Yesu kwa Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - KITABU cha MBINGU - Juzuu na. 19 – Septemba 15, 1926🖋📄📖📔

Yesu kwa Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - KITABU cha MBINGU - Juzuu na. 19 – Septemba 15, 1926🖋📄📖📔


Baada ya kufanya kazi ya kuandika kwa masaa manne na zaidi, nilijiona nimechoka kabisa na nimeishiwa nguvu. Nikiwa nimeingia katika dakika za kusali, kama nilivyozoea, nikisali katika Utashi Wake Mtukufu, Yesu Wangu Mtamu, alikuja nje toka ndani mwangu, alinikumbatia kwa upenzi wote na akaniambia:

“Binti Yangu, umechoka, jipumzishe mikononi Mwangu. Jinsi gani na ni kiasi gani huu Ufalme wa FIAT Kuu unavyotugharimu Mimi na wewe wakati ambapo wanadamu wengine wote au wanalala usiku, wengine wanastarehe na wengine wanafikia hata kunitukana. Kwangu Mimi na kwako wewe hakuna nafasi za mapumziko hata iwe ni usiku: Wewe unabanwa na kuandika na Mimi ninakuwa nikikulinda, ninakusogezea maneno ya kuandika, na ninakusogezea mafundisho mintarafu Ufalme wa Utashi Mkuu. Na pale ninapokuona ukiandika, Mimi ninakuwa nikikushikilia mikononi Mwangu kwa ajili ya kukusaidia uwe unaendelea badala ya kuchoka haraka. Nafanya hivyo kusudi uandike kile nipendacho Mimi, ili uweze kufikisha mafundisho yote, haki zote, upendeleo wote, utakatifu na utajiri usio na kikomo uliopo katika Ufalme huu. Laiti ungelijua jinsi na kiasi gani ninavyokupenda, ninavyokufurahia, ninapokuona unajitolea hata usingizi wako, na nafsi yote ya wewe mwenyewe, kwa ajili ya kuipenda FIAT Yangu inayotaka ijulikane kwa vizazi vya binadamu! Inatugharimu sana, ni kweli kabisa Binti Yangu. Na Mimi, kwa ajili ya kukulipa, karibu kila mara, kila baada ya kuwa umeandika, huwa ninakupatia fursa ya kupumzika juu ya Moyo Wangu uliochoka na kuvunjika kwa maumivu na kwa Pendo. Umevunjika kwa maumivu kwa vile Ufalme Wangu haujafahamika bado, na umevunjika kwa Pendo kwani nina hamu kubwa ya kufanya Ufalme huo ujulikane. Ninakupumzisha juu ya Moyo Wangu kusudi wewe unaposikia na kuonja teso Langu na moto unaoniunguza, uweze kutolea sadaka ya nafsi yako yote bila kujisaza katika chochote kwa ajili ya ushindi wa Utashi Wangu”.

Kishapo, wakati nipo bado mikononi mwa Yesu, ule Mwanga mkubwa kabisa wa Utashi wa Mungu, uliokuwa unaijaza Mbingu na dunia, ukawa unaniita nitembee kuzunguka ndani yake ili uniwezeshe kutekeleza matendo yangu ya kawaida, ili kuniwezesha kurekodisha sauti yangu na kauli yangu ya ‘nakupenda’, ili kuniwezesha kufanya uabudu wangu ndani ya Uumbwa wote. Utashi huo uliniita ili upate kusindikizwa na uwepo wa Binti Yake Mdogo katika kila kitu kilichoumbwa ambamo ulikuwa ukitawala na kuamrisha. Basi, baada ya kutekeleza hilo, Yesu Wangu Mtamu aliniambia:

“Binti Yangu, ni mwanga ulioje, ni uwezo ulioje na ni utukufu ulioje, kujipatia lile tendo la mwanadamu linalotekelezwa katika Utashi Wangu! Matendo hayo huwa ni zaidi ya jua ambalo pindi likiwa bado juu angani, mwanga wake hupiga na kupofusha hata nyota na hujaza dunia yote na kufikisha busu lake kwa vitu vyote, hufikisha joto lake na hufikisha faida zote na mema yote yanayotokana nalo. Ni tabia yake mwanga kuenea na kusambaa. Wala hauhitaji kufanya kazi ya ziada kwa ajili ya kutoa kwa binadamu anayetaka, manufaa yale ambayo huo mwanga unashikilia kwa asili yake.

