Yesu kwa Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - KITABU cha MBINGU - Juzuu Na. 18 - Januari 28, 1926🖋📃📖📔

Yesu kwa Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - KITABU cha MBINGU - Juzuu Na. 18 - Januari 28, 1926🖋📃📖📔


Mimi nilikuwa nikitafakari juu ya Utashi Mtakatifu wa Kimungu, na ndipo nikawa nawaza moyoni mwangu: ‘Hivi iliwezekanaje kutokea kwamba Adamu, baada ya kutenda dhambi, akiwa tayari ameung’oa utashi wake kutoka kwenye Utashi wa Mungu, kwamba kapoteza nguvu, kapoteza mamlaka, na kwamba matendo yake yakawa hayapokeleki tena na Mungu, na wala hayakumletea Mungu furaha yoyote ile? Na kweli, kabla ya kutenda dhambi, Adamu alikuwa akitenda matendo yake kwa Mungu, na alikuwa amejifunza hayo matendo. Sasa, katika kuyarudia baadaye hayo matendo, kwa nini hayo matendo hayakuweza kutoa sauti ile ile, kwa nini hayakubeba tena pale ndani yao ule ujazo wote wa pendo la kimungu, na ujazo wote wa utukufu timilifu wa Mungu?’ Basi, pindi nikiyawaza hayo, Yesu Mpendevu Wangu, aliingia pale ndani mwangu, na kupitia mwanga alioulenga kwangu, aliniambia hivi:

“Binti Yangu, kwanza kabisa, pale kabla ya kujiondoa mwenyewe toka kwenye Utashi Wangu, Adamu alikuwa ni mtoto Wangu. Ndani yake aliubeba Utashi Wangu kama makao makuu ya uhai wake na ya matendo yake yote, na kwa hiyo alikuwa na nguvu fulani ya kimungu kabisa, alikuwa na himaya, na pia alikuwa na mvuto fulani uliokuwa wote ni wa kimungu kabisa. Pumzi yake, pigo lake la moyo, na matendo yake yalikuwa yakitoa mambo ya kimungu. Kiwiliwili chake chote kilikuwa kikinukia marashi ya kimbingu tu ambayo yalikuwa yakituvutia Sisi Sote kwake. Basi, kutoka pande zote, Sisi tulionja kujeruhiwa na huyu mtoto. Kama alipumua, kama alizungumza, kama katenda chochote, hata kile kilicho bila waa kabisa, hata vitendo vyake visivyohuisha utashi wake na vya kimaumbile tu, hayo yote, Kwetu Sisi, yalikuwa ni majeraha ya pendo lake kwetu Sisi. Na Sisi Wenyewe, katika kujiburudisha naye, tukawa tumemjaza zaidi na zaidi kwa mema Yetu, kwa sababu, chochote alichokuwa anakitenda kilikuwa kikitokea katika kona moja tu pekee, ambayo ilikuwa ni Utashi Wetu. Kwa hiyo basi, Sisi sote tukawa tunampenda mno - yaani hatukukiona chochote kinachoweza kikatuudhi Sisi.

