Yesu kwa Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - KITABU cha MBINGU - Juzuu Na. 19 - Juni 26, 1926🖋📃📖📔

Yesu kwa Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - KITABU cha MBINGU - Juzuu Na. 19 - Juni 26, 1926🖋📃📖📔


Nilikuwa nikiendelea na matendo yangu ndani ya Utashi Mkuu wa Juu kwa mtindo niliouzoea, yaani ule wa kuyapokea na kuyakumbatia mambo yote – Uumbaji, Ukombozi na kila moja la matendo hayo, ili hatimaye niweze kumrudishia Muumba Wangu, kumlipa pendo na utukufu ambao wanadamu wote tunawiwa kwake. Ndipo Yesu Wangu Mtamu akijimudu ndani ya nafsi yangu aliniambia:

“Binti Yangu, jukumu la Binti Mdogo wa Utashi Wangu, lisiwe lile tu la kuwazia na kujishughulisha na namna ya kutetea haki za Muumba Wake katika ujumla wake wote, wala jukumu siyo tu namna ya kumlipa fidia kwa pendo na kwa utukufu ule ambao wanadamu wote wanawiwa kwake, na wala jukumu lisiwe tu kuwazia namna ya kutekeleza hilo kama tendo moja, na kama la mtu mmoja, na wala jukumu lisiwe tu kuwazia namna ya kuhakikisha kuwa vitu vyote na watu wote wawepo na waonekane ndani ya nafsi yake. Hilo tu peke yake halitoshi kwa vile Utashi Wetu huwa unahusisha daima kila kitu na kila mtu, na tena yule anayeishi ndani ya Utashi Wetu, tayari anayo mitindo ya ujumla wote na mbinu mbalimbali za ujumla wote. Kwa sababu hiyo, inawezekana kabisa pale akatupatia kila kitu na hata fidia na madeni ya kulipana. Lakini, kwa Binti Yetu Sisi, jukumu lake lingine la lazima ni kwamba atetee pia haki za Malkia Mtawala Mwenye Mamlaka.

Huyu alitenda yote katika mtazamo na msimamo wa ulimwengu mzima. Kwa hiyo, alikuwa na pendo, alikuwa na utukufu, alikuwa na sala, na uchungu kwa ajili ya Muumba Wake, na daima alifanya hivyo kwa jina la wanadamu wote, kwa ajili ya mambo yote na kwa ajili ya kila mmoja. Yeye hakuachilia kitendo chochote kisahaulike au kiachwe ambacho wanadamu walimwia Muumba wao. Na kwa vile ndani ya moyo wake wa kimama alikuwa daima akibeba watu wote bila kumwacha hata mmoja nje, yeye alikuwa anapenda wote na kila mmoja. Kwa minajili hiyo, pale ndani yake Sisi tulikuwa tunakuta na kuona utukufu wetu wote. Hakuwahi kutukatalia chochote, siyo tu kile alichopasika kutupatia yeye binafsi, bali alitupatia pia kila kitu ambacho wanadamu wengine walikuwa wakitukatalia. Na kuonyesha kuwa yeye ni Mama mkarimu sana, Mama wa upendo sana, Mama anayejimaliza kwa ajili ya watoto wake, yeye aliwaingiza watu wote na kuwatunga mimba ndani ya moyo wake wa mateso. Kila mshipa wa moyo wake uligeuka ukawa ni teso linalomchoma, ambamo alikuwa akitoa uhai kwa kila mtoto wake, hadi alipofikia kwenye pigo lile la mauti la kifo cha Mtoto Wake aliye Mungu. Uchungu wa kifo hiki, ndio uliotia mhuri wa kuzaliwa upya wa uhai kwa watoto wapya wa huyu Mama Mteseka.

Na hatimaye, Malkia Bikira, aliyekuwa ametupenda kiasi hicho, ndiye ametetea haki zetu zote. Mama huyu, laini namna hii, ambaye alikuwa na pendo na maumivu kwa ajili ya watu wote, ndiye anastahili kupendwa kabisa kabisa na Binti mzaliwa mpya wetu Mdogo wa Utashi Mkuu wa Juu. Umpende kwa niaba ya wote, umlipe fidia kwa kila kitu. Ukikusanya na kukumbatia matendo yote ya Malkia Bikira huyu katika Utashi Wetu, chukua na utashi wako ukauunganishe kwenye Utashi Wake Malkia, kwani yeye hatenganiki na Sisi. Utukufu wake ni utukufu Wetu, na utukufu Wetu ni utukufu wake, na hasa hasa kwa vile Utashi Wetu huwa unaweka na kuunganisha kila kitu pamoja”.

