Yesu kwa Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - KITABU cha MBINGU - JUZUU na. 18 - Agosti 15, 1925🖋📄📖📔

Yesu kwa Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - KITABU cha MBINGU - JUZUU na. 18 - Agosti 15, 1925🖋📄📖📔


Mimi nilikuwa nikiendelea na zoezi langu la kujiyeyushia mimi mwenyewe ndani ya Utashi wa Mungu kwa minajili ya kumrudishia Yesu Wangu upendo wangu mdogo na shukrani kwa yale yote aliyoutendea uzao wa binadamu katika Uumbwa. Ndipo Yesu Wangu Mpendwa, huku akija ndani mwangu, akitaka kuongeza thamani kwenye upendo wangu mdogo, akaanza kutenda na yeye vitendo vile nilivyokuwa nikifanya mimi. Pindi akifanya hivyo aliniambia hivi:

“Binti Yangu, vitu vyote vilivyoumbwa vilikuwa vimefanywa kwa ajili ya binadamu, na kwa hiyo, vyote vinakimbilia kuelekea kwake binadamu. Vitu hivi havina miguu, lakini vyote vinatembea, vyote vina mwendo fulani au wa kumfikia binadamu au mwendo wa kujifanya vifikiwe naye binadamu. Mwanga wa jua huanza kule juu kabisa kwenye Mbingu ili kuweza kumfikia mwanadamu, ili kumwangazia na ili kumpasha joto. Maji hutembea hadi kuweza kufikia matumboni mwa mwanadamu ili kutuliza kiu chake na ili kumburudisha. Mmea, mbegu, hutembea, hukausha ardhi, hutengeneza tunda lake kwa ajili ya kujitoa kwake binadamu. Hakuna kitu chochote kilichoumbwa ambacho hakichukui hatua fulani au kufanya mwendo fulani kuelekea kwa yule ambaye kwake Mtengenezaji Mkuu alikuwa amekielekeza kitu hicho wakati wa uumbaji, yaani kuelekea kwa binadamu. Utashi Wangu Mimi unazingatia kabisa utaratibu, harmonia, na unashikilia vitu vyote katika njia inayokwenda kwa wanadamu, na kwa namna hiyo, ni Utashi Wangu ndio unaotembea daima katika vitu vilivyoumbwa ukielekea navyo kwa mwanadamu. Hausimami kamwe. Upo daima katika mwendo na umejaa mwendo ukielekea kwa yule ambaye anampenda mno – mwanadamu. Lakini ajabu, ni nani anayewazia kusema asante kwa Utashi Wangu ambao unamletea mwanga wa jua, unamletea maji ya kunywa ili kutuliza kiu chake, unamletea mkate kushibisha njaa yake, unamletea tunda, unamletea ua kwa ajili ya kumburudisha, na unamletea vitu vingine vingi vingi sana ili kumfanya afurahi? Je si neno la haki tu kwamba, kama Utashi Wangu Mimi unafanya kila kitu kwa ajili yake, binadamu huyo naye afanye kila liwezekanalo ili kutimiza Utashi Wangu?

Oh, laiti ungejua wewe, sherehe unayofanya huu Utashi Wangu, ndani ya vitu vilivyoumbwa, wakati ule unapomtumikia na unapoambatana na mtu ambaye anatimiza Mapenzi Yangu! Utashi Wangu unakuwa umekaa na unatenda kazi ndani ya mwanadamu na Utashi Wangu ule unaotenda kazi ndani ya vitu vingine vilivyoumbwa, pale vinapokutana pamoja huwa wanabusiana, wanapatanisha mambo, wanafanyiana upendano na wanatunga hata utenzi, wanafanya na uabudu kwa Muumba Wao. Hapo hutokea lile tukio kubwa kabisa la Uumbwa wote. Vitu vilivyoumbwa hujiona na kujisikia vimepewa heshima kubwa sana wakati vinapokuwa vikimtumikia mwanadamu ambaye ndanimo amehuishwa na ule Utashi Wenyewe, ambao ndio unatengeneza uhai ule wa kwao. Kinyume chake lakini, huo Utashi Wangu Wenyewe, huingia katika uchungu ndani ya hivyo hivyo vitu vilivyoumbwa, pale unapopasika umtumikie mtu ambaye hatekelezi Mapenzi Yangu. Ndipo inapotokea mara nyingi sana kuwa vitu vilivyoumbwa, husimama na kupingana na kukabiliana na binadamu. Vitu hivyo vinampiga na vinamwadhibu mwanadamu, na kwa hilo vinajitwalia madaraka kuwa juu ya binadamu. Ni kwa vile vitu hivyo vimekuwa vikihifadhi bila dosari yoyote, na kuuzingatia kwa utii ule Utashi wa Mungu uliovihuisha tangu siku ya kwanza ya kuumbwa kwao. Lakini binadamu ameteremka na kushuka kilindini kwa kosa la kutozingatia ndani yake ule Utashi wa Mwumbaji Wake”.

