@Furqanbot
[1] Sababun-Nuzuwl: Aayah hii imeteremka kama alivyohadithia Mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها): “Kuna bwana mmoja alimuoa binti ambaye ni yatima aliyekuwa akimlea na msimamizi wake kwa sababu hakuwa na mtu wa kumsimamia. Huyo bwana hakumuoa kwa sababu ya kumpenda kwani alikuwa haamiliani naye vizuri. Akamuoa kwa ajili yatima huyo alikuwa ana (mali) shamba la mitende. Hapo ikateremka Aayah hii.” [Al-Bukhaariy na Muslim].
[2] Sababun-Nuzuwl: Aayah hii imeteremka ikiwa inabainisha hukmu kuhusu mali ya yatima. Mlezi wa yatima huyo anapokuwa ni fakiri, basi anaweza kula katika mali hiyo kwa wema bila ya israaf. [Amehadithia Mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها) ameipokea Al-Bukhaariy na Muslim].
[3] Sababun-Nuzuwl: Aayah hii pamoja na Aayah ya mwisho katika Suwrah hii (3: 176) imeteremka kuhusu Jaabir bin ‘Abdillaah (رضي الله عنه) pale alipotembelewa na Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) akiwa na Abuu Bakr Asw-Swiddiyq (رضي الله عنه) wakamkuta amezimia. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akatawadha na akamrashia maji kutokana na wudhuu wake. Kisha Jaabir (رضي الله عنه) akamuuliza Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم): “Niifanye vipi mali yangu?“ Hapo ikateremka hii Aayah. [Amehadithia Jaabir (رضي الله عنه) aimeipokea Al-Bukhaariy na Muslim].
[4] An-Naasikh Wal-Mansuwkh: Aayah hii imefutwa hukmu yake kwa Aayah ya kupigwa mijeledi mia moja kwa bikra waliozini, na Hadiyth za rajmi (kuwapiga mawe) waliozini baada ya ndoa, imehadithiwa kutoka kwa ‘Ubaadah bin Asw-Swaamit (رضي الله عنه) kwamba: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Chukueni kutoka kwangu, chukueni kutoka kwangu, Allaah Amekwishawajalia wanawake njia; bikra kwa bikra, wakizini hukmu yao ni kuchapwa mijeledi mia moja, na kutolewa maeneo hayo mwaka mzima, na Ath-Thayyib(aliyekwishaoa au kuolewa) kwa Ath-Thayyib, wakizini hukmu yao ni mijeledi mia moja, na rajmu (kupigwa mawe) [Muslim].
[5] Sababun-Nuzuwl: Walikuwa Waarabu zama za Jaahiliyyah pindi anapokufa mwanaume na akaacha mke, basi wale ndugu wa mume wake wanakuwa na haki zaidi kwa mwanamke, na baadhi yao wakitaka wanamuoa, na wakitaka wanamuozesha, na wakitaka hawamuozeshi, na wao wanakuwa wana haki naye zaidi kuliko hata ndugu zake mwanamke na wazazi wake. Ndipo Allaah (عزّ وجلّ) Akateremsha Aayah hii. [Amehadithia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) ameipokea Al-Bukhaary].
[6] Sababun-Nuzuwl: Aayah hii imeteremka kwa kuwa watu wa zama za Jaahiliyyah walikuwa wanaharamisha yaliyo ya haramu isipokuwa mke wa baba. Na walikuwa wanakusanya mabinti wawili ambao ni ndugu katika ndoa moja na wakati mmoja, kisha ikateremka Aayah hii pamoja na kauli ya Allaah Aliposema: “Na (mmeharamishwa) kuwaoa dada wawili kwa wakati mmoja, isipokuwa yaliyokwisha pita.” [An-Nisaa 4: 23] Amehadithia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما)ameitaja Ibn Jariyr Atw-Twabariy katika Tafsiyr yake].
[7] Sababun-Nuzuwl: Aayah hii imeteremka kuhusu Maswahaba (رضي الله عنهم) kwani wao siku ya Awtwaas (eneo lilipo baina ya Makkah na Twaaif ambapo walipatikana mateka baada ya vita vya Hunayn mwaka wa 8 Hijriyyah) walipata wanawake ambao ni mateka, basi wakaona uzito kuwaingilia kwa sababu waume zao ni washirikina. Allaah (عزّ وجلّ) Akateremsha hii Aayah: “Na (Mmeharamishiwa pia) wanawake walio katika ndoa isipokuwa iliyowamiliki mikono yenu ya kuume.” [Amehadithia Abuu Sa’iyd(رضي الله عنه) ameipokea Muslim].
Uharamisho wa ndoa ya mut’ah: Sabrah bin Ma’bad Al-Juhniy (رضي الله عنه) amehadithia kwamba baba yake aliandamana na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) katika Fat-hi Makkah akasema: “Enyi watu! Nilikuruhusuni ndoa ya mut’ah hapo mwanzo. Leo Allaah Ameiharamisha mpaka Siku ya Qiyaamah! Basi ikiwa kuna yeyote ambaye ana mke wa ndoa ya mut’ah amwache na wala asichukue chochote katika alichompa.” [Muslim na wengineo].
[8] Al-Kabaair (madhambi makubwa): ni yaile yaliyotajiwa ndani yake laana, au haddi (adhabu) hapa duniani, au yameahidiwa juu yake ghadhabu za Allaah au moto. Na pia kuhusu madhambi saba yanayoangamiza [Al-Bukhaariy, Muslim].
[9] An-Naasikh Wal-Mansuwkh: Hapo mwanzo Muhaajiriyn walipofika Madiynah, Answaar walichukua viapo vya kuungana nao kiundugu na kurithiana. Kisha hukmu ya Aayah hii ikafutwa baada ya hukmu ya Aayah (8: 75) katika Suwrat Al-Anfaal nayo ni kauli ya Allaah: “Na ndugu wa uhusiano wa damu wanastahikiana wenyewe kwa wenyewe (kwa kurithiana), katika shariy’ah (na hukmu) ya Allaah. Hakika Allaah ni Mjuzi wa kila.”
