@Furqanbot

@Furqanbot


 

[1] Faida: Atw-Twabaraaniy amenukuu kwamba Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما)amehadithia kuwa: “Suwrah nzima ya Al-An’aam imeteremshwa Makkah, usiku, ikifuatiliwa na Malaika elfu sabini wakinyanyua sauti zao kumsabihi Allaah.”

[2] Faida:

Wamekhitilafiana Wafasiri katika kauli nne kuhusu kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):

وَهُوَ اللَّـهُ فِي السَّمَاوَاتِ وَفِي الْأَرْضِ

Na Yeye ni Allaah mbinguni na ardhini.

Kauli ya kwanza:

Maana yake ni: Yeye Allaah (سبحانه وتعالى) ni Ilaah Anayeabudiwa mbinguni na katika ardhi kwa sababu Yeye Pekee Ndiye Mwabudiwa wa haki katika ardhi na mbingu, kwa ushahidi wa kauli Yake(تعالى):

وَهُوَ الَّذِي فِي السَّمَاءِ إِلَـٰهٌ وَفِي الْأَرْضِ إِلَـٰهٌ ۚ  

Na Yeye Ndiye Mwabudiwa wa haki mbinguni na ardhini pia (Ndiye Huyo Huyo) Ilaah. [Az-Zukhruf 42: 84)]

 

[Al-Qurtwubiy, Ibn Kathiyr, Ash-Shanqiytwiy, Ibn Al-Anbaariy na wengineo. Taz. Al-Jaami’u li-Ahkaamil-Qur-aan (6/390), Tafsiyr Al-Qur-aan Al-‘Adhwiym (3/240), Adhwaau Al-Bayaan(7/4)].

 

Kauli Ya Pili: 

 

Kwamba maana ni: Yeye Allaah Anajua siri zenu mbinguni na katika ardhi na ushahidi ni kauli Yake (تعالى)

قُلْ أَنزَلَهُ الَّذِي يَعْلَمُ السِّرَّ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ  

Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Ameiteremsha Ambaye Anajua siri katika mbingu na ardhi. [Al-Furqaan (25: 6)].

 

Kwa kuzingatia kwamba kauli Yake: 

 

“mbinguni na ardhini” [Al-An’aam (6: 3)] inahusiana na: “Anajua siri zenu.”

 

Na amesema Imaam Ad-Daaniyy: Na imesemwa kuwa maana ni:

 

Yeye Ndiye Mwabudiwa mbinguni na katika ardhi.

 

Na kadhaalika, Al-Ashmuwniyy kaunga mkono ufafanuzi huo.

 

Na amesema An-Nahhaas kuwa kauli hiyo ni bora katika yaliyoelezwa juu ya Aayah hiyo.

 

[Al-Muktafaa Fiy Al-Waqf Wal-Ibtidaa Fiy KitaabiLLaah ‘Azza Wa Jalla (273), Manaaru Al-Hudaa Fiy Bayaan Al-Waqf Wal-Ibtidaa (265). Adhwaau Al-Bayaan Fiy Iydhwaah Al-Qur-aan bil-Qur-aan (4/7)].

 

Kauli Ya Tatu:

Kwamba maana yake ni:

Yeye Allaah Ambaye Yeye Yuko mbinguni na katika ardhi Anajua siri zenu na ya dhahiri yenu katika ardhi. Naye Yuko juu ya ‘Arsh Yake Akiwa juu ya viumbe Vyake wote, Akiwa Anajua siri za watu wa ardhini na ya dhahiri yao, hakuna kinachofichika Kwake katika hayo. Na ushahidi ni kauli Yake (تعالى):

أَأَمِنتُم مَّن فِي السَّمَاءِ أَن يَخْسِفَ بِكُمُ الْأَرْضَ فَإِذَا هِيَ تَمُورُ﴿١٦﴾

Je, mnadhani mko katika amani na (Allaah) Aliyeko mbinguni kwamba Hatokudidimizeni ardhini, tahamaki hiyo inatikisika?

 

أَمْ أَمِنتُم مَّن فِي السَّمَاءِ أَن يُرْسِلَ عَلَيْكُمْ حَاصِبًا ۖ فَسَتَعْلَمُونَ كَيْفَ نَذِيرِ﴿١٧﴾

Au mnadhani mko katika amani na (Allaah) Aliyeko mbinguni kwamba Hatokutumieni tufani ya mawe basi mtajua vipi maonyo Yangu. [Al-Mulk (67: 16-17)]

 

Na kauli Yake (تعالى):

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ ﴿٥﴾

Ar-Rahmaan juu ya ‘Arsh Istawaa.[Twaahaa (20: 5)].

 

 

Kauli Ya Nne: 

 

Ina maana kutangulizwa na kuakhirishwa; yaani: Yeye Allaah Anajua siri zenu na ya dhahiri yenu mbinguni na ardhini. Na hii kauli ya Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) .

 

Kauli iliyo na nguvu kabisa katika kauli hizo nne ni:

Kauli ya kwanza ambayo ni kauli ya wengi katika Mufassariyn, pamoja na kwamba kuna uwezekano wa kauli nyingine katika hizo kwa sababu kila kauli ina ushahidi wake katika Qur-aan.

Shaykh Al-Islaam Ibn Taymiyyah (رحمه الله): “Maimaam wakubwa kama Imaam Ahmad na wengineo wameifasiri kwamba: “Kuwa Yeye ni Mwabudiwa mbinguni na ardhini.” [Al-Furqaan Bayna Awliyaair-Rahmaan Wa-Awliyaai Ash-Shaytwaan (244)]

Ibn Kathiyr (رحمه الله) amesema: “Kauli iliyo sahihi kabisa ni kwamba: “Anaombwa Allaah mbinguni na ardhini; yaani Anaabudiwa na Anapwekeshwa na Anakiriwa kwa Uabudiwa Aliyekuwa mbinguni na katika ardhi na Anaitwa Allaah, na Anaombwa kwa utashi na khofu, isipokuwa aliyekanusha katika majini na bin Aadam.” [Tafsiyr Al-Qur-aan Al-‘Adhwiym, (3/240)]

 

 

[3]Sababun-Nuzuwl: Sa’ad (رضي الله عنه)amehadithia kwamba: Tulikuwa watu sita pamoja na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم), na Ibn Mas’uwd alikuwa mmoja wao. Washirikina wakamwambia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): “Usiwaweke watu hawa karibu yako.” (Katika riwaayah nyingine ya Muslim): “Wafukuze.” Hapo ikateremka Aayah hii: “Na wala usiwafukuze wale wanaomwomba Rabb wao asubuhi na jioni wanataka Wajihi Wake…” (6: 52).

[4] Faida: Mahali pa kustakiri ni tumboni mwa mama au duniani. Mahali pa kuhifadhiwa ni ima migongoni mwa baba au kaburini.

[5] Faida: Masruwq (رضي الله عنه) amehadithia kwamba: Nilimwambia ‘Aaishah (رضي الله عنها) : Ee Mama! Je Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) alimuona Rabb wake? Akasema: Hayo uliyoyasema yamefanya nywele zangu zisimame kunisisimka mwili! Tambua kwamba mtu akikutajia mambo matatu yafuatayo basi yeye ni muongo! Atakayesema kwamba Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) amemuona Rabb wake; Kisha akasoma:“Macho hayamzunguki bali Yeye Anayazunguka macho yote; Naye ni Mjuzi wa yaliyofichika, Mjuzi wa yaliyodhahiri na yaliyofichikana.” (6: 103) “Na wala haikuwa kwa mtu yeyote kwamba Allaah Amsemeze isipokuwa kwa (njia ya) Wahy au kutoka nyuma ya kizuizi” (42: 51). Kisha akaendelea kusema: Na atakayesema kwamba Nabiy anajua yatakayotokea kesho basi ni muongo. Kisha Akasoma: “Na nafsi yoyote haijui nini itachuma kesho” (31: 34). Kisha akasema: Na Atakayesema kuwa Nabiy ameficha aliyofunuliwa Wahyi (na maamrisho) basi ni muongo! Kisha akasoma: “Ee Rasuli! Balighisha yale yaliyoteremshwa kwako kutoka kwa Rabb wako. Na usipofanya, basi utakuwa hukubalighisha ujumbe Wake…” (5: 67). Kisha akasema: Lakini Nabiy alimuona Jibriyl katika umbile lake khalisi mara mbili.[Al-Bukhaariy].

Kwa upande mwengine Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) alisema kuwa Rasuli (صلى الله عليه وآله وسلم)alimuona Allaah, na akasema kuwa Rasuli(صلى الله عليه وآله وسلم) alimuona Rabb wake mara mbili. [Tafsiyr Ibn Kathiyr].

 

Al-Haafidhw, Ibn Hajar alisema, “Maelezo ya Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) yamekuja katika hali ya kutodhibitiwa (hayaelezi kama Rasuli (صلى الله عليه وآله وسلم) alimuona Rabb wake kwa macho yake au vipi) wakati kauli za mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها) na wenziwe zimedhibitiwa kwa kusema Rasuli (صلى الله عليه وآله وسلم) hakumuona Allaah “Kwa macho yake”. Tunaweza kuunganisha kauli hizo mbili kwa kusema mama wa Waumini ‘Aaishah(رضي الله عنها) alikataa muono “Kwa macho yake” na kauli ya Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) kuwa ni kamuona kiroho.” [Fat-hul-Baariy, 8/608].

 

Pili, kauli hizo mbili, ya mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها) na ya Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما), kwa njia nyingine kuwa kauli ya Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) alisema kuwa Rasuli (صلى الله عليه وآله وسلم) alimuona Rabb wake wakati akiwa katika usingizi, jambo ambalo ni ndoto ya kweli na isiyokuwa alimuona Siku ya Mi’iraaj wakati kauli ya mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها) inakataa kuwa Rasuli hakumuona Rabb wake wakati yeye akiwa macho, lakini kauli hiyo haikatazi kuwa Rasuli (صلى الله عليه وآله وسلم) alimuona Rabb wake akiwa usingizini. Alichokana hapa ni kuwa Rasuli (صلى الله عليه وآله وسلم) hakumuona Allaah kwa macho yake meupe, akiwa macho.

 

Wale ambao wanao msimamo kuwa Rasuli(صلى الله عليه وآله وسلم) alimuona Rabb wake kwa macho yake meupe wanaleta Hadiyth dhaifu. Hakuna Hadiyth Sahihi ambayo inaeleza ya kuwa Rasuli (صلى الله عليه وآله وسلم) alimuona Rabb wake kwa macho yake akiwa macho. Wenye msimamo huo wanaleta Hadiyth ya At-Tirmidhiy ambayo Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) anasema kuwa Rasuli (صلى الله عليه وآله وسلم)alimuona Rabb wake. Ikrimah alimuuliza: “Vipi Aayah ambayo inasema, “Macho hayamfikilii bali Yeye anayafikilia macho.” Alijibu, kuwa ni wakati tu Allaah amezungukwa na Nuru, lakini Rasuli (صلى الله عليه وآله وسلم) alimuona Rabb wake mara mbili. “Hadiyth hii ni dhaifu.”

 

Kwa hali hiyo kwa namna jinsi ilivyo hakuna mgongano wa kauli, na Allaah Anajua zaidi. [Sharh ya Uswuul Al-I’itiqaad cha Al-Laalika’iy, 93/512, As-Sunnah 1/181 na Swifaat Al-Maqdisiy ukurasa 109-111].

 

Hapa kunathibitishwa kuwa Rasuli (صلى الله عليه وآله وسلم) hakumuona Rabb wake wakati wa alipopelekwa katika safari ya Mi’raaj, na hii ndio ‘Aqiydah ya Ahlus-Sunnah wal-Jumaa’ah kuwa Allaah Haonekani duniani, kinyume na ‘Aqiydah ya Masufi wanaoamini kuwa Allaah Anaonekana duniani kwa kuegemeza tukio hilo la Mi’raaj. Kadhaalika, Aayah hiyo vilevile haikanushi kuonekana Allaah Qiyaamah, bali Qiyaamah Allaah Ataonekana katika kisimamo cha Qiyaamah na kwenye Pepo kwa dalili nyingi kutoka katika Qur-aan na Sunnah, kinyume na ‘Aqiydah ya makundi potofu yanayoamini kuwa Allaah Hatoonekana Aakhirah.

 

[6] Sababun-Nuzuwl: Amehadithia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) Kuhusu kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى): “Na hakika mashaytwaan wanadokeza marafiki wao wandani”Walikuwa washirikina wakisema: Kilichochinjwa kwa ajili ya Allaah msile! Lakini mnachochinja nyinyi basi kuleni! Hapo Allaah Akateremsha: “Na wala msile katika ambavyo halikutajwa Jina la Allaah.”[Ameipokea Abuu Daawuwd].

 

[7] Faida: Rejea tanbihi: (1: 6).

 

[8] Faida: Aayah (6: 161- 162) ni mojawapo ya du’aa ya kufungulia Swalaah: Pia Aayah hii ni dalili mojawapo ya haramisho la kuchinja kwa kukusudia asiyekuwa Allaah (سبحانه وتعالى).




Report Page