Yesu kwa Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - KITABU cha MBINGU - Juzuu Na. 19 - Julai 14, 1926 🖋📄📖📔

Yesu kwa Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - KITABU cha MBINGU - Juzuu Na. 19 - Julai 14, 1926 🖋📄📖📔


Mimi nilikuwa naendelea na kawaida yangu ya kujiyeyusha mimi mwenyewe ndani ya Utashi Mtakatifu. Mara nyingi Yesu Wangu Mtamu alikuwa ananifuata na kuambatana nami pale ninapokuwa nakariri na kurudia vitendo hivyo. Wakati mwingine alikuwa anasimama kuangalia endapo kuna kitu fulani nilichosahau au kilichonipita bila mie kukitambua kati ya mambo aliyokuwa amekwisha kuyatenda, iwe katika Uumbaji au katika Ukombozi. Yeye, kwa wema wake wote, amekuwa akinijulisha au kunikumbusha kusudi nami kwa upande wangu niweze daima kuongeza angalau neno dogo la ‘nakupenda’ au la ‘asante’ au niweze kufanya uabudu kidogo. Amenieleza kuwa ni lazima kwangu kujua na kukumbuka Utashi Wake umepanua hadi wapi mipaka ya Ufalme wake kwa ajili ya kumpenda mwanadamu.

Utashi umepanua mipaka ya Ufalme wake kusudi mwanadamu awe akizunguka humo kwa ajili ya kuufurahia, na pia Utashi, kwa pendo lake, unataka umiliki wa Ufalme uwe ni wa uhakika zaidi. Tena Mbingu na dunia zitakapomwona mwanadamu anakaa tayari na daima ndani ya Ufalme huo, zote zitaweza kukumbuka na kujua kwamba yule mrithi asilia wa Ufalme wa Utashi Wangu amekwisha kujitokeza na kwamba huyo mrithi anaupenda Ufalme na anafurahia kuweza kuumiliki tena.

Halafu, nilipokuwa naonja kuzama kilindini mwa huo Utashi wa Milele, Yesu Wangu Mpendwa alijionyesha kwangu akiwa amefungua Moyo Wake wazi kabisa.

Katika kila pigo lake la Moyo kulikuwa kunatoka mwonzi wa mwanga ambao pale penye ncha yake ilionekana imeandikwa FIAT. Kwa vile pigo la moyo ni endelevu na la mfululizo, wakati mwonzi mmoja unapotoka, mara ulifuata mwonzi mwingine, halafu mwingine tena. Mionzi haikukoma kutoka. Mionzi hiyo ilifyatuliwa ikilenga kwenye Mbingu na dunia na yote ilipeleka FIAT iliyoandikwa pale penye ncha. Mionzi haikuwa inaibuka kutoka kwenye Moyo Wake tu, bali ilitoka pia kwenye macho Yake alipokuwa akitazama, ilitoka mdomoni alipokuwa akizungumza, ilitoka mikononi na miguuni wakati akitembeza mikono Yake na miguu Yake. Mionzi hiyo yote ilitoka ikiwa imebeba FIAT Kuu kama utukufu na ushindi. Kweli, kumtazama Yesu ilikuwa ni kitu cha kuvutia na kupendeza sana: Yesu mzuri, amebadilika kabisa katika mionzi ile ya mwanga iliyokuwa ikitoka katika mwili wake mwabudiwa wote. Na kile kilichokuwa kinaleta zaidi ukuu, utukufu, mbwembwe na madoido na mapambo, hadhi na uzuri ilikuwa ni ile FIAT. Mwanga Wake ulikuwa unanipofusha macho kabisa. Mimi ningeweza kubaki pale pale kumtazama Yesu hata kwa karne na karne bila hata kumwambia kitu, kama isingekuwa ni Yeye Mwenyewe aliyekatisha kimya kile cha mshangao kwa kuniambia:

“Binti Yangu, utukufu kamili na heshima timilifu kwa Utashi Wangu ilitolewa na Ubinadamu Wangu. Kwa kweli ilikuwa ni hapa ndani Yangu Mwenyewe, katika kiini cha Moyo Wangu huu, ndipo nilipoujenga Ufalme wa Utashi Mkuu. Kwa vile mwanadamu alikuwa ameupoteza Ufalme, na kwa vile hapakuwepo tena matumaini ya kuupata tena, Ubinadamu Wangu ndio ulioshughulika kuupata tena kwa maumivu ya ndani yasiyowahi kusikika. Ubinadamu Wangu ndio ukatoa kwa Utashi Mkuu zile heshima zote zilizotakiwa na ule utukufu ulioondolewa na mwanadamu. Ubinadamu ulitoa hivyo vyote kwa Utashi Mkuu kusudi sasa viweze kurejeshwa tena kwa mwanadamu. Ndivyo hivyo Ufalme wa Utashi Wangu ulivyojengwa ndani ya Ubinadamu Wangu. Ndiyo maana, kila kitu kilichokuwa kikiundwa ndani ya Ubinadamu Wangu na kikawa kinajitokeza nje, kilikuwa kikibeba ule mhuri wa FIAT. Kila wazo Langu, utazamo Wangu, pumzi Yangu, pigo la moyo, kila tone la Damu Yangu, vyote vyote vilibeba muhuri huo wa FIAT ya Ufalme Mkuu. Hiyo FIAT ndiyo iliyokuwa ikinipa utukufu kabisa na iliyonipamba kabisa hata Mbingu na dunia zikabaki chini Yangu na kuonekana kama zina giza kidogo mbele Yangu kwani Utashi Wangu wa kimungu upo juu na ni mkuu zaidi ya kila kitu na huweka kila kitu chini yake kama kigoda chake.

