Yesu kwa Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - KITABU cha MBINGU - JUZUU na. 13 - Novemba 28, 1921🖋📄📖📔

Yesu kwa Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - KITABU cha MBINGU - JUZUU na. 13 - Novemba 28, 1921🖋📄📖📔


Pindi nikiendelea katika hali yangu ya kawaida, nilijikuta nikiwa ndani ya bahari kuu ya mwanga - mtu hukuweza kuona ukingo inakomalizikia na wala ilikoanzia. Halafu pakawa na mtumbwi mdogo uliokuwa umetengenezwa pia kwa mwanga: yaani sakafu ya mtumbwi ilikuwa ni ya mwanga, na hata matanga yake yalikuwa ni ya mwanga - kwa ujumla, kila kitu kilikuwa ni mwanga tu. Hata hivyo, yale mambo mbalimbali yanayotumika katika kutengeneza mtumbwi, yaliweza kutambulikana kutokana na utofauti wa mwanga - yaani, kitu kimoja kinatoa mwanga zaidi kuliko kingine. Kwa spidi kali ya ajabu sana, huo mtumbwi mdogo ulikuwa ukiivuka ile bahari kuu ya mwanga. Mimi nilibaki nikistaajabu tu. Zaidi hasa, nilikuwa ninastaajabu kuona kuwa punde tu mtumbwi ule ungefifia ndani ya ile bahari na wala usingeweza kuonekana tena machoni, halafu ule ule mtumbwi ungeweza kujitokeza tena.

Na ingawa kama ulikuwa mbali kabisa, ukiendelea kukata mbio baharini, baada ya muda mfupi ungerudi tena na kujikuta mahali pale pale ulipokuwa umeanzia safari yake. Yesu Wangu Mpendevu wa daima alikuwa akijiburudisha sana sana kwa kuangalia ule mtumbwi mdogo.

Aliniita akaniambia:

“Binti Yangu, hiyo bahari unayoiona, ndiyo Utashi Wangu.

Utashi Wangu ni mwanga, na hakuna mtu anayeweza akaivuka bahari hii isipokuwa yule anayetaka kuishi katika mwanga. 

Ule mtumbwi unaouona ukivuka bahari hii kwa jinsi ya kupendeza vile, ndiyo mtu yule anayeishi ndani ya Utashi Wangu. Kwa kuendelea kuishi ndani ya Mapenzi Yangu, huyo mtu amekuwa akipumua hewa ya Utashi Wangu, na Utashi Wangu umemwondolea mbao, umemwondolea matanga, umemwondolea nanga, umemwondolea hata ule mlingoti, na mwishowe umegeuza vyote kuwa mwanga.

Kwa hiyo, kadiri mtu anavyoendelea kutekeleza matendo yake ndani ya Utashi Wangu, mtu huyo anajiondolea mwenyewe nafsi yake, na badala yake anajijaza mwanga.

Nahodha wa huo mtumbwi sasa ni Mimi - Ni Mimi Mwenyewe ndiye ninayemwongoza katika ile spidi yake. Ni mimi ndiye ninayemkimbiza hadi ndani kabisa baharini ili kumpatia pumziko kidogo na pia ili kumpatia muda kutosha wa kukabidhiwa zile siri za Utashi Wangu.

Hakuna mtu ambaye angeweza kumwongoza, kwa vile, kwa kutokuijua bahari, hawataweza kuijua njia ya kumwelekeza, na wala Mimi Mwenyewe nisingeweza kumwamini mtu yeyote. Sana sana, Mimi ningeweza kumchagua kiongozi fulani awe kama mtazamaji na msikilizaji tu wa yale mambo makuu ambayo Utashi Wangu unayatenda.

Ni nani huyo ambaye angekuwa na uwezo wa kuongoza mashindano ya mbio ndani ya Utashi Wangu? 

Kumbe Mimi, kwa dakika moja tu, ninamwezesha mtu kukimbia mbio zile ambazo kiongozi mwingine angeweza kumfanya akimbie mbio hizo katika muda wa karne moja nzima”. 

Halafu aliongeza kusema:

“Ebu ona jinsi alivyo mzuri na wa kupendeza - anakimbia, anapiga mbizi, na mara huyo anajikuta amerudi pale alipoanzia. Ni sayari ya Umilele ndiyo inayomzunguka, lakini anaonekana kuwa daima mahali pale pale pamoja. Ni Utashi Wangu usiobadilika ndio unaomfanya awe anakimbia ndani ya sayari yake ambayo haina mwanzo wala mwisho, kiasi kwamba, anapokimbia, mtu huyo hujikuta amefika pale penye uthabiti, pasipotikisika, yaani mahali Pangu pale pasipokuwa na mabadiliko yoyote kwa upande Wangu.

