Yesu kwa Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - KITABU cha MBINGU - Juzuu Na. 31 - Oktoba 9, 1932🖋📃📖📔  

Yesu kwa Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - KITABU cha MBINGU - Juzuu Na. 31 - Oktoba 9, 1932🖋📃📖📔  


Nimekuwa naendelea na maisha yangu ya kujitoa na kujikabidhi ndani ya FIAT. Kadiri nilivyozidi kujikabidhi ndani Yake, ndivyo nimezidi kuionja nguvu Yake ikiniimarisha, nimeonja Uhai Wake ukihuisha uhai wa kwangu, mwanga Wake umezidi kunituliza, kuniangaza na pia umefanya kazi Yake ya kuzidi kunifunulia Yule ambaye katika mikono Yake nimekuwa nimejikabidhi kikamilifu kabisa. Kwa nguvu Yake ya sumaku alinivuta nizunguke kutembelea kazi Zake, akataka na akapenda huyu Binti Yake mdogo awe mtazamaji wa kila kitu alichokwisha kufanya kwa ajili ya Pendo kwa wanadamu. Hapo nilipokuwa nikizunguka, Mtukufu Yesu Wangu Mkuu na Mwenye Mamlaka, alinisimamisha pale katika tendo la kumuumba binadamu akaniambia:

“Binti Yangu, kumbukumbu tamu ilioje ya tendo la kuumbwa binadamu! Yeye alikuwa ameumbwa katika ekstasi Yetu mojawapo ya Pendo. Pendo Letu lilikuwa kubwa hivi hata tulibakia tumetekwa mbele ya kazi Yetu yenyewe tuliyokuwa tukiitoa na kuileta hadharani. Ulikuwa unatuvuta na kututeka ule uzuri upendezao tuliokuwa tumemvika huyu binadamu, ulituteka utakatifu tuliokuwa tumemjaza, lilituteka umbo lake na uuwiano ambamo tulimtengeneza. Mapaji yake na kila moja ya sifa zake vikawa ni kitu kilicholeta ekstasi ya Pendo tuliyoionja na iliyotuvuta na kututeka tuwe tunampenda. Kwa namna hiyo Pendo Letu lilitikiswa na lilitawaliwa sana. Baada ya kutuingiza katika ekstasi liliamsha ndani yetu Pendo la utendaji na lenye kutusukuma na kutulazimisha tuwe tunafanya kitu zaidi kwa binadamu. Tukiwa katika ekstasi hiyo ya Pendo, kwa jinsi ile tulivyokuwa tumetekwa, hatukuwa tukiangalia kitu chochote sasa, hatukuwa na mipaka fulani sasa, bali tulijimwaga mno katika kumpenda na katika kumtajirisha kwa mema yote, hata hatukuachia pengo lolote la wazi bila kumjazia mema, ili tu pendo lake kwetu liwe daima limejaa, na hivyo angekuwa akiendelea kutuvutia, ili tuwe tunampenda daima. Kwa sababu hiyo, tupatapo tu kukumbuka jinsi binadamu alivyoumbwa huwa inaturudia ile ekstasi yetu ya upenzi na binadamu.

Kwa hiyo sasa, mtu yule anayezunguka kufanya ziara katika Utashi Wetu, anapofika kuziona kazi Zetu, ambazo ndizo zilikuwa kama maandalizi kwa ajili ya kumwumba binadamu hapo baadaye, anakuwa kama anagonga kengele ya kuviita viumbe vyote vilitambue Pendo hilo la Mungu kwa ajili ya binadamu. Na sauti hiyo tamu ya kengele inatushitua na kutuita hata Sisi, inatuamshia lile Pendo Letu na linafufua tena ndani Yetu ile ekstasi Yetu ya Pendo kwa binadamu. Ekstasi ina maana ya kujimwaga kikamilifu kabisa kumwelekea mtu unayempenda. Yule anayeingia katika Utashi Wetu huwa ana nguvu ya kutuvuta Sisi tuendelee kuivumilia ekstasi Yetu ya Pendo hadi hapo tutakapojimwaga ndani yake. Na Sisi kwa upande Wetu, kwa nguvu tuliyo nayo, tunamvuta huyo mwanadamu katika ekstasi ya kutupenda Sisi, hata afikie kujimwaga mwenyewe kikamilifu kabisa ndani ya Uwepo Wetu wa Juu . Huwa panatokea tendo la kila upande kujimwaga ndani ya mwenzake. Kwa sababu hiyo, hakuna kitu kinachotupendeza zaidi kama hiki cha kumwona mwanadamu akiwa katika Utashi ule ule alioumbwa nao. Tulipoviumba vitu vingi na mbalimbali, pamoja na Uumbwa wote, tulikuwa tumemwandalia na kumkabidhi binadamu zawadi ya seti ya mapaji mbalimbali. Ni kama vile, uwezo wa kuangalia na kustaajabia kazi Zetu, uwezo wa kuzijua, uwezo wa kusikia na kuonja pumzi za Pendo Letu, pumzi ambazo zipo ndani ya kila kiumbe. Sasa je, ni nani anayepata Uhai wa jema lile lililopo ndani ya viumbe? Ni nani aliye na haki ya kufaidi matumizi ya seti ya zile zawadi nzuri kabisa? Ni nani ana uwezo wa kuzifahamu? Wakati binadamu anapovifahamu hivyo viumbe ndipo analikuta Pendo Letu linalotoa pumzi Zake pale, anaukuta Utashi Wetu ukitenda kazi, anavipenda viumbe hivyo, na hatimaye, ndani ya viumbe hivyo anafikia hata kumpenda Yule Mkuu wa Juu kabisa ambaye ndiye anayempenda mno. Kwa hiyo basi, uwe makini na thabiti sana katika kutekeleza ziara zako za kutembelea kazi Zetu. Ndivyo hivyo tutashikana mkono katika kupendana, tutajiingiza katika ekstasi na wewe utaweza kutumia vema ile seti ya mapaji aliyokupatia Muumba wako katika upendo mkubwa”.

Kishapo, akili yangu ndogo ilianza matembezi yake kuzungukia matendo ya Utashi wa Mungu. Nilipopitia moja baada ya lingine, nilifikia lile tendo la Bikira Mtakatifu kutungwa katika mimba. Oh, Mungu Wangu! Mbingu zote zinaduwaa na zimekuwa bubu mbele ya tendo hilo lililotekelezwa na Utashi wa Mungu. Malaika wameshikwa na kigugumizi, na kwa kile kidogo wanachojaribu kusema yaelekea inawashinda kutoa maelezo ya bayana juu ya ajabu kubwa ya namna hiyo. Ni Mungu peke Yake anaweza akalizungumzia, kwani Ndiye mwanzilishi wa tukio hilo la ajabu lililopelekea kupatikana kwa mimba hiyo. Pindi nikistaajabia hivyo, Yesu Wangu Mpendevu alinishitua na kuniambia:

“Binti Yangu, tukio la Bikira Immakulata kutungwa katika mimba lilikuwa ni tendo jipya la Utashi Wetu, lilikuwa ni jipya katika mtindo wake, jipya katika wakati wake, jipya katika Neema. Katika huyu Bikira Immakulata Uumbwa wote umeupyaishwa. Katika uwezo Wetu wa kuona yote na popote na katika ukuu Wetu usio na kikomo, tulikuwa tunaita na kukusanya wanadamu wote wote, tulikusanya matendo yao mema yote ya sasa, yaliyopita na yajayo, tuliyakusanya yakawa ni tendo moja tu. Tuliwaita na kuwakusanya kwa minajili ya kutengeneza ile mimba juu ya wanadamu wote na juu ya matendo yao yote kusudi tuweze kutoa haki kwa wanadamu wote, siyo wapate haki ya maneno tu, bali wapate haki kwa vitendo juu ya kila kitu. Utashi Wetu unapotekeleza tendo fulani, lenye kuleta manufaa kwa wanadamu wote ulimwenguni, huwa haumbagui yeyote wala kumwacha mmoja pembeni. Na kwa kutumia uwezo wake mkuu huwa unaunganisha kila kitu pamoja, yaani wanadamu na matendo yao – isipokuwa dhambi, kwa vile uovu hauhesabiki kati ya matendo Yetu, - na ndipo huwa unatenda jambo unalolitaka kulitekeleza. Ona basi, hata matendo yako yalikuwa yamechangia, yaani nawe ulikuwa umetia pale mchango wako. Kwa hiyo, ni kwa haki kabisa wewe ni Binti Yake na kwa haki kabisa huyu Malkia Bikira ni Mama yako.

Lakini, je wajua ni kwa nini Sisi tulichagua mtindo huo wa kumleta duniani huyu Kiumbe Mtakatifu? Ni kwa lengo la kuupyaisha Uumbwa wote, kwa ajili ya kuupenda kwa Pendo jipya na kwa ajili ya kuwaweka wanadamu wote na kila kitu katika usalama hakika, kwa mtindo wa kuwakabidhi wote chini ya mabawa ya huyu Kiumbe Mama wa Mbinguni. Kazi Zetu huwa kamwe hatuzitekelezi moja moja peke yake, bali huwa daima tunaanzia na lile tendo letu moja pekee, ambalo kwa upekee wake, ndilo linalounganisha na kujumlisha ndanimo kila kitu, hata kufanya yote yawe ni tendo moja tu. Hayo ndiyo Maweza Yetu, ndiyo Nguvu Yetu ya Uumbaji: Yaani, kutenda yote katika na kwa tendo moja tu, kuyaona yote na kuyatenda vema kwa wote”.

Kila siku, hatua kwa hatua, jisomee hapa, ili upate kukua katika Paji la Uhai, ndani ya UTASHI WA MUNGU, kulingana na Mafundisho aliyoyatoa YESU kwake Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA

Swahili - Telegram Channel: Utashi Wa Mungu Na Upendo Wa Mungu

Swahili - Telegram Channel: Saa 24 Za Mateso Ya Bwana Weto Yesu Kristo

English - Telegram Channel: Divine Will Divine Love

English - Telegram Channel: The Virgin Mary in the Kingdom of the Divine Will

Français - Chaine de Telegram: Divine Volonte Divin Amour

Français - Chaîne de Telegram: Lettres de Luisa Piccarreta

Lingala - Chaine de Telegram: Mpo Elingi Nzambe Bolingi bwa Nzambe

Website all languages: www.divinewilldivinelove.com

Vitabu yote vilivyo katika faili za PDF vinaweza kupakuliwa bila gharama yoyote ile wakati wote ule. Pia, upo huru kabisa kuchapisha VITABU hivyo wewe mwenyewe binafsi au kuchapisha kwenye kiwanda chochote kile. Lakini vitabu hivyo ni kwa matumizi binafsi tu na siyo kwa ajili ya biashara! Hata hivyo una ruhusa ya kuwashirikisha na kuwapatia watu wengine vitabu hivyo kadiri unavyopenda!!

Swahili landing page: click here

English landing page: click here

Lingala landing page: click here

Kikongo landing page: click here

French landing page: click here

Italian landing page: click here

Report Page