Yesu kwa Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - KITABU cha MBINGU - Juzuu na. 14 - Novemba 6, 1922🖋📄📖📔

Yesu kwa Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA Binti Mdogo wa Utashi wa Mungu - KITABU cha MBINGU - Juzuu na. 14 - Novemba 6, 1922🖋📄📖📔


Wakati nikiwa bado katika hali yangu ile ya siku zote, Yesu Wangu Mpendevu wa siku zote alijitokeza. Mikononi Mwake alikuwa akivishika vyanakondoo vidogovidogo vingi sana - baadhi viliegama penye kifua chake, vingine mabegani pake, vingine vilikuwa vimeshikilia kwenye shingo Yake, vingine juu ya mkono wa kulia, vingine juu ya mkono wa kushoto, na vingine, kwa vichwa vyao vidogo, vilikuwa vikichungulia kutoka ndani ya moyo Wake. Hata hivyo, miguu ya vyanakondoo vyote hivyo, ilikuwa yote ndani ya Moyo wa Bwana Wetu. Na lishe aliyokuwa akiwapatia ilikuwa ni pumzi Yake: vikondoo vyote vilipinduka kuuelekea mdomo wa Yesu Wangu Mtamu, huku vikiwa vimefungua midomo yao wazi, ili kupokea pumzi Yake iliyokuwa ndiyo lishe yao. Ilikuwa ni nzuri na inapendeza kweli kuangalia jinsi Yesu alivyokuwa akifurahia kabisa, na alivyokuwa makini katika kuwalisha na katika kujiburudisha nao. Ni kweli walionekana kuwa kama machango mengi sana yaliyokuwa yametoka ndani ya Moyo Wake Mtukufu sana. Basi, alinigeukia kunitazama akiniambia:

“Binti Yangu, hivi vikondoo vidogo vidogo vingi unavyoviona mikononi Mwangu ndio watoto wa Utashi Wangu, wakiwa ni machango halali kabisa kutoka kwenye Utashi Wangu Mkuu wa Juu. Watajitokeza nje kutoka ndani ya Moyo Wangu, ingawa kama wataendelea kuiacha miguu yao pale katikati ya Moyo Wangu, ili kusudi wasichukue chochote kutoka duniani, na hawatashughulikia chochote kingine isipokuwa Mimi hapa basi. Ebu uwatazame na uone jinsi walivyokuwa wazuri na wanavyopendeza. Jinsi walivyo safi, wanavyolishwa vema, wanavyokua na hata kunenepeana vizuri, wote wakiwa wamelishwa kwa pumzi Yangu tu. Hawa watakuwa ndio utukufu na ndio taji la Uumbwa Wangu”.

Halafu aliongeza kusema:

“Utashi Wangu unamfanya mtu awe johari liangazalo. Kama vile kitu kikiwekwa mbele ya johari ling’aalo, ndani ya hilo johari hutengenezwa kitu kingingine sawa kabisa na kile kilichopo pale mbele ya johari, hali kadhalika, Utashi Wangu huwa unaingiza kila jambo ulitendalo kwa kuling’aza ndani ya watu hao, na kwa maweza ya Kwangu, unalifanya jambo hilo kuwa johari ndani ya mtu husika. Na watu huendelea kurudia kutenda hicho hicho kinachotekelezwa na Utashi Mkuu wa Juu. Na kwa vile Utashi Wangu upo kila mahali, kule Mbinguni, hapa duniani, na mahali popote, watu hao, kwa vile wanaubeba Utashi Wangu ndani yao kama uhai wao wenyewe, popote pale ambapo Utashi Wangu unatenda kazi, wao wanauingiza na kuunywa ndani yao, na wanaanza na wenyewe kurudia tendo la Kwangu. Kwa hiyo, ninapotenda jambo, Mimi huwa ninafurahia sana sana kujiweka mbele yao ili kuliona tendo Langu Mwenyewe likiwa linarudiwa ndani ya watu hao. Watu hao ni vioo Vyangu vya kujitazamia, na Utashi Wangu huwa unavirudufu vioo hivi kwa kila tendo unaolitenda na kwa kila mahali. Kwa hiyo, hakuna hata kitu kimoja kilichoumbwa ambamo hawa watu hawamo: katika wanadamu, katika bahari, katika jua, katika nyota mbalimbali, na hata katika Empireo. Na ndipo, kutoka kwa mwanadamu, Utashi Wangu, kwa mtindo wa kimungu, unapokea malipo kwa tendo Langu.