Ebu angalia kwenye jua - limesimikwa pale, halitikisiki, lakini katika dakika moja mwanga wake unaenea na kufunika dunia nzima.

Ndivyo ilivyo na mtumbwi huu: Ni mtumbwi usiobadilika pamoja na Mimi. Na wala haondoki kutoka mahali pale ambapo Utashi Wangu ulimtoa - alitoka mahali pa milele, na pale anabaki na kuendelea.

Na kama anaonekana akikimbia, huwa ni matendo yake ndiyo yanayokimbia, ni matendo ambayo, mithili ya mwanga wa jua, yanakimbia na kwenda kila mahali na popote. 

Hiyo ndiyo ajabu yenyewe: Kukimbia na kubaki bila ujimudu. 

Ndivyo nilivyo, na ndivyo yanipasa nimfanye yule ambaye anaishi ndani ya Utashi Wangu.

Lakini, je, unataka ujue huo mtumbwi ni nani?

Ni yule mtu ambaye anaishi ndani ya Utashi Wangu.

Kadiri anavyoyatoa matendo yake katika Mapenzi Yangu, ndivyo anavyofanya mbio zake.

Na hivyo anaupatia Utashi Wangu nafasi ya kuyatoa matendo mengine mengi muhimu sana ya neema, ya upendo, ya utukufu, kutoka katika makao yake makuu.

Na Mimi, niliye ndiye nahodha wa mtu huyo, ndiye huongoza tendo lile.

Mimi ninakimbia pamoja na lile tendo, ili kusudi liwe ni tendo lisilokosa kitu, bali liwe ni tendo stahiki kwa Utashi Wangu.

Lakini katika mambo hayo Mimi ninajifurahisha na kuburudika sana.

Hapo huwa ninamwona huyo Binti Wangu Mdogo wa Utashi Wangu ambaye, akiwa pamoja Nami, anapiga mbio, na papo hapo anabaki ametulia. 

Yeye hana miguu, lakini ndiye hatua ya watu wote. Hana mikono, lakini ndiye ujimudu wa kazi zote. Hana macho, lakini ndani ya mwanga wa Utashi Wangu yeye ni zaidi ya macho na ni zaidi ya mwanga kwa watu wote.

Oh! Ni jinsi gani anavyomwiga vema Muumba Wake - ni jinsi gani anavyojitahidi kufanana na Mimi.

Kuiga kihalisia kwaweza kupatikana ndani ya Utashi Wangu peke yake. 

Sikioni mwangu ninasikia tena ile sauti Yangu tamu kabisa na ile sauti ya uumbaji ikisema: ‘Tumwumbe mtu kwa sura na mfano wetu’.

Na kwa furaha isiyokoma Mimi ninasema: ‘Hawa hapa ndio sura Zangu - zile haki za Uumbwa zinarudishwa Kwangu, lile lengo ambalo kwalo nilimwumba binadamu limetimilika. Ni furaha ilioje Kwangu’.

Na hapo ninaiita Mbingu yote ianze kufanya sherehe”.

Kila siku, hatua kwa hatua, jisomee hapa, ili upate kukua katika Paji la Uhai, ndani ya UTASHI WA MUNGU, kulingana na Mafundisho aliyoyatoa YESU kwake Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA

Swahili - Telegram Channel: Utashi Wa Mungu Na Upendo Wa Mungu

Swahili - Telegram Channel: Saa 24 Za Mateso Ya Bwana Weto Yesu Kristo

English - Telegram Channel: Divine Will Divine Love

English - Telegram Channel: The Virgin Mary in the Kingdom of the Divine Will

Français - Chaine de Telegram: Divine Volonte Divin Amour

Français - Chaîne de Telegram: Lettres de Luisa Piccarreta

Lingala - Chaine de Telegram: Mpo Elingi Nzambe Bolingi bwa Nzambe

Website all languages: www.divinewilldivinelove.com

Vitabu yote vilivyo katika faili za PDF vinaweza kupakuliwa bila gharama yoyote ile wakati wote ule. Pia, upo huru kabisa kuchapisha VITABU hivyo wewe mwenyewe binafsi au kuchapisha kwenye kiwanda chochote kile. Lakini vitabu hivyo ni kwa matumizi binafsi tu na siyo kwa ajili ya biashara! Hata hivyo una ruhusa ya kuwashirikisha na kuwapatia watu wengine vitabu hivyo kadiri unavyopenda!!

Swahili landing page: click here

English landing page: click here

Lingala landing page: click here

Kikongo landing page: click here

French landing page: click here

Italian landing page: click here

Report Page