@Furqanbot

@Furqanbot





[1] Faida: ‘Umar bin Al-Khattwaab (رضي الله عنه)amehadithia kwamba Myahudi mmoja alimwambia: Ewe Amiri wa Waumini, lau ingeliteremka kwetu sisi Aayah hii “Leo Nimekukamilishieni Dini yenu, na Nimekutimizieni neema Yangu, na Nimekuridhieni Uislamu uwe Dini yenu.” (5: 3)tungeliifanya ‘Iyd siku hiyo. ‘Umar akasema: Wa-Allaahi, naijua siku gani imeteremka Aayah hii. Imeteremka Siku ya ‘Arafah siku ya Ijumaa. [Al-Bukhaariy].

[2] Sababun-Nuzuwl: Aayah hii imeteremshwa kama ilivyoelezewa katika tanbihi ya Aayah (4: 43) kuhusiana na hukmu ya tayammum.

[3] An-Naasikh Wal-Mansuwkh:  Kufutwa hukmu ya kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى): “Basi wasamehe na achilia mbali. Hakika Allaah Anapenda wafanyao ihsaan.” Amri ya kuwasamehe baada ya kuvunja kwao ahadi na fungamano na kufanya khiyana, imefutwa na Aayaat za As-Sayf (upanga); “Piganeni na wale wasiomwamini Allaah na wala Siku ya Mwisho, na wala hawaharamishi Aliyoyaharamisha Allaah na Rasuli Wake, na wala hawafuati Dini ya haki…” (9: 29) kwa kuwa baada ya hapo waliamrishwa kupigana jihaad na Makafiri.

 

[4] Sababun-Nuzuwl: Aayah hii imeteremshwa baada ya Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alipotuma watu waliokuwa mahodari wa kufuatilia na kukamata wakaletwa kwake. Hapo Allaah (تبارك وتعالى)Akateremsha: “Hakika jazaa ya wale wanaompiga vita Allaah na Rasuli Wake na wanafanya bidii kufanya ufisadi katika ardhi…” (5: 33) [Amehadithia Anas bin Maalik(رضي الله عنه) ameipokea Abuu Daawuwd katika Kitaab Al-Huduwd].

 

Faida: Maana ya kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):“au ikatwe mikono yao na miguu yao kwa kutofautisha”; ni kukatwa mikono ya kulia kwa miguu ya kushoto au miguu ya kushoto kwa mikono ya kulia.

[5] Sababun-Nuzuwl: Aayah hii imeteremka kama alivyohadithia Baraa bin ‘Aazib (رضي الله عنه) kwamba: Myahudi mmoja aliyejaa weusi usoni na aliyepigwa mijeledi alipita kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم). Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akamwita akaumuuliza: “Je, hivyo ndivyo mlivyokuta (shari’yah) katika Kitabu chenu kuhusu hadd ya mzinifu?” Wakasema: Ndio. Akamwita mtu mmoja miongoni mwa wanachuoni wao akasema: “Nakuuliza kwa kuapia Jina la Allaah Ambaye Ameteremsha Tawraat kwa Muwsaa; je, hivyo ndivyo mnavyokuta hadd ya mzinifu katika Kitabu chenu?” Akasema: Hapana! Usingeniuliza hilo kwa kuapia Jina la Allaah, nisingelikuelezea. (Ni kweli) Tunaikuta Ar-Rajm (adhabu ya kupigwa mawe mpaka kufa) kama ilivyo shari’yah katika Tawraat lakini jarima imezoeleka kwa watu wetu wenye hadhi tu. Hivyo, tunapomkamata tajiri (aliyezini) tunamuachia (huru), lakini tukimkamata aliye duni tunamsimamishia adhabu ya hadd. Kisha tukasema: Njooni tukubaliane (adhabu) tutakayoisimamisha kwa wote; matajiri na walio duni. Hivyo tukaamua kumpaka (mzinifu) masinzi usoni na kumpiga mijeledi badala ya rajm. Hapo Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Ee Allaah, hakika mimi wa kwanza kuihuisha amri Yako wakati wao (Mayahudi) wameifisha. Basi akaamrisha, na (mkhalifu huyo) akasimamishiwa rajm. Hapo Allaah (سبحانه وتعالى) Akateremsha: “Ee Rasuli, wasikuhuzunishe wale wanaokimbilia kukufuru… (mpaka kauli ya): “Mkipewa haya basi yachukueni.” (5: 41) Ikasemwa na Mayahudi: Nendeni kwa Muhammad, akikuamrisheni kukupakeni masinzi na kupigwa mijeledi basi pokeeni, lakini akikupeni hukumu ya rajm, basi tahadharini (jiepusheni). Hapo Allaah (سبحانه وتعالى) Akateremsha: “Na yeyote asiyehukumu kwa yale Aliyoyateremsha Allaah, basi hao ndio makafiri” (5: 44). “Na yeyote asiyehukumu kwa yale Aliyoyateremsha Allaah, basi hao ndio madhalimu.” (5: 45). “Na yeyote asiyehukumu kwa yale Aliyoyateremsha Allaah, basi hao ndio mafasiki.” (5: 47) Aayah zote hizo (5: 41 – 47) zimeteremshwa kuwahusu makafiri.

