Yesu kwa Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - KITABU cha MBINGU - Juzuu Na. 20 - Februari 13, 1927🖋📄📖📔

Yesu kwa Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - KITABU cha MBINGU - Juzuu Na. 20 - Februari 13, 1927🖋📄📖📔


Nilikuwa nikiendelea kufuatilia Utashi wa Mungu katika matendo yake ya Uumbwa, na ndipo likaja shaka fulani kichwani mwangu: ‘Hivi inakuwaje kwamba Yesu anasema eti kama Ufalme wa Utashi Wake utakuwa haujafika hapa duniani, basi utukufu wa Uumbwa, na ule wa Ukombozi utakuwa haujatimilika bado? Inakuwaje hivyo? Kwani huo Utashi Mkuu wa Juu hauna nguvu ya kujitukuza kwa uwezo wake wenyewe? Ni hakika kwamba unayo hiyo nguvu na pia kwamba nguvu hiyo ni zaidi ya ile itakiwayo kwa utukufu wake. Halafu Yesu anasema pia kwamba, kama Utashi Wake hautaeneza na kupanua Ufalme wake kati ya wanadamu, utukufu wake, unaohusu Uumbwa utakuwa haujatimilika’. Sasa, pindi nikiwa nawaza hivyo, Yesu Wangu Mwabudiwa, huku akinishitua kwa mwanga wenye nguvu mno uliokuwa unatokea Kwake, akawa ameniambia:

“Binti Yangu, jambo ambalo kwa lenyewe ni wazi kabisa ni hili kwamba, kama Utashi Wangu hautafahamika, na kama utakuwa haujapata nafasi yake ya kwanza ya heshima na ya himaya ndani ya kila kiumbe kilichotoka katika mikono Yetu umbaji, utukufu wake utakuwa daima siyo timilifu. Hoja yake ni wazi kabisa, ni kwamba, katika Uumbwa, lengo Letu la kwanza lilikuwa ni kwamba, huu Utashi Mkuu wa Juu, unapotokea Kwetu, na kwa tendo letu la kuuweka ndani ya Uumbwa wote kwa wakati ule ule, ukawa unaenea popote pale, iwe angani, iwe ndani ya jua, ndani ya bahari, ndani ya ua, ndani ya mimea, na hata ndani ya ardhi na ndani ya kila kiumbe kilichotokea kwenye mikono Yetu umbaji, na pale, Utashi Wetu ulijiweka kuwa uhai wa kila kitu kwa ajili ya kutengeneza uhai wake ndani ya kila kiumbe. Na kwa kujiingiza wenyewe ndani ya kila mwanadamu, uliweza, kwa jinsi hiyo, kuwa na aina nyingi za uhai wake na pia kuwa na himaya nyingi za kutawala na kuamrisha, himaya kadiri ya idadi ya wanadamu waliokuwa wakijitokeza duniani.

Mpaka sasa, Utashi Wangu haujajiondoa kurudi nyuma, yaani, hakuna kona ambako haujaeneza Uhai wake wa Kimungu, na hakuna mwanadamu ambaye hajafunikwa na huo Utashi Mkuu wa Juu. Na pindi unapokuwa umeenea popote pale, na pindi unapofunika kila kitu na kila mtu, hauwezi sasa hivi kutengeneza uhai wa kwake wenyewe. Ni uhai wa kimungu mwingi ilioje unaokabwa na kuzuiwa ndani ya hawa wanadamu! Ni wanadamu wengi wangapi wanaougomea kuupatia nafasi ya kwanza katika matendo yao! Ni wengi wangapi wanaoahirisha na kuupatia nafasi ya nyuma kabisa huku wakitanguliza kutoa nafasi kwa matendo yasiyostahilika na machafu, huku wakiugomea Utashi Wangu kuruhusiwa kusimika himaya yake! Je, kwako wewe, unaona ni kitu kidogo huo uharibifu na uvunjifu wa hizo aina nyingi kabisa za Uhai wa Kimungu wa Utashi Wangu ndani ya wanadamu? Huo uharibifu wa matendo yake mengi yaliyo adhimu na matukufu kabisa, uharibifu unaoweza kuonjeka ukiendelezwa daima wakati hao wanadamu wanautumia bado Utashi Wangu, wanauvunja na kuuharibu, eti, kwa ajili ya kutengenezea uhai wao mbalimbali wa kibinadamu, uhai ovyo na wa kutisha ajabu, ukiwa ni madudu yatakayofaa kwa kuwatupa motoni mwa milele? Na je, ni neno dogo hilo kwako, ewe Binti Yangu? Athari au hasara ambayo utukufu Wetu unaipata kutokana na Uumbwa ni kubwa na haiwezi kukadiriwa, kwa jinsi kwamba, hata mema yale na manufaa yote yaliyotokana na Ukombozi hayakuweza kutulipa fidia, kwani, hata kwa huo huo Ukombozi, binadamu hajaweza bado kurejea katika ule umoja wa Utashi Wetu, na wala Utashi Wetu haujafikia kutawala kitimilifu kabisa ndani ya wanadamu. Ni uhai wa aina nyingi ilioje ambao eti husemekana kuwa ni mzuri na mtakatifu, wakati aina hizo za uhai zimegawanyikagawanyika kati ya Utashi wa Mungu na utashi wa binadamu! Kwa minajili hiyo, utukufu Wetu, ndani ya Uumbwa, bado haujatimilika. Hapo baadaye, utakuja kutimilika wakati vitu vilivyoumbwa Nasi vitakapotumikia Utashi Wetu ule ule, na vitakapowatumikia wale ambao watatoa nafasi ya kwanza ya heshima kwa Utashi huo, wakiwa ni wale watakaoufahamu na kuutambua na kuukiri pale ndani ya vitu vyote, na wale watakaoufanya Utashi utawale katika matendo yao yote, na watakaousimika Utashi kama Malkia Mkuu kabisa na Mfalme anayetawala na kuamrisha. Je, wewe huoni kama ni vema na haki kabisa, kwamba, kila kitu kije kuwa ni cha Utashi Wangu, na Utashi Wangu uje kuwapo popote pale, na uwe ni kwa ajili ya watu wote, na papo hapo uje kuwa ni uhai wa kwanza wa kila kitu, watu wote waje kuutambua na kuukiri, na watu wote wafikie kubadilika na kuwa ni Utashi wa Mungu, na waje wote kuwa ni mali yake?