Sasa, baada ya dhambi, Adamu, kutoka ile hali ya mwana, aliteremka na kujitweza yeye mwenyewe, hata kurudi kwenye hali ya mtumishi. Na mara tu baada ya kutengana na kuachana na Utashi Mkuu wa Juu, ile nguvu ya kimungu, ile himaya ya kimungu, ule mvuto wa kimungu, yale marashi ya kimbingu, vyote vilimtoka na kumwacha. Kwa hiyo, matendo yake, na nafsi yake, havikutoa tena mambo ya kimungu, bali, vikawa vimejaa na hisia za kibinadamu. Na hivyo vyote, kwa vile vilimfanya apoteze mvuto, vilifikia kutufanya Sisi tusionje tena kule kujeruhiwa naye, bali, tukawa tu tunazingatia umbali wetu fulani - yeye toka Kwetu, na Sisi kutoka kwake. Hata kama alijaribu kurudiarudia yale yale matendo aliyokuwa akiyatenda pale kabla ya kutenda dhambi, kama vile alivyokuwa akifanya katika hali halisi, ikawa sasa Kwetu Sisi haisemi chochote tena. Lakini wewe, je, unafahamu yanakuwa ni kitu gani, matendo ya mwanadamu, yanapokuwa hayana ujazo wa Utashi Wetu? Huwa yanakuwa sawa kama vile vyakula visivyoungwa na chochote na visivyoleta shibe yoyote ile, yaani, vile vyakula, ambavyo, badala ya kuvifurahia, vyenyewe vinakichefua kinywa cha binadamu. Na ndivyo vinavyochefua kinywa cha kimungu. Huwa kama yale matunda mabichi, matunda ambayo hayana utamu wowote, wala ladha fulani. Huwa kama yale maua yasiyo na marashi yoyote. Huwa kama vile vyungu ambavyo huwa vinajaa, ndiyo, lakini, vimejaa mambo ya kale, yanayovunjika vunjika, na vimejaa virakaviraka. Vyote hivyo vinaweza labda vikafaa kwa dhiki tu ya binadamu, na vinaweza labda vikafaa tu kama kivuli fulani cha ule utukufu wa Mungu. Lakini haviwezi vikawa ni furaha na ni afya timilifu ya mwanadamu, na wala haiwezi ikawa ni ujazo wote wa ule utukufu wa Mungu. Lakini sasa, ni kwa hamu gani kubwa mtu huwa anakula kile chakula kilichoungwa vizuri na chenye kuleta lishe? Ni jinsi gani chakula hicho kinavyoleta nguvu kwa mtu mzima. Ile harufu tu ya viungo vyake huwa inalowesha tayari ile njaa ya mtu na inalowesha na kuamsha ile hamu ya kupenda kula kile chakula. Hali kadhalika, pale kabla ya kutenda dhambi, Adamu alikuwa ameunga matendo yake yote kwa kile kiungo kikuu cha Utashi Wetu, na kwa hiyo, alilowanisha ile hamu ya lile Pendo Letu, kuanza mara kutwaa yale matendo yake yote, kama ndicho chakula kinachofurahisha kabisa Kwetu Sisi. Na Sisi, kwa upande Wetu, tukampatia chakula cha kwetu kilichokuwa kinanoga - yaani ule Utashi Wetu. Lakini pale baada ya dhambi, masikini huyu, akawa amepoteza ile njia ya moja kwa moja ya mawasiliano na Muumba Wake. Lile pendo safi kabisa halikuwa linatawala tena pale ndani mwake. Pendo likawa limegawanyika kutokana na hali ya wasiwasi, na kutokana na hofu. Na kwa vile alikuwa hana tena mamlaka kamili juu ya