 

[6] Sababun-NuzuwlAmehadithia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) kwamba: Walikuweko Quraydhwah na An-Nadhwiyr (makabila ya Mayahudi Madiynah). An-Nadhwiyr walikuwa wenye hadhi zaidi kuliko Quraydhwah. Ikawa pale mtu wa Quraydhwah anapoua mtu wa An-Nadhwiyr, huuliwa, lakini inapokuwa mtu wa An-Nadhwiyr ameua mtu wa Quraydhwah huitwa akapigwa mikaanga mia ya mitende kama diya. Kisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alipotumwa kuwa ni Rasuli, mtu mmoja wa An-Nadhwiyr alimuua mtu wa Quraydhwah wakasema: Mleteni kwetu tumuue! Wakajibu: Sasa baina yetu na yenu yupo Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) basi mleteni (atuhukumu)! Hapo ikateremka: “Na kama ukihukumu, basi hukumu baina yao kwa uadilifu” (5: 42) Na uadilifu ni (kisasi cha) nafsi kwa nafsi. Kisha ikateremka: “Je, wanataka hukumu ya kijaahiliyyah?” (5: 50) [Abuu Daawuwd, An-Nasaaiy, Ibn Hibbaan na wengineo] Ibn Kathiyr amesema: Inaweza kuwa zimejumuika sababu mbili hizi (5: 41-42) kwa wakati mmoja zikateremka Aayaat hizo kuhusu hayo na Allaah Mjuzi zaidi.

 

 

[7] Sababun-Nuzuwl: Kuhusu kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى): “Na Allaah Atakuhifadhi dhidi ya watu.” Imeteremka pale Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) aliposhuka chini ya kivuli cha mti na akalitundika panga lake juu ya huo mti kisha akasinzia. Bedui mmoja akamjia akiwa katika hali ya usingizi, akalikamata panga la Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kisha akamuamsha, akamwambia huku amelishika panga lake juu: Nani ana uwezo wa kunizuia nisikuue? Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akamjibu yule bedui: “Allaah Ndiye mwenye uwezo wa kukuzuia.” Hapo ikateremka kauli hii ya Allaah (سبحانه وتعالى): “Na Allaah Atakuhifadhi dhidi ya watu.” (5: 67) [Amehadithia Abuu Hurayrah(رضي الله عنه) - Ameipokea Ibn Hibbaan].

Faida: Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ametimiza Risala: Hakika Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) aliifikisha na kuitangaza Dini ya Allaah (سبحانه وتعالى) na akaieneza da’wah yake mpaka ikawafikia majini na watu. Na akawafundisha yote aliyoyaweka Allaah (سبحانه وتعالى) kuwa ni shariy’ah. Akausimamia uwajibu huu kwa nguvu zote, na Allaah (سبحانه وتعالى) Hakumfisha mpaka Alipoinyoosha kupitia yeye dini iliyopindishwa na Akayafungua kupitia yeye macho yenye upofu na kuzifungua nyoyo zilizokuwa zimefunikwa na ujinga.

 

[8] Sababun-Nuzuwl: Aayah hii na zinazofuatia (5: 82-85) zimeteremshwa kuhusuAn-Najaashiy ambaye alikuwa mfalme wa Habash pamoja na watu wake. Aliwakilisha wajumbe wamwendee Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ili wamsikilize maneno yake na watambue sifa zake. Walipokutana na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) na akawasomea Qur-aan, waliingia Uislamu wakalia na kunyenyekea. Kisha wakarudi kwa An-Najaashiy kumjulisha yaliyojiri. [Athar kutoka kwa Saiy’d bin Jubayr, As-Suddi na wengineo – Tafsiyr Ibn Kathiyr].