Sasa, baada ya karne nyingi, nilikuwa nachunguza kumpata mtu wa kumkabidhi Ufalme huu. Nimekuwa kama mama aliye mjamzito, anayetweta katika maumivu yake ya kutaka ajifungue kumzaa mtoto wake, lakini hafanikiwi. Masikini mama huyu, ni mateso yalioje! Ni vile hafanikiwi kufaidi tunda la tumbo lake. Mbaya zaidi ni kwamba mimba imekomaa, lakini haitoki. Uhai wake mwenyewe upo hatarini daima.

Kwa karne hizi nyingi, nimekuwa ni zaidi ya mama mjamzito. Ni jinsi gani nilivyoteseka! Nimehangaika kiasi gani kushuhudia mambo ya utukufu Wangu yakiathirika, iwe yale ya Uumbaji, au yale ya Ukombozi. Zaidi ya hilo, ni kwamba nilikuwa naushikilia Ufalme huu kama siri Yangu niliyoificha ndani ya Moyo Wangu bila kuwa na mahali pa kupumulia ili niuonyeshe nje kwa watu. Jambo hilo lilinifanya niwe nahangaika na kutweta zaidi na zaidi. Katika wanadamu nilikuwa sioni bado utayari na uhiari wa kutosha wa kuniruhusu Mimi kuwakabidhi huyo mtoto Wangu nitakayejifungua. Pia kwa kuwa siyo mema yote yaliyopo katika Ufalme wa Ukombozi yamekwisha kuwafikia wanadamu. Mimi nisingeweza kujitumbukiza katika hatari ya kuwakabidhi Ufalme wa Utashi Wangu, ambao kwa kweli unashika mema makubwa zaidi. Halafu tena, ni kwamba mema ya Ukombozi yatatumika hasa kama vazi maalum, kama kinga dhidi ya sumu ili wanapoingia katika Ufalme wa Utashi Wangu wasiweze kurudia kwa mara nyingingine kwenye mwanguko kama ule aliotenda Adamu.

Ndiyo kusema, kama katika mema hayo yote, si yote yaliyopokelewa, yaani yamedharauliwa, yamechukuliwa vibaya na kuchafuliwa, huyo mtoto wa Ufalme Wangu aliye tumboni Mwangu, angetoka namna gani toka ndani ya Ubinadamu Wangu? Kwa hoja hiyo, Mimi nilijiridhisha kuendelea kutweta katika mahangaiko, katika mateso, katika kusubiri zaidi ya mama yeyote, ili tu nisihatarishe uhai wa mtoto Wangu mpenzi wa Ufalme Wangu. Basi, niliendelea kutamanitamani sana kujifungua ili nitoe Utashi wa Mungu, nijifungue ili niutoe Ufalme wake kama zawadi kwa wanadamu, nijifungue ili kusalimisha na kuthibitisha malengo yote ya Uumbaji na ya Ukombozi, ambayo yote yalikuwa yapo katika hatari ya kupotea kabisa. Kwa kipindi chote hiki ambapo mwanadamu harejei katika Ufalme wa Utashi Mkuu, malengo Yetu na malengo ya mwanadamu yanabaki daima katika hali hatarishi. Mwanadamu aliye nje ya Utashi Wetu huwa daima ni vurugu na fujo katika kazi Yetu ya Uumbaji, huwa ni noti chafu katika musiki, noti inayoharibu harmonia timilifu ya utakatifu wa kazi zetu.