Baada ya hapo mimi niliingia katika kuwaza juu ya Sikukuu ya Mama yangu wa Mbinguni aliyechukuliwa katika Mbingu. Na Yesu Wangu Mtamu, kwa sauti laini kabisa na ya kunigusa sana moyoni aliongeza kusema:

“Binti Yangu, tukitaka jina halisi la Sikukuu hii, ilibidi iitwe: ‘Sikukuu ya Utashi wa Mungu’. Ilikuwa ni utashi wa kibinadamu ndio uliofunga Mbingu, ndio uliovunja na kukata kile kiungo cha mwanadamu na Muumba Wake, ndio uliofungulia matatizo yakatoka nje kwa mwanadamu, ulifungulia maumivu na mateso, ndio uliokomesha zile sikukuu ambazo mwanadamu alipasika kuzifaidi kule Mbinguni. Sasa lakini, huyu kiumbe mwanadamu, aliyekuwa ndiye Malkia wa vitu vyote, kwa kutimiza Mapenzi ya Utashi wa Milele, daima na katika kila kitu, yaani unaweza ukasema kuwa, uhai wake ulikuwa ni Utashi wa Mungu peke yake, ndiye aliyefungua Mbingu na ndiye aliyeunganisha tena Yule aliye ni wa Umilele na mwanadamu; na ndiye akafaulu kufanya zirejeshwe tena zile Sikukuu za Mbinguni kati ya Mungu na mwanadamu. Kila tendo alilokuwa anatekeleza katika Utashi Mkuu, likawa ni Sikukuu iliyokuwa ikianzia kule Mbinguni, matendo yake yakawa ni majua aliyoyatengeneza kuwa mapambo ya Sikukuu hii, matendo hayo yakawa ndio musiki aliokuwa anautuma kuja kufurahisha Yerusalemu ya Mbinguni. Kwa jinsi hiyo chimbuko halisi na la kweli la Sikukuu hii ni Utashi wa Milele unaotenda kazi na unaokaa ndani ya Mama Yangu wa Mbinguni, Utashi uliotenda mambo makuu kabisa ndani yake Mama huyu, Mama aliyeduwaza na kustaajabisha Mbingu na dunia, Mama aliyeufunga hata Umilele kwa minyororo ya vifungo vya upendo visivyoweza kuyeyuka kamwe, Mama aliyemteka Neno hadi kumwingiza ndani ya tumbo lake. Na hata wale Malaika wenyewe waliokuwa wametekwa na Mama huyu wakawa wanarudiarudia kusema kati yao: ‘Utukufu wote huu watokea wapi? Heshima yote hii, Ukuu wote huu na matendo makubwa haya ambayo hayajawahi kuonekana tunayoona sasa ndani ya Mwanadamu huyu wa pekee, yote haya hutokea wapi? Na halafu ajabu, tunamwona akitokea uhamishoni!’ Wakiwa wameshikwa na mshangao mkubwa sana waliutambua Utashi wa Muumba Wao kama ndiyo Uhai wa Mama na ndio uliokuwa unatenda kazi ndani yake. Mara hiyo, wakitetemeka kwa uchaji wakawa wanasema: ‘Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Heshima na Utukufu kwa Utashi wa Bwana Mtawala Wetu, na Utukufu na Mtakatifu mara tatu kwa Yeye Mama aliyefaulu kutekeleza huu Utashi Mkuu!’

