Yesu kwa Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - KITABU cha MBINGU - JUZUU na. 17 - Mei 4, 1925🖋📄📖📔

Yesu kwa Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - KITABU cha MBINGU - JUZUU na. 17 - Mei 4, 1925🖋📄📖📔


Baada ya kuyaandika hayo yaliyoandikwa hapo juu, mimi nilianza zoezi la uabudu kwa Yesu Wangu Msulibiwa, huku nikijiyeyushia nafsi yangu yote ndani ya Utashi Wake Mtukufu. Ndipo Yesu Wangu Mpendwa alijitokeza kutoka pale ndani mwangu, alisogeza uso Wake Mtukufu na kuuweka kando ya uso wangu, na katika upole wake wote aliniambia hivi:

“Ewe Binti Yangu, je umeandika kila jambo lihusulo utume wa Utashi Wangu?”

Na mimi nilimjibu nikisema: ‘Ndiyo, ndiyo, niliandika kila jambo’. Na Yeye akasema tena:

“Na itakuweje kama nitakuambia kwamba wewe hujaandika kila jambo?

Iweje nikikuambia, mbona umeliacha jambo lililokuwa muhimu kweli kweli. Basi wewe endelea bado kuandika, na sasa uongeze:

‘Utume wa Utashi Wangu, mithili ya pazia, utakuja kuufunika, Utatu Mtakatifu hapa duniani.

Kama vile kule Mbinguni kuna Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu wasiotenganika kati Yao, lakini wakiwa kila mmoja na nafsi Yake inayotofautikana, hao wakiwa wanatengeneza ile heri yote ya Mbinguni, hali kadhalika, hapa duniani patakuwa na nafsi tatu, ambao, kwa mujibu wa utume wao mbalimbali, watakuwa tofauti tofauti, lakini papo hapo watakuwa hawatenganiki kati yao.

Atakuwepo yule Bikira, na utume wake wa Umama, utume ambao, mithili ya pazia, unaufunika Ubaba wa Mungu Baba wa Mbinguni, na papo hapo huo Umama utayabeba maweza yale ya Baba kwa ajili ya kuweza kutekeleza utume wake wa Mama wa Neno wa Milele, na utume wa Mkombozi Mshiriki wa kizazi cha binadamu.

Utakuwepo Ubinadamu Wangu, kwa utume wake wa Mkombozi, Ubinadamu uliokuwa umefungilia ndani yake Umungu na Neno, bila kuyatenganisha kamwe hayo mawili kutoka kwa Baba na kwa Roho Mtakatifu, Ubinadamu huo ulionyesha hekima Yangu ya Mbinguni - ukawa umeongeza na kile kifungo cha Mimi kujifanya Mimi Mwenyewe nisitenganike na Mama Yangu.

Na utakuwepo na wewe, kwa mujibu wa utume wako mintarafu Utashi Wangu, kadiri Roho Mtakatifu atakavyokuwa anaonyesha Pendo Lake, atakavyokuwa anakufunulia wewe zile siri, yale maajabu ya Utashi Wangu, yale mema yaliyomo ndani yake, atakufunulia wewe kwa ajili ya kuwafurahisha wale wote watakojitoa wenyewe kufahamu mema mengi mangapi yapo ndani ya huo Utashi Mkuu wa Juu, kuwafurahisha wale watakaojitoa kuupenda huo Utashi na wale watakaojitoa kuruhusu utawale pale kati yao, na kuwafurahisha wale watakaotoa roho zao ili Utashi uweze kuingia na kusetiri pale ndani ya mioyo yao, hata uweze kutengeneza Uhai wake pale ndani yao - na wale watakaokuwa wanaongeza kile kifungo cha kutotenganika kati ya wewe, Mama na Neno wa Milele.

Aina hizo tatu za utume zipo tofauti tofauti lakini hazitenganiki. Zile aina mbili za kwanza ndizo zilizoandaa neema mbalimbali, zilizoandaa mwanga, zilizoiandaa kazi, na zilikuwa na maumivu makali yasiyosemekana. Ziliandaa hayo kwa ajili ya ule utume wa aina ya tatu, utume wa Utashi Wangu. Halafu aina zile mbili za kwanza zilijiyeyushia zenyewe zote ndani ya Utashi Wangu bila kuliacha lile jukumu lao, ili pale ndani ya Utashi Wangu ziweze kujipatia pumziko kwa vile Utashi Wangu pekee ndio ni pumziko la Mbinguni. Hizo aina mbili za utume hazitarudiwa kwa vile ule utele wa neema, wa mwanga, wa maarifa ni mkubwa mno hivi kwamba vizazi vyote vya binadamu vinaweza vikajazwa na neema hizo. Na zaidi ni kwamba, hivyo vizazi vya binadamu havitaweza kamwe kubeba yale mema yote yaliyomo pale ndani ya aina hizo za utume.

