Kilio cha malalamiko ya Roho Mtakatifu pale ndani ya Sakramenti mbalimbali - Yesu kwa Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - Kitabu cha Mbingu – Juzuu na. 18 - Novemba 5, 1925🖋📃📖📔

Kilio cha malalamiko ya Roho Mtakatifu pale ndani ya Sakramenti mbalimbali - Yesu kwa Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - Kitabu cha Mbingu – Juzuu na. 18 - Novemba 5, 1925🖋📃📖📔


Kulingana na mazoea yangu, nilikuwa katika kujiyeyushia nafsi yangu ndani ya Utashi Mtakatifu wa Mungu. Pindi nikijaribu kwa uwezo wangu wote, na kwa lile pendo langu dogo, kumlipa Yesu Wangu kwa yale yote aliyoyatenda katika Ukombozi, Yesu Wangu Mpendevu, aliye ni Pendo Langu Tamu, aliingia pale ndani mwangu, na akaniambia hivi:

“Binti Yangu, kwa mruko wa ndege yako hapa ndani ya Utashi Wangu, nenda ukazifikie upesi Sakramenti zote nilizokuwa nimezianzisha Mimi, kateremke na kaingie mpaka chini kilindini mwa hizo Sakramenti, na pale ukanipatie Mimi yale malipo yako madogo ya pendo lako. Lo! Utakuta pale machozi Yangu mengi mangapi ya siri, mitweto Yangu mingapi ya machungu, na vilio vingi vingapi vya Roho Mtakatifu aliyekabwa kooni. Mbele ya Pendo Letu kudanganyika mara nyingi sana, kilio cha Roho Mtakatifu cha malalamiko ni endelevu. Sakramenti zilikuwa zimewekwa kwa ajili ya kuendeleza Uhai Wangu pale duniani kati ya watoto Wangu. Lo! kumbe lakini, ni uchungu na mateso mengi mangapi. Ndiyo maana ninaonja sana ulazima wa lile pendo lako dogo. Linaweza kuonekana kuwa ni dogo tu, lakini, Utashi Wangu ndio utakaolikuza liwe pendo kuu. Pendo Langu huwa haliwezi kuvumilia kama mtu anayepasika kuishi ndani ya Utashi Wangu hatajihusisha na mateso Yangu, na kama hatakuwa ananiletea malipo yake madogo ya pendo kwa mambo yale yote niliyokuwa nimetenda na kwa yale niliyoteseka. Kwa hiyo, Binti Yangu, nenda ukaone jinsi pendo Langu linavyolalamika pale ndani ya Sakramenti mbalimbali.    

Ninapomwona kichanga akibatizwa, Mimi huwa ninapiga kelele kwa masikitiko.

Ni kwa sababu, wakati kwa Ubatizo Mimi ninamrejeshea ule ubilawaa wake, kwa Ubatizo ninamkuta tena yule mtoto Wangu, kwa Ubatizo ninamrejeshea tena zile haki zake zote juu ya Uumbwa ambazo alikuwa amezipoteza, kwa Ubatizo ninamtazama kwa tabasamu na kwa pendo na kwa kuridhika, kwa Ubatizo ninamfukuza na kumkimbiza yule adui wake hata huyo asiwe na haki yoyote ile juu yake huyu Mbatizwa, na kwa Ubatizo ninamkabidhi huyo Mbatizwa kwa Malaika, na ndipo wale wote wa Mbinguni huwa wanamsherehekea huyo Mbatizwa - kumbe lakini, punde tu baadaye, ile tabasamu Yangu huwa inageuka kuwa uchungu, ile sherehe hugeuka kuwa ni maombolezo. Huwa ninaona kwamba yule anayebatizwa hugeuka kuwa ni adui Wangu Mimi, anageuka kuwa Adamu mpya, na pengine hugeuka kuwa ni mtu wa kupotea kabisa. Lo! ni jinsi gani pendo Langu huwa linalia na kulalamika katika kila Ubatizo. Halafu, mbaya zaidi, ukiongeza ukweli kwamba pengine yule mhudumu anayebatiza haadhimishi kwa heshima ile itakiwayo, wala kwa adhama na hadhi na usafi unaotakiwa kwa Sakramenti hii ambayo inabeba tendo la uzalishaji mpya! Ah! Mara nyingi sana hawa wahudumu huwa wanaangalia zaidi mambo ya nje, ya usanii, na maigizo, badala ya kuzingatia adhimisho la Sakramenti. Ndipo pendo Langu huwa linaonja kuwa linachomwa kwa miiba au kwa sindano na huyo anayebatiza na pia na mwenyewe anayebatizwa. Ndipo Pendo Langu hulia na kulalamika kwa vilio visivyoelezeka. Sasa, je wewe, usingependa kweli kuniletea Mimi malipo ya pendo kwa njia ya malipo ya kilio chenye pendo kwa kila Ubatizo, ili kusudi wewe uweze kuvisindikiza hivyo vilio Vyangu vya uchungu?.