Matendo yanayofanyika katika Utashi Wangu huweza kufananishwa na tabia hiyo ya jua: Wakati unapoanza tendo fulani, Utashi Wangu unaingiza au kutia mwanga wake ili kutengeneza jua. Jua hilo hujipandisha au kujiinua juu kwa vile ndiyo tabia asilia ya jua kukaa na kubaki juu na siyo chini. Vinginevyo jua lisingeweza kutenda mazuri mengi kama linavyofanya, kwani vitu vilivyo chini vipo daima katika hali ya kuzungukwa, vipo kimoja kimoja binafsi, ni vitu vya muda mfupi, ni vitu vilivyofungamana na mahali fulani, siyo vitu vyenye manufaa ya ulimwengu mzima wala havijui kuzalisha manufaa mapana ya kiulimwengu. Kumbe jua hilo lililotengenezwa na Utashi Wangu na kwa tendo la mwanadamu, hujiinua lenyewe juu hadi kwenye kiti cha utawala cha Mungu wake, na halafu husababisha kupatwa halisia, yaani kupatwa kwa Mbingu, kwa Watakatifu na kwa Malaika. Urefu wa mionzi yake unagonga moja kwa moja hadi juu ya dunia. Mwanga wake uliojaa mema hufikisha hadi mbinguni utukufu, furaha, na raha. Papo hapo unafikishwa duniani mwanga wa zile kweli, unafukuza giza, mateso yatokanayo na dhambi na kufukuza udanganyifu wa mambo yapitayo.

Jua ni moja tu, lakini mwanga wake unashika ndani yake aina zote za rangi na ndanimo pia mna nguvu zote zinazoleta uhai kwenye ardhi. Kadhalika tendo la Utashi ni moja na jua linalotengenezwa katika Utashi Wangu pia ni moja. Lakini mema yatokayo humo na matokeo yanayoletwa na jua hilo ni mengi mengi. Kwa hiyo Ufalme wa FIAT Kuu utakuwa ni Ufalme wa mwanga, Ufalme wa utukufu na wa ushindi. Usiku wa dhambi hautaingia humo bali Ufalme huo utakuwa ni mchana kamili na daima. Mionzi mikali ya mwanga wa Ufalme itaangaza na kupenya hivi, hata kujipatia ushindi wa kupanda na kutoka kwenye lile lindi kilimoangukia kizazi cha wanadamu. Kwa sababu hiyo nimekuwa nakuambia mara kwa mara: 'Kwa kitendo cha Mimi kukukabidhi Utashi Wangu wa Kimungu, jukumu lako wewe ni kubwa sana’ kwani, kwa kuufanya Utashi Wangu ujulikane, wewe utaokoa zile haki za vizazi vya wanadamu, haki zilizokuwa hazijulikani kwao kwa muda mrefu sana. Faida zitakazotokana na kazi hiyo zitakuwa ni kubwa kweli kweli. Ndipo wewe na Mimi tutapata furaha mara dufu kwa kazi tutakayokuwa tumeitekeleza kwa ajili ya kujenga Ufalme huo”.