Ebu jaribu kumfikiria mfalme fulani ambaye anao ufalme wake: tujali ardhi zote ni zake, maeneo yote ya starehe, ya burudani na ya mapumziko ni yake, na miji yote ikawa ni mali yake pekee, na pasiwepo na chochoe ambacho yeye hamiliki, na wala siyo tu kwamba ufalme ni wake kwa haki kabisa, bali kwamba mambo yote hayo ni yake kwa haki ya hati miliki kabisa. Na tujali mfalme huyo, kwa ule ukarimu wake mkuu alio nao, anapenda kuwaona raia wake wakiwa na furaha, na huyo, bure kabisa, akagawa kwa watu wake, yale mashamba yake, zile nyumba zake za burudani na za starehe, anagawa ardhi zake, anawagawia watu wake hata yale makazi ya miji yake, ili mradi watu wake waweze kujipatia utajiri, wawe na mali teletele, kila mmoja wao kadiri ya hali zake. Na hilo jema kuu analotenda kwa watu wake likiwa na lengo moja pekee, kwamba wamjue na kumtambua na kumkiri kuwa ni Mfalme wao, na wampatie mamlaka kamili kabisa, na pia wakiri kwamba zile ardhi ambamo sasa wanakaa zimetolewa kwao bure kabisa na yeye mfalme, ili hatimaye, yeye mfalme aweze kutukuzwa, ajulikane na kutambulikana, na apendwe nao kutokana na lile jema alilowatendea. Sasa tujali watu hao, katika utovu wao wa shukrani, wakawa hawamtambui na kumkiri kama mfalme wao, na zile ardhi wanazozimiliki, eti wanaanza kubadilishana zile hati miliki kati yao jinsi wanavyotaka wao wakisahau kwamba zilikuwa ni zawadi walizokuwa wamepewa na mfalme. Je, huyo mfalme, katika utukufu wake, hatakuwa amenyang’anywa na kuporwa lile jema alilokuwa amewatendea hawa watu wake? Halafu ebu jaribu kuongeza, iwapo watu wale hawazitumii zile ardhi kwa manufaa yoyote yale: wako wale wasiozitumia kabisa, wako wale wanaong’oa yale mazao yote yaliyokuwemo, na wale wanaozichafua na kuziharibu zile bustani zake za fahari kiasi cha kuwaletea wao wenyewe adha zao na ufukara wao. Hayo yote yangezidi kuongeza ile athari na hasara kwa utukufu wa yule mfalme. Yangeongeza madhalilisho na uchungu ambao hakuna mtu ambaye ataweza kuja kuuponya.