Ebu fikiria na Sakramenti ya Kipaimara. Ah! Kuna mitweto mingi mingapi ya uchungu. Wakati, Mimi, katika Sakramenti ya Kipaimara, ninamrejeshea mtu ule uhodari wake, ninamrejeshea nguvu zake zile zilizopotea, huwa ninamwezesha asishindwe mbele ya maadui wake wote, mbele ya matamaa yake yote, na kwa Kipaimara mtu anajiunga na vile vikosi vya jeshi la Muumba Wake, ili awe anapigana daima kwa ajili ya kuipata ile inchi ya Baba wa Milele, na pale Roho Mtakatifu huwa anampatia kwa mara nyingine busu Lake, huwa anamwagia mipapaso Yake elfu juu ya mwanakipaimara, na pia Roho Mtakatifu anajitoa Mwenyewe ili awe ni mwenzi wa huyo mtu katika ajira yake. Lakini kumbe, mara nyingi sana, Roho Mtakatifu, huwa anaonja kuwa analipwa kwa busu la msaliti. Ile mipapaso Yake huwa inadharauliwa na kubezwa. Ule usindikizi Wake huwa unakataliwa na kukwepwa. Ni vilio vingapi vya Roho Mtakatifu, ni mitweto mingapi kwa ajili ya kurejea kwa huyo mwanakipaimara, ni sauti za siri ngapi zinazokuja kwenye moyo Wake, yote kwa ajili ya huyo anayemkwepa Roho Mtakatifu - ambaye huwa anaendelea kutoa sauti zake za siri hadi anafikia kuchoka kuzungumza. Hata hivyo - hapana, yote huwa ni kazi bure. Kwa hiyo basi, je wewe hupendi kutoa malipo yako ya pendo, hutaki kutoa lile busu lako la upendo, hutaki kumsindikiza Roho Mtakatifu, anayelia na kulalamika kutokana na kusahauliwa mno kiasi hicho? 

Hata hivyo, wewe usisitishe zile ziara zako, endelea kuruka ndani ya Utashi Wangu, na utafikia kusikia vilio vyenye maumivu vya Roho Mtakatifu pale katika Sakramenti ya Upatanisho. Kuna utovu ulioje wa shukrani, kuna matumizi mabaya mangapi, na kuna makufuru mengi mangapi yanayoletwa na wale wanaoadhimisha Sakramenti hii na yanayoletwa pia na wale wanaoipokea. Katika Sakramenti hii, Damu Yangu huwa inakuja kutenda kazi yake juu ya mdhambi anayetubu, ili kusudi iteremke juu ya roho yake na kumwosha, kumpamba na kumremba, ili kumponya, ili kumpa nguvu, ili kumrejeshea ile neema iliyopotea, ili kukabidhi mikononi mwake zile funguo za Mbinguni, funguo ambazo dhambi ilikuwa imemnyang’anya toka pale mikononi mwake, na ili Damu Yangu ibandike, juu ya panda lake la uso, lile busu la msamaha wa dhambi linaloleta upatanisho wa amani. Lakini, ah! Ni vilio vya malalamiko vingi vingapi vya kutisha unapoona watu wanaiendea Sakramenti hii ya Upatanisho bila majuto yoyote yale, wengine wanaipokea kwa mazoea tu, na wengine wanaipokea kama kitulizo tu cha moyo wao wa kibinadamu. Na kwa wengine, ni jinsi gani inavyotisha hata kueleza, badala ya kuiendea Sakramenti hii kwa ajili ya kutafuta uhai wa roho zao na uhai wa neema, wao wanakwenda kutafuta mauti ya roho, na kwa ajili ya kwenda kumwaga tu matamaa yao. Kwa jinsi hiyo, Sakramenti hii imegeuzwa kuwa ni mzaha na maigizo tu, imegeuzwa kuwa ni fursa ya kusimuliana visa mbalimbali. Kumbe basi, Damu Yangu, badala ya kuteremka kama bafu, sasa huteremka kama moto utakaowanyausha zaidi na zaidi. Kwa hiyo hasi, katika kila Kitubio, lile Pendo Letu huwa linalia bila kufarijika, na, linapodondosha machozi, huwa linarudia kusema: ‘Ewe utovu wa shukrani wa binadamu, mbona umekuwa ni mkubwa kiwango hicho. Mbona, popote pale unajaribu kunichukiza. Na Mimi ninapotaka kukuletea uhai, wewe unaugeuza, huo huo uhai ninaokuletea, kuwa kifo’. Basi sasa, uone wewe mwenyewe jinsi vilio Vyetu Sisi vinavyongojea sana malipo yako ya pendo hata katika Sakramenti ya Upatanisho.