Utashi Mkuu wa Juu, yale matendo yake ya pale awali, yanapotendeka sasa baada ya dhambi, hayakuweza tena kuwa na thamani ile ile. Zaidi zaidi, kwa vile Uumbwa mzima, akiwemo na binadamu, vilitokea kwa Yule Muumba wa Milele kama chimbuko la Uhai wao, na ambamo wangekuwa wanahifadhiwa tu pamoja na Uhai wa Utashi wa Mungu, kila kitu kilitakiwa kiwe na msingi wake juu ya Utashi a Mungu, na huo msingi ndio uliotakiwa kuhifadhi vitu vyote viweze kubaki vizuri, vya kupendeza, vyenye adhama, sawa kabisa kama vile vilivyokuwa vimefika toka kwa Mungu. Na kwa kweli, viumbe vyote vipo kama vile vilivyokuwa vimeumbwa - hakuna hata kimoja kilichopoteza chochote cha ile asili yake. Ni binadamu peke yake ndiye aliyekuwa amepoteza uhai wake, ambao ndio uliokuwa ni msingi. Kwa sababu hiyo binadamu akawa amepoteza adhama yake, nguvu yake, na ule ufanano wake kwa Muumba Wake. Lakini hata hivyo, Utashi Wangu haukumwacha binadamu kabisa kabisa. Ingawa kama Utashi wa Mungu, sasa, ulikuwa unashindwa kuendelea kuwa ni chimbuko la uhai wa binadamu, na ingawa kama ulishindwa kuwa ni msingi ambao ungemtegemeza binadamu, kwa vile ni yeye mwenyewe binadamu ndiye aliyejiondoa toka kwenye Utashi wa Mungu, Utashi wa Mungu ukajitolea wenyewe kuwa kama dawa ili huyo binadamu asiangamie moja kwa moja. Basi, Utashi Wangu ni tiba, ni afya, ni hifadhi, ni chakula, ni uhai, ni ujazo wa ule utakatifu wa juu kabisa. Utashi wa Mungu unajitoa wenyewe katika namna yoyote ile ambayo mwanadamu anautaka. Endapo mwanadamu anautaka kama dawa au tiba, Utashi wa Mungu utajitoa wenyewe ili ukamsaidie kumwondolea ile homa ya matamaa mbalimbali, ili kumwondolea madhaifu ya kukosa saburi, ili kumwondolea ile mizizi ya majivuno, ili kumwondolea maradhi ya kugandamana na watu au na mambo. Na hivyo kwa maovu mengine yote yaliyobaki. Kama binadamu anautaka Utashi wa Mungu kama afya, wenyewe utajitoa ili kuihifadhi afya ya mtu husika, na ili kumwokoa mtu huyo kutoka maradhi yoyote ya kiroho. Endapo atautaka kama chakula, utajitoa wenyewe kama chakula ili kukuza nguvu mbalimbali za mtu husika na ili aweze kukua zaidi katika utakatifu. Endapo mtu atauhitaji kama uhai na kama ujazo wa utakatifu - lo! hapo Utashi Wangu hufanya sherehe, kwa vile, hapo huwa unamwona binadamu akirejea ndani ya tumbo la asili yake, ambako alikuwa ametokea. Ndipo utajitoa wenyewe ili kumpatia mtu husika ule ufanano na Muumba Wake, ambalo ndilo lengo pekee la kuumbwa kwake. Utashi Wangu huwa haumwachi binadamu. Endapo ungemwacha, huyo binadamu angeyeyuka na kuwa si kitu. Na kama binadamu hatajitoa mwenyewe kwa hiari yake ili Utashi Wangu umfanye kuwa mtakatifu, basi Utashi Wangu utatumia angalau ile mitindo mbalimbali ya kuweza kumwokoa”.