[10] Faida: Kuhusu: “na wahameni katika malazi.” Imekusudiwa kutokulala nao na kutokujimai nao, kwa ujumla ni kuwagomea. Ama kuhusu: “na wapigeni.” Imekusudiwa kipigo kidogo kisichokuwa cha kumdhuru, wala haipasi kupigwa usoni.
[11] Sababun-Nuzuwl: Sababu ya kuteremshwa hukmu ya tayammum: Mama wa ‘Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها) amehadithia: “Tulikwenda katika moja ya safari tukafika Al-Baydaa au Dhaatul-Jaysh ambako kidani changu kilivunjika (na kikapotea). Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akawa anakitafuta, kisha pia watu wengineo wakainuka kukitafuta. Hapakuweko na maji sehemu hiyo, basi watu wakamwendea Abuu Bakr Asw-Swiddiyq na kusema: Huoni alivyofanya ‘Aaishah? Kamfanya Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) pamoja na watu wakae sehemu ambayo hakuna maji! Abuu Bakr akaja wakati Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa amelaa akiwa amelaza kichwa chake mapajani mwangu. Akaniambia: Umemzuia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) na watu sehemu ambako hakuna maji na wala hawana (akiba ya) maji. Basi akanigombesha na akasema Aliyomjaalia (Allaah) kusema kuhusu mimi na akanipiga ubavuni kwa mkono wake. Hakuna kilichonizuia kusogea (kutokana na maumivu) isipokuwa kwa vile Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alilala mapajani mwangu. Hapo Allaah Akateremsha Aayah ya tayammum, basi wakatayammam. ‘Usayd bin Al-Hudhwayr akasema: Ee ahli ya Abuu Bakr! Hii si baraka ya kwanza kwenu. Kisha akaendeshwa ngamia ambaye nilikuwa nimempanda na tukakipata kidani chini yake.” [Al-Bukhaariy].
Sababun-Nuzuwl: Kuhusu kuteremshwa kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى): “Enyi waloamini! Msikaribie Swalaah na hali mmelewa.” Ni kwamba, hatua ya kwanza kuhusu pombe imetahadharishwa katika Suwratul-Baqarah (2: 219): “Wanakuuliza kuhusu pombe na kamari. Sema…” Hii ni hatua ya pili ya kukatazwa pombe katika nyakati za Swalaah kwa sababu Maswahaba walikosea kusoma Qur-aan katika Swalaah kutokana na kulewa. Baada ya hapo ikafutwa hukmu hii na ikabakia pombe kuwa ni haramu nyakati zote kwa kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى) katika Suwrat Al-Maaidah (5: 90): “Enyi walioamini!Hakika pombe na kamari na (kuabudu) masanamu, na kutazamia kwa mishale ya kupigia ramli; ni rijsun (uchafu na uovu) katika kitendo cha shaytwaan; basi jiepusheni navyo, mpate kufaulu.”
[12] Miongoni mwa ada za Mayahudi ni kuyapotosha maneno ya Allaah (عزّ وجلّ) kuyatoa kwenye makusudio yake na pia wanayatafsiri kwa isiyokuwa tafsiri yake. Na watu wa bid’ah wamejifananisha nao katika kupindisha na kupotosha maana ya Majina ya Allaah na Sifa Zake.
[13] Ifahamu historia ya Mayahudi kwa mukhtasari namna walivyokuwa jeuri kwa Manabii wao: Mayahudi walikatazwa na Allaah (سبحانه وتعالى) kuvua samaki siku ya As-Sabt (Jumamosi) lakini wao kwa ujeuri wao wakavua samaki siku hiyo na kwa kutumia hila. Pia Allaah (سبحانه وتعالى) Akawakumbusha wajukuu zao kuhusu siku hiyo ya As- (Jumamosi) ambayo babu zao Mayahudi waliasi ndani yake kiasi kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Aliwageuza kuwa nyani na nguruwe. Na mwenye kusoma visa vya Mayahudi dhidi ya Manabii wao na miongoni mwa swaalihiyna katika wao, atakuta kuwa waliwaudhi mno Manabii wao na wakawapinga na kwenda kinyume nao. Na pia wakafanyia inadi na ujeuri maamrisho ya Allaah (سبحانه وتعالى) na wakawa na ujeuri uliopindukia. Miongoni mwa mifano ya hayo ni; kisa cha ng’ombe na ndama. Pia kutaka kwao kumuona Allaah (سبحانه وتعالى) wazi wazi. Tena hayo wameyafanya baada tu ya kuvukishwa bahari kwa salama na kuokolewa kutona na adui wao Fir-‘awn aliyezamishwa baharini. Pia uasi wao kuwaua baadhi ya Manabii bila ya haki. Na mifano mingine mingi kuhusu uasi na ujeuri wa Mayahudi.
[14] Sababun-Nuzwul: Aayah hii imeteremshwa kama alivyohadithia ‘Ikrimah kwamba: Huyay bin Akhtab na Ka’b Al-Ashraf (Wakuu wa ki-Yahudi) walikuja kwa watu wa Makkah (washirikina) wakawaambia: Nyinyi (Mayahudi) ni Ahlul-Kitaab na wenye ‘ilmu, hivyo basi tujulisheni (tofauti zetu) kuhusu sisi na kuhusu Muhammad. Wakasema: Jielezeni kuhusu nyinyi na kuhusu Muhammad. Wakasema: Sisi tunaunga ujamaa wa uhusiano wa damu, tunachinja ngamia (kwa ajili ya mafukara), tunasamehe madeni, tunawapa maji Mahujaji. Ama Muhammad, yeye hana watoto wa kiume, amekata ujamaa wa uhusiano wa damu, na wevi wa Mahujaji (kabila la) Ghifar wanamfuata. Basi je, sisi bora au yeye? Wakasema: Nyinyi bora zaidi na mlioongoka zaidi katika njia. Hapo Allaah Akateremsha: “Je, huwaoni wale waliopewa sehemu ya Kitabu wanaamini itikadi potofu na twaghuti na wanasema juu ya wale waliokufuru kuwa: “Hawa wameongoka zaidi katika njia kuliko wale walioamini... mpaka kauli Yake: “basi hatopata wa kumnusuru.” (4: 52).
