Yesu kwa Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - KITABU cha MBINGU - Juzuu Na. 16 - Novemba 10, 1923🖋📃📖📔

Yesu kwa Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - KITABU cha MBINGU - Juzuu Na. 16 - Novemba 10, 1923🖋📃📖📔


Nilikuwa nikijiachia nafsi yangu nzima pale ndani ya mikono ya Yesu Wangu Mtamu. Na nilipokuwa nikisali, nikawa ninaiona roho yangu ikiwa kidinya kabisa, na kwa kweli ilikuwa na udogo wa kupindukia. Ndipo nikawa nawaza moyoni mwangu: ‘Ni jinsi gani nilivyo ni kidinya! Yesu alikuwa sahihi kabisa kuniambi kwamba mimi ndiye mdogo kabisa kwa wote. Kwa kweli ningependa kufahamu kama mimi ndiye kidinya kabisa kati ya watu wote’. Basi, wakati nikiliwazia hilo, Yesu Mpendevu Wangu wa daima, aliingia pale ndani mwangu, akanionyesha jinsi alivyokuwa anambeba huyu kidinya pale ndani ya mikono Yake, na pia jinsi alivyokuwa akimbania kwenye Moyo Wake, na yeye kidinya, alivyokuwa akimwacha Yesu amtendee chochote kile alichokitaka. Ndipo Yesu aliniambia:

 “Ewe kidinya Wangu, Mimi nimekuchagua wewe kidinya, kwa vile walio wadogo huwa wanamruhusu mtu awatendee lolote lile analolitaka yeye. Wao huwa hawatembei kwa utashi wao, bali huwa wanakubali kuongozwa. Aidha, wao hao huwa wanaogopa hata kukanyaga hatua moja peke yao. Kama wanapokea zawadi zozote zile, kwa kujihisi kutoweza kuzihifadhi, wao wanazitua hizo zawadi pale penye paja la mama yao. Wadogo huwa wamevuliwa kila kitu, na wala hawajali kama wao ni tajiri au maskini. Wao hawahangaikii chochote kile. Lo! umri wa uchanga, ni jinsi gani ulivyo ni mzuri na upendezavyo - umejaa kabisa neema, umejaa uzuri na umejaa upya. Kwa hiyo, Mimi, kadiri inavyozidi kuwa kuu kazi yoyote ninayotaka kuitenda ndani ya mtu, ndivyo nitakavyomchagua aliye ni mdogo zaidi. Mimi ninapenda kabisa ule upya na uzuri wa utoto. Ninapenda mno hivi kwamba Mimi huwa ninawatunza na kuwashikilia watu hao katika ule udogo wa ule u-sikitu wa kule walikokuwa wametokea. Ninawahifadhi kwa kutoruhusu chochote kile cha kwao wenyewe kuingia pale ndani mwao, ili nisiwaruhusu hao kupoteza ule udogo wao, na kwa hiyo, waweze kutunza ule upya na uzuri wa kimungu walikotokea”.

 Katika kuyasikia hayo, mimi niliweza kusema: ‘Ewe Yesu, Pendo Langu, kwangu mimi inaelekea kuwa mimi ni mbaya mno mno na ndiyo maana nipo kidinya kiasi hiki. Na Wewe unasema eti Unanipenda mimi kweli kweli kwa sababu mimi ni mdogo? Inawezekanaje jambo hili?’. Ndipo Yesu akaniambia tena kwa kusema:

 “Ewe kidinya wangu, ubaya hauwezi ukawaingia wale walio ni wadogo kihalisia. Je unafahamu ni lini ubaya, na makuzi yanapoanza kuingia? Ni pale utashi wa mtu binafsi unapoanza kuingia. Kadiri utashi binafsi unavyoingia, ndivyo mwanadamu anaanza kujijaza nafsi yake mwenyewe na anaanza kuishi kufuata nafsi yake mwenyewe. Yule aliye ni vyote na yote huondoka toka kwenye ule udogo wa mwanadamu, na kwake huyo mwanadamu, ule udogo wake unaanza kuwa mkuu zaidi na zaidi - lakini huwa ni ukuu ambao unaleta kilio na majonzi. Kwa vile Mungu huwa sasa haishi kitimilifu tena pale ndani ya mtu husika, mtu huyo huondoka na kuuacha ule mwanzo wake, anadharau na kubeza ile asili yake, anaupoteza mwanga, anaupoteza uzuri, anaupoteza utakatifu, na hata ule upya wa Muumba Wake. Huyo mtu anaonekana kana kwamba anakua mbele yake yeye mwenyewe na labda hata mbele ya binadamu. Lakini mbele Yangu Mimi - lo! ni jinsi gani anavyopunguka na kudhoofika! Anaweza akawa ni mkuu sana na muhimu sana, lakini, kamwe mtu huyo hataweza kuwa ni yule mpendwa Wangu mdogo. Hatakuwa tena ni yule ambaye, ninapokuwa nimeshikwa na upendo kwake, Mimi huwa ninaingia ndani yake na kumjaza kwa Nafsi Yangu, ili awe anabaki vile kama nilivyokuwa nimemuumba, na yule ambaye Mimi ndiye ninamfanya kuwa mkuu kupita wengine wote, na ambaye hakuna mtu yeyote atakayeweza kulingana naye.