Hilo si kitu kingine isipokuwa ni kivuli tu cha kile ambacho Utashi Wangu Mkuu wa Juu umetenda na unatoa mpaka hivi sasa. Hakuna mtu aliyetulipa hata senti moja kwa kupokea yale manufaa ya jua, ya bahari, ya ardhi, ingawa kama tumekuwa tukiyatoa yote hayo bure kabisa bila kudai malipo yoyote. Yote hayo ni kwa ajili ya kumfurahisha tu, na ili kusudi, wafikie kuijua na kuitambua ile FIAT Yangu Kuu ya Juu ambayo imekuwa ikiwapenda kabisa, na yenyewe haitafuti kitu kingine isipokuwa pendo na himaya. Sasa, ni nani atakayeweza kumlipa fidia yule mfalme kwa ile hasara na athari ya utukufu ambao wale watu wake hawakumpatia kabisa, na ni nani huyo atakayeweza kupoza yale maumivu yake makali? Ebu jaribu kufikiria bado kwamba, mmoja kati ya watu wake wale wale, akishikwa na ule uchungu halisi wa mfalme wake, na kwa kutaka kumlipa deni la ule utukufu wake, angeanza kwanza kwa kutengeneza upya ile ardhi anapokaa, kwa jinsi kwamba anafanya iwe ni bustani nzuri ya fahari kabisa katika ule ufalme, halafu huyo awaeleze watu wote kuwa hiyo bustani yake ni zawadi aliyokuwa ameitoa mfalme kwake kwa vile anampenda; halafu tujali mtu huyo anamwalika mfalme kuja kutembelea ile bustani yake na pale anamwambia: ‘Hizo zote ni himaya zako. Ni vema na haki kwamba ziwe kwa ajili ya matumizi yako’. Hapo yule mfalme anafurahia sana huo utiifu na uaminifu, na ndipo anasema: ‘Mimi ninakutaka wewe uwe sasa mfalme pamoja nami, njoo tuwe tunatawala pamoja’. Oh! Ni jinsi gani atakavyoona utukufu ukimrejea juu yake, ni jinsi gani atakavyoona maumivu yake yakipozwa na huyo mtu mmoja, huyo ni mmoja wa watu wake! Halafu tujali mtu huyo hakomi hapo. Anaanza kupita katika njia na barabara zote za ufalme, anawatikisa na kuwaamsha watu wote kwa maneno yake, anawaita kikundi maalum cha watu pekee, anawaalika wamwunge mkono na kumwiga yeye, na kutoka hao anaunda kundi la watu waaminifu wampendao mfalme, na hao wanampa yule mfalme wao haki ya kuwa na himaya. Ndipo mfalme anajiona amelipwa fidia na amerejeshewa hadhi yake katika utukufu wake. Na ili kuwaenzi, anawapatia hao watu kile cheo cha kuitwa watoto wake na anawaambia: ‘Huu ufalme wangu sasa ni wenu. Hebu mtawale ninyi watoto wangu! Hilo ndilo lengo Langu Mimi: Kwamba katika ufalme Wangu pasiwepo watumishi au watumwa bali wawepo watoto na wafalme wanaolingana na Mimi’. Ndivyo hivyo itakuwa kwa Utashi Wangu wa Kimungu. Oh! Ni jinsi gani Utashi Wangu unavyongojea utukufu wake timilifu urejeshwe pale ndani ya Uumbwa, na kwamba, itambulikane kwamba kila kitu ni cha kwake, hata uweze kusema: ‘kila kitu ni chenu, ebu tutawale sote pamoja’. Ni jinsi gani Utashi Wangu unavyosubiri yale maarifa yake kuhusu FIAT Kuu ya Juu yapite kutembea katika zile njia na barabara kwa ajili ya kuwatikisa, kuwaamsha na kuwaita na hata kuwasukuma wanadamu wafike kuingia ndani ya Ufalme Wangu. Na jinsi gani Utashi Wangu unavyoniundia watoto Wangu halisi, ambao nitaweza kuwapatia cheo cha kuwa wafalme! Ni kwa sababu hiyo ni hamu Yangu kubwa kwamba haya maarifa juu ya Utashi Wangu wa Kimungu yajulikane. Ni kwa sababu yanahusu lile tendo Langu Kuu kabisa ambalo ni kule kutimilika kwa utukufu Wangu, na ni jema lililotimilika la wanadamu”.

Juzuu na. 20 ku download - click here

Kila siku, hatua kwa hatua, jisomee hapa, ili upate kukua katika Paji la Uhai, ndani ya UTASHI WA MUNGU, kulingana na Mafundisho aliyoyatoa YESU kwake Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA

Swahili - Telegram Channel: Utashi Wa Mungu Na Upendo Wa Mungu

Swahili - Telegram Channel: Saa 24 Za Mateso Ya Bwana Weto Yesu Kristo

English - Telegram Channel: Divine Will Divine Love

English - Telegram Channel: The Virgin Mary in the Kingdom of the Divine Will

Français - Chaine de Telegram: Divine Volonte Divin Amour

Français - Chaîne de Telegram: Lettres de Luisa Piccarreta

Lingala - Chaine de Telegram: Mpo Elingi Nzambe Bolingi bwa Nzambe

Website all languages: www.divinewilldivinelove.com

Vitabu yote vilivyo katika faili za PDF vinaweza kupakuliwa bila gharama yoyote ile wakati wote ule. Pia, upo huru kabisa kuchapisha VITABU hivyo wewe mwenyewe binafsi au kuchapisha kwenye kiwanda chochote kile. Lakini vitabu hivyo ni kwa matumizi binafsi tu na siyo kwa ajili ya biashara! Hata hivyo una ruhusa ya kuwashirikisha na kuwapatia watu wengine vitabu hivyo kadiri unavyopenda!!

Swahili landing page: click here

English landing page: click here

Lingala landing page: click here

Kikongo landing page: click here

French landing page: click here

Italian landing page: click here

Report Page