[15] Sababun-Nuzuwl: Aayah hii ni ya pekee katika Suwrah hii ya An-Nisaa (4: 58) ambayo imeteremka Makkah. Imeteremshwa Siku ya Fat-hu Makkah (Ushindi). Ibn Jurayj amehadithia kwamba imeteremshwa kuhusu ‘Uthmaan bin Twalhah ambaye pale Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alichukua ufunguo wa Ka’bah kutoka kwake akaingia Ka’bah. Alipotoka nje ya Ka’bah, alitoka huku akiwa anasoma: “Hakika Allaah Anakuamrisheni kurudisha amana kwa wenyewe.” Hapo akamwita ‘Uthmaan bin Twalhah na akampa funguo [Tafsiyr Ibn Kathiyr]. Funguo hizo zimeendelea kubakia katika ukoo huo, kizazi baada ya kizazi mpaka sasa, na mpaka Siku ya Qiyaamah ukoo huo umefadhilishwa kuwa ndio wenye amana ya kukamata funguo za Al-Ka’bah.
[16] Sababun-Nuzuwl: Aayah hii imeteremka kuhusu ‘Abdullaah Ibn Hudhaafah (رضي الله عنه)pale alipotumwa na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kwenye msafara wa Jihaad. [Amehadithia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما)ameipokea Al-Bukhaariy na Muslim].
Pia Imeteremshwa pale Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alipotuma jeshi chini ya uongozi wa mtu mmoja wa Answaar. Walipoondoka, aliwaghadhibikia kwa sababu fulani akawaambia: Kwani Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) hakukuamrisheni mnitii? Wakasema: Ndio! Akasema: Okoteni kuni. Kisha akawasha moto akasema: Nakuamrisheni muingie motoni humu. Wakakaribia watu kuuingia lakini kijana mmoja miongoni mwao akasema: Nyinyi mmekimbia moto kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) hivyo msikimbilie mpaka mrudi kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kisha akikuamrisheni kuingia hapo muuingie. Waliporudi kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) wakamwelezea yaliyojiri, kisha yeye akasema: “Mngeliuingia, msingetoka kamwe humo. Hakika utiifu ni katika mema.” [Al-Bukhaariy na Muslim].
Amri ya kuwatii kwa wema watawala na viongozi wa mambo ya Waislamu, ni jambo ambalo limenukuliwa na Ijmaa’ juu yake, bali ndiyo ‘Aqiydah iliyokuwa sahihi ya Ahlus-Sunnah wal-Jamaa’ah. Lakini kwa masikitiko makubwa jambo hili wamelipuuza wengi katika Waislamu na wale wasiofahamu mafunzo ya Dini yao. Na matokeo ya kwenda kinyume na jambo hilo na ‘Aqiydah hiyo ni kuleta munkari mkubwa katika Ummah na ufisadi mpana; kuna wanaofanya maandamano kupinga viongozi kuna wanaojilipua kwa mabomu na kuua watu, kuna wanaoua watu kwa njia mbali mbali na kadhalika kumwaga damu za bin Aadam bure! Na wametumia njia hiyo maadui wa Uislamu ili kuuchafua Uislamu na kuudidimiza.
[17] Sababun-Nuzuwl: Aayah hii pamoja na mbili zinazofuatia (4: 60-62) zimeteremka kama alivyohadithia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما)kuwa alikuwa Abuu Barzat Al-Aslamiyy ni Kuhani akitoa hukumu kuhusu magomvi yanayotokea baina ya Mayahudi. Siku moja baadhi ya watu katika washirikina walileta magomvi kwake, kisha Allaah Akateremsha Aayah hii: “Je, huoni wale wanaodai kwamba wao wameamini yaliyoteremshwa kwako…” [Abuu Haatim Atw-Twabaraaniy, Ibn Hajar Al-‘Asqalaaniy (4/19) amesema isnaad yake ni nzuri].
Sababun-Nuzuwl nyingine pia ya Aayah hii ni kwamba waligombana mtu kutoka Answaar na Myahudi kisha Myahudi akasema: “Twende kwa Muhammad akatuhukumu.” Na yule Answaar akasema: “Twende kwa Ka’ab Al-Ashraf.” Imesemwa pia kuwa miongoni mwa wanafiki walliokuwa wakijidai kuwa ni Waislamu, lakini huku wakitafuta hukmu za kijaahiliyyah. [Tafsiyr Ibn Kathiyr].
Pia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) amesema: “Abuu Barzah Al-Aslamiy alikuwa mtabiri na akihukumu magomvi ya Mayahudi. Baadhi ya Waislamu walipomwendea kutaka awahukumu, Allaah (سبحانه وتعالى) Akateremsha: “Je, huoni wale wanaodai kwamba wao wameamini yaliyoteremshwa kwako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) na yale yaliyoteremshwa kabla yako… mpaka:“Wa-Allaahi hatukutaka ila mazuri na mapatano.” (4: 60-62) [Atw-Twabaraaniy].
[18] Sababun-Nuzuwl: Aayah hii imeteremka kuhusu Az-Zubayr bin Al-‘Awwaam (رضي الله عنه) na bwana mmoja katika Answaar, pale walipokhitilafiana kuhusu mfereji wa kupitisha maji ya mvua waliokuwa wakitumia maji yake. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akatoa hukmu baina yao kwamba Az-Zubayr amwagilie maji ardhini mwake kisha ayaache yatiririke kwa Answaar. Akakasirika Answaar huyo na kumwambia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): “Umempendelea yeye kwa kuwa ni mtoto wa ‘ammat yako! Hapo Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akabadilika uso rangi kwa hasira akamwambia tena Az-Zubayr amwagie maji kwanza kisha yatiririke kwa jirani yake huyo kwa kuwa hukumu hiyo ilikuwa kwa manufaa ya wote wawili. Hivyo akampatia Az-Zubayr haki yake. Ikateremka Aayah hii: “Basi Naapa kwa Rabb wako, hawatoamini mpaka wakufanye wewe ni mwamuzi katika yale wanayozozana baina yao… (4: 67). [Amehadithia Az-Zubayr (رضي الله عنه)ameipokea Al-Bukhaariy na Muslim].