 Ndivyo nilivyokuwa nimemtendea Mama Yangu wa Mbinguni. Katika vizazi vyote vya binadamu, yeye ndiye aliye kidinya kabisa, kwa vile, utashi wake haukuwahi kumwingia kwa ajili ya kutenda lolote, bali, ni Utashi Wangu wa Milele ndio ulioingia daima ndani mwake. Na huo Utashi wa Milele siyo tu ulioshikilia abaki mdogo, abaki mzuri, abaki mpya, sawa kama vile alivyokuwa ametoka Kwetu, bali, ulimfanya awe daima ni mkuu wa wote. Lo! Ni jinsi gani alivyokuwa ni mzuri. Alikuwa mdogo kwa nafsi yake, lakini alikuwa mkuu na juu ya wote kwa nguvu Yetu Sisi Wenyewe. Na ni tu kwa mujibu wa ule udogo wake, alikuwa amepandishwa juu hadi kwenye kile kilele cha kuwa Mama wa Yule aliyekuwa amemtengeneza. Basi, unavyojionea mwenyewe, manufaa yote ya binadamu yapo katika kutekeleza Utashi Wangu. Na ubaya wote wa binadamu upo katika kutekeleza utashi wake mwenyewe. Ndiyo maana, katika kuja kumkomboa binadamu, Mimi nilikuwa nimemchagua Mama Yangu kwa vile alikuwa mdogo, na nikamtumia yeye kama mkondo wa kupitishia mema yote na matunda yote ya Ukombozi ili yateremke na kukifikia kizazi chote cha binadamu.

 Basi, ili Utashi Wangu uweze kujulikana, na ili Mbingu ifunguliwe ili Utashi Wangu uteremke kuja duniani na uje kutawala hapa duniani kama ilivyo kule Mbinguni, ilinipasa kumchagua mtu mdogo mwingine kutoka katika vizazi vyote vya binadamu. Kwa vile hiyo ni kazi kuu kupita zote ambayo natarajia kuitekeleza - yaani, kumrejesha binadamu kule kwenye asili yake, kule alikotokea, kumfungulia ule Utashi wa Mungu ambao alikuwa ameugomea, kumfungulia mikono Yangu ili kumpokea kwa mara nyingine ndani ya tumbo la Utashi Wangu - hekima Yangu isiyokuwa na mipaka, inamwita yule aliye ni kidinya kabisa kutoka katika u-sikitu. Ilikuwa ni vema na haki kwamba awe ni mdogo: Kama nilikuwa nimemweka aliye mdogo awe kichwa cha Ukombozi, ilinipasa nimweke mdogo mwingine awe kichwa cha Mapenzi Yako yatimizwe duniani kama kule Mbinguni. Kati ya hawa wadogo wawili, Mimi nilipasika kulifungilia lile lengo la kumwumba binadamu - ilinipasa nifanikishe mipango yangu juu ya huyu binadamu: kwa kupitia kwa mdogo moja nilipasika kumkomboa binadamu, nilipasika, kwa Damu Yangu, kumwosha binadamu toka uchafu wake na kumpatia msamaha. Na kwa kupitia yule mdogo mwingine, nilipasika kumfanya binadamu arejee kwenye mwanzo wake, arejee kwenye asili yake, arejee kwenye ile adhama yake, arejee kwenye vifungo vya Utashi Wangu vilivyokuwa vimevunjwa naye, nilipasika kumkaribisha tena binadamu kwenye ile tabasamu ya Utashi Wangu wa Milele, kumkaribisha akabusiane na Utashi Wangu wa Milele, na akaishi pale ndani ya Utashi wa Milele, nao Utashi wa Milele uishi tena ndani yake binadamu. Hilo ndilo lililokuwa ni lengo pekee la kumwumba binadamu. Na kile nilichokuwa nimekipanga na kukiweka, hakuna mwingine atakayeweza kukipinga. Karne na karne zitapita - sawa kama ilivyokuwa katika Ukombozi, ndivyo itakavyokuwa pia kwa jambo hili. Hata hivyo, binadamu atarejea ndani ya mikono Yangu kama vile alivyokuwa ameumbwa na Mimi. Lakini, ili kufanikisha hilo, kwanza kabisa, yanipasa kumchagua yule mmoja anayepasika kuwa ni wa kwanza wa kuishi maisha ndani ya Utashi Wangu wa Milele. Yanipasa, baada ya kumchagua, nikafungilie pale ndani yake yale mahusiano yote na Muumba, na budi niishi naye bila utengano wowote ule wa tashi zetu. Badala yake, iwe kwamba, utashi wake mtu husika na Utashi Wetu viwe ni utashi mmoja.

