Yesu kwa Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - KITABU cha MBINGU - Juzuu Na. 20 - Januari 1, 1927🖋📃📖📔

Yesu kwa Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - KITABU cha MBINGU - Juzuu Na. 20 - Januari 1, 1927🖋📃📖📔


Nikawa ninatafakari juu ya mwaka uliokuwa unakwisha na juu ya mwaka mpya uliokuwa unazaliwa.

 Hali yangu inaendelea ndani ya mruko wa mwanga wa Utashi wa Mungu na nikawa ninamwomba yule Mtoto mzuri kabisa kwamba, kama vile mwaka uliopita ulivyokuwa unakufa bila uwezekano wa kuzaliwa tena, ndivyo ajalie utashi wangu ufe bila kuwepo uwezekano kwa utashi huo kuishi tena. Na kama zawadi kwa mwaka mpya, Yeye anipatie Utashi Wake kama mimi nilivyokuwa nikimpatia Yeye zawadi ya utashi wangu ili nikauweke kama kikanyagio cha tumiguu twake tule tudogo na laini, ili kusudi, utashi wangu huo usiwe tena na uhai mwingine isipokuwa ule Utashi wa Kwake. Sasa, pindi nikiyazungumza hayo na mengineyo, Yesu Wangu Mtamu alikuja toka pale ndani mwangu na akaniambia:

 “Ewe Binti wa Utashi Wangu, ni jinsi gani ninavyopenda, ninavyotaka, na ninavyochuchumia kwamba utashi wako ukomeshwe ndani yako! Oh! Ni jinsi gani ninavyoipokea hiyo zawadi yako, ni jinsi gani itakavyonifurahisha Mimi kuuweka huo utashi wako kama kikanyagio laini cha miguu Yangu! Ni kwa vile utashi wa kibinadamu, unapokuwa bado ndani ya mwanadamu, yaani, nje ya makao yake makuu, ambayo ni Mungu, huwa ni mgumu sana, lakini kumbe, wakati utashi huo unapoingia ndani ya makao yake makuu ambako ulitokea na wakati unapotumika kama kikanyagio cha miguu ya Mtoto Yesu Wake, hapo utashi huo huwa unakuwa laini na huwa unasaidia kunituliza na kuniburudisha Mimi. Kwani si vema na haki kwamba Mimi, ninapokuwa bado mdogo niwe ninapata burudani? Tena, je, si vema Mimi, katika maumivu hayo mengi sana, na ninapokuwa ninakosa mambo mengi hivyo, na katika machozi mengi hivyo, niwe ninashikilia huo utashi wako ili uwe unanichekesha ninapouchezea? Basi sasa, ni vema ujue kwamba yule anayeukomesha utashi wake, huyo huwa anarejea kwenye chanzo chake alikokuwa ametokea, na ndani yake, huanza uhai mpya, yaani, uhai wa mwanga, na uhai wa kudumu daima wa Utashi Wangu.

Ebu angalia, Mimi nilipokuwa ninakuja duniani, nilikuwa nimependa kutoa mifano mingi na vielelezo vingi. Kwa vile nilitaka kwamba utashi wa kibinadamu ufikie kukoma, nikawa nimependa nizaliwe usiku wa manane saa sita usiku, kwa ajili ya kutenganisha usiku wa utashi wa kibinadamu kutoka ule mchana angavu wa Utashi Wangu. Na licha kwamba ulikuwa ni usiku wa manane, usiku unaoendelea bila kumalizika, hata hivyo, lakini, usiku ule ukawa ni mwanzo wa siku mpya. Na wale Malaika Wangu, walitoa heshima juu ya kuzaliwa Kwangu, na waliwajulisha watu wote juu ya ile siku ya Utashi Wangu. Na tangu ile saa sita ya usiku na kuendelea, Malaika wakawa wanashangilia, na katika dari ya zile anga mbalimbali, nyota mpya, na majua mapya, vikawa navyo vinashangilia, kiasi cha kuugeza ule usiku kuwa zaidi ya mchana: ilikuwa ni heshima kuu ambayo Malaika walikuwa wakiitoa kwa ule Ubinadamu Wangu mdogo, ambamo hukaa ile siku timilifu ya lile Jua la Utashi Wangu wa Kimungu, na ambamo hukaa ule wito mpya wa mwanadamu kuja ndani ya siku timilifu ya huo Utashi Wangu. 