[19] Sababun-Nuzuwl: Aayah hii imeteremka kuhusu Answaar mmoja ambaye alikuwa kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akiwa na huzuni. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akamuuliza: “Mbona nakuona umehuzunika?” Akasema: Ee Rasuli wa Allaah! Nilikuwa natafakari jambo. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Jambo gani?” Akajibu: Kila siku tunakuja kwako asubuhi na usiku tukitazama uso wako na kukaa kitako nawe. Kesho (Aakhirah), utakuja kufufuliwa pamoja na Manabii na hivyo sisi hatutoweza kukuona tena. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) hakusema kitu, kisha Jibriyl (عليه السلام) akamjia kumteremshia Aayah hii: “Na atakayemtii Allaah na Rasuli, basi hao watakuwa pamoja na wale Allaah Aliowaneemesha miongoni mwa Manabii... (4: 69)” [Ibn Jariyr, Tafsiyr Ibn Kathiyr].
Sababun-Nuzuwl nyingine pia ya Aayah hii, ni kama alivyohadithia Mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها) kwamba: Mtu mmoja alikuja kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Ee Rasuli wa Allaah! Hakika wewe ni kipenzi kwangu kuliko nafsi yangu na kipenzi kwangu kuliko ahli yangu, na kipenzi kwangu kuliko wanangu, na hakika ninapokuwa nyumbani kwangu nakukumbuka basi huwa siwezi kusubiri mpaka nije kukutazama. Na napokumbuka mauti yangu na mauti yako, hutambua kwamba wewe utakapoingia Jannah utapanda pamoja na Manabii, lakini nitakapoingia mimi Jannah nakhofu kuwa sitokuona! Basi Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) hakumjibu mpaka hapo ikateremshwa: “Na atakayemtii Allaah naRasuli, basi hao watakuwa pamoja na wale Allaah Aliowaneemesha miongoni mwa Manabii...(4: 69)” [At-Twabaraaniy katika Al-Mu’jamu Asw-Swaghiyr].
[20] Sababun-Nuzuwl: Aayah hii imeteremshwa kama alivyohadithia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) kwamba: ‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf na Maswahaba wenzake (رضي الله عنهم) walipokuwa Makkaah walimwendea Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na kumwambia: Ee Rasuli wa Allaah! Tulipokuwa washirikina tulikuwa kwenye ‘izzah (hadhi na utukufu) lakini sasa tumeingia Uislamu tumekuwa madhalili. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Hakika mimi nimeamrishwa kusamehe basi msifanye qitaal (vita).” Kisha Allaah Alipomuamrisha Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kuhajiri Madiynah, Alimuamrisha jihaad na qitaal (kwa washirikina), basi (wao Waislamu) wakasita. Hapo ikateremshwa Aayah hii. [An-Nasaaiy na Al-Haakim].
[21] Faida: Aayah hii ni miongoni mwa dalili na radd juu ya madh-hab ya Al-Mufawwidhwah (wanaokubali sifa ya Allaah lakini wakidai maana yake haijulikani; kwa hivyo, wanamzulia Allaah kuwa kawaletea mafundisho waja Wake ambayo hayajulikani maana yake!) ambao wanasema kuwa Majina ya Allaah na Swifaat Zake hazifahamiki maana yake, na hiyo ni itikadi batili mno, bali Shaykhul-Islaam (رحمه الله) amesema alipolizungumzia hili pote la Mufawwidhwah kuwa ni katika mapote ya bid’ah yaliyokuwa ya shari. Kisha wakainasibisha kauli hii kuwa ndiyo kauli ya Salaf! Huko ni kuwazulia wema waliotangulia (رحمهم الله). Imaam Ahmad anawaona Mufawwidhwah kuwa ni wabaya zaidi kuliko Jahmiyyah.
[22] Sababun-Nuzuwl: Aayah hii imeteremka kama alivyohadithia ‘Umar (رضي الله عنه) kwamba: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alipojitenga mbali na wake zake, niliingia Masjid nikakuta watu wakipiga ardhi kwa changarawe wakisema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amewataliki wake zake! Na hivyo ni kabla ya kuamrishwa hijaab. ‘Umar akasema: Nitatambua hilo leo. Basi nikamwendea ‘Aaishah (رضي الله عنها)nikamwambia: Yaa bint Abiy Bakr! Je, hivi imekufikia kumuudhi Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)? Akasema: Haijakuhusu jambo kwangu, nami hainihusu jambo kwako yaa bin Al-Khattwaab, juu yako kumuwaidhi (bint yako)! Nikamwendea Hafswah bint ‘Umar nikamwambia: Yaa Hafswah! Imenifikia (khabari) kwamba umemuudhi Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) na nimetambua kuwa hakupendi! Na lau ningekuwa (si baba yako) angekutaliki! Hafswah akalia sana. Nikamwambia: Yuko wapi Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)? Akasema: Yuko chumba cha darini. Nikaenda nikamkuta Rabaah, mtumishi wa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amekaa kitako kingoni mwa dirisha akinin’giniza miguu yake juu katika ufumbi wa shina la mtende ambalo likimsaidia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kupanda (chumba cha darini) na kuteremkia. Nikamwambia: Yaa Rabaah! Niombee idhini kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم). Rabaah akatazama chumbani kisha akanitazama mimi wala hakusema kitu. Kisha nikasema: Yaa Rabaah! Niombee idhini kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم). Rabaah akatazama chumbani kisha akanitazama mimi wala hakusema kitu. Kisha nikapandisha sauti yangu nikasema: Yaa Rabaah! Niombee idhini kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم), mimi nadhani kuwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) anadhania kuwa nimekuja kwa ajili ya Hafswah! Wa-Allaahi kama Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ataniamrisha nimpige (nimkate) shingo yake nitampiga! Nikapandisha sauti yangu akaniashiria nipande (kuingia chumba cha darini). Nikaingia kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) nikamkuta amelalia jamvi.