Aina hizo za utume zinafananishwa na jua. Kwa kweli, Mimi, nilipoliumba jua, nilikuwa nimelijaza kwa mwanga mkubwa mno na kwa joto kali mno hivi kwamba, vizazi vyote vya binadamu vimeweza kupata mwanga na joto vinavyofurika zaidi ya kiwango wanachohitaji. Na wala Mimi sikuwa nimeangalia kwamba, pale mwanzoni mwa Uumbaji, kwa vile palikuwepo Adamu na Eva peke yao ambao ndio walihitaji kulifaidi jua, ningeweza kuweka tu kiwango cha mwanga kitakachowatosha wao wawili peke yao, halafu, baadaye, vizazi vilipozidi kuongezeka, ningeweza Nami kuongeza mwanga mpya zaidi. Kumbe lakini, hapana, sivyo kabisa, Mimi nililifanya jua lenye mwanga timilifu kabisa kama lilivyo sasa hivi na kama litakavyokuwa hivyo hapo mbeleni.

Kazi Zangu Mimi, kwa ajili ya ile hadhi na ile heshima ya Maweza Yetu, ya Hekima Yetu na ya Pendo Letu, zimetendeka daima kwa ujazo wa kila jema lililopo pale ndani yake. Kazi hizo hazikabiliwi na hali ya kukua au kupungua. Na ndivyo hivyo nililifanya lile jua. Ndani yake nililijaza na ule mwanga utakaoweza kumtosha hadi binadamu wa mwisho kabisa. Lakini hata hivyo, ni faida nyingi ngapi ambazo jua halishushi kamwe juu ya ardhi? Ni utukufu gani, ambao, katika huo mwanga wake bubu, jua halifikii kutoa kwa Muumba Wake? Mimi naweza nikasema kwamba, kutokana na yale mema mengi makubwa kabisa, ambayo jua hutenda kwa ardhi, katika lugha ya ububu wake hilo hilo jua linanitukuza Mimi na linanifanya Mimi nijulikane zaidi kuliko vinavyofanya vitu vingine vyote vikichukuliwa kwa pamoja. Na jua linaweza kufanya hivyo kwa vile huwa limejaa kabisa mwanga na kwa vile jua ni thabiti katika mkondo wa safari yake. Nilipoliangalia jua, ambalo, licha ya ule mwanga mwingi mno, ni Adamu na Eva peke yao ndio walikuwa wakilifaidi, niligeuka na kuviangalia vitu vingine vyote vyenye uhai. Na nilipong’amua kwamba sasa ule mwanga unatakiwa uwe unawafaa watu wote na vitu vyote, ukarimu Wangu uliruka na ulishangilia kwa furaha, na ndipo nikabaki nimetukuzwa ndani ya zile kazi Zangu zote.

Ndivyo nilivyotenda na Mama Yangu: Nilimjaza kwa neema kubwa mno, kiasi kwamba yeye anaweza kutoa neema mbalimbali kwa watu wote bila hofu yoyote ya kuweza kuimaliza neema hata mojawapo. 

Ndivyo hivyo nilivyotenda juu ya Ubinadamu Wangu: hakuna jema hata moja ambalo Ubinadamu Wangu haulibebi. Ubinadamu Wangu umefungilia ndani mwake kila kitu, na hata ule Umungu wenyewe, umeufungilia ili uweze kuutoa kwa yeyote yule anayeutaka huo Umungu.

Ndivyo nilivyotenda juu ya wewe: Ndani yako wewe nimeufungilia Utashi Wangu, na, pamoja na Utashi huo nimefungilia hapo hata Nafsi Yangu Mimi Mwenyewe. Ndani yako wewe nimefungilia maarifa mbalimbali ya Utashi Wangu, siri zake mbalimbali, na nimefungilia hapo hata mwanga wake. Mimi nimeijaza roho yako pomoni kabisa. Nimeijaza roho yako na mambo mengi mno kiasi kwamba hicho unachokiandika siyo kitu bali ni ufuriko tu wa yale mambo mengi unayoyabeba kutokana na Utashi Wangu. Na hata kama, kwa sasa, hayo mambo yanakufaa wewe peke yako, na labda dozi chache za mwanga zinawafaa wachache wengine, Mimi, kwa upande Wangu, ninaridhika kwani, kwa wewe kuwa mwanga, ukiwa ni mwanga zaidi ya jua la pili, huo mwanga kwa wenyewe, utatoka na kwenda kuviangaza vizazi mbalimbali vya binadamu, na utakwenda kufanikisha utimilizo wa kazi Zetu: yaani, kwamba Utashi Wetu ujulikane, na upendwe, na kwamba Utashi Wetu utawale kama uhai ndani ya wanadamu.