 

Sababun-Nuzuwl: Pia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) amehadithia kwamba: Waislamu walipohajiri kutoka Makkah kwenda Habash wakiwa katika uongozi wa Ja’far bin Abiy Twaalib na Ibn Mas’uwd (رضي الله عنهم), walimkuta mfalme wao An-Najaashiy akiwa mkarimu na mwenye huruma kwao. Akawauliza kama wana chochote cha Wahyi kutoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى). Walipomsomea Aayaat za Qur-aan wakati alikuwa pamoja na makasisi na wamonaki wake, wakamiminikwa na machozi kutokana na kutambua haki. Ndipo Allaah (سبحانه وتعالى) Akateremsha: “Hivyo ni kwa kuwa miongoni mwao kuna Makasisi na Wamonaki na kwamba wao hawatakabari. Na wanaposikia yale yaliyoteremshwa kwa Rasuli utaona macho yao yanachuruzika machozi kutokana na yale waliyoyatambua ya haki…” (5: 82-84). Na katika riwaayah nyengine: “Ja’far (رضي الله عنه) aliwasomea Suwrat Maryam wakamiminkwa machozi…”

[9] Sababun-Nuzuwl: Kuhusu kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى): “Basi kafara yake ni kulisha maskini kumi chakula cha wastani mnachowalisha ahli zenu.” (5: 89) Imeteremka kutokana na mtu alikuwa akilisha familia yake chakula kingi cha kutosheleza, lakini akilisha wengine chakula hafifu kisichotoleza. Hapo ikateremshwa: “cha wastani mnachowalisha ahli zenu.” [Amehadithia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) ameipokea Ibn Maajah].

 

[10] Sababun-Nuzuwl: Aayah hii imeteremshwa kuwa ni haramisho la mwisho kunywa pombe. Rejea tanbihi za (2: 219), (4: 43) ambako kuna maelezo bayana ya Sababun-Nuzuwl ya Aayah hii na ifuatayo (5: 90-91). Baada ya kuteremshwa Aayah hizi, hapo hapo Swahaba wakaacha moja kwa moja kulewa ikawa ndio kikomo cha kunywa pombe.

 

Sababun-NuzuwlPia,

Imeteremshwa kuhusu makabila mawili katika Answaar walipokunywa pombe mpaka wakalewa mno kisha wakagombana na kuchafuana baadhi yao kwa baadhi mpaka athari zikawa zinaonekana katika nyuso zao. Kisha pale ulevi ulipowaondokea na akili zao zikawarejea, viliingia vinyongo katika nyoyo zao, hapo zikateremka Aayah hizi zinazoharamisha pombe moja kwa moja:“Enyi walioamini! Hakika pombe na kamari na masanamu na kutazamia kwa mishale ya kupigia ramli; ni najisi na chukizo kutokana na kitendo cha shaytwaan; basi jiepusheni navyo, mpate kufaulu. Hakika shaytwaan anataka kukutilieni baina yenu uadui na bughudha katika pombe na kamari na akuzuieni kumdhukuru Allaah na Swalaah; basi je mtakoma?” (5: 90 - 91). [Amehadithia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) – amepokea Ibn Jariyr].

 

[11] Sababun-Nuzuwl: Aayah hii imeteremshwa baada ya kuteremshwa Aayah za uharamisho wa pombe moja kwa moja (5: 90 -91). Kisha baadhi ya Swahaba wakasema kuwa watu wengi wamefariki wakiwa wana pombe matumboni mwao, wakataka hukmu yake, hapo ikateremka Aayah hii: “Hakuna lawama juu ya wale walioamini na wakatenda mema katika vile walivyokula (kabla ya kuharimishwa) ikiwa watakuwa na taqwa na wakaamini na wakatenda mema;…” (5: 93).[Amehadithia Anas (رضي الله عنه), wameipokea; Al-Bukhaariy na Muslim].

 

 

[12] Sababun-Nuzuwl: Aayah hii imeteremshwa kwa sababu ya wingi wa maswali waliyokuwa wakiuliza watu katika hali na wakati mbali mbali; ima kwa istihzaa au mitihani iliyowasibu au kwa talbiys (kufunika haki na kuipotosha). Mfano pale ilipoteremka Aayah ya kuwajibika Hajj: “Na kwa ajili ya Allaah ni wajibu kwa watu watekeleze Hajj katika Nyumba…” (3: 97) akashikilia mtu kuuliza kuhusu kuwajibika Hajj kama inawajibikia kila mwaka, jambo ambalo Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) angejibu kuwa “Naam”, basi ingewajibikia kisha hapo ingekuwa ni amri na jambo gumu mno kulitekeleza. [Al-Bukhaariy, Muslim na wengineo].