Kufikia hapo, baada ya kulisikia jambo hilo, mimi nikawa nimevurugika kidogo. Kwa vile sikujua namna ya kutekeleza kile ambacho Yesu alikuwa ameniambia, nikawa ninamwomba anipe uwezo wa kufanya hilo. Yesu hapo aliendelea kunipa maelezo yake akisema:

“Binti Yangu, Utashi Wangu unashika ndanimo kila kitu, na unashikilia na kuhifadhi matendo yake yote kama vile lingekuwa ni tendo moja tu. Ndivyo pia unahifadhi matendo yote ya Malkia Mtawala Mwenye Mamlaka, na unayashikilia na kuyahifadhi kama vile yangekuwa yote ni matendo ya kwake. Ni kwa vile yeye alitenda yote akiwa ndani ya Utashi Wangu. Kwa sababu hiyo, ni Utashi Wangu wenyewe ndio utakaoyaweka matendo hayo ndani yako.

Sasa, ni lazima ujue kuwa yule aliyetenda vema kwa watu wote, akawapenda wote, na amefanya kazi zake kwa mtindo ulio wa watu wote, na unaokubalika na wote, akatenda yote kwa ajili ya Mungu na kwa ajili ya wote, huyo anazo haki zote, kihalali kabisa, juu ya kila kitu na kupita watu wote. Kutenda mambo kwa mtindo wa ujumla na kwa ajili ya watu wote ndio huo mtindo wa kimungu. Na Mama Yangu wa Mbinguni alikuwa akiweza kutenda mambo kwa mitindo ya Muumba Wake kwani ndani yake alikuwa anao ule Ufalme wa Utashi Wetu.

Yeye Malkia, kwa vile alikuwa akitenda ndani ya Utashi Wetu Mkuu wa Juu, basi anazo haki zote juu ya mali, vitu na mambo aliyofanikisha katika Ufalme Wetu. Mtu gani mwingine anaweza akamlipa kama siyo mtu ambaye naye anaishi katika Ufalme huo huo?

Kwa kweli, ni katika Ufalme huu tu, ndipo kunapatikana utendaji huu wa kiulimwengu, yaani ulio kwa masilahi ya wote na unaounganika na watu wote – pendo lipendalo kila mmoja, pendo linalokumbatia kila kitu, pendo lisiloachilia kitu chochote kikatoroka.

Lakini, budi ujue pia kuwa yule aliye na Ufalme wa Utashi Wangu hapa duniani, huyo ndiye anayo haki ya utukufu ule wa wote na wa vyote kule mbinguni. Na itakuwa kwa namna iliyo rahisi na ya kawaida kabisa inayoendana na maumbile yake.

Utashi Wangu unabeba kila kitu na unashirikisha kila mtu. Kwa hiyo kutoka kwa yule mwenye Utashi Wangu, hutokea mema yote pamoja na ule utukufu ambao upo ndani ya mema hayo. Na wakati utukufu huo wa jumla unatokea kwake, yeye mwenyewe pia anaupata. Je unadhani ni jambo dogo hilo la kuubeba utukufu wa jumla na wa wote pale katika Makao ya Mbinguni?

Basi, angalia sana. Ufalme wa Utashi Mkuu wa Juu unayo hazina kwa hazina ya utajiri. Kuna hela na hela zinazokuja toka huko. Kwa minajili hiyo, kila mtu anategemea kupata kitu fulani toka kwako, na hata Mama Yangu anategemea apate kufidiwa lile pendo la jumla kwa watu wote alilokuwa amelionyesha kwa vizazi vyote vya binadamu. Na wewe, kwa upande wako, unawiwa pia utukufu wa jumla na wa wote kule katika Makao ya Mbinguni – yaani, ule urithi anaoupata mtu ambaye aliubeba ule Ufalme wa Utashi Wangu hapa duniani”.

Juzuu na. 19 ku download - click here

Kila siku, hatua kwa hatua, jisomee hapa, ili upate kukua katika Paji la Uhai, ndani ya UTASHI WA MUNGU, kulingana na Mafundisho aliyoyatoa YESU kwake Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA

Swahili - Telegram Channel: Utashi Wa Mungu Na Upendo Wa Mungu

Swahili - Telegram Channel: Saa 24 Za Mateso Ya Bwana Weto Yesu Kristo

English - Telegram Channel: Divine Will Divine Love

English - Telegram Channel: The Virgin Mary in the Kingdom of the Divine Will

Français - Chaine de Telegram: Divine Volonte Divin Amour

Français - Chaîne de Telegram: Lettres de Luisa Piccarreta

Lingala - Chaine de Telegram: Mpo Elingi Nzambe Bolingi bwa Nzambe

Website all languages: www.divinewilldivinelove.com

Vitabu yote vilivyo katika faili za PDF vinaweza kupakuliwa bila gharama yoyote ile wakati wote ule. Pia, upo huru kabisa kuchapisha VITABU hivyo wewe mwenyewe binafsi au kuchapisha kwenye kiwanda chochote kile. Lakini vitabu hivyo ni kwa matumizi binafsi tu na siyo kwa ajili ya biashara! Hata hivyo una ruhusa ya kuwashirikisha na kuwapatia watu wengine vitabu hivyo kadiri unavyopenda!!

Swahili landing page: click here

English landing page: click here

Lingala landing page: click here

Kikongo landing page: click here

French landing page: click here

Italian landing page: click here

Report Page