Yesu kwa Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - KITABU cha MBINGU - Juzuu na. 19 - Agosti 8, 1926 🖋📄📖📔

Yesu kwa Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - KITABU cha MBINGU - Juzuu na. 19 - Agosti 8, 1926 🖋📄📖📔


Wakati nikiwa katika ile hali yangu ya siku zote, nilikuwa nikionja kuwa nimekabidhi nafsi yangu yote katika mikono ya Yesu. Na Yeye alipoingia ndani mwangu aliniambia:

“Binti Yangu, kadiri mtu atakavyozidi kujiainisha na Mimi, ndivyo na Mimi nitakavyozidi kutoa kwake, na ndivyo na yeye atazidi kupokea toka Kwangu Mimi.

Panatokea kitu kama kile cha Bahari na kijito ambacho, kwa njia ya ukuta tu kimetenganishwa kutoka hiyo bahari kiasi kwamba utakapoondoa huo ukuta, basi bahari na kijito vinakuwa ni bahari moja peke yake.

Sasa, wakati bahari inapofurika, kwa vile ipo kando, kijito kile kitapokea maji ya bahari. Na kama mawimbi yangurumayo yatazidi kupanda, yatakapoteremka tena yatatua ndani ya kile kijito kilicho kando ya bahari. Tena, maji ya bahari yatakuwa yakimwagikia ndani ya kijito kile kwa kupita katika mianya iliyopo katika ukuta ule unaotenganisha bahari na kijito. Kwa jinsi hiyo, kile kijito huendelea kupokea daima maji kutoka baharini, na kwa vile ni kijito kidogo, kitakuwa nacho kikiendelea kujaa maji na kitaendelea kuyatoa na kuyarudisha baharini yale yale maji ambayo kimekuwa kinayapokea, na tena kitakuwa kinaendelea kupokea maji mengine toka baharini.

Lakini, hilo litaendelea kutokea kwa vile kijito kipo kando ya bahari. Lakini kama kingekuwa mbali na bahari, hiyo bahari isingeweza kutoa maji kwa kijito, na wala kijito kisingeweza kuwa kinapokea maji - ule umbali wake ungekizuia kijito hata kisiweze kuifahamu kabisa ile bahari”.

Alipokuwa akizungumza hayo, alinionyesha akilini mwangu, kwa namna ya uhalisia wake, kile kitendo cha bahari na cha kijito kile. Ndipo aliendelea kusema:

“Binti Yangu, ile bahari ni Mungu, kile kijito kidogo ni mtu, na ule ukuta unaotenganisha bahari na kijito ni hulka ya kibinadamu inayomfanya mtu aweze kutofautisha kati ya Mungu na mwanadamu. Yale mafuriko, yale mawimbi yanayopanda mara kwa mara na kujimwaga ndani ya kile kijito ndiyo Utashi Wangu unaotamani kutoa mambo mengi kabisa kwa mwanadamu, kiasi kwamba, kile kijito kidogo, kwa vile ni kidogo na tayari kinajaa na kufurika, kitaweza kujaa zaidi na kufurika, kinaweza kikatengeneza nacho mawimbi yake. Na kwa vile kinaweza nacho kuvimbishwa kwa upepo utokao kwa Utashi Mkuu wa Juu, kitaweza nacho pia kikayarudisha maji na kuyamwagia tena katika bahari ya kimungu. Papo hapo kijito kitaweza kuzidi kujazwa maji tena hata kitaweza kujisemea: ‘Mimi nami ninayaishi maisha ya bahari. Na hata kama mimi ni mdogo, lakini nami pia ninakitenda kile kile inachokitenda: huwa ninafurika, huwa natengeneza mawimbi yangu, huwa ninavimba na kupanda juu, na hata huwa ninajaribu kupeleka baharini kile ambacho yenyewe huwa inaniletea’. 