Nikiwa bado kadogo sana, nilijitoa kwa hiari Yangu kulikabili lile donda kali kabisa la kukatwa wakati wa kutahiriwa, donda ambalo, kutokana na maumivu makali, lilinifanya nimwage machozi ya uchungu mkali. Na siyo Mimi tu, bali, pamoja Nami, wakawa wanalia machozi Mama Yangu na hata yule mpenzi Mtakatifu Yosefu: hilo lilikuwa ni donda nililotaka Mimi liwe ni kwa ajili ya kukatia mbali utashi wa kibinadamu. Nilitaka wanadamu watitirishie Utashi wa Mungu ndani ya donda hilo la kukatwa, ili kusudi, utashi uliokwisha kukatwa usije kupata tena uhai, bali, Utashi Wangu peke yake, niliokuwa nimeuingiza ndani ya donda hilo, ndio huo uanze kuwa na uhai wake. 

Aidha, nikiwa bado kadogo sana, nikawa nimependa kutorokea Misri: ni kutokana na utashi wa kikatili, utashi mchafu, ndio uliotaka kuniua Mimi, picha mfano ya utashi wa kibinadamu uliotafuta kuuua ule Utashi wa Kwangu, na Mimi nilitoroka ili kuonyesha kwamba: ‘Ebu torokeni huo utashi wa kibinadamu kama ninyi hamtaki Utashi Wangu uuawe’. Maisha Yangu yote yamekuwa siyo kitu kingine isipokuwa ni mwito wa Utashi wa Mungu ndani ya utashi wa kibinadamu. Pale Misri nilikuwa nikiishi kama mgeni kati ya watu wale, ambao, ni picha mfano ya Utashi Wangu ambao binadamu huwa wanaushikilia kama mgeni tu kati yao, na pia ni picha mfano kwamba yule anayetaka kuishi kwa amani na ameunganika na Utashi Wangu, ni budi awe anaishi kama mgeni wa utashi wa kibinadamu. Vinginevyo patatokea daima vita kati ya tashi hizo mbili kwa vile, hizo mbili huwa hazipatanishiki.

Baada ya siku hizo za uhamishoni, nilirejea tena kwenye nchi Yangu, ikiwa ni picha mfano ya Utashi Wangu ambao baada ya kipindi chake kirefu cha kukaa uhamishoni kwa karne na karne utakuja kurejea kwenye nchi yake pendwa, kati ya watoto wake, kwa ajili ya kuweza kutawala, Na Mimi nilipokuwa nikipitia hatua hizo katika uhai Wangu, ndivyo nilikuwa nikiujenga Ufalme wake ndani Yangu, na, kwa sala zisizokoma, kwa maumivu, na kwa machozi, nilikuwa nikiuita Utashi Wangu ufike kuja kutawala kati ya wanadamu.

Nilirejea katika nchi Yangu, na pale niliishi katika kificho na bila kujulikana. Oh! Ni jinsi gani inavyokuwa ni picha mfano ya maumivu ya Utashi Wangu, ambao, wakati unaishi kati ya mataifa, huwa unaishi kifichoni na bila kujulikana. Na Mimi, kwa njia ya kificho changu, nilikuwa nikiita na kuomboleza kwamba Utashi Mkuu wa Juu uweze kujulikana, ili hatimaye uweze kupokea ile heshima kuu na ule utukufu wake stahiki. Hakuna chochote kilichotendeka na Mimi ambacho hakikuwa ni picha mfano ya maumivu ya Utashi Wangu, kilichokuwa picha mfano ya yale mazingira ambamo wanadamu wanauingiza Utashi Wangu, na kilichokuwa picha mfano ya mwito mpya niliokuwa nikiutoa kwa ajili ya kuwarejeshea hao wanadamu ule Ufalme wa Utashi Wangu. Na hayo ndiyo nataka yawe ni maisha ya wewe pia: kuwa mwito endelevu wa Ufalme wa Utashi Wangu kati ya wanadamu”.