Na kwa sababu hiyo Mimi nilikuwa nafuatilia mzunguko wa hizi karne huku nikiwa ninasubiri tu mzaliwa Wangu, Binti Mdogo, mzaliwa Wangu mpya katika Ufalme wa Utashi Wangu. Kwa ajili ya usalama na uhakika wa Ufalme wa Utashi Wangu, niliyaweka mema yote ya Ukombozi kwa kuyapanga kumzunguka huyu mzaliwa mpya. Zaidi ya mama aliye katika maumivu na aliyekwisha kuhangaika sana sana, sasa Mimi ninakukabidhi wewe mtoto huyo nitakayejifungua na masuala yote yahusuyo huo Ufalme Wangu. Siyo Ubinadamu Wangu tu ndio unatamani kujifungua mtoto Wangu huyo anayenigharimu kweli, bali Uumbwa wote una mimba ya Utashi Wangu, na unatweta kutamani kujifungua kwa ajili ya viumbe ili kujenga upya Ufalme wa Mungu Wao kati ya wanadamu. Kwa hiyo Uumbwa ni kama nguo inayoficha Utashi Wangu kama mimba, lakini wanadamu wanafika na kufunua nguo hiyo na kusukumia mimba ndani tena ili isitoke. Hata jua lina mimba ya Utashi Wangu. Wakati watu wanafaidi matokeo ya mwanga, ambao mithili ya nguo hufunika na kuficha Utashi Wangu, wao huendelea kufaidi mema yatokanayo na huo mwanga, halafu lakini wanasukumia mbali Utashi Wangu, hawataki kuutambua, na wala hawataki kutawaliwa nao. Ndio maana wanafaidi mema ya kimaumbile yaliyomo ndani ya jua. Lakini Mema ya kiroho, yaani Ufalme wa Utashi Wangu, unaotawala ndani ya jua na unaopenda kuwafikia wao, wanausukumia mbali, hawautaki. Oh, ni jinsi gani Utashi Wangu unavyohangaika kwa mateso pale ndani ya jua, Utashi unaotaka kujifungua toka kule juu mbinguni kwenye makao yake, na unataka utawale kati ya wanadamu wote.

Anga pia lina mimba ya Utashi Wangu. Kwa macho yake ya mwanga, ambayo ni nyota, anga hilo huwaangalia wanadamu kuona kama wanapenda kuupokea huo Utashi, ili utawale kati yao. Bahari nayo ina mimba hiyo hiyo ya Utashi Wangu. Kutokana na sauti ya mawimbi yake ya dhoruba, tunaweza kuisikia na maji yake, mithili ya ile nguo, huuficha Utashi Wangu, hata kama mwanadamu anaitumia sana bahari. Anachukua samaki zake, lakini kuhusu Utashi Wangu hajali kitu kabisa; badala yake, huufanya uteseke na kuumia kama katika mimba inayogomewa kutoka nje ya tumbo la maji hayo ya bahari. Ndivyo vitu vyote vina mimba hiyo ya Utashi Wangu: Yaani upepo, moto, ua, ardhi yote, vyote hivyo vimekuwa ni nguo zinazofunika na kuficha mimba. Je sasa ni nani atakayeleta pumzi hiyo na unafuu kwa Ubinadamu Wangu? Nani atakayepasua hayo mapazia ya nguo yatokanayo na vitu vingi vilivyoumbwa ambavyo vinauficha Utashi? Nani kati ya vitu vyote, atamtambua mtu yule ambaye ndiye anabeba Utashi Wangu, ambaye kwa kuutolea heshima zitakiwazo ataufanya utawale ndani ya roho yake mwenyewe, huku akiupatia mamlaka, na yeye mwenyewe kuupa heshima na utii? Basi, hatimaye, Binti Yangu, uwe makini: Toa raha hii kwa Yesu na umridhishe. Hadi sasa, ameteseka na kuhangaika sana na mateso ya kujifungua mtoto huyu wa Ufalme Wangu Mkuu. Na Uumbwa wote pamoja Nami, katika tendo moja na pekee, utapasulia mbali mapazia yale yote na watamtwaa na kumweka ndani yako yule mtoto mzaliwa wa Utashi Wangu ambaye mapazia yalikuwa yanamficha muda wote huu”.

Juzuu na. 19 ku download - click here

Kila siku, hatua kwa hatua, jisomee hapa, ili upate kukua katika Paji la Uhai, ndani ya UTASHI WA MUNGU, kulingana na Mafundisho aliyoyatoa YESU kwake Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA

Swahili - Telegram Channel: Utashi Wa Mungu Na Upendo Wa Mungu

Swahili - Telegram Channel: Saa 24 Za Mateso Ya Bwana Weto Yesu Kristo

English - Telegram Channel: Divine Will Divine Love

English - Telegram Channel: The Virgin Mary in the Kingdom of the Divine Will

Français - Chaine de Telegram: Divine Volonte Divin Amour

Français - Chaîne de Telegram: Lettres de Luisa Piccarreta

Lingala - Chaine de Telegram: Mpo Elingi Nzambe Bolingi bwa Nzambe

Website all languages: www.divinewilldivinelove.com

Vitabu yote vilivyo katika faili za PDF vinaweza kupakuliwa bila gharama yoyote ile wakati wote ule. Pia, upo huru kabisa kuchapisha VITABU hivyo wewe mwenyewe binafsi au kuchapisha kwenye kiwanda chochote kile. Lakini vitabu hivyo ni kwa matumizi binafsi tu na siyo kwa ajili ya biashara! Hata hivyo una ruhusa ya kuwashirikisha na kuwapatia watu wengine vitabu hivyo kadiri unavyopenda!!

Swahili landing page: click here

English landing page: click here

Lingala landing page: click here

Kikongo landing page: click here

French landing page: click here

Italian landing page: click here

Report Page