Yesu kwa Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - KITABU cha MBINGU - JUZUU na. 30 - Desemba 25, 1931🖋📄📖📔
Najihisi nimezama katika mafuriko ya bahari ya mwanga wa Utashi wa Mungu. Oh! Ni jinsi gani ningependa niwe ni kasamaki kadogo kabisa ndani ya bahari hii, niwe ni kasamaki kasikoona kitu kingine isipokuwa mwanga tu, kasamaki kanakogusa mwanga tu, kanakopumua mwanga tu na kanakoishi mwanga tu. Oh! Ni jinsi gani ningefurahia kuambiwa kuwa mimi ndiye Binti ya yule Baba wa Mbinguni. Lakini, pindi nilipokuwa nikiwazia hilo, pamoja na mambo mengine, ndipo Yesu, Uhai Wangu Mpenzi, Mtamu Wangu na Mwenye Mamlaka, alikuja kutembelea roho yangu, huku akijionyesha mwenyewe akiwa na mabahari makubwa mno ya mwanga yasiyo na mipaka, yakitokea ndani ya Nafsi Yake abudiwa. Na kutoka ndani ya mwanga huo zilijitokeza roho za watu wengi sana waliokuwa wakijaza sana Mbingu yote na dunia yote. Hapo Yesu aliniita na kuniambia:
“Binti Yangu, njoo ndani ya mwanga huu. Ninakutaka uwe hapa. Nguvu ya mwanga Wangu na ujimudu wake, kama chemchemi ya Uhai, hautendi kitu kingine isipokuwa kutoa na kuachilia roho mbalimbali – yaani ni kutoa na kuachilia Uhai wa wanadamu – kutokea tumboni mwa mwanga. Uwezo Wake ni mkali sana kiasi kwamba, kadiri mwanga huo unavyojimudu, au kutikisika, ndivyo unavyozidi kutoa na kuachilia roho mbalimbali. Mimi nataka mpendwa Wangu awe pamoja Nami ndani ya tumbo la mwanga Wangu – yaani ndani ya tumbo la Utashi Wangu. Kadiri roho zinavyozidi kutengenezwa na kutolewa nje, Mimi sipendi nikabaki peke Yangu, bali nataka uwe unakaa na Mimi hapa, ili uwe unatambua hilo tukio kuu la kutengeneza roho mbalimbali – yaani, Pendo Letu Kuu Kupindukia. Na kwa vile ninakutaka wewe uwe unabaki ndani ya Utashi Wangu, ninapenda kuziweka roho hizi na kuzihifadhi na kuzikabidhi ndani yako wewe. Siwezi kuziacha peke yao, wakati zinaposafiri kama wahujaji hapa duniani, bali nataka ziwe na mtu mwingine anayezisindikiza na ambaye, akiwa pamoja nami, atakuwa pia ndiye anayezilinda badala Yangu.
Oh! Ni tamu ilioje kusindikizwa na mtu yule, ambaye anatunza Uhai wa watu mbalimbali uliotoka ndani Yangu Mimi. Hii inanifurahisha sana hivyo kiasi kwamba, ninapendelea kumchukua mtu anayeishi katika Utashi Wangu, na kumfanya awe ni hifadhi ya shughuli ya utengenezaji wa roho, awe ndiye mfereji ninamozipitishia roho hizo, pale ninapozitoa nje kwenye mwanga, na pia anakuwa ndiye mfereji wa kuzipitisha roho hizo, ili kuzirudisha katika makao ya Mbinguni. Ninapenda kutoa kila kitu na kumpa mtu yule ambaye anapenda kuishi ndani ya FIAT Yangu. Usindikizi wa watu hao ni wa lazima kabisa kwa ajili ya Pendo Langu, kwa ajili ya kuwamwagia na kuwapumulia mambo Yangu nje, na kwa ajili ya kazi Zangu kwani zenyewe zinataka zijulikane. Kuwa na matendo ambayo hayajulikani huwa sawa na kazi ambazo haziwezi kujivunia chochote, wala haziwezi zikaimbilia ushindi wowote wala utukufu wowote. Kwa hiyo, basi wewe usinikatalie kuwa msindikizi Wangu. Ukifanya hivyo utakuwa unamgomea Yesu Wako mahali pa kupumulia Pendo Lake, na halafu kazi Zangu zingekosa kuwa na wasindikizi na hivyo zingekosa kutambulikana na kukosa kupata heshima na wala kuthaminiwa na mwanadamu. Zingebaki kuwa kama kazi peke, na moja moja. Na hapo, Pendo Langu, baada ya kulazimishwa na hali hiyo, lingegeuka kuwa ni suala la haki basi”.
