Yesu kwa Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - KITABU cha MBINGU - Juzuu Na. 14 - Oktoba 6, 1922🖋📃📖📔

Yesu kwa Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - KITABU cha MBINGU - Juzuu Na. 14 - Oktoba 6, 1922🖋📃📖📔


Nilikuwa katika kusali, na ndipo Yesu Wangu Mpendevu wa daima alinijia, akatupa mikono Yake na kuizungusha kwenye shingo yangu huku akiwa ananiambia:

“Binti Yangu, ebu tusali pamoja, ebu tuingie katika ile bahari kuu ya Utashi Wangu, ili kutoka ndani mwako kisiweze kutoka chochote kile ambacho hakikuwa kimetumbukizwa kwanza ndani ya huo Utashi Wangu. Mambo yote, yaani, wazo, neno, pigo la moyo, kazi, na hatua, ni budi zishike nafasi yao katika Utashi Wangu. Kila jambo ambalo utakuwa unalitenda ndani yake, wewe utakuwa unajipatia umiliki wa kitu kimoja zaidi na utakuwa unajipatia haki zaidi juu ya kitu hicho.

Matendo yote ya binadamu, kadiri ya lengo la Uumbwa, yalitakiwa yawe na uhai ndani ya Utashi Wangu, na yalitakiwa yatengeneze ndani ya huo Utashi mpangilio wa matendo yote ya binadamu yaliyogeuzwa kuwa ni matendo ya kimungu, matendo yenye ile alama ya Uadhimu, na ya Hekima kuu ya juu.

Haukuwa ni Utashi Wetu kwamba binadamu ajiondoe toka Kwetu, bali mpango ulikuwa ni kwamba awe anaishi pamoja Nasi, awe anaendelea kuongezeka katika ufanano Nasi, na awe anatenda mambo kadiri ya ile ile mitindo yetu. Ni kwa sababu hiyo nilikuwa nikitaka matendo yake yote yawe yakitendeka ndani ya Utashi Wangu, ili kumpatia mahali patakapomfaa kutengenezea kamto kake katika ile bahari kuu ya Utashi Wangu.

Mimi nilikuwa nikitenda kama yule baba, ambaye, kwa vile alikuwa akimiliki maeneo makubwa ya ardhi, alisema kwa mwanae: ‘Mimi ninakupa mamlaka ya kumiliki makao makuu ya milki zangu, ili kusudi, wewe usitoke nje ya mipaka yangu, na ili uwe unakua ndani ya huu utajiri wangu mwingi, huku ukiwa na uadhimu ule ule wa kwangu, na ukiwa na ule ule ukuu wa kazi zangu, ili hatimaye, watu wote wapate kukutambua na kukukiri kuwa wewe ni mwanangu’.

Sasa, je, tutaweza kusema nini mintarafu mtoto yule, kama asingekubali kupokea ile zawadi kuu ya baba, kama angeondoka na kwenda kuishi katika nchi ya kigeni yenye mahangaiko na ya taabu, na kama angejishusha na kujihinisha chini ya utumwa wa maadui katili? 

Hivyo ndivyo alivyokuwa binadamu.

Basi, mpango huo, na kale kamto ndani ya Utashi Wangu, ninautaka kutoka kwako wewe: kila moja ya mawazo yako litiririkie ndani ya Utashi Wangu, ili, katika picha–kioo ya akili Yetu, ambayo ni lile wazo la kila mtu, hilo wazo lako lipande juu ya kila akili na likatuletee Sisi ile heshima ya kila wazo, lakini katika mtindo wa kimungu. 

Maneno yako na hata kazi zako nazo zitiririke pia ili katika picha-kioo ya Neno letu ‘FIAT’, ambalo ndilo katengeneza vitu vyote, na ambalo pia ni neno la kila mtu, na katika picha-kioo cha utakatifu wa kazi Zetu, utakatifu ambao ni uhai na ujimudu wa kila kitu, hayo maneno yako na hizo kazi zako, ziweze kupanda juu na kuendelea kuruka juu ya kila kitu, ili kuweza kutupatia Sisi ule utukufu wa kila neno na wa kila kazi, pamoja na lile neno Letu Wenyewe la FIAT, na pamoja na ule ule utakatifu wa kazi Zetu.

Binti Yangu, kama kila kitu kilicho ni cha kibinadamu - hata ikiwa ni wazo moja tu - hakitatendeka ndani ya Utashi Wangu, ule mpangilio wa kibinadamu hautaweza kutwaa umiliki, na kale kamto hakatatengenezwa, na Utashi Wangu hautaweza kuteremka kuja hapa duniani, ili uweze kujulikana na uweze pia kutawala”

Nilipoyasikia maneno hayo, mimi nikamwambia: ‘Ewe Yesu Pendo Langu, inakuwaje kwamba, baada ya karne nyingi zote hizi za uhai wa Kanisa, ambalo limekwisha kutoa Watakatifu wengi hivi - na wengine wengi wa hao wameweza kuishangaza Mbingu na dunia kwa fadhila zao na kwa miujiza waliyoitenda - iweje watakatifu hao hawajafikia kutenda kikamilifu ndani ya Utashi wa Mungu, ili kuweza kutengeneza ule mpangilio unaouzungumzia? Hivi ulikuwa unaningojea nije kutekeleza mimi tu, mimi nisiyeweza kitu kabisa, niliye mdogo na mbaya kabisa, na pia niliye mjinga kabisa? Hilo ni karibu halisadikiki kabisa’.  

Na Yesu akasema: 

“Ebu angalia Binti Yangu, hekima Yangu ina mbinu na njia zake ambazo binadamu huwa anazisahau, kiasi kwamba, huwa analazimika kuteremsha panda lake la uso na kuiabudu katika ukimya wa mtu bubu. Na wala si suala lake binadamu kuniamrishia Mimi juu ya sheria na taratibu, juu ya nani nimchague, na juu ya muda muafaka ambao wema Wangu unauandaa. Aidha, kabla ya yote ilinipasa kwanza niwatengeneze Watakatifu ambao wangetakiwa kufanana Nami, na ambao wangenakili Ubinadamu Wangu kwa namna iliyo kamilifu zaidi, kadiri inavyowezekana kwao wenyewe. Na hilo nimekwisha kulitekeleza tayari.

Sasa wema Wangu unataka kusonga mbele zaidi, na unataka  kusalimu amri kwa viwango vikubwa zaidi vya pendo-pindukia.

Na kwa sababu hiyo ninataka watu waingie kwanza ndani ya Ubinadamu Wangu, na pale wakanakili kile ambacho roho ya Ubinadamu Wangu ilitenda ndani ya Utashi wa Mungu.

Kama wale wa kwanza wameweza kushirikiana na Ukombozi Wangu kwa ajili ya kuwaokoa watu, kwa ajili ya kuwafundisha sheria, kwa ajili ya kuifukuza dhambi, licha ya kuzuilika kwa kiasi fulani kutokana na nyakati za kila karne walimoishi, wale wa pili wataweza kusonga mbele zaidi kwa kunakilisha kile ambacho roho ya Ubinadamu Wangu ulikitenda ndani ya Utashi wa Mungu.

Hao watu watazikumbatia karne zile zote, watawakumbatia wanadamu wote, na kwa kuinuka na kwenda kuwa juu ya watu wote, watazihuisha zile haki za Uumbaji ambazo wananiwia Mimi na zile zinazowahusu wao wanadamu. Watarejesha mambo yote kwenye ule mwanzo wa asilia wa wakati wa Uumbaji na watalirejesha lile lengo ambalo kwalo Uumbwa ulitoka.

Mambo yote yamepangwa kwa utaratibu ndani ya Mimi: Kama Mimi niliuleta Uumbwa, basi na wenyewe budi urejee Kwangu ukiwa katika taratibu, na kwa namna ile ulivyotoka katika mikono Yangu.

