@Ribbiyyuwna
[1] Rejea tanbihi (2: 1).
[2] Sababun-Nuzuwl: Sa’iyd bin Jubayr amehadithia kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) kwamba: Washirikina wanawake na wanaume walikuwa wakitufu Al-Ka’bah. Wanaume wakitufu mchana na wanawake wakitufu usiku. Wanawake wakisema wanapotufu: Leo baadhi yake (uchi) au wote uonekane na kitakachoonekana sikitolei ruhusa. Hapo ikateremka: “Enyi wana wa Aadam! Chukueni mapambo yenu katika kila Masjid” (7: 31).
Faida: Aayah hii ni dalili la pendekezo kwa Muislamu kuvaa nguo nzuri safi (na siwaak) anaposwali. Na nguo bora kabisa ni ya rangi nyeupe (kwa wanaume) kama alivyohadithiaIbn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Vaeni nguo nyeupe kwani ndio nguo zenu bora kabisa, na kafinini kwazo maiti wenu...”[Ahmad].
Faida: Kutokula mno mpaka mtu ashindwe kutekeleza ‘ibaadah zake. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Bin Aadam hajijazii chombo vibaya kama anavyojaza tumbo lake. Inamtosheleza bin Aadam ale kidogo tu kiasi cha kumtia nguvu uti wa mgongo wake. Lakini akitaka kula zaidi, basi thuluthi ya chakula, na thuluthi ya maji na thuluthi aache kwa ajili ya hewa.”[Amehadithia Al-Miqdaam bin Ma’diykarib(رضي الله عنه) amepokea Ahmad, At-Tirmidhiy].
[3] Faida: Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) amehadithia kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Allaah Ana hisia ya ghera, na ghera ya Allaah (inachomoza) pale mtu anapofanya (maasi) Aliyoyaharamisha Allaah.” [Al-Bukhaariy na Muslim].
Na pia amesema Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):“Hakuna mwenye ghera zaidi ya Allaah wakati anapozini mja wake au ummah Wake uzini.”[Al-Bukhaariy].
Faida: Kuhusu haramisho la kumshirikisha Allaah (سبحانه وتعالى) rejea tanbihi (4: 48).
[4] Faida: Imaam Bin Baaz (رحمه الله) amesema alipoulizwa kuhusu Aayah hii: “Hakika wale waliokadhibisha Aayaat Zetu na wakatakabari nazo, hawatofunguliwa milango ya mbingu na wala hawatoingia Jannah mpaka ngamia aingie katika tundu ya sindano…” (7: 40). “Ni dhahiri kuwa mwenye kukadhibisha Aayat za Allaah Akatakabari kufuata haki, hivyo ndivyo itakavyokuwa hali yake, haitopanda roho yake mbinguni, bali itarudishwa ardhini katika mwili wake atahiniwe na aadhibishwe kaburini mwake. Kisha atahamishwa motoni, tunamuomba Allaah Al-‘Aafiyah. Kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى) kuhusu Fir’awn: “Wanadhihirishiwa Moto asubuhi na jioni, na Siku itakayosimama Saa (itasemwa): “Waingizeni watu wa Fir’awn (katika) adhabu kali kabisa.” (Ghaafir 40: 46). Hivyo ndivyo hali ya wengineo; kila atakayetakabari na haki na asifuate uongofu, haitofunguliwa milango ya mbingu wala hairudishwi roho zao mbinguni wala kwa Allaah (عزّ وجلّ) bali itarudi roho yake katika mwili wake muovu na ataadhibiwa kaburini mwake pamoja na adhabu ya moto Siku ya Qiyaamah. Tunamuomba Allaah Al-‘Aafiyah. Na pia hawatoingia Jannah kamwe ndipo Allaah (سبحانه وتعالى) Anabainisha kuwa hatoingia kamwe Jannah mpaka iwezekane ngamia aingie katika tundu ya sindano. Na inajulikana wazi kuwa ngamia hawezi kuingia kamwe katika tundu ya sindano, na lilokusudiwa hapa ni jambo hili kuwa mustahili aingie Jannah kama vile ilivyokuwa mustahili ngamia aingii katika tundu ya sindano, kutokana na kufru zao na upotofu wao, ni mustahili kuingia Jannah bali wao waitaingia motoni milele. Tunamuomba Allaah Al-‘Aafiyah. Jazaakumu Allaahu khayraa.” [Fataawa Ibn Baaz].