Nilipolisikia hilo, nikajisemea moyoni mwangu: ‘Ewe Yesu, Pendo Langu, kama kweli Wewe unapenda kwamba Utashi Wako utende kazi pale ndani ya mwanadamu sawa kama katika lile tendo ambamo Wewe ulimwumba - kana kwamba hapakuwahi kutokea uvunjivu kati ya Utashi Wako na ule utashi wa kibinadamu - sasa, Wewe ulipofika hapa duniani kuja kutukomboa, kwa nini basi hukutupatia hilo jema kuu - kwamba Utashi Wako, katika kusherehekea ushindi wake juu ya mambo yote, ungetuweka sisi pale katika utaratibu wa Uumbwa, sawa kama vile tulivyokuwa tumetokea kwenye mikono ya Baba Yetu wa Mbinguni?’. Na Yesu, akitokea pale ndani mwangu, alinikumbatia kwa kunibania kwenye Moyo Wake, na kwa sauti ya upole na ulaini usiosemekana, aliniambia hivi:

“Binti Yangu, lengo la kwanza kabisa la Mimi kuja hapa duniani lilikuwa hasa ni hili - kwamba binadamu arudi tena ndani ya tumbo la Utashi Wangu, kwa vile, ndipo mahali alipotokea wakati ule alipoumbwa. Lakini, ili kulitekeleza hilo, ilibidi Mimi, kwa njia ya Ubinadamu Wangu, nitengeneze ule mzizi, lile shina, yale matawi, yale majani, na yale maua, ambayo kwayo yatatoka yale matunda ya kimbingu ya Utashi Wangu. Hakuna mtu yeyote atakayeweza kupata tunda bila kuwa na mti. Mti huo ulikuwa umemwagiliwa maji kwa Damu Yangu. Ulikuwa umelimiliwa na kupaliliwa kwa maumivu Yangu, kwa mitweto Yangu, na kwa machozi Yangu. Jua lililowaka juu ya mti huo lilikuwa ni lile Jua la Utashi Wangu peke yake. Kwa hiyo, ni uhakika kwamba, yale matunda ya Utashi Wangu, yatapatikana tu. Lakini, ili mtu afikie kuyatamani hayo matunda, ni budi mtu afahamu kwanza jinsi matunda hayo yalivyo ni azizi, budi afahamu manufaa yanayoletwa na matunda hayo, na utajiri ule ambao matunda hayo huzalisha. Basi, hiyo ndiyo hoja kwa yale maelezo mengi niliyokuwa nimekupatia mintarafu Utashi Wangu. Ni kwa vile, maarifa au ufahamu ndio utakaoleta hamu ya kula huo Utashi Wangu. Na baada ya wanadamu kuonja maana ya kuishi kwa ajili ya kutekeleza Utashi Wangu peke yake, basi, kama siyo watu wote, lakini, baadhi, hakika watarudi kwenye njia ya Utashi Wangu, zile tashi mbili zitabusiana kwa umilele, na wala hapatakuwa tena mvutano na mgongano kati ya utashi wa kibinadamu na Ule Utashi wa Muumba, na ule Ukombozi Wangu, utaongeza kutoa hata lile tunda la Mapenzi Yako Yatimizwe Duniani kama Mbinguni[1]. Basi wewe, na uwe ni wa kwanza kulipokea tunda hilo, na wala usitamani tena chakula kingine, wala uhai mwingine isipokuwa Utashi Wangu peke yake”.

[1] Mapenzi Yako Yatimizwe Duniani kama Mbinguni = Kilatini: Fiat Voluntas Tua sicut in Coelo et in Terra.


Website all languages: www.divinewilldivinelove.com

Vitabu yote vilivyo katika faili za PDF vinaweza kupakuliwa bila gharama yoyote ile wakati wote ule. Pia, upo huru kabisa kuchapisha VITABU hivyo wewe mwenyewe binafsi au kuchapisha kwenye kiwanda chochote kile. Lakini vitabu hivyo ni kwa matumizi binafsi tu na siyo kwa ajili ya biashara! Hata hivyo una ruhusa ya kuwashirikisha na kuwapatia watu wengine vitabu hivyo kadiri unavyopenda!!

Swahili landing page: click here

English landing page: click here

Lingala landing page: click here

Kikongo landing page: click here

French landing page: click here

Italian landing page: click here

🤍☀️🤍☀️🤍☀️ 

Kila siku, hatua kwa hatua, jisomee hapa, ili upate kukua katika Paji la Uhai, ndani ya UTASHI WA MUNGU, kulingana na Mafundisho aliyoyatoa YESU kwake Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA

⬇️⬇️⬇️

Swahili - Telegram Channel: click here Utashi Wa Mungu Na Upendo Wa Mungu

English - Telegram Channel: click here Divine Will Divine Love

Français - Chaîne Telegram: click here Divine Volonte Divin Amour

Lingala - Chaîne Telegram: click here Mpo Elingi Nzambe Bolingi bwa Nzambe


Report Page