutolee upendo wa mioyo yote, na wakutolee Wewe pambazuko la kazi zao zote na pambazuko la nafsi zao zote litakalopambazukia ndani ya mwanga ambao siku hii ya leo itaangazishia juu ya vizazi vyote vya binadamu’. 

Mimi nilipokuwa nikisema hilo na mengineyo, Yesu Wangu Mtamu aliingia ndani mwangu na kuniambia:

“Binti Yangu, katika Utashi Wangu hazipo siku wala usiku, hayapo mapambazuko wala machweo, ila kuna kitu kimoja peke yake, ndiyo siku yake - yaani Utashi Wangu upo daima katika ujazo wote wa mwanga wake.

Na yule anayeishi ndani yake huweza akasema: ‘Hapa hakuna usiku kwangu mimi, bali hapa kwangu ni mchana daima. Kwa hiyo, kwangu ni kitu kimoja tu, yaani, ni mchana wangu’. Na kadiri anavyotenda kwa ajili ya kutekeleza Utashi Wangu na kwa ajili ya kuendesha maisha yake ndani ya Utashi Wangu, huyo mtu huwa anazidi kutengeneza mianga mingi ya ziada, mianga inayoangaza mno, anaitengeneza katika mchana wa uhai wake. Na mianga hiyo ing’aayo, huwa inaifanya siku ya Utashi Wangu, wanamoishi watu hao, iwe tukufu, nzuri na ipendezayo zaidi. Kwani wewe, unajua, mchana na usiku, mapambazuko na machweo, huwa yametengenezwa kwa ajili ya nani? Ni kwa ajili ya yule ambaye, sasa huwa anatekeleza Utashi Wangu, na punde tu baadaye, anatekeleza utashi wake. Pale anapotekeleza Utashi Wangu, hapo anatengeneza mchana. Pale anapotekeleza utashi wake mwenyewe, hapo anatengeneza usiku. Yule anayeishi kikamilifu ndani ya Utashi Wangu, huyo anatengeneza ujazo wa mchana kutwa. Yule asiyeishi kikamilifu ndani yake, bali anautekeleza Utashi Wangu kwa taabu taabu tu, huyo anatengeneza mapambazuko. Na yule anayenung’unika na kulalamika juu ya yale yanayoandaliwa na kuletwa na Utashi Wangu, na hivyo anayetaka kujiondoa toka kwenye Utashi Wangu, huyo huwa anatengeneza machweo. Na kwa yule ambaye hatekelezi kamwe Utashi Wangu, kwake huyo huwa ni usiku daima na kwa kudumu - huo ndio ule mwanzo wa ule usiku wa milele unaoletwa na moto wa milele, na ndio usiku usiokoma kamwe”.

Juzuu na. 20 ku download - click here

Kila siku, hatua kwa hatua, jisomee hapa, ili upate kukua katika Paji la Uhai, ndani ya UTASHI WA MUNGU, kulingana na Mafundisho aliyoyatoa YESU kwake Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA

Swahili - Telegram Channel: Utashi Wa Mungu Na Upendo Wa Mungu

Swahili - Telegram Channel: Saa 24 Za Mateso Ya Bwana Weto Yesu Kristo

English - Telegram Channel: Divine Will Divine Love

English - Telegram Channel: The Virgin Mary in the Kingdom of the Divine Will

Français - Chaine de Telegram: Divine Volonte Divin Amour

Français - Chaîne de Telegram: Lettres de Luisa Piccarreta

Lingala - Chaine de Telegram: Mpo Elingi Nzambe Bolingi bwa Nzambe

Website all languages: www.divinewilldivinelove.com

Vitabu yote vilivyo katika faili za PDF vinaweza kupakuliwa bila gharama yoyote ile wakati wote ule. Pia, upo huru kabisa kuchapisha VITABU hivyo wewe mwenyewe binafsi au kuchapisha kwenye kiwanda chochote kile. Lakini vitabu hivyo ni kwa matumizi binafsi tu na siyo kwa ajili ya biashara! Hata hivyo una ruhusa ya kuwashirikisha na kuwapatia watu wengine vitabu hivyo kadiri unavyopenda!!

Swahili landing page: click here

English landing page: click here

Lingala landing page: click here

Kikongo landing page: click here

French landing page: click here

Italian landing page: click here

Report Page