Hilo ndilo lilikuwa ni lengo la Uumbaji - huu ndio mwanzo wa lengo hilo, na huu utakuwa ndiyo njia na jinsi ya utekelezaji wa lengo, na huu utakuwa ndiyo uhitimisho wa lengo.

Kwa hiyo basi, wewe uwe sasa makini sana, kwani, jambo hili linahusu kuuweka Utashi wa Milele katika usalama wake, Utashi ambao, kwa pendo kubwa kabisa, unataka kusetiri pale ndani ya wanadamu. Hata hivyo, unataka ujulikane, hautaki ubaki kama mgeni mpitanjia, bali unataka ukatoe mema yake na unataka uje kuwa ni Uhai wa kila mmoja.

Hata hivyo, Utashi Wangu unazidai haki zake, unadai nafasi yake ya heshima.

Unataka utashi wa kibinadamu uwekwe kando kabisa - kwani huo ndio adui pekee kwa Utashi Wangu na kwa binadamu. Utume wa Utashi Wangu ulikuwa ndilo lile lengo la Uumbaji wa binadamu. Umungu Wangu haukuwa umehama toka kule Mbinguni - naam, kutoka kule kwenye kiti Chake cha ufalme, kumbe lakini, Utashi Wangu siyo uliondoka tu, bali uliteremkia chini kwa viumbe vyote na pale ulitengeneza Uhai wake pale ndani yao.

Lakini, wakati vitu vyote vyote vilinitambua Mimi, na wakati Mimi niliingia na kukaa ndani yao, na ninakaa pale katika utukufu na heshima, binadamu peke yake ndiye aliyenisukuma na kunifukuzia mbali.

Hata hivyo, Mimi ninataka nimkabili, nimshinde na kumteka. Kwa hiyo basi, utume Wangu Mimi haujamalizika bado.

Ndiyo maana, nimekuita wewe.

Ninakukabidhi wewe ule utume wa Kwangu Mwenyewe, ili wewe, hapo juu ya magoti ya Utashi Wangu, ukamlete na kumweka yule ambaye alikuwa amenisukuma na kunifukuzia Mimi mbali. Na ndipo hapo kila kitu kitaweza kurejea Kwangu katika Utashi Wangu.

Basi, wewe usishangae na kuduwaa juu ya hayo mambo mengi makuu na ya ajabu ninayoweza kukueleza kwa ajili ya utume huo, au kushangaa juu ya zile neema nyingi na mbalimbali ambazo ninaweza kukujalia wewe.

Suala hilo halihusu kumtengeneza mtakatifu fulani au suala la kuviokoa vizazi fulani vya binadamu. Bali hili ni suala la kuuweka Utashi wa Mungu katika usalama, ili kusudi, watu wote waweze kurejea kule kwenye asili yao, kwenye mwanzo ambako walikuwa wametokea wote, na ni suala kwamba lengo la Utashi Wangu lifikie utimilifu wake’.”

Juzuu na. 17 ku download - click here

Kila siku, hatua kwa hatua, jisomee hapa, ili upate kukua katika Paji la Uhai, ndani ya UTASHI WA MUNGU, kulingana na Mafundisho aliyoyatoa YESU kwake Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA

Swahili - Telegram Channel: Utashi Wa Mungu Na Upendo Wa Mungu

Swahili - Telegram Channel: Saa 24 Za Mateso Ya Bwana Weto Yesu Kristo

English - Telegram Channel: Divine Will Divine Love

English - Telegram Channel: The Virgin Mary in the Kingdom of the Divine Will

Français - Chaine de Telegram: Divine Volonte Divin Amour

Français - Chaîne de Telegram: Lettres de Luisa Piccarreta

Lingala - Chaine de Telegram: Mpo Elingi Nzambe Bolingi bwa Nzambe

Website all languages: www.divinewilldivinelove.com

Vitabu yote vilivyo katika faili za PDF vinaweza kupakuliwa bila gharama yoyote ile wakati wote ule. Pia, upo huru kabisa kuchapisha VITABU hivyo wewe mwenyewe binafsi au kuchapisha kwenye kiwanda chochote kile. Lakini vitabu hivyo ni kwa matumizi binafsi tu na siyo kwa ajili ya biashara! Hata hivyo una ruhusa ya kuwashirikisha na kuwapatia watu wengine vitabu hivyo kadiri unavyopenda!!

Swahili landing page: click here

English landing page: click here

Lingala landing page: click here

Kikongo landing page: click here

French landing page: click here

Italian landing page: click here


Report Page