[5] Faida: Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy (رضي الله عنه)amehadithia kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Baada ya Waumini kuokolewa na moto, watazuiliwa wangojee katika qantwarah (daraja) baina ya Jannah na moto. Kisha watahojiwa kuhusu dhulma zote walizotendeana duniani. Watakapotakaswa (madhambi yao kuhukumiwa) na kutengenezwa nidhamu, watapewa ruhusa kuingia Jannah. Naapa kwa Ambaye nafsi yangu imo Mikononi Mwake, kila mtu atatambua makazi yake Jannah kuliko anavyotambua makazi yake ya duniani.” [Al-Bukhaariy].
Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) amehadithia kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Kila mmoja katika watu wa Jannah ataona sehemu yake ya kikao chake cha motoni atasema: Ingekuwa Allaah Hakunihidi! Basi itakuwa ni shukurani kwake. Na kila mtu wa moto ataona sehemu yake ya kikao Jannah atasema: Ingekuwa Allaah Kanihidi! Basi huwa ni majuto kwake.” [An-Nasaaiy].
[6] Faida: Al-A’raaf: Ibn ‘Abbaas, Ibn Mas’uwd, Ibn Jariyr na Salaf wengineo wamesema kwamba sehemu watakayosimama watu ambao ‘amali zao njema na mbaya zimelingana sawasawa. ‘Amali zao ovu zimewazuia kuingia Jannah, na ‘amali zao njema zimewastahiki waepukane na moto kwa hiyo watasimamishwa hapo katika mnyanyuko wa Al-A’raaf mpaka Allaah Awahukumu. [Tafsiyr Ibn Kathiry].
[7] Faida: Maana ya Istawaa: Yuko juu kabisa kwa namna inayolingana na Utukufu Wake Yeye Mwenyewe Allaah. Pia rejea tanbihi (2: 29).
[8] Faida: Abuu Hurayrah (رضي الله عنه)amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Allaah (عزّ وجلّ)Ameumba mchana siku ya Jumamosi, Akaumba milima Jumapili, Akaumba miti Jumatatu, Akaumba yanayochukiza Jumanne, Akaumba nuru Jumatano, kisha Akaeneza humo viumbe vinavyotembea Alkhamiys. Kisha Akamuumba Aadam (عليه السلام) Ijumaa baada ya Alasiri. Alikuwa ni wa mwisho kuumbwa katika saa ya mwisho katika saa za Ijumaa, baina ya Alasiri na usiku.” [Ahmad].
[9] Faida: Miongoni mwa adabu za kuomba du’aa ni kuomba kwa unyenyekevu na kwa siri. Abuu Muwsaa Al-Ash-‘ariyy (رضي الله عنه)amehadithia kwamba: Tulikuwa pamoja na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) na tukawa kila tukipanda bonde, tulifanya tahliyl(Laa Ilaaha Ila-Allaah), tulikabbir (Allaahu Akbar), zikapanda sauti zetu, akasema Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) “Enyi watu, jizuieni nafsi zenu kwani hamumwombi kiziwi wala asiyekuwepo, hakika Yeye Yupo nanyi (kwa ujuzi Wake), hakika Yeye Mwenye kusikia yote, Yupo Karibu Ametakasikia Jina Lake na Ametukuka ...” [Al-Bukhaariy].
Rejea pia tanbihi (2: 186).
[10] Faida: Abuu Muwsaa Al-Ash-‘ariyy (رضي الله عنه) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Mfano wa uongofu na elimu ambayo Allaah Amenituma kufikisha ni kama mvua kubwa inayoanguka juu ya ardhi, baadhi yake (hufikia) katika ardhi yenye rutuba imenyonya maji ya mvua na ikaleta mimea na majani kwa wingi. Na baadhi yake (ardhi) ilikuwa nzito na ikazuia maji ya mvua (kupenya katika ardhi) na Allaah Akawanemeesha watu kutokana nayo na wakaitumia kwa kunywa, kunyweshea wanyama wao na kwa ajili ya umwagiliaji na kilimo kwenye ardhi hiyo. Na baadhi yake ilikuwa si yenye rutuba ambayo haikuweza kukamata maji wala kutoa mimea (hivyo ardhi hiyo haikutoa faida yoyote). (Ardhi) Ya mwanzo ni mfano wa mtu anayetambua Dini ya Allaah na akapata faida (kutoka na elimu) ambayo Allaah Ameishusha kupitia kwangu (Manabii na Wanachuoni) na akaisomesha kwa wengine. (Ardhi) Ya mwisho ni mfano wa yule mtu asiyeijali na hachukui (hafuati) uongofu wa Allaah Alioushusha kupitia kwangu (Ni mfano wa hiyo ardhi isiyo na rutuba).” [Al-Bukhaariy].