 Ndipo hapa upo ule ulazima kwamba yeye mtu husika awe ndiye mdogo kabisa tunayemtoa katika Uumbaji - ili kwamba, yeye mwenyewe atakapojiona kuwa ni mdogo vile, atakuwa mwenyewe anaukwepa utashi wa kwake. Na hata zaidi, yeye mwenyewe ataufungilia huo utashi wake kwenye Utashi Wetu Sisi hata asiweze kamwe kutekeleza ule utashi wake. Na licha ya kuwa ni mdogo vile, yeye ataweza bado kuishi pamoja na Sisi, kutokana na ile pumzi tuliyokuwa tumempulizia na ambayo ndiyo aliumbwa nayo. Utashi Wetu unaendelea kumshikilia akiwa mpya, akiwa ni mzuri. Yeye huyo ndiye anayetuletea tabasamu Yetu, anayetuletea burudani Yetu, na pamoja naye huyu, Sisi huwa tunatenda lolote lile tunalolitaka. Lo! ni jinsi gani alivyojaa furaha. Na wakati anapofurahia huo udogo wake, na hiyo hatima yake yenye heri, yeye atakuwa papo hapo anawalilia ndugu zake na atakuwa anajishughulisha, siyo na kitu kingine, isipokuwa tu na kulipa malipizi na fidia Kwetu Sisi. Atakuwa akitoa fidia kwa ajili ya watu wote na kwa ajili ya kila mmoja wao. Atalipa fidia kwa ya yale makosa yote wanayotutendea Sisi kwa wao kujiondoa  kutoka kwenye Utashi Wetu. Yale machozi ya mtu anayeishi ndani ya Utashi Wetu yatakuwa na nguvu sana. Na hasa hasa, kwa vile, huyo mtu hataki chochote kile isipokuwa kile ambacho na Sisi Wenyewe tunakitaka. Na baada ya ule mkondo wa kwanza wa Ukombozi, Sisi, kwa njia yake huyo mtu, tutafungua ule mkondo wa pili wa Mapenzi Yako yatimizwe duniani kama kule Mbinguni”.

Website all languages: www.divinewilldivinelove.com

Vitabu yote vilivyo katika faili za PDF vinaweza kupakuliwa bila gharama yoyote ile wakati wote ule. Pia, upo huru kabisa kuchapisha VITABU hivyo wewe mwenyewe binafsi au kuchapisha kwenye kiwanda chochote kile. Lakini vitabu hivyo ni kwa matumizi binafsi tu na siyo kwa ajili ya biashara! Hata hivyo una ruhusa ya kuwashirikisha na kuwapatia watu wengine vitabu hivyo kadiri unavyopenda!!

Swahili landing page: click here

English landing page: click here

Lingala landing page: click here

Kikongo landing page: click here

French landing page: click here

Italian landing page: click here

🤍☀️🤍☀️🤍☀️ 

Kila siku, hatua kwa hatua, jisomee hapa, ili upate kukua katika Paji la Uhai, ndani ya UTASHI WA MUNGU, kulingana na Mafundisho aliyoyatoa YESU kwake Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA

⬇️⬇️⬇️

Swahili - Telegram Channel: click here Utashi Wa Mungu Na Upendo Wa Mungu

English - Telegram Channel: click here Divine Will Divine Love

Français - Chaîne Telegram: click here Divine Volonte Divin Amour

Lingala - Chaîne Telegram: click here Mpo Elingi Nzambe Bolingi bwa Nzambe

Report Page