Nikakaa kitako akaivuta shuka yake na hakuwa na nyingine (isipokuwa hiyo tu) na jamvi hilo lilimfanyia alama ubavuni mwake. Nikatazama kwa macho yangu hicho kijichumba cha Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) nikakuta shayiri kiasi kiasi cha kibaba kimoja na kiasi cha matawi ya mimosa yamewekwa pembeni mwa chumba na mkoba wa ngozi uliobadilishwa rangi. Nikatokwa na machozi (kuona maisha duni anayoishi).
Akasema: “Nini kinachokuliza yaa Ibn Al-Khattwaab?” Nikasema: Ee Nabiyy wa Allaah! Na kwanini nisilie na hali jamvi limekufanyia alama ubavuni mwako na sioni kitu chumbani mwako humu (isipokuwa vitu vichache mno); (Mfalme) Qayswar na Kisraa wanaishi maisha ya kifakhari lakini wewe Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ambaye Amekuteua (Allaah) hichii ndio kijichumba chako? Akasema: “Ee Ibn Al-Khattwaab! Hivi huridhiki kuwa sisi tuna Aakhirah nao wana dunia?” Nikasema: Ndio. Kisha nilipoingia kwanza niliona usoni mwake alama za ghadhabu, basi nikasema: Ee Rasuli wa Allaah! Unatatizwa nini na wanawake? Ungeliwataliki basi hakika Allaah Yuko pamoja nawe, na Malaika Wake na Jibriyl, na Mikaaiyl na mimi, na Abuu Bakr, na Waumini (wote) tuko nawe. Na kichache nilichosema (siku ile) na namhimidi Allaah, nilitaraji kwamba Allaah Atasadikisha kauli yangu. Basi ikateremka Aayah hii ya At-Takhyiyr (chaguo):“Ikiwa nyinyi wawili mtatubia kwa Allaah (ni khayr kwenu) kwani kwa hakika nyoyo zenu zimeelemea (kumchukiza Nabiy صلى الله عليه وآله وسلم). Na mkisaidiana dhidi yake, basi hakika Allaah Ndiye Mlinzi (na Msaidizi) wake na Jibriyl na Waumini wema, na zaidi ya hayo, Malaika pia watasaidia. Akikutalikini, asaaRabb Wake Akambadilishia wake bora kuliko nyinyi; Waislamu…” (66: 4- 5) Na walikuwa ni ‘Aaishah bint wa Abuu Bakr na Hafswah ambao walishikilia na kusaidiana (kudai mali) kuliko wake wote wengine wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم). Nikasema: Ee Rasuli wa Allaah! Je, umewataliki? Akasema: “Hapana.” Nikasema: Ee Rasuli wa Allaah! Hakika niliingia Masjid nikakuta Waislamu wanacheza kwa vichangarawe (huku dhana zimewashughulisha) wakisema kuwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amewataliki wake zake. Je, niende kuwajulisha kuwa hukuwataliki? Akasema: “Naam ukipenda.” Nikaendelea kuongea naye mpaka (nikatanabahi) alama za ghadhabu zimepotea usoni mwake na mpaka (huzuni yake ikageuka kuwa ni furaha na hivyo) uso wake ukarudi kuwa na bashasha kama kawaida yake, akacheka na meno yake yalikuwa ya kupendeza mno kuliko watu wote! Kisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akateremka, nami nikateremka huku nikikamata shina la mtende, naye Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akateremka (kwa wepesi kabisa) bila ya kukamata chochote mkononi mwake (kujizuilia). Nikasema: Ee Rasuli wa Allaah! Ulikuwa chumbani mwako siku ishirini na tisa. Akasema: (Mara nyingine) “Mwezi huwa ni siku ishirini na tisa.” Nikasimama mlangoni mwa Masjid nikaita kwa sauti yangu ya juu kabisa: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) hakuwataliki wake zake! Hapo ikataremka Aayah hii: “Na linapowafikia jambo lolote la amani au la khofu hulitangaza. Na lau wangelirudisha kwa Rasuli na kwa wenye madaraka kati yao, wale wanaotafiti miongoni mwao wangelielewa… (4: 83). Ikawa ni mimi niliyetafiti jambo hilo. Na Allaah Akateremsha Aayah ya At-Takhyiyr (At-Tahriym 66: 4 – 5)[Al-Bukhaariy na Muslim].
[23] Sababun-Nuzuwl: Aayah hii imeteremka kuhusu baadhi ya watu ambao walikuwa wametoka pamoja na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) pamoja na Maswahaba zake kwenda katika vita vya Uhud. Wakarejea nyuma na hawakuungana na wenzao. Pakawa katika Maswahaba, kuna makundi mawili; kundi moja likawa linasema tuwapige vita! Na kundi jingine likawa linasema hapana! Hapo ikateremka Aayah hii: “Basi mna nini (hata) mkawa makundi mawili kuhusu wanafiki… (4: 88) [Amehadithia Zayd bin Thaabit (رضي الله عنه)ameipokea Al-Bukhaariy na Muslim].
Sababun-Nuzuwl: Pia Al-‘Awf (رضي الله عنه) amehadithia kwamba Aayah hii imeteremshwa kuhusu baadhi ya watu Makkah ambao walisema wameingia Uislamu lakini huku wakiwaunga mkono washirikina. Walipokwenda Makkah kutimiza mahitaji yao wakaambizana: “Tutakapokutana na Maswahaba wa Muhammad hakutakuwa na madhara yoyote upande wetu.” Waumini walipopata khabari kwamba watu hao wameenda Makkah, wakasema baadhi yao: “Twendeni kwa waoga hao tuwaue kwa sababu wanawaunga mkono maadui zenu dhidi yenu!” Lakini kundi jingine la Waumini wakasema: “Subhaana Allaah! Mnataka kuua watu wanaosema kama mlivyosema kwa sababu tu hawakuhajiri au kuacha ardhi yao. Kwani inaruhusiwa kumwaga damu na kutaifisha mali yao katika hali hii?” Basi wakagawanyika makundi mawili, na wakati huo Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa nao na hakukataza kundi lolote kuhusu mabishano yao. Hapo Allaah Akateremsha: “Basi mna nini (hata) mkawa makundi mawili kuhusu wanafiki…” (4: 88) [Ibn Abiy Haatim Tafsiyr Ibn Kathiyr].