Tafadhali, hilo pendo lako lisisimame. Uendelee kuzungukia Tabernakulo zote, uzungukie kila Hostia Takatifu ya Sakramenti, na katika kila Hostia utamsikia pale Roho Mtakatifu akilia kwa kulalamika kwa uchungu usioelezeka. Sakramenti ya Ekaristi Takatifu siyo tu ni uhai wao ambao watu hupokea, bali zaidi, ni Uhai Wangu Mimi Mwenyewe unaojitoa Wenyewe kwao. Basi, tunda la Sakramenti hii huwa ni kujenga Uhai Wangu pale ndani mwao, na kila Komunyo Takatifu wanayopokea ni kwa ajili ya kustawisha na kuuendeleza Uhai Wangu, kwa jinsi hii kwamba mtu aweze kufikia kusema: ‘Mimi ni Kristo Mwingine’. Kumbe lakini, kwa sikitiko! Ni wachache sana wangapi ambao wanalifaidi hilo. Na zaidi zaidi, ni mara nyingi ngapi, Mimi huwa ninateremkia na kuingia ndani ya mioyo, na kumbe wao wananipelekea kuzigundua pale zile silaha wanazotumia kunijeruhi Mimi, na hivyo ndivyo wanavyoniletea Mimi tena ule mkasa wa yale Mateso Yangu. Na pale wanapokula yale maumbo ya Sakramenti, hawa watu, badala ya kunisihi Mimi niendelee kubaki pamoja nao, wao wananilazimisha na kunifukuza nitoke nje huku nikiwa nimelowa kwa machozi, huku nikilia na kupiga kelele juu ya mkasa Wangu huo wa ki-Sakramenti. Na huwa simpati mtu hata mmoja anayekuja kunituliza katika kilio changu na katika yale malalamiko Yangu ya uchungu sana. Kama ungeweza kupasua yale mapazia ya Hostia Takatifu, mapazia yale yanayonifunika na kunificha, hakika ungeniona ninaoga mwenye machozi Yangu, huku nikifahamu fika, ule mkasa unaoningojea wakati nitakapoingia na kuteremkia ndani ya mioyo ya watu. Kwa hiyo, tafadhali, uache yale malipo yako ya pendo kwa ajili ya kila Hostia yawe daima ni endelevu, ili kusudi, yawe yanatuliza kilio changu na yasaidie kupunguza yale malalamiko ya uchungu ya Roho Mtakatifu.

Na wala usimalizikie na kusimama hapo. Vinginevyo Sisi, katika vilio vyetu na malalamiko na katika yale machozi Yetu ya siri, hatutakuwa tunakukuta wewe ukiwa pamoja Nasi daima. Hapo tutakua tunalionja lile ombwe la yale malipo yako ya pendo. Ebu sasa uteremkie kwenye Sakramenti ya Daraja Takatifu. Hapa, ni kweli kabisa, utayakuta yale machungu Yetu yaliyofichikana, ya siri za ndani kabisa mno, utayakuta machozi Yetu yaliyochachuka mno, utayakuta malalamiko Yetu ya kutisha na kushangaza mno. Daraja Takatifu humpandisha binadamu kwenye kilele kikuu cha juu, kinampandisha hadi kwenye tabia ya kimungu - humfanya awe ni kipazasauti cha Uhai Wangu Mimi, hupandisha awe ni mhudumu wa Sakramenti mbalimbali, kuwa mfunuaji wa siri Zangu, mfunuaji wa Injili Yangu, na mfunuaji wa yale maarifa matakatifu kabisa. Humfanya awe ni mleta amani kati ya Mbingu na dunia, na humfanya awe mbebaji na mpelekaji wa Yesu kwa watu. Kumbe lakini, kwa masikitiko, ni mara nyingi ngapi Sisi huwa tunaona, ndani ya yule aliyepewa Daraja Takatifu, jinsi atakavyokuwa ni Yuda fulani Kwetu Sisi, jinsi atakavyokuwa ni mvamizi na mporaji wa ule mhuri unaobandikwa juu yake. Lo! Ni jinsi gani Roho Mtakatifu anavyolia na akilalamika kwa kuona, pale ndani ya huyu aliyepewa Daraja, namna yale matakatifu mno, na ule mhuri mkuu kabisa unaoweza kupatikana kati ya Mbingu na dunia, hivyo vyote vinavyoporwa toka mikononi Mwake. Kuna makufuru mengi mangapi! Kila kitendo cha huyu mpakwa mafuta, anachokitekeleza kinyume cha ule mhuri aliobandikwa, kitakuwa ni kilio cha mateso na masikitiko, kitakuwa ni kilio cha uchungu, kitakuwa ni lalamiko linalorarua moyo. Daraja Takatifu ni Sakramenti inayobeba ndanimo, kwa pamoja, zile Sakramenti nyingine zote. Kwa hiyo basi, kama aliyepewa Daraja Takatifu ataweza kuhifadhi vema, pale ndani yake, ule mhuri alioupata, huyo atakuwa anaziweka karibu zile Sakramenti nyingine zote katika usalama. Huyo atakuwa ni mlinzi na mtetezi na ni mwokozi wa Yesu Mwenyewe. Kumbe lakini, pale ambapo Sisi hatulioni hilo ndani ya yule aliyepata Daraja Takatifu, masikitiko Yetu huongezeka na kuwa makali zaidi, na vilio vyetu vya malalamiko huzidi kuwa endelevu na vya uchungu zaidi. Kwa hiyo basi, ebu acha hayo malipo yako ya pendo, yatiririkie ndani ya kila tendo la kipadre, ili likawe msindikizi kwa lile pendo la Roho Mtakatifu, linalolia na kulalamika.

Tafadhali, sasa utupatie Sisi hilo sikio la moyo wako ili ukasikilize vilio vyetu vya malalamiko kuhusu Sakramenti ya Ndoa Takatifu. Kuna vurugu nyingi ngapi! Ndoa Takatifu ilikuwa imepandishwa na kupewa hadhi yake na Mimi hata ikawa Sakramenti. Niliipandisha ili ndani yake niweke kile kifungo kitakatifu ambacho ni ishara ya Utatu Mtakatifu, na ishara ya pendo la kimungu linalobebwa pale ndani yake. Kwa hiyo, lile pendo lililotakiwa liwe likitawala ndani ya baba, ndani ya mama na ndani ya watoto, ule uelewano, na ile amani vilitakiwa viashirie ile Familia ya Mbinguni. Kwa hapa duniani, Mimi nilitakiwa niwe nazo familia nyingine nyingi zinazofanana na ile Familia ya Muumba. Hizo familia zilipangwa ziwe kwa ajili ya kuongeza idadi ya watu ili kuijaza dunia, ili watu wawe sawa kama malaika wengi wa hapa duniani, watu ambao baadaye wangerudi kwenda kuyajaza yale maeneo ya Mbinguni. Lakini, ah! Ni vilio vingi ilioje vya malalamiko tunapoona jinsi familia za dhambi zinavyozaliwa ndani ya Ndoa. Ni familia zinazoashiria moto wa milele, familia zenye magomvi, familia bila upendo, familia zenye chuki, na familia zinazoongeza idadi hapa dunia mithili ya malaika wengi waasi ambao watafaa tu kwa ajili ya kuijaza jahanamu. Hapa Roho Mtakatifu, katika kila Ndoa, analia kwa malalamiko mengi mno, na ya kukatisha na tamaa, anapoona jinsi mahandaki mengi mno ya moto wa milele yanayochimbwa hapa duniani. Kwa hiyo basi, wewe, tafadhali, nenda kaingize malipo yako ya pendo pale ndani ya kila Ndoa, na ukaingize pia ndani ya kila mwanadamu ambaye anazaliwa. Kwa jinsi hiyo, kilio chako cha malalamiko kitasaidia kupunguza yale machungu ya vilio Vyetu vya malalamiko endelevu.