Ni kwa hoja hii, umekuwa ni Utashi Wangu ndio ambao umekuwa unasherehekewa na unaendelea kusherehekewa katika Siku ya Kuchukuliwa Mbinguni kwa Mama Yangu Mtakatifu. Ilikuwa ni Utashi Wangu pekee ndio uliomfanya apande juu kabisa hata kumtofautisha na watu wote. Mambo yake yote yangebakia kuwa si kitu kama asingekuwa ndani yake na hili jambo Kuu kabisa la Utashi Wangu. Ilikuwa ni Utashi Wangu ndio uliompatia rutuba ya kimungu na ukamfanya awe Mama wa Neno. Ilikuwa ni Utashi Wangu ndio uliomfanya awaone na awakumbatie wanadamu wote kwa pamoja, huku akijifanya Mama wa wote na akawa anawapenda wote kwa pendo la Umama wa kimungu. Utashi Wangu, kwa kumfanya Mama awe Malkia wa wote, ulimwezesha kuwa na mamlaka juu ya himaya yote na kuanza kutawala. Ndiyo kusema, tangu siku ile Utashi Wangu ulipopata Utukufu na Heshima za kwanza, na ulipopata matunda tele tele ya kazi yake katika Uumbwa, siku ile ulipoanza kuadhimisha Sikukuu Yake ambayo haitawahi kukatishwa. Yote hiyo ni Sikukuu kwa ajili ya kutukuza utendaji ambao Utashi Wangu ulikwisha kuufanikisha ndani ya Mama Yangu mpendwa. Ingawa kama Mbingu ilikuwa imefunguliwa na Mimi, na ingawa kama Watakatifu wengi walikuwa tayari wamekwisha kupata Makao ya Mbinguni wakati huyu Malkia wa Mbinguni alipochukuliwa katika Mbingu, lakini hata hivyo, ni yeye huyu Mama ndiye hasa ambaye amekuwa ni chanzo asilia na ndiye huyu aliyekuwa kapewa jukumu juu ya kila kitu cha Utashi Mkuu. Ni kwa hoja hiyo, Utashi Mtakatifu, ili kuweza kuadhimisha Sherehe ya kwanza kwa ajili ya Utashi Mkuu, ulimsubiria yeye Mama, ambaye ndiye aliyekuwa ameutolea heshima kubwa kabisa, na ambaye aliyekuwa amebeba ndani yake ule muujiza mkuu halisia wa Utashi Mtakatifu. Huyu Malkia wa ajabu aliingia katika Himaya, akiwa amezungukwa na majeshi ya Mbinguni yaliyokuwa yakimsindikiza, akiwa na kiwiliwili chake kikiwa kimezungukwa na Jua la Milele la  Utashi Mkuu. Oh, ilipomwona huyo Malkia akiingia hivyo, ona jinsi Mbingu yote ilivyoanza kuutukuza, kuushangilia, na kuusifu Utashi wa Milele! Wote wa Mbinguni walikuwa wanamwona amefunikwa na maweza ya FIAT Kuu. Hapakuwa ndani yake na pigo la moyo hata moja tu ambalo halikuwa halijagonga mhuri wa hiyo FIAT. Wakiwa wamepigwa butwaa waliendelea kumwangalia huku wakisema: ‘Kwea, kwea juu, kwea juu zaidi! Ni vema na haki kabisa kwamba Wewe uliyekuwa umeiheshimu kabisa FIAT Kuu, na kwamba sisi tupo sasa katika Makao ya Mbinguni kutokana na hii FIAT Kuu, Wewe sasa twaa kiti cha utawala kilicho cha juu kabisa na Wewe uwe sasa Malkia wetu!’ Na heshima kuu kabisa aliyokuwa ameipata Mama Yangu ikawa ni kuona na kushuhudia Utashi wa Mungu ukitukuzwa”.

Juzuu na. 18 ku download - click here

Kila siku, hatua kwa hatua, jisomee hapa, ili upate kukua katika Paji la Uhai, ndani ya UTASHI WA MUNGU, kulingana na Mafundisho aliyoyatoa YESU kwake Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA

Swahili - Telegram Channel: Utashi Wa Mungu Na Upendo Wa Mungu

Swahili - Telegram Channel: Saa 24 Za Mateso Ya Bwana Weto Yesu Kristo

English - Telegram Channel: Divine Will Divine Love

English - Telegram Channel: The Virgin Mary in the Kingdom of the Divine Will

Français - Chaine de Telegram: Divine Volonte Divin Amour

Français - Chaîne de Telegram: Lettres de Luisa Piccarreta

Lingala - Chaine de Telegram: Mpo Elingi Nzambe Bolingi bwa Nzambe

Website all languages: www.divinewilldivinelove.com

Vitabu yote vilivyo katika faili za PDF vinaweza kupakuliwa bila gharama yoyote ile wakati wote ule. Pia, upo huru kabisa kuchapisha VITABU hivyo wewe mwenyewe binafsi au kuchapisha kwenye kiwanda chochote kile. Lakini vitabu hivyo ni kwa matumizi binafsi tu na siyo kwa ajili ya biashara! Hata hivyo una ruhusa ya kuwashirikisha na kuwapatia watu wengine vitabu hivyo kadiri unavyopenda!!

Swahili landing page: click here

English landing page: click here

Lingala landing page: click here

Kikongo landing page: click here

French landing page: click here

Italian landing page: click here

Report Page