[24] Sababun-Nuzuwl: Aayah hii imeteremka kuhusu bwana mmoja ambaye alionekana kwenye vita akiwa ana msururu wa ghanima (ngawira) kisha Waislamu wakamfuata mbio. Yule bwana alipoona Waislamu wamemfikia akawasalimia lakini Waislamu wakamuua na wakachukua ghanima zake, hapo ikateremka hii Aayah: “Enyi walioamini! Mnaposafiri (kupigana jihaad) katika njia ya Allaah thibitisheni, wala msimwambie anayekutoleeni (maamkizi ya) salamu (kwamba): “Wewe si Muumini” kwa kutamani mafao yapitayo ya uhai wa dunia…” (3: 94). [Amehadithia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما)ameipokea Al-Bukhaariy na Muslim]
Na At-Tirmidhiy na Imaam Ahmad wamerekodi kwamba: Wakanong’onezana kwamba: “Anasema salaam apate kujihami tu!” Wakamuua kisha wakaenda kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) pamoja na kondoo hao, ndipo ikateremshwa Aayah hii (3: 94)
Na Imaam Ahmad amerekodi kwamba Al-Qa’qaa’ bin ‘Abdillaah bin Abiy Hadrad amehadithia kwamba baba yake ‘Abdullaah bin Abiy Hadrad alisema: Rasuli wa Allaah(صلى الله عليه وآله وسلم) alitutuma (maeneo ya) ‘Adhwam. Nikatoka pamoja na kundi la Waislamu ambamo alikuweko Abuu Qataadah, Al-Haarith bin Rab’iy na Muhallam bin Juthmaamah bin Qays. Tukaendelea mpaka tukafika eneo la ‘Adhwam ambako ‘Aamir Al-Ashja’iy alitupitia akiwa amepanda ngamia wake. Alipotupitia akatusalimia na hatukumhujumu. Lakini Muhallam bin Juthmaamah alimuua na kuchukua ngamia wake kwa sababu ya matatizo baina yao. Tuliporudi kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) tukamuhadithia yaliyotokea, hapo ikatuteremkia Qur-aan: “Enyi walioamini! Mnapotembea katika njia ya Allaah thibitisheni, wala msimwambie anayekuamkieni kwa “As-salaam…” mpaka“kwa yale myatendayo ni Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika.” (4: 94)
[25] Sababun-Nuzuwl: Ilipoteremka kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى): “Hawawi sawa kati ya Waumini wanaokaa (nyumbani).” Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akamuamrisha Zayd bin Thaabit (رضي الله عنه) kuiandika, mara hapo akaja ‘Abdullaah bin Ummi Maktuwm(رضي الله عنه) akilalamika kuhusu upofu wa macho yake, hapo ikateremka kauli ya Allaah kwa kuongezeka: “Wasiokuwa na dharura…” “Hawawi sawa kati ya Waumini wanaokaa (nyumbani) wasiokuwa na dharura…” (4: 95)[Amehadithia Baraa bin ‘Aazib na Zayd bin Thaabit (رضي الله عنهما) ameipokea Al-Bukhaariy na Muslim].
Na katika riwaayah nyingine ya Al-Bukhaariy, Sahl bin Sa’d As-Saa’idiy amehadithia kwamba: Nilimuona Marwaan bin Al-Hakam amekaa kitako Masjid. Nikamkabili na nikaketi karibu naye. Akatujulisha kwamba Zayd bin Thaabit amemwambia kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesomea imla Aayah hii: “Hawawi sawa kati ya Waumini wanaokaa (nyumbani) wasiokuwa na dharura na kati ya Mujaahiduwn katika njia ya Allaah… (4: 95). Kisha Ibn Ummi Maktuwm akaja kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) wakati akanisomea Aayah ili niiandike. Ibn Ummi Maktuwm akasema: Ee Rasuli wa Allaah! Ningekuwa na uwezo bila shaka ningeshiriki katika jihaad. Alikuwa ni kipofu basi hapo Allaah Akamteremshia Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) wakati mapaja yake yalikuwa juu yangu na yakawa mazito mno kwangu (kutokana na Wahyi kuteremka) mpaka nikakhofia kuwa mapaja yangu yatavunjika. Kisha Allaah Akateremsha: “wasiokuwa na dharura…”
Pia At-Tirmidhiy amerekodi kwamba Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) amehadithia kwamba:“Hawawi sawa kati ya Waumini wanaokaa (nyumbani) wasiokuwa na dharura (4: 95) inahusiana na wale wasiotoka kwenda kupigana vita vya Badr na ambao waliokwenda Badr. Wakati vita vya Badr vilipokaribia kuanza, Abuu Ahmad bin Jahsh na Ibn Maktuwm walisema: Ee Rasuli wa Allaah! Sisi ni vipofu, je, tuna udhuru? Hapo ikateremshwa: “Hawawi sawa kati ya Waumini wanaokaa (nyumbani) wasiokuwa na dharura…”
[26] Sababun-Nuzuwl: Aayah hii imeteremka kama alivyohadithia Muhammad bin ‘Abdir-Rahmaan bin Al-Aswad (رضي الله عنه) kwamba:Watu wa Madiynah walilazimishwa kuandaa jeshi (kupigana na watu wa Ash-Shaam katika khilaafah ya Ibn Az-Zubayr Makkah) na nikawa nimeandikwa humo. Kisha nikakutana na ‘Ikrimah, mtumwa wa Ibn ‘Abbaas aliyekuwa huru, nikamjulisha (hayo), akanikataza mno (kuingia katika orodha ya jeshi), akasema: Ibn ‘Abbaas amenijulisha kwamba baadhi wa Waislamu walikuwa na washirikina hivyo wakikithiri idadi ya washirikina dhidi ya Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم). Mshale ulikuwa unarushwa ambao ulimpiga mmoja wao (Waislamu wakiwa pamoja na washirikina) na kumuua, au hupigwa na kuuliwa (kwa upanga).” Hapo Allaah Akateremsha: “Hakika wale ambao Malaika wamewafisha, hali wamejidhulumu nafsi zao…” (4: 97) Abuu Aswad akaongezea:“Isipokuwa wale waliokandamizwa kati ya wanaume na wanawake na watoto… (4: 98) [Al-Bukhaariy].