[11] Kukatwa mikono ya kulia kwa miguu ya kushoto au miguu ya kushoto kwa mikono ya kulia.
[12] Faida: Salmaan (رضي الله عنه) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Allaah (عزّ وجلّ) Ana rahmah mia, basi katika hizo rahmah moja wanarehemiana viumbe baina yao, hata mnyama mwitu anamhurumia kizazi chake. Rahmah tisini na tisa Ameziweka kwa ajili ya Siku ya Qiyaamah.” [Ahmad].
[13] Rejea tanbihi (2: 65), (4: 47).
[14] Faida: Ahadi ya “Alastu” ambayo viumbe vyote viliahidi kwa Allaah (سبحانه وتعالى) kutokumshirikisha na kumtii amri Zake. Ahadi hiyo waliichukua viumbe kabla ya kuzaliwa kwao wakati roho zao zimeshaumbwa kwa kuwa kuna uhai miwili na mauti mawili kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى) (Ghaafir 40: 10-11) na (Al-Baqarah 2: 28). Na Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakuna kizazi kinachozaliwa (mtoto mchanga) isipokuwa anazaliwa katika 'fitwrah' kisha wazazi wake (humbadilisha na) humuingiza katika dini ya Uyahudi, au Unaswara au Umajusi, kama mfano mnyama mwenye pembe anavyomzaa mnyama mwenye pembe kama yeye, je, mtahisi kuwa hana pembe?” Kisha Abuu Hurayrah akasema: Someni mkipenda: (kauli ya Allaah): “Umbile la asili la kumpwekesha Allaah Aliyowaumbia watu. Hakuna mabadiliko katika uumbaji wa Allaah.” (Ar-Ruwm 30: 30). [Al-Bukhaariy na Muslim].
[15] Sababun-Nuzuwl: Aayah hii na zinazofuatia (7: 175-177) zimeteremshwa kuhusu kisa cha Bal’aam ibn Baa’uwraa katika kizazi cha Bani Israaiyl. Alijaaliwa kuwa ‘ilmu ya hali ya juu na akajulishwa Jina tukufu kabisa la Allaah (سبحانه وتعالى) lakini akapotoka kwa kufuta matamanio na anasa za dunia. Baada ya kushawishiwa na waovu, alikubali kuomba du’aa dhidi ya Nabiy Muwsaa (عليه السلام) kwa ajili ya kuchuma maslahi ya kidunia. Riwaaya nyengine inasema zimeteremka kumhusu Umayyah bin Abi Asw-Swalt. Riwaayah nyingine ni mtu kutoka Yemen aliyeita Bal’am. [Tafsiyr Ibn Kathiyr].
[16] Faida: ‘Aqiydah ya Ahlus-Sunnah wal-Jamaa’ah kuhusiana na Majina Mazuri kabisa ya Allaah (سبحانه وتعالى) na Sifa Zake nitawqifiyyah; yanathibitishwa Aliyoyathibitisha Mwenyewe Allaah (سبحانه وتعالى) katika Qur-aan na Sunnah bila kuzifanyia ta'twiyl(kuzipinga, kukanusha uwezekano), wala tamthiyl (kumithilisha, kulinganisha), wala takyiyf (kuainisha; namna gani zimefungamana au kuambatana na Allaah na kuziulizia namna yake au kuuliza ni vipi Sifa hiyo), wala tahriyf (kupotosha na kubadilisha maana) wala tahriyf (kubadilisha maana, kupotosha Sifa ya Allaah (سبحانه وتعالى) kwa kutoa maana isiyo sahihi).
Na Abuu Hurayrah Radhwiya Radhwiya (رضي الله عنه) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Allaah Ana Majina tisini na tisa, atakayehifadhi ataingia Jannah)). [Al-Bukhaariy na Muslim] Maana ya ahswaahaa: Kuyafahamu maana Zake, kuyahifadhi, kufanyia kazi, kuomba du’aa.
[17] Faida: Mu’aawiyah bin Abiy Sufyaan (رضي الله عنه) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Kutakuweko kundi katika Ummah wangu litaendelea kuwa juu ya haki likiwa na nguvu, hawezi kuwadhuru yeyote aliyekwenda nao kinyume au aliyesaliti mpaka siku ya Qiyaamah.” [Al-Bukhaariy na Muslim]
[18] Rejea tanbihi (6: 158).