Na kwa hoja hiyo hiyo Mimi ninatamani kabisa kabisa kwamba mtindo wa kuishi ndani ya Utashi Wangu ufahamike: yaani, zoezi la kurudufu zaidi hivyo vioo vya kujitazama, ambavyo, kwa nguvu ya Utashi Wangu, vinafanywa kuwa kama johari liangazalo, ili kazi Zangu ziweze kuwa zinarudiwa ndani yao. Baada ya hapo basi, Mimi sitaweza kubaki tena peke Yangu, bali nitakuwa naambatana daima na mwanadamu. Atakuwa daima pamoja Nami, atakuwa katika upenzi kabisa Nami, atakuwa katika kina cha Utashi Wangu, atakuwa karibu hatenganiki Nami, atakuwa kama vile alivyojitokeza toka tumboni Mwangu siku ile nilipomwumba, alipokuwa bado hajafuata mitindo yoyote iliyo kinyume cha Utashi Wangu. Ni jinsi gani nitakavyofurahia!”.

Nilipoyasikia hayo, mimi nilimwambia: ‘Ewe Pendo Langu na Uhai Wangu, mimi siwezi bado nikaamini. Imekuweje kwamba mpaka hivi sasa, hakuna Mtakatifu hata mmoja ambaye amekuwa akitekeleza daima Utashi Wako Mtukufu, na ambaye ameweza kuishi kwa mtindo huu unaoelezea sasa - yaani, mtindo wa kuishi ndani ya Utashi Wako?’ Ndipo Yesu alijibu:

“Ah! Binti Yangu, wewe bado hutaki kusadiki mwenyewe kwamba, mtu anaweza akapokea mwanga mwingi, neema nyingi, tofauti mbalimbali, thamani, kulingana na kiwango cha uelewa anaoupata? Ni kweli kabisa, kulikuwa na Watakatifu waliokuwa wakitimiza daima Utashi Wangu, lakini walikuwa wakiuchukua Utashi Wangu kwa kiwango kile tu walichokuwa wanakijua. Walifahamu kwamba kutekeleza Utashi Wangu ni tendo kuu kabisa, na ndilo tendo lililokuwa linanipatia heshima Mimi kwa ngazi ya juu kabisa, na ni tendo lililokuwa linaleta utakatifu. Kulingana na nia hiyo, walilitekeleza hilo tendo kuu. Na walichokipata ni hicho, utakatifu, kwa vile hakuna utakatifu bila ya Utashi Wangu. Na hakuna jema, wala utakatifu, kwa kiwango kiwe kidogo au kiwe kikubwa, unaoweza ukajitokeza bila Utashi Wangu.

Ni budi ukajua kile kilichokuwa ni Utashi Wangu, kilicho ni Utashi Wangu na kitakachokuja kuwa ni Utashi Wangu: Hakijabadilika katika lolote lile. Lakini, kwa vile Utashi Wangu upo katika kujionyesha wenyewe, basi unaanza kuonyesha utajiri wa rangi zake, wa matokeo yake, na utajiri wa thamani zile unazozibeba. Na wala si kwamba unajionyesha tu, bali unatoa kwa mtu na kumpatia ule utajiri wa rangi zake, matokeo yake, na thamani zake. Vinginevyo ingekuwa na maana gani ya kuzionyesha? Utashi Wangu ulikuwa ukitenda mithili ya bwana mkubwa mmoja ambaye alikuwa katika kuonyesha makao yake makuu kweli, na ya kianasa mno. Kwa watu wa kundi la kwanza, aliwaonyesha barabara ya kufika kwenye makao yake. Kwa watu wa kundi la pili aliwaonyesha mpaka geti la kuingilia. Kwa wale wa kundi la tatu aliwaonyesha ngazi zinazoelekea darini. Kwa wale wa kundi la nne aliwaonyesha vyumba vya mwanzoni. Na kwa kundi la mwisho aliwafungulia kuona vyumba vyote, akawamilikisha vyumba vile na mali zote zilizomo katika vyumba hivyo. Basi, lile kundi la kwanza wamechukua mali zilizokuwa katika barabara. Wale wa kundi la pili wamechukua mali zilizopo pale getini, lakini ni mali bora zaidi kuliko zile za barabarani. Kundi la tatu limechukua mali zile zilizo kwenye ngazi. Kundi la nne wamechukua mali za vyumba vya mwanzoni ambamo kulikuwa na mali nyingi zaidi na pia zilizokuwa zimehifadhiwa kwa usalama zaidi. Lile kundi la mwisho wameambulia mali za makao makuu yote.

Ndivyo hivyo ulivyotenda Utashi Wangu. Ilibidi uonyeshe njia, uonyeshe geti, uonyeshe ngazi, na uonyeshe hata vile vyumba vya mwanzoni, ili kusudi uweze kusonga mbele hadi ukaifikie ile bahari yake nzima. Baada ya kufika hapo uliweza kuwaonyesha watu yale mema makubwa yaliyopo ndani yake. Ndipo uliweza kueleza pia jinsi mwanadamu, atendaye katika mema hayo ya Utashi Wangu, anavyoweza kujipatia utajiri wa rangi zake, anavyoweza kujipatia ile bahari yake ya mali, anavyoweza kujipatia utakatifu na maweza, na hata anavyoweza kupata mambo ya utendaji Wangu wote. Pale ninapojulisha au kufahamisha jambo kwa mtu, Mimi ninatoa kwa mtu huyo na ninagonga ndani yake mhuri wa ile sifa ya kimungu ambayo ninaielezea. Laiti ungejua ni ndani ya mawimbi makuu gani ya neema mbalimbali wewe upo, wakati ninapoendelea kukufahamisha juu ya matokeo mengine ya Utashi Wangu, na ninapoendelea kukuelezea, jinsi, mithili ya mchoraji stadi, ninavyochora ndani ya roho yako, kwa kutumia rangi hai na zinazong’aa kabisa, ninachora yale matokeo, zile thamani mbalimbali ambazo ninakuelezea - kama ungejua ungebaki umepondeka pale chini ya mawimbi Yangu! Hata hivyo, kwa kukuonea huruma kwa udhaifu wako, Mimi ninakutegemeza wewe. Na ninapoendelea kukutegemeza, nitazidi kutia ndani yako na kukugongea mhuri wa mambo mengi zaidi ya yale ninayokuelezea, kwani, Mimi ninapozungumza ndivyo huwa ninatenda. Kwa hiyo, uwe makini na mwaminifu”.

Juzuu na. 14 ku download - click here

Kila siku, hatua kwa hatua, jisomee hapa, ili upate kukua katika Paji la Uhai, ndani ya UTASHI WA MUNGU, kulingana na Mafundisho aliyoyatoa YESU kwake Mtumishi wa Mungu LUISA PICCARRETA

Swahili - Telegram Channel: Utashi Wa Mungu Na Upendo Wa Mungu

Swahili - Telegram Channel: Saa 24 Za Mateso Ya Bwana Weto Yesu Kristo

English - Telegram Channel: Divine Will Divine Love

English - Telegram Channel: The Virgin Mary in the Kingdom of the Divine Will

Français - Chaine de Telegram: Divine Volonte Divin Amour

Français - Chaîne de Telegram: Lettres de Luisa Piccarreta

Lingala - Chaine de Telegram: Mpo Elingi Nzambe Bolingi bwa Nzambe

Website all languages: www.divinewilldivinelove.com

Vitabu yote vilivyo katika faili za PDF vinaweza kupakuliwa bila gharama yoyote ile wakati wote ule. Pia, upo huru kabisa kuchapisha VITABU hivyo wewe mwenyewe binafsi au kuchapisha kwenye kiwanda chochote kile. Lakini vitabu hivyo ni kwa matumizi binafsi tu na siyo kwa ajili ya biashara! Hata hivyo una ruhusa ya kuwashirikisha na kuwapatia watu wengine vitabu hivyo kadiri unavyopenda!!

Swahili landing page: click here

English landing page: click here

Lingala landing page: click here

Kikongo landing page: click here

French landing page: click here

Italian landing page: click here

Report Page