Kwa sababu hiyo basi, mtu ambaye anajiainisha na Mimi na anayekubali kutawaliwa na Utashi Wangu huyo huwa anarudia kutenda matendo ya Kimungu. Pendo lake, uabudu wake mbalimbali, sala zake, na chochote kile anachotenda, huwa ni ufurikaji wa Mungu anaoupata kiasi cha kuweza kujisemea mwenyewe: ‘Ni pendo Lako ndilo linalokupenda Wewe, ni uabudu Wako ndio unaokuabudu Wewe, ni sala Zako ndizo zinazokuomba Wewe. Ni Utashi Wako ndio, ambao, unaponifunika mimi, ndipo unanifanya mimi nitende kile unachotenda Wewe, ndio unaniwezesha mimi kukurudishia Wewe matendo hayo kama matendo ya Kwako Mwenyewe’”.

Yesu alinyamaza. Lakini halafu, akigutuka kama vile kaguswa na kutekwa na pendo kali, aliongeza kusema:

“Oh, nguvu ya Utashi Wangu, u mkuu ilioje!

Ni wewe peke yako ndiye unayeunganisha Yule aliye Mkuu kabisa na wa Juu kabisa kwa yule aliye mdogo kabisa na wa chini kabisa, unawaunganisha na kuwafanya kitu kimoja. Wewe peke yako una nguvu ya kufagilia mbali, toka kwa mwanadamu, chochote kile kisichokuwa cha Kwako, ili kutengeneza ndani yake, kwa njia ya mimemetuko Yako, lile Jua la Milele, ambalo, linapojaza Mbingu na dunia kwa mionzi Yake, huenda kuyeyushiana na lile Jua la Ukuu Mtukufu wa Juu.

Wewe peke yako unayo hiyo nguvu ya kuwasilisha ile nguvu kuu ya juu, kiasi kwamba, kwa nguvu yako, mwanadamu anaweza akakwea kufikia kwenye lile tendo pekee la Mungu Muumbaji. Ah, Binti Yangu, pale ambapo mwanadamu haishi ndani ya umoja wa Utashi Wangu, huwa anapoteza hiyo nguvu moja, na hivyo huwa anabakia kama vile ametenganishwa na nguvu hiyo, inayozijaza Mbingu na dunia, na ambayo huwa inashikilia ulimwengu wote, kana kwamba ungelikuwa ni unyoya mmoja mdogo kabisa. Basi, kama mtu hatakubali kutawaliwa na Utashi Wangu, hapo huwa anapoteza ile nguvu moja katika kila moja ya matendo yake. Kwa hiyo, matendo yake yote, kwa vile hayatoki kwenye ile nguvu moja pekee, huwa yanabaki yakiwa yametengana kati yao yenyewe - pendo huwa limegawanyika, utendaji huwa umetenganika, na sala huwa imenyofolewa. Katika utengano huo, matendo yote ya mwanadamu huwa ni duni, hafifu, na hukosa kuwa na mwanga. Na kwa hiyo, subira ni duni, upendo ni dhaifu, utii huwa lemavu, unyenyekevu huwa kipofu, sala huwa ni bubu, sadaka huwa jifu, haina nguvu. Yote ni kwa vile, kwa kukosekana Utashi Wangu, huwa panakosekana ile nguvu moja, ambayo, kwa kuunganisha mambo yote, huwa inatoa nguvu ile ile kwa kila tendo la mwanadamu. Basi, matendo huwa yanaachwa yakiwa, siyo tu, yamegawanyika kati yao, bali, yakiwa yamechafuliwachafuliwa na utashi wa kibinadamu, na kwa hiyo kila tendo huwa limeachwa katika mapungufu yake.

Ndilo hilo lilitokea kwa Adamu.