Baada ya hapo nikawa nafikiri peke yangu: “Huyu Mpendwa Wangu Yesu ananieleza tu mambo mengi sana ya kustaajabisha. Lakini kwa kuonekana na kwa nje hatuoni chochote cha mambo hayo ya ajabu. Laiti pangekuwa na uwezekano wa kuyaona makuu haya, pangekuwa na uwezekano wa kuziona zile faida zake kubwa, uwezekano wa kuona ile furaha iliyopo ndani ya Ufalme, hakika uso wa dunia hii ungebadilika, na ndani ya mishipa ya binadamu kungetiririka popote damu iliyo safi, damu takatifu, damu azizi kiasi kwamba hata maumbile yenyewe yangebadilika na kujipatia utakatifu, furaha, na amani inayodumu daima”. Pindi nilipokuwa nawaza hayo, Yesu alijitokeza ndani yangu na akawa ameniambia:

“Binti Yangu, huo Ufalme wa FIAT Kuu budi kwanza uanzishwe vema kati ya Mimi na wewe, ni budi Ufalme tuujenge vizuri, ni budi Ufalme ukomae vizuri. Kishapo ni budi Ufalme uwafikie watu na uenee kwa watu. Hilo lilikwisha kutokea kati ya Mimi na Bikira. Kwanza Mimi nilijitengeneza Mwenyewe ndani yake; nilikuwa tumboni mwake, nilipata lishe Yangu pale kifuani pake. Tuliishi pamoja hata kuunda uhusiano wa ana kwa ana katika kupendana na kuhudumiana kwa utaratibu wa ‘toka kwako na kwa ajili yako’ kana kwamba kusingekuwepo na mtu mwingine. Na kati yetu tuliujenga Ufalme wa Ukombozi. Halafu uhai Wangu mwenyewe niliutoa na kuufikisha kwa wanadamu wengine wote. Nilifikisha kwao pia matunda yote ya Ukombozi yaliyotokana na uhai Wangu wenyewe.

Ndivyo itakavyokuwa na FIAT Kuu: Kwanza tutatekeleza kati yetu sisi wawili, wewe na Mimi peke yetu, kwa wewe na kwa ajili ya wewe. Ufalme ukiisha kujengwa kati yetu, itakuwa ni jukumu langu Mimi kwani rahisi zaidi kufanikisha vema kazi fulani iwapo kwa vyovyote utekelezaji wake unaanza na wawili tu, peke yao, katika siri ya ukimya wa watu wawili wanaopenda sana ile kazi. Kazi ikiisha kuanzishwa itakuwa ni rahisi kuizindua na kuwagawia watu wengine kama zawadi. Basi uniache Mimi kwanza nifanye kazi Yangu, wewe usiwe na wasiwasi”.

Deo Gratias![1]

[1] Shukrani kwa Mungu


Juzuu na. 19 ku download - click here

Kila siku, hatua kwa hatua, jisomee hapa, ili upate kukua katika Paji la Uhai, ndani ya UTASHI WA MUNGU, kulingana na Mafundisho aliyoyatoa YESU kwake Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA

Swahili - Telegram Channel: Utashi Wa Mungu Na Upendo Wa Mungu

Swahili - Telegram Channel: Saa 24 Za Mateso Ya Bwana Weto Yesu Kristo

English - Telegram Channel: Divine Will Divine Love

English - Telegram Channel: The Virgin Mary in the Kingdom of the Divine Will

Français - Chaine de Telegram: Divine Volonte Divin Amour

Français - Chaîne de Telegram: Lettres de Luisa Piccarreta

Lingala - Chaine de Telegram: Mpo Elingi Nzambe Bolingi bwa Nzambe

Website all languages: www.divinewilldivinelove.com

Vitabu yote vilivyo katika faili za PDF vinaweza kupakuliwa bila gharama yoyote ile wakati wote ule. Pia, upo huru kabisa kuchapisha VITABU hivyo wewe mwenyewe binafsi au kuchapisha kwenye kiwanda chochote kile. Lakini vitabu hivyo ni kwa matumizi binafsi tu na siyo kwa ajili ya biashara! Hata hivyo una ruhusa ya kuwashirikisha na kuwapatia watu wengine vitabu hivyo kadiri unavyopenda!!

Swahili landing page: click here

English landing page: click here

Lingala landing page: click here

Kikongo landing page: click here

French landing page: click here

Italian landing page: click here

Report Page