Pia Adhw-Dhwahaak amesema kwamba Aayah hii imeteremshwa kuhusu baadhi ya wanafiki ambao hawakuungana na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم), bali walibakia Makkah kisha wakatoka na washirikina katika vita vya Badr. Wakauawa pamoja na waliouawa. Hapo Aayah hii (4: 97) ikateremshwa kuhusu hao waliobakia pamoja na washirikina hali ya kuwa waliweza kufanya hijrah lakini hawakufanya na wakashindwa kuthibitisha Uislamu wao. Watu kama hao wamejidhulumu nafsi zao na wakaingia katika uharamisho kama ilivyokubalika na ijmaa’ na kutokana na kauli ya Allaah: “Hakika wale ambao Malaika wamewafisha, hali wamejidhulumu nafsi zao” (4: 97).
[27] Sababun-Nuzuwl: Ilipoteremka kauli ya Allaah: “Hakika wale ambao Malaika wamewafisha, hali wamejidhulumu nafsi zao”(4: 97). Palikuweko mtu mmoja Makkah akiitwa Dhwamrah, yeye alikuwa ni mgonjwa akaiambia familia yake: “Nitoeni Makkah kwani nahisi joto kali la maradhi.” Familia yake wakamuuliza: “Tukupeleke wapi?” Akaashiria kwa mkono wake kuwa wampeleke Madiynah. Hapo ikateremka Aayah hii: “Na anayehajiri katika njia ya Allaah atapata katika ardhi mahali pengi pa kukimbilia na wasaa. Na atakayetoka nyumbani kwake…” (4; 100). [Amehadithia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) ameipokea Ibn Jariyr].
[28] Sababun-Nuzuwl: ‘Abuu ‘Ayyaash Az-Zuraqiy amesema: “Tulikuwa pamoja na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) eneo la ‘Usfaan (sehemu maarufu karibu na Makkah) wakati washirikina walikutana na sisi wakiwa chini ya uongozi wa Khaalid bin Waliyd, nao walikuwa baina yetu na Qiblah. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akatuswalisha Swalaah ya Adhuhuri, basi washirikina wakasema: “Wameshughulishwa na jambo ambalo tulikuwa na fursa ya kuwahujumu.” Kisha wakasema: “Inayofuatia ni Swalaah (ya ‘Alasiri) ambayo ni kipenzi zaidi kwao kuliko watoto wao na nafsi zao.” Hapo Jibriyl (عليه السلام) aliteremka kuleta Aayah hizi wakati wa baina ya Adhuhuri na Alasiri: “Na utakapokuwa upo kati yao, ukawaswalisha…”(4: 102) [Imaam Ahmad, Tafsiyr Ibn Kathiyr].
Na Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) amehadithia kwamba kuhusu kauli ya Allaah: “Na wala si dhambi kwenu ikiwa mna maudhiko kutokana na mvua au mkiwa wagonjwa kuweka (chini) silaha zenu… (4: 102) inahusiana na ‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf ambaye alijeruhiwa [Al-Bukhaariy].
[29] Maamrisho ya kutimiza Swalaah kwa wakati wake, na makemeo ya kuipuuza yamesisitizwa katika Qur-aan ana Sunnah na miongoni mwa Hadiyth za Rasuli wa Allaah(صلى الله عليه وآله وسلم) ni: “Kitu cha kwanza atakachohesabiwa nacho mja Siku ya Qiyaamah katika ‘amali zake ni Swalaah, ikitengenea atakuwa amefuzu na amefanikiwa, na ikiharibika atakuwa ameshapita patupu na amekhasirika…” [At-Tirmidhy na amesema Hadiyth hii ni Hasan Swahiyh].
Imaam ibn Baaz (رحمه الله) amesema: “Yeyote atakayeweka kengele ya saa makusudi imuamshe baada ya kutoka jua akakosa Swalaah ya Alfajiri, basi mtu huyo amepuuza kuswali kwa wakati wake na hivyo ni kufru kubwa kama walivyokubaliana ‘Ulamaa wengi kwa sababu amekusudia kuswali baada ya jua kutoka. Ni sawa na mtu ambaye anachelewesha kuswali Alfajiri akaiswali karibu na Adhuhuri. [Fataawa Ibn Baaz, Kitaab As-Swalaah 10/374].
[30] Sababun-Nuzuwl: Sababu ya kuteremka kauli ya Allaah: “na nitawaamrisha watabadili maumbile ya Allaah. Na atakayemfanya shaytwaan kuwa rafiki mwandani badala ya Allaah basi kwa yakini amekhasirika khasara bayana.” (4: 119). Imeteremka katika jambo la kuwahasi beberu kuwa ni katika njia ya kumtii shaytwaan. [Amehadithia Ibn ‘Abbaas(رضي الله عنهما) Athar hii ameipokea Ibn Jariyr].
[31] Sababun-Nuzuwl: Al-‘Awfiy amehadithia kwamba Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) alisema kuhusu Aayah hii (4: 123): Watu wa Dini mbali mbali walibishana; Watu wa Tawraat walisema: “Kitabu chetu ni Kitabu bora kabisa na Nabiy wetu (Muwsaa عليه السلام) ni Nabiy bora kabisa.” Watu wa Injiyl wakasema kama hivyo. Waislamu wakasema: “Hakuna Dini isipokuwa ya Kiislamu, Kitabu chetu kimefuta vitabu vyote vingine na Nabiy wetu ni Nabiy wa mwisho na nyinyi mmeamrishwa katika vitabu vyenu kuamini na kufuata Kitabu chetu.” Hapo Allaah Akateremsha Aayah hii:“Si kwa matamanio yenu wala si (kwa) matamanio ya Ahlil-Kitaab Atakayefanya uovu atalipwa kwayo. (4: 127) [Tafsiyr Ibn Kathiyr].