Kwa kitendo cha kujiondoa mwenyewe toka kwenye ule Utashi Mkuu wa Juu, alipoteza ile nguvu moja ya Muumba Wake. Na kwa vile kaachwa tu na nguvu zake hafifu za kibinadamu, akawa anaonja magumu katika utendaji wake. Na hasa zaidi, kwa vile nguvu aliyokuwa akitumia katika kutekeleza kitendo kimoja ilikuwa inamdhoofisha, na hivyo ilipompasa kutekeleza tendo lingine, hakuweza tena kuionja nguvu ileile ya awali. Basi, kwa mkono wake mwenyewe, akawa anaugusa uduni wa matendo yake: Kwa vile matendo yake hayakuwa na nguvu ile ile moja, yakawa siyo tu yamegawanyika, bali kila moja ya matendo yake likawa na kasoro ya kwake.

Ikawa inatokea kama inavyokuwa kwa mtu mmoja tajiri, mwenye kumiliki vitu vya gharama kubwa sana: pindi vitu hivyo vinamilikiwa na mtu mmoja peke yake, atakuwa anajigamba, atakuwa anaagiza na kununua bidhaa kubwa kubwa. Kwani ni nani ajuaye, sijui, kuna watumishi wa ngapi chini yake, na kwa mapato makubwa anayojipatia, yeye ataendelea kuagiza na kununua bidhaa mpya. Lakini, tujali mali yake hiyo yote ingegawiwa kwa warithi wengine: ndipo hapo - nguvu yake kubwa tayari ingepotea, hawezi akawa anajigamba kama pale awali, na wala hawezi akawa anaagiza kununua bidhaa mpya. Itampasa ajikusuru katika matumizi yake, na itampasa awe na watumishi wachache zaidi. Kwa hiyo ukubwa wake na ubwenyenye wake wote umefifia. Kinachosalia kwake ni tu alama chache za ile mali aliyokuwa nayo.

Ndivyo ilivyotokea kwa Adamu. Kwa kujiondoa toka kwenye Utashi Wangu, alikuwa amepoteza ile nguvu moja pekee ya Muumba Wake, na pamoja na hiyo kapoteza enzi yake, himaya yake, na wala hakuweza tena kuonja nguvu ya kujigamba katika mema. Ndivyo hivyo hutokea kwa mtu yule ambaye hajajisalimisha kikamilifu ndani ya mikono ya Utashi Wangu, kwani, mtu akiwa na Utashi Wangu, ile nguvu ya mema huwa inageuka kuwa ni hulka ya mtu, na hapo ufukara huwa haupo tena”.

Juzuu na. 19 ku download - click here

Kila siku, hatua kwa hatua, jisomee hapa, ili upate kukua katika Paji la Uhai, ndani ya UTASHI WA MUNGU, kulingana na Mafundisho aliyoyatoa YESU kwake Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA

Swahili - Telegram Channel: Utashi Wa Mungu Na Upendo Wa Mungu

Swahili - Telegram Channel: Saa 24 Za Mateso Ya Bwana Weto Yesu Kristo

Swahili - Telegram Channel: Bikira Maria katika Ufalme wa Utashi wa Mungu

English - Telegram Channel: Divine Will Divine Love

English - Telegram Channel: The Virgin Mary in the Kingdom of the Divine Will

Français - Chaine de Telegram: Divine Volonte Divin Amour

Français - Chaîne de Telegram: Lettres de Luisa Piccarreta

Lingala - Chaine de Telegram: Mpo Elingi Nzambe Bolingi bwa Nzambe

Website all languages: www.divinewilldivinelove.com

Vitabu yote vilivyo katika faili za PDF vinaweza kupakuliwa bila gharama yoyote ile wakati wote ule. Pia, upo huru kabisa kuchapisha VITABU hivyo wewe mwenyewe binafsi au kuchapisha kwenye kiwanda chochote kile. Lakini vitabu hivyo ni kwa matumizi binafsi tu na siyo kwa ajili ya biashara! Hata hivyo una ruhusa ya kuwashirikisha na kuwapatia watu wengine vitabu hivyo kadiri unavyopenda!!

Swahili landing page: click here

English landing page: click here

Lingala landing page: click here

Kikongo landing page: click here

French landing page: click here

Italian landing page: click here

Report Page