Ule mpango wa kwanza wa matendo ya binadamu uliokuwa umegeuzwa ukawa ni wa kimungu ndani ya Utashi Wangu, ulikuwa umefanyika na Mimi. Mpango huo niliusimamisha ukawa kama unasubiri, na mwanadamu hakuwa amejua lolote juu ya hilo, isipokuwa Mama Yangu Mpenzi asiyeweza kutenganika Nami. Hiyo ilikuwa ni lazima. Kama binadamu alikuwa haijui njia ya kupita, hakujua mlango, na hakuvijua hata vyumba vya Ubinadamu Wangu, je angewezaje kuingia ndani Yangu Mimi na kuanza kunakili na kuiga kile nilichokuwa nikitenda?

Sasa ndio umefika wakati kwa mwanadamu kuweza kuingia ndani ya mpango huo na anaweza kuanza hata kutenda mambo fulani ya kwake ndani ya mambo ya Kwangu. Hivi sasa ni ajabu gani kama Mimi nimekuita wewe kuwa mtu wa kwanza?

Aidha, ni kweli kabisa kwamba Mimi nimekuita wewe kama mtu wa kwanza. Ni kweli kwani, kwa mtu mwingine yeyote yule, hata kama ni mpenzi Kwangu, Mimi sijawahi kuelezea namna ya kuishi ndani ya Utashi Wangu, juu ya matokeo yake, juu ya maajabu yake, na juu ya zile faida ambazo hupata mwanadamu yule anayetenda ndani ya Utashi Mkuu wa Juu.

Unaweza ukachunguza maisha ya Watakatifu wengi kadiri unavyotaka, na hata chunguza vitabu vya mafundisho ya imani - ndani ya hata Mtakatifu moja au ndani ya kitabu kimoja hutaweza kuyaona yale maajabu ya Utashi Wangu ukitenda kazi ndani ya mwanadamu na utashi wa mwanadamu ukitenda kazi ndani ya Utashi Wangu.

Sana sana, utakuta mtu akijikabidhi na tashi hizo mbili zikiungana, lakini, katika yeyote yule, hutaona Utashi Wangu ukitenda kazi ndani ya utashi wa binadamu na utashi wa binadamu ukitenda kazi ndani ya Utashi Wangu.

Hiyo ina maana kwamba, muda ulikuwa bado haujawadia kwa Ukarimu Wangu kupasika kumwita binadamu aje kuishi katika hali hiyo ya juu kabisa.

Hata huo mtindo ninaokufundisha kusali hutaukuta ndani ya mtu mwingine.

Basi, angalia uwe makini sana. Hukumu Yangu ya Haki inataka lazima nitekeleze, lakini Pendo Langu linalia kwa dukuduku. Kwa hiyo, Hekima Yangu inaandaa mambo yote kwa ajili ya kufikia lengo. Kutoka kwako wewe Sisi tunapenda tupate haki na utukufu wa Uumbaji”.

Juzuu na. 14 ku download - click here

Kila siku, hatua kwa hatua, jisomee hapa, ili upate kukua katika Paji la Uhai, ndani ya UTASHI WA MUNGU, kulingana na Mafundisho aliyoyatoa YESU kwake Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA

Swahili - Telegram Channel: Utashi Wa Mungu Na Upendo Wa Mungu

Swahili - Telegram Channel: Saa 24 Za Mateso Ya Bwana Weto Yesu Kristo

English - Telegram Channel: Divine Will Divine Love

English - Telegram Channel: The Virgin Mary in the Kingdom of the Divine Will

Français - Chaine de Telegram: Divine Volonte Divin Amour

Français - Chaîne de Telegram: Lettres de Luisa Piccarreta

Lingala - Chaine de Telegram: Mpo Elingi Nzambe Bolingi bwa Nzambe

Website all languages: www.divinewilldivinelove.com

Vitabu yote vilivyo katika faili za PDF vinaweza kupakuliwa bila gharama yoyote ile wakati wote ule. Pia, upo huru kabisa kuchapisha VITABU hivyo wewe mwenyewe binafsi au kuchapisha kwenye kiwanda chochote kile. Lakini vitabu hivyo ni kwa matumizi binafsi tu na siyo kwa ajili ya biashara! Hata hivyo una ruhusa ya kuwashirikisha na kuwapatia watu wengine vitabu hivyo kadiri unavyopenda!!

Swahili landing page: click here

English landing page: click here

Lingala landing page: click here

Kikongo landing page: click here

French landing page: click here

Italian landing page: click here

Report Page