Baada ya hayo yote, nikawa natafakari juu ya Mtoto Yesu, hasa katika tendo lake la dakika alipotoka tumboni mwa Mama Yake. Mtoto wa Mbinguni aliniambia:
“Binti Yangu mpenzi sana, ni lazima ufahamu kuwa, mara tu nilipojitoa nje ya gereza la tumbo la Mama Yangu, nilionja sana hitaji la Pendo la Kimungu na hitaji la upenzi. Elewa kwamba nilikuwa nimetoka kumwacha Baba Yangu wa Milele pale katika Mbingu za juu, ambapo tulikuwa tukipendana kwa Pendo timilifu kabisa la Kimungu. Pale kila kitu kilikuwa ni cha Kimungu tu kati ya Sisi Nafsi Tatu – yaani, upenzi wetu, utakatifu wetu, maweza na mengineyo. Sasa nilipokuwa nakuja duniani, sikutaka nibadili zile namna zangu za kufanya mambo. Utashi Wangu wa Kimungu uliniandalia Mama wa Kimungu, kwa jinsi kwamba nikawa ninaye Baba wa Kimungu Mbinguni na Mama wa Kimungu hapa duniani. Kwa hiyo basi, mara tu nilipotoka tumboni mwa Mama, nikiwa ninaonja lile hitaji kali kabisa la Pendo la Kimungu na upenzi wa Kimungu, nilikimbilia mara mikononi mwa Mama Yangu kwenda kupokea Pendo lake la Kimungu, ambalo ndilo likawa ni chakula Changu cha kwanza, likawa ndiyo pumzi Yangu ya kwanza na likawa ndilo tendo la kwanza kabisa kwa ajili ya Uhai wa Ubinadamu Wangu Mdogodogo. Na Yeye Mama, pale pale alinitolea yale mabahari ya pendo la Kimungu ambalo FIAT Yangu ilikuwa imetengeneza ndani yake. Basi Mama akanipenda kwa Pendo hilo la Kimungu, sawa kama vile Baba Yangu alivyokuwa kanipenda pale Mbinguni. Na Oh! Ni furaha ilioje niliyoipata! – Nilikuwa nimeipata Paradisi Yangu katika lile pendo la Mama Yangu.
Lakini unajua kwamba, Pendo la kweli huwa halifikii kusema ‘yatosha’. Kama lingefikia kusema ‘yatosha’, hapo lingepoteza tabia yake asilia ya Pendo la Kimungu la kweli. Kwa minajili hiyo, hata kutoka pale mikononi mwa Mama Yangu, wakati ule niliponyonya, nilipokuwa napumua, nilipokuwa napata upendo, nilipokuwa napata ile Paradisi aliyokuwa akinipa, Pendo Langu Mimi lilikuwa linapanuka, linaenea na kuwa bahari kuu iliyobeba ndanimo karne zote. Pendo Langu lilitafuta hapa na pale, lilikimbia huko na huko, liliita kila mahali, lilisaka na kuwinda popote kwani lilikuwa linawataka watoto wake wa Kimungu. Nao Utashi Wangu, ili kulituliza Pendo Langu, uliwaleta Watoto wa Kimungu mbele Yangu, watoto ambao Utashi wenyewe utawatengeneza kwa ajili Yangu katika kila karne. Mimi niliwatazama, nikawakumbatia, nikawapenda, na nikapata pumzi mbalimbali ya upenzi wao wa Kimungu. Hapo nikagundua kuwa Malkia wa Mungu hataweza kubaki peke yake, bali atakuwa amezungukwa na kizazi chote cha watoto wa Kimungu wa kwake na wa Kwangu.
Utashi Wangu ndio unaojua namna ya kugeuza hata kuweza kuleta mabadiliko na kutengeneza vipandikizi kutoka vile vya kibinadamu na kuvifanya viwe ni vya Kimungu. Kwa hiyo ninapokuacha wewe sasa ukitenda mambo ndani ya Utashi Wangu, ninaonja kabisa kuwa ninapewa na ninakabidhiwa tena ile ile Paradisi ambayo Mama Yangu alikuwa amenipa pale aliponishika kwa mara ya kwanza katika mikono yake wakati nilipokuwa bado Kichanga. Kwa hiyo, wale wanaotekeleza Utashi Wangu, na wanaoishi ndani yake, wanaamsha na wanatengeneza lile tumaini tamu na nzuri, na la kupendeza la kuwa Ufalme wa Utashi wa Mungu utafika duniani, na Mimi nitakuwa ninafurahia katika Paradisi ya mwanadamu ambayo FIAT Yangu imetengeneza ndani yao”.
Wakati huo nilipoendelea kutafakari juu ya yale ambayo Yesu amenieleza, Yeye, kwa Pendo kali sana na laini zaidi, aliongeza kusema:
“Binti Yangu mwema, Pendo letu Sisi huwa linakimbilia daima kumwelekea mwanadamu. Ujimudu wetu wa kupenda, ambao kamwe huwa haukomi, unaendelea kukimbia ndani ya mapigo ya Moyo, katika mawazo ya akili, katika kupumua kwa mapafu, na katika Damu inayozunguka mwilini. Ujimudu huo unakimbia – na unakimbia daima. Kwa nguvu ya noti za musiki wetu na kwa mwendo wa Pendo Letu, ujimudu huo wetu, unapita ukihuisha pigo la Moyo, unahuisha wazo na pumzi. Kwa jinsi hiyo, Pendo Letu linataka kukutana na pendo linalogonga moyoni, linataka likutane na pumzi inayopenda, na likutane na wazo linalopokea na linalotutolea Sisi pendo. Kwa vile Pendo la Kwetu Sisi huwa linakimbia kwa kasi kubwa mno isiyoshikika, pendo la mwanadamu linashindwa kulishika lile la Kwetu. Lenyewe pendo la binadamu linabaki nyuma, linashindwa kufuata mbio za Pendo Letu ambalo hukimbia bila kusimama popote. Sisi tunapoona kwamba pendo la mwanadamu linashindwa kutukuta, tunaamua kupita kuzungukia katika pigo la Moyo, katika pumzi yake, na katika kila nafsi nzima ya mwanadamu. Tunapoiona hali hii, tunafikia kulia kwa uchungu: ‘Pendo letu, kumbe halijulikani, wala halijapokelewa, na wala halipendwi na mwanadamu! Na mwanadamu anapolipokea, kumbe halijui bado. Oh! Ni jinsi gani ilivyo ni vigumu kupenda bila kuweza kupendwa!’.
Kwa upande mwingine, endapo Pendo Letu lingeacha kukimbia, basi Uhai wake ungekoma pale pale. Halafu, ingetokea kama inavyokuwa katika saa ya ukutani au nyingine yoyote. Kama mnyororo wa hiyo saa upo bado, mtu ataendelea kusikia sauti yake ya tic tic, na kwa uzuri kabisa saa inaendelea kuonyesha majira ya muda, yaani saa, na dakika na sekundi zake. Na kwa njia hiyo itakuwa ikitumika kutunza ratiba ya siku na pia kutunza taratibu ya umma. Lakini kama mnyororo ukisimama tu, ile tic tic haitasikika tena. Itasimama bila Uhai kama vile imekufa. Na kwa kukosekana kwa saa itembeayo, panaweza pakatokea fujo nyingi katika umma husika.
Mnyororo wa mwanadamu ni Pendo Langu. Pale mnyororo huo wa mbinguni unapotembea, Moyo huwa unapiga, Damu hutembea, na pumzi inatengenezwa. Vitendo hivyo unaweza ukaviita ni mifano ya muda wa saa, dakika na sekunde za saa ya ukutani ya Uhai wa mwanadamu. Endapo sitauwezesha kutembea mnyororo wa Pendo Langu, basi maana yake wanadamu hawataweza kuishi. Lakini pia, endapo Mimi sipendwi, ina maana kwamba Pendo Langu linapita na mbio zake huku likiingia katika hali ya kuwa Pendo linaloteseka na linalolia kwa uchungu kutaka kufa.
Sasa lakini, ni nani yule ambaye atatuondolea sisi hilo teso? Nani atakayenogesha huo uchungu wetu wa kukosa upenzi? Ni yule ambaye ataushika Utashi Wetu wa Kimungu kama Uhai wake. Utashi Wetu huo, ukiwa ndiyo Uhai, utatengeneza mnyororo ndani ya pigo la Moyo, ndani ya pumzi, na kadhalika, ndani ya kila kitendo cha mwanadamu. Utafanya pawezekane kutokea makutano mazuri na matamu kati ya Pendo la Kwetu na mnyororo wa Kwetu kwa upande mmoja, na pendo la kwao na mnyororo wao kwa upande mwingine. Halafu hivyo vitakuwa vikitembea sawa na pamoja. Tic tic endelevu ya kwetu Sisi itakuwa kila mara inafuatwa na Tic tic ya kwao wanadamu. Na Pendo Letu Sisi halitaachwa liwe linakimbia peke yake, bali litakuwa linakimbia pamoja na mwanadamu.
Basi, kwa hiyo Mimi sitaki kitu kingine isipokuwa Utashi Wangu. Utashi Wangu ndani ya Mwanadamu!”
Kila siku, hatua kwa hatua, jisomee hapa, ili upate kukua katika Paji la Uhai, ndani ya UTASHI WA MUNGU, kulingana na Mafundisho aliyoyatoa YESU kwake Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA
Swahili - Telegram Channel: Utashi Wa Mungu Na Upendo Wa Mungu
Swahili - Telegram Channel: Saa 24 Za Mateso Ya Bwana Weto Yesu Kristo
English - Telegram Channel: Divine Will Divine Love
English - Telegram Channel: The Virgin Mary in the Kingdom of the Divine Will
Français - Chaine de Telegram: Divine Volonte Divin Amour
Français - Chaîne de Telegram: Lettres de Luisa Piccarreta
Lingala - Chaine de Telegram: Mpo Elingi Nzambe Bolingi bwa Nzambe
Website all languages: www.divinewilldivinelove.com
Vitabu yote vilivyo katika faili za PDF vinaweza kupakuliwa bila gharama yoyote ile wakati wote ule. Pia, upo huru kabisa kuchapisha VITABU hivyo wewe mwenyewe binafsi au kuchapisha kwenye kiwanda chochote kile. Lakini vitabu hivyo ni kwa matumizi binafsi tu na siyo kwa ajili ya biashara! Hata hivyo una ruhusa ya kuwashirikisha na kuwapatia watu wengine vitabu hivyo kadiri unavyopenda!!
Swahili landing page: click here
English landing page: click here
Lingala landing page: click here
Kikongo landing page: click here
French landing page: click here
Italian landing page: click here