Vile vilio Vyetu havijamalizika bado. Basi, hebu acha hayo malipo yako ya pendo yakafike hadi kwenye kitanda cha yule aliye mahututi wakati inatolewa huduma ya Sakramenti ya Mpako Mtakatifu. Lakini, ah! Kuna vilio vingi vingapi, na kuna mengi mangapi yale machozi Yetu ya siri! Sakramenti hii, kwa gharama yoyote ile, inayo nguvu ya kumweka katika usalama mtu yule aliye mahututi. Hii Sakramenti ni uthibitisho wa utakatifu kwa ajili ya wale walio wema na watakatifu. Kwa njia ya Mpako wake Mtakatifu, Sakramenti hii huwa inaweka kifungo cha mwisho kabisa kati ya mwanadamu na Mungu. Mafuta ya Sakramenti hii ni mhuri wa Mbinguni ambao Sakramenti hii inaubandika juu ya mtu aliyekombolewa. Mpako huo ni tendo la kuingiza mastahili mbalimbali ya Mkombozi ndani ya mtu, kwa ajili ya kumtajirisha kiroho, kwa ajili ya kumsafisha na kwa ajili ya kumpamba. Mpako Mtakatifu ni mpako wa brashi ya mwisho ambayo Roho Mtakatifu anatoa kwa mtu ili kumwandaa kwa ajili ya kuiaga dunia na kumfanya aweze kusimama mbele ya Muumba Wake. Kwa ufupi ni kwamba, Mpako wa Mwisho ndiyo maonyesho ya mwisho ya Pendo Letu, na ni zoezi la mwisho la kumvalisha mwanadamu. Ni zoezi la mwisho la kupanga upya kazi zote njema za yule aliye mahututi. Kwa hiyo, Mpako Mtakatifu unatenda kazi kwa namna ya kushangaza ndani ya wale ambao huwa wapo bado hai katika neema. Kwa njia ya Mpako wa Mwisho, mtu huwa kama vile amefunikwa na umande wa mbinguni, ambao, mithili ya pumzi moja pekee, huzima yale matamaa yote ya mtu huyo, huzima mafungamano yake na dunia, na huzima mafungamano yake na chochote kile kisichoihusu Mbingu. Lakini, kwa sikitiko kubwa! Kuna vilio vingi vingapi, kuna machozi mengi mangapi ya uchungu, kuna ugumu mwingi ilioje wa kuitikia, na kuna uzembe mwingi ulioje kuhusu Sakramenti hii. Ni roho nyingi ngapi zinazopotea. Na ni hali za utakatifu chache ilioje ambazo Sakramenti hii inazikuta kwa ajili ya kuzithibitisha kwa dakika ya mwisho. Na huwa kuna matendo mema machache ilioje yanayosubiri kuwekwa katika taratibu tena na kuingizwa katika mpangilio wa dakika ya mwisho. Lo! Kama watu wote wangesikia yale malalamiko Yetu, kama wangesikia vile vilio Vyetu pale penye kitanda cha yule mgonjwa mahututi, pale wakati wa kutoa Sakramenti ya Mpako Mtakatifu wa Mwisho - hakika wote wangelia kwa uchungu sana. Basi sasa, je wewe, kweli hupendi kutupatia Sisi yale malipo yako ya pendo kwa ajili ya mara zile zote inapotolewa Sakramenti hii, nafasi ambayo huwa ndiyo maonyesho ya mwisho kabisa ya Pendo Letu kwa mwanadamu? Utashi Wetu Sisi unakusubiri wewe kila mahali, ili Sisi tuweze kupata yale malipo yako ya pendo na ili tupate usindikizi wako katika vilio Vyetu vya malalamiko na katika mitweto Yetu”

Kila siku, hatua kwa hatua, jisomee hapa, ili upate kukua katika Paji la Uhai, ndani ya UTASHI WA MUNGU, kulingana na Mafundisho aliyoyatoa YESU kwake Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA

⬇️⬇️⬇️

Swahili - Telegram Channel: Utashi Wa Mungu Na Upendo Wa Mungu

Swahili - Telegram Channel: Saa 24 Za Mateso Ya Bwana Weto Yesu Kristo

Swahili - Telegram Channel: Bikira Maria Katika Ufalme wa Utashi wa Mungu

English - Telegram Channel: Divine Will Divine Love

English - Telegram Channel: The Virgin Mary in the Kingdom of the Divine Will

Français - Chaîne Telegram: Divine Volonte Divin Amour

Français - Chaîne Telegram: Lettres de Luisa Piccarreta

Lingala - Chaîne Telegram: Mpo Elingi Nzambe Bolingi bwa Nzambe

Website all languages: www.divinewilldivinelove.com

Vitabu yote vilivyo katika faili za PDF vinaweza kupakuliwa bila gharama yoyote ile wakati wote ule. Pia, upo huru kabisa kuchapisha VITABU hivyo wewe mwenyewe binafsi au kuchapisha kwenye kiwanda chochote kile. Lakini vitabu hivyo ni kwa matumizi binafsi tu na siyo kwa ajili ya biashara! Hata hivyo una ruhusa ya kuwashirikisha na kuwapatia watu wengine vitabu hivyo kadiri unavyopenda!!

Swahili landing page: click here

English landing page: click here

Lingala landing page: click here

Kikongo landing page: click here

French landing page: click here

Italian landing page: click here

Report Page