Kishapo, mimi niliendelea na ziara ya kuzungukia Uumbwa mzima, ili, pamoja nami mwenyewe, niweze kupeleka ile anga, zile nyota mbalimbali, lile jua, ule mwezi, ile bahari, yaani, kwa kifupi, niweze kupeleka mambo yote mbele ya miguu ya Mtoto Yesu, kwa ajili ya kumwomba, sote kwa pamoja, kwamba, ujio wa huo Ufalme wa Utashi Wake hapa duniani, ufike haraka, na hapo, katika tamaa yangu nikawa ninamwambia:

‘Tafadhali angalia, siyo mimi peke yangu ndiye nikuombaye, bali anga linakuomba Wewe kwa sauti za nyota zote zilizopo, na jua linakuomba kwa sauti ya mwanga wake, na kwa sauti ya joto lake, na bahari pia inakuomba kwa sauti yake ile ya kunung’unika. Vitu vyote vinakuomba kwamba Utashi Wako ufike hapa duniani. Utawezaje kukataa hata usisikilize hizo sauti nyingi zinazokuomba Wewe? Hizo zote ni sauti bila waa lolote, ni sauti zilizorohoishwa na wenyewe Utashi Wako ambao wanauomba’. Basi, nilipokuwa nikiyazungumza hayo, yule Yesu Wangu Mdogo, alijitokeza toka ndani mwangu kuja kupokea ile heshima kuu ya Uumbwa mzima na kuja kusikia ile lugha yao ya ububu, na huku akinikumbatia na kunibania kwake kwa nguvu aliniambia:

“Binti Yangu, njia iliyo rahisi kabisa ya kuharakisha ujio wa Utashi Wangu hapa duniani ni yale maarifa juu yake. Hayo maarifa yanaleta mwanga na joto na yanatengeneza ndani ya wanadamu lile Tendo la kwanza la Mungu ambamo mwanadamu atalikuta tendo la kwanza litakalosaidia kurekebisha tendo la kwake. Kama mwanadamu hatalipata hilo Tendo la kwanza la Mungu, huyo mwanadamu hataweza kuwa na nguvu ya kutengeneza tendo lake la kwanza, na hivyo atakosa kuwa na matendo, yaani, yale mambo yenye ulazima kabisa kwa ajili ya kujenga huo Ufalme. Ebu ona sasa nini maana ya kupata ujuzi mmoja wa ziada juu ya Utashi Wangu: kwa vile maarifa juu ya Utashi Wangu yanalileta lile Tendo la kwanza la Mungu, ndiyo hayo yataleta ndani yao ile nguvu ya sumaku, yaani sumaku kali kabisa yenye maweza ya kuwavuta wanadamu wawe wanaweza kurudiarudia kutenda lile Tendo la kwanza la Mungu, na, hilo Tendo, kwa nguvu ya mwanga wake, litaondolea mbali ule udanganyifu wa utashi wa kibinadamu, na kwa joto lake, sumaku hiyo itailainisha mioyo ile migumu kabisa, hata iweze kubadilika mbele ya matendo hayo ya kimungu. Na ndipo wanadamu wataonja kule kutekwa kwa ajili ya kupenda kujirekebisha na kujilinganisha na hilo tendo. Kwa sababu hiyo, jinsi ninavyozidi kuonyesha na kuelezea maarifa juu ya Utashi Wangu, ndivyo unavyozidi kuharakishwa ujio wa Ufalme wa FIAT ya Kimungu duniani”.  

Juzuu na. 20 ku download - click here

Kila siku, hatua kwa hatua, jisomee hapa, ili upate kukua katika Paji la Uhai, ndani ya UTASHI WA MUNGU, kulingana na Mafundisho aliyoyatoa YESU kwake Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA

Swahili - Telegram Channel: Utashi Wa Mungu Na Upendo Wa Mungu

Swahili - Telegram Channel: Saa 24 Za Mateso Ya Bwana Weto Yesu Kristo

English - Telegram Channel: Divine Will Divine Love

English - Telegram Channel: The Virgin Mary in the Kingdom of the Divine Will

Français - Chaine de Telegram: Divine Volonte Divin Amour

Français - Chaîne de Telegram: Lettres de Luisa Piccarreta

Lingala - Chaine de Telegram: Mpo Elingi Nzambe Bolingi bwa Nzambe

Website all languages: www.divinewilldivinelove.com

Vitabu yote vilivyo katika faili za PDF vinaweza kupakuliwa bila gharama yoyote ile wakati wote ule. Pia, upo huru kabisa kuchapisha VITABU hivyo wewe mwenyewe binafsi au kuchapisha kwenye kiwanda chochote kile. Lakini vitabu hivyo ni kwa matumizi binafsi tu na siyo kwa ajili ya biashara! Hata hivyo una ruhusa ya kuwashirikisha na kuwapatia watu wengine vitabu hivyo kadiri unavyopenda!!

Swahili landing page: click here

English landing page: click here

Lingala landing page: click here

Kikongo landing page: click here

French landing page: click here

Italian landing page: click here

Report Page