[32] Sababun-Nuzuwl: Aayah hii imeteremka kama alivyohadihtia Mama wa waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها) kwamba: Kuhusu kauli ya Allaah: “Na wanatafuta fatwa kwako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kuhusu wanawake. Sema: “Allaah Atakupeni hukmu kuhusu wao na yale mnayosomewa kwenu katika Kitabu kuhusu mayatima wanawake ambao hamuwapi (mahari) waliyoandikiwa; na mna raghba ya kuwaoa.” (4: 127)imeteremshwa kuhusu kesi ya bwana aliyekuwa anamlea bint yatima na ni msimamzi wake na mrithi wake. yatima huyo alishirikiana naye katika mali ya huyo bwana mpaka katika (shamba la) mtende. Mlezi huyo akawa na raghba ya kumuoa yatima (juu ya kuwa hakumpenda) na hakupenda kumuozesha mtu mwengine asije kushirikiana naye mali yake (ya yatima) ambayo anashirikiana naye (huyo bwana mlezi) kwa hiyo kwa sababu hii mlezi huyo alimzuia yatima huyo kuolewa, hapo ikateremshwa Aayah hii (4: 127) na inayofuatia (4: 128) [Al-Bukhaariy].
Katika riwaayah nyengine, ‘Urwah alimuuliza ‘Aaishah (رضي الله عنها) kuhusu Aayah: “Na mkikhofu kuwa hamtoweza kufanya uadilifu kwa mayatima; basi oeni waliokupendezeni katika wanawake;…” (4: 3). Aaishah (رضي الله عنها) akahadithia kisa kama hicho cha bint yatima kwa nyongeza kuwa huyo bwana mlezi alitaka kumuoa kwa mahari kidogo kabisa kuliko walivyokuwa wakipewa wanawake wengine walio kama hali yake. Kisha watu wakaenda kutafuta fatwa kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم), ndipo Allaah Akateremsha Aayah: “Na wanatafuta fatwa kwako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kuhusu wanawake” (4: 127). [Al-Bukhaariy na Muslim].
Dhulma waliyokuwa wakifanyiwa mayatima zama za jaahiliyyah: ‘Aliy bin Abiy Twalhah amesema: Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) amehadithia kwamba: Ilikuwa wakati wa jahaaliyya, Mlezi wa yatima mwanamke humfunga kamba binti yatima, hapo huwa hakuna ruhusa mtu kumuoa. Akiwa mzuri na akipenda kumuoa anamuoa na kudhibiti mali yake. Akiwa si mzuri, hamruhusu aolewe mpaka afariki, na hapo akifariki yeye hurithi mali yake. Allaah Akaharamisha hii Akasema:“Na juu ya wanaokandamizwa miongoni mwa watoto…” (4: 127).
[33] Sababun-Nuzuwl: Aayah hii imeteremshwa kuhusu bwana mmoja aliyekuwa na mke lakini hakuwa akimuonyesha mahaba wala hamkithirishii katika mahaba na wala hamuonyeshi mwenendo uliokuwa mzuri. Huyo bwana hakutaka kuendelea (kuwa katika ndoa naye), na alishazaa naye mtoto, lakini huyo mke hakupenda apewe talaka. Basi akamwambia mumewe: “Nakuruhusu uishi na mke mwengine” [Al-Bukhaariy na Muslim]. Katika riwaaya nyengine mwanamke huyo alisema: “Naachilia mbali haki zangu, lakini usinitaliki.” Hapo ikateremka Aayah hii: “Na ikiwa mke atakhofia kutoka kwa mumewe nushuwzaa (uonevu wa ndoa) au kutengwa…”(4: 120).
[34] Faida: Miongoni mwa yanayomtoa mtu nje ya Uislamu ni kufanyia istihzai Maneno ya Allaah (سبحانه وتعالى) na kama ilivyotajwa katika Nawaaqidhw Al-Islaam: “Mwenye kufanyia istihzai (shere) kwa chochote katika Dini ya Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) au akafanya utani katika thawabu au katika adhabu za Allaah, basi amekufuru.”[Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab,Nawaaqidhw Al-Islaam].
[35] As-Sabt: Rejea tanbihi (2: 65) (4: 47).
[36] Faida: Hii Aayah pia ni dalili nyengineyo inayothibitisha kwamba Nabiy ‘Iysaa (عليه السلام) hakufishwa bali amenyanyuliwa na Allaah mbinguni. Maelezo zaidi rejea tanbihi (3: 55).
[37] Faida: Rejea tanbihi (3: 55) ni hoja na dalili bayana kwa wanaokanusha kuteremka kwa Nabiy ‘Iysaa (عليه السلام) zama za mwisho kukaribia Qiyaamah kama ni dalili mojawapo kubwa ya kutokea Qiyaamah. Nabiy ‘Iysaa ('Alayhis-Salaam) atateremka kutoka mbinguni kuja duniani kama ni miongoni mwa alama kubwa za Qiyaamah.
وَإِن مِّنْ أَهْلِ الْكِتَابِ إِلَّا لَيُؤْمِنَنَّ بِهِ قَبْلَ مَوْتِهِ ۖ وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يَكُونُ عَلَيْهِمْ شَهِيدًا ﴿١٥٩﴾
Na hakuna yeyote katika Ahlil-Kitaabi ila atamwamini kabla ya kufa kwake. Na Siku ya Qiyaamah atakuwa shahidi juu yao. [An-Nisaa: 159].
((وَالَّذِي نَفْسِي بِيَدِهِ لَيُوشِكَنَّ أَنْ يَنْزِلَ فِيكُمْ ابْنُ مَرْيَمَ حَكَمًا مُقْسِطًا))
((Naapa kwa Yule Ambaye nafsi yangu iko Mikononi Mwake, hivi karibuni atateremka kwenu mwana wa Maryam ('Iysaa) akiwa ni kiongozi muadilifu)). [Al-Bukhaariy, Muslim].
Na pia kuna Ahaadiyth nyingi nyingine za Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) zