Yesu kwa Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - KITABU cha MBINGU - JUZUU na. 25 - Machi 25, 1929🖋📄📖📔

Yesu kwa Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - KITABU cha MBINGU - JUZUU na. 25 - Machi 25, 1929🖋📄📖📔


Lile zoezi langu la kujiachia ndani ya FIAT ya Kimungu huendelea. Pale katikati ya viumbe vyote nilikuwa naonja sana ule udogo wa roho yangu duni. Ndipo na mimi, nikiwa kana kwamba nina ujimudu wa peke yangu, kana kwamba ninazo mbio endelevu za peke yangu, zile mbio zangu za daima pale ndani ya Uumbwa wote, nikawa ninajionja kutotenganika kutoka kwa hiyo FIAT. Utashi wangu na ule wa Uumbwa vimekuwa ni kitu kimoja, yaani umekuwa ni ule mmoja na pekee, yaani, ni ule Utashi wa Mungu peke yake. Kwa hiyo, maadam Utashi wa wote ni moja tu, basi sote tunatenda kitu kimoja na kile kile, na sisi sote tunakimbia kana kwamba tunaelekea kwenye yale makao yetu ya kwanza, yaani, kwenda kule kwa Muumba Wetu, tunakwenda wote kumwambia:

‘Pendo Lako ndilo lililotuleta sisi duniani, na Pendo Lako hilo hilo ndilo linatuita turejee hapo ndani Yako, turejee kwa mbio za furaha na shangwe ili tukuambie: “Tunakupenda Wewe, tunakupenda Wewe”. Turejee kwako kwa mbio kuja kuimba zile sifa za lile Pendo Lako lisilozimika na wala lisilokoma’. 

Basi, kwa njia hiyo, tunatoka tena kule kwenye yale Makao Makuu Yake, ili tukaendelee na zile mbio zetu, ambazo huwa hazikatishwikatishwi. Hatufanyi kitu kingine chochote isipokuwa tunaingia na kutoka pale ndani ya lile tumbo Lake la Kimungu, kwa ajili ya kutekeleza ile ziara yetu ya pendo, yaani zile mbio zetu za kwenda kwa Muumbaji Wetu.

Basi, pindi nikikimbia pamoja na ule Uumbwa mzima ili kutekeleza mbio zangu za upendo kwa Ukuu Mtukufu wa Kimungu, Yesu Mpendevu Wangu wa daima, alijitokeza nje kutoka pale ndani mwangu, akaniambia:

“Binti Yangu, yule anayeishi ndani ya Utashi Wangu wa Kimungu huwa amefungiliwa kwenye Uumbwa wote: yaani, wala Uumbwa hauwezi ukafanya kitu bila huyu mwanadamu aliyebarikiwa, na wala mwanadamu huyu mwenyewe hawezi akajifungulia yeye mwenyewe na kujiachilia toka kwa vile viumbe.

Ni kwa sababu, maadam utashi wa mmoja wao na wa yule mwingine zimekuwa ni utashi moja tu, ambao ni ule Utashi Wangu wa Kimungu, hao wawili sasa wametengeneza mwili mmoja pekee wenye viungo vingi visivyoweza kutenganika kati yao. Kwa sababu hiyo Mimi ninapomwangalia mtu anayeishi ndani ya Utashi Wangu wa Kimungu, pale ndani yake huwa ninaiona ile anga yake. Ninaporejea kumwangalia tena ndipo ninaliona jua lake. Macho Yangu, yakiwa yametekwa na ule uzuri wake mkubwa mno, yanakaza juu yake na kumwangalia na ndipo yanaiona bahari yake. Kwa kifupi, Mimi, ndani yake huyo, ninaona zile aina mbalimbali zote za kila kitu kilichoumbwa, na ndipo huwa ninasema:

<<Lo! Ewe maweza ya FIAT Yangu ya Kimungu - ni jinsi gani unavyonifanyia awe mzuri na wa kupendeza huyu anayeishi ndani Yako. Wewe unampatia kipaumbele juu ya Uumbwa mzima, unamfanya ashinde mbio kwa kumsaidia kukimbia kwa spidi kali hivi hata anakimbia zaidi kuliko upepo. Anakimbia kupita na kushinda kila kitu hata anakuwa ndiye wa kwanza kuingia hapa katika makao Yangu Makuu, anawahi hapa kuja kuniambia: ‘Ninakupenda Wewe, Ninakutukuza Wewe, Ninakuabudu Wewe’. Na anapotengeneza mwangwi wake ndani ya Uumbwa wote, viumbe vyote huwa vinamwiga na kurudia kutamka vile viitikio vyake vitamu kabisa>>. 

“Binti Yangu, hii ndiyo hoja ya Mimi kushikwa na upendo mkubwa mno katika kukuelezea mambo yale yote yahusuyo Utashi Wangu wa Kimungu: yaani, chochote kila nilichokwisha kukuelezea juu ya Utashi Wangu, siyo kitu kabisa isipokuwa ni ule utaratibu wote wa Ufalme Wake. Na yote hayo yalitakiwa yawe yameelezwa tangu pale mwanzoni mwa Uumbaji kama Adamu asingekuwa ametenda dhambi, kwa vile, katika kila aina ya maelezo Yangu mintarafu FIAT Yangu ya Kimungu, binadamu alipasika akue na kuongezeka katika utakatifu na uzuri wa Yule Muumba Wake, na kwa hiyo, nilikuwa nimeazimia kutekeleza kidogokidogo, hatua kwa hatua, kwa kumpatia kwanza dozi ndogo ndogo za ule Uhai wa Kimungu, ili, kumfanya akue na kuongezeka kulingana na jinsi Utashi Wangu wa Kimungu ulivyokuwa ukitamani.

Kwa hiyo, kwa kutenda dhambi, binadamu alikatisha na kuvuruga yale mazungumzo Yangu na akaninyamazisha.

Baada ya hizi karne nyingi, ninapomtaka binadamu arejee ndani ya FIAT Yangu, Mimi, kwa upendo mkubwa mno, nimerejea tena kwenye yale mazungumzo Yangu.

Ninatenda hivyo, zaidi na kupita mama laini mwenye upenzi, anapopenda, na kutamani na kulilia kujifungua mtoto wake, anatamani na kumlilia ili kusudi aanze kumbusu, amfunike kwa upenzi mbalimbali, ili amfurahie, na ili amkumbatie na kumbania kwa nguvu pale kwenye kifua chake cha kimama, na hata kumjazia mema yake yote na raha zake mbalimbali zote. 

Basi ndivyo Mimi nilivyotenda pale niliporudia mazungumzo Yangu na pale nilipokuelezea wewe juu ya utaratibu wa ule Ufalme wa Utashi Wangu wa Kimungu, na nilipokuelezea njia na mtindo ambao mwanadamu budi aufuate pale ndani ya Ufalme Wangu.

Kwa sababu hiyo, kule kukueleza wewe zile kweli nyingi juu ya FIAT Yangu, hakikuwa kitu kingine, bali, imekuwa ni Mimi kuleta tena uwanjani ule utaratibu wote, na lile pendo lote ambalo ningekuwa nimeliendeleza kama binadamu asingetenda dhambi, na kama Ufalme Wangu ungekuwa umeendesha uhai wake hapa duniani.

Katika yale maelezo Yangu kwako nimekuwa nikizingatia kabisa ule utaratibu kwamba, ukweli moja huwa umeunganika kabisa na ukweli mwingine, kiasi kwamba, kama ukweli moja ukitaka kujiondoa na kujificha wenyewe, hapo kweli hizo zingesababisha ombwe katika Ufalme wa FIAT Yangu ya Kimungu, na zingeiondoa, katika wanadamu, nguvu fulani ya kuwasukuma na kuwawezesha kuishi ndani ya Ufalme Wangu.

Ni kwa vile, kila ukweli unaohusu Utashi Wangu wa Kimungu ni nafasi ambayo Utashi Wangu huwa unachukua na kutumia kwa ajili ya kutawala pale katikati ya wanadamu, na pia, kila ukweli huwa ni njia na ni ombwe ambavyo wanadamu huwa wanavipata kwa ajili ya kuweza kujipatia kweli zote.

Kwa hiyo basi, zile kweli zote nilizokueleza wewe zinahusiana kabisa kati yao zenyewe, kwa jinsi kwamba, kama mtu ataziondoa baadhi yao, basi mahali hapo zilipoondolewa, mtu angefikia kana kwamba anaona anga fulani bila nyota zozote zile, au, analiona ombwe fulani bila jua lolote, au kuiona ardhi bila maua yoyote yale.

Kwa kweli, katika kweli hizo zote nilizokuwa nimekueleza wewe, kuna ule uupyaisho wa Uumbwa mzima, na katika kila ukweli, FIAT Yangu, zaidi kuliko hata jua, huwa inatamani sana kujitokeza na kuingia uwanjani tena, sawa kama vile ilivyokuwa imetenda wakati wa Uumbaji.

Na wakati inapochukua uwanja wake wa utendaji, kwa nguvu ya ule mwanga Wake, huwa inataka kuyatia kiza yale maovu yote ya wanadamu, na kwa kuwafunika wanadamu wote kwa pazia lake la mwanga, FIAT huwa inataka kuwapatia wanadamu neema nyingi kabisa hata kufikia kuwapatia mkono Wake wa uumbaji, ili kuwawezesha kuingia tena pale ndani ya tumbo la Utashi Wake wa Kimungu.

Kwa hiyo, kila jambo nililokuwa nimekueleza wewe juu ya Utashi Wangu wa Kimungu lina umaana mkubwa hivi kwamba, linanigharimu Mimi hapa zaidi na kupita hata Uumbwa mzima.

Ni kwa vile jambo hilo ni uupyaisho wa huo Uumbwa, na pale ambapo tendo linaupyaishwa, hapo huwa linagharimu pendo maradufu. 

Na ili kuwa na uhakika zaidi, Sisi huwa tunaleta neema maradufu, na mwanga maradufu, ili vitolewe kwa wanadamu, ili kusudi, tuepuke kupata uchungu wa pili, labda hata uchungu wenye kutuumiza zaidi kuliko ule wa kwanza, tuliokuwa tumeupata pale mwanzoni mwa Uumbaji, pale binadamu alipotenda dhambi na kusababisha, ndani yake mwenyewe, kule kuanguka kwa Pendo Letu, na kushindwa kwa ule Mwanga Wetu, na kule kushindikana kwa ule urithi adhimu wa Utashi Wetu Mkuu wa Juu.

Ndiyo maana Mimi, ninaangalia sana sana kwamba, wewe usipoteze chochote kile ninachokueleza juu ya Utashi Wangu - kuna umuhimu mkubwa mno katika kweli hizo, kwa jinsi hii kwamba, kwa kuzificha baadhi yao, ingekuwa ni kana kwamba mtu angetaka kuliondoa jua toka pale mahali lilipo, au kama mtu angeifanya bahari iondoke nje ya ule ufuko wake. Je kungetokea nini kwa ardhi yote?

Hebu jaribu kulifikiria hilo wewe mwenyewe.

Ndivyo hivyo ingetokea endapo ungekosekana ukweli wowote kati ya zile kweli zote nilizokuwa nimekueleza wewe juu ya Utashi Wangu wa Kimungu, kweli zile nilizokuelezea kwa utaratibu mkubwa sana sana”.

Juzuu na. 25 ku download - click here

Kila siku, hatua kwa hatua, jisomee hapa, ili upate kukua katika Paji la Uhai, ndani ya UTASHI WA MUNGU, kulingana na Mafundisho aliyoyatoa YESU kwake Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA

Swahili - Telegram Channel: Utashi Wa Mungu Na Upendo Wa Mungu

Swahili - Telegram Channel: Saa 24 Za Mateso Ya Bwana Weto Yesu Kristo

English - Telegram Channel: Divine Will Divine Love

English - Telegram Channel: The Virgin Mary in the Kingdom of the Divine Will

Français - Chaine de Telegram: Divine Volonte Divin Amour

Français - Chaîne de Telegram: Lettres de Luisa Piccarreta

Lingala - Chaine de Telegram: Mpo Elingi Nzambe Bolingi bwa Nzambe

Website all languages: www.divinewilldivinelove.com

Vitabu yote vilivyo katika faili za PDF vinaweza kupakuliwa bila gharama yoyote ile wakati wote ule. Pia, upo huru kabisa kuchapisha VITABU hivyo wewe mwenyewe binafsi au kuchapisha kwenye kiwanda chochote kile. Lakini vitabu hivyo ni kwa matumizi binafsi tu na siyo kwa ajili ya biashara! Hata hivyo una ruhusa ya kuwashirikisha na kuwapatia watu wengine vitabu hivyo kadiri unavyopenda!!

Swahili landing page: click here

English landing page: click here

Lingala landing page: click here

Kikongo landing page: click here

French landing page: click here

Italian landing page: click here

Report Page