 

Sababun-Nuzuwl: Pia, kama alivyohadithiaAnas bin Maalik (رضي الله عنه) kwamba: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alitoa khutbah ambayo sijapatapo kuisikia kama hiyo kisha akasema: “Mngelikuwa mnayajua yale ninayoyajua, basi mngelicheka kidogo na mngelilia sana.” Waliposikia hivyo Swahaba wa Rasuli wa Allaah walijifunika nyuso zao wakalia mpaka sauti za vilio vyao vikasikika. Kisha mtu mmoja hapo akamuuliza: Nani baba yangu? Akamjibu: “Fulani.” Hapo ikateremka Aayah hii: “Enyi walioamini!Msiulizie mambo ambayo mkifichuliwa yatakuchukizeni…” (5: 101) [Al-Bukhaariy].  

 

Sababun-Nuzuwl: Pia Anas (رضي الله عنه)amehadithia kwamba: Siku moja walianza kumuuliza Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) maswali mengi mpaka akaghadhibika akapanda minbar akasema: “Hamtaniuliza lolote leo ila nitawajibu tu.” Nikatazama kuliani na kushotoni nikaona kila mtu amejifunika uso wake kwa nguo akilia. Hapo alikuweko mtu mmoja ambaye kila alipogombana na wenziwe aliitwa ‘mwana wa fulani asiyekuwa ni baba yake’. Akamuuliza: Ee Rasuli wa Allaah, nani baba yangu? Akasema: “Hudhaafah.” Hapo ‘Umar akainuka akasema: Tumeridhika na Allaah kuwa ni Rabb, na Uislamu kuwa Dini, na Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) kuwa ni Rasuli. Tunajikinga kwa Allaah na fitnah! Hapo Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Sijapatapo kuona khayr au shari kama siku ya leo, kwani imedhihirishwa mbele yangu Jannah na moto hadi kwamba nimeviona viwili hivi nyuma ya ukuta.” Qataadah alipokuwa akihadithia Hadiyth hii alikuwa akitaja Aayah hii: “Enyi walioamini! Msiulizie mambo ambayo mkifichuliwa yatakuchukizeni…” (5: 101) [Al-Bukhaariy].

 

 

 

[13] An-Naasikh Wal-Mansuwkh: Kufutwa hukmu kuhusu kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):“au wawili wengineo wasiokuwa nyinyi.”Imefutwa baada ya kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى): “Na mshuhudishe mashahidi wawili wenye uadilifu miongoni mwenu, na simamisheni ushahidi kwa ajili ya Allaah.”[Atw-Twalaaq (65: 2)].

[14] Sababun-Nuzuwl: Aayah hii imeteremshwa pamoja na Aayah mbili kabla yake (5: 106-107) pale bwana mmoja katika Baniy Sahm alitoka pamoja na Tamiym Ad-Daariy na ‘Adiyy kisha katika msafara wao akafariki huyu mtu ambaye ni katika Baniy Sahm, na walikuwa katika kijiji ambacho hakuna Muislamu. Pale waliporejea akina Tamiym na vitu vyake alivyoviacha baada ya kufariki, walikikosa chombo kimoja cha fedha ambacho kimezibiwa kwa dhahabu. Kisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akawaapisha. Kisha baada ya hapo walikuja kukipata kile chombo Makkah. Wakasema wale waliokipata huko Makkah kwamba: Tulikinunua kwa ‘Adiy na Tamiym. Wakasimama watu wawili katika ndugu wa yule As-Sahm wakaapa na wakasema kumuambia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kuwa ushahidi wetu ni bora kuliko ushahidi wao, na kwamba hao ni waongo wanamsingizia Tamiym na ‘Adiy na kuwa hicho chombo si cha huyo ndugu yao bali ni cha jamaa yao wenyewe, hapo zikateremka Aayaat hizi: “Enyi walioamini! Mauti yanapomfikia mmoja wenu wakati anapousia, basi chukueni ushahidi wa wawili wenye uadilifu miongoni mwenu… (5 : 106) mpaka mwisho wa Aayah (5 : 108). [Amehadithia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما), ameipokea Al-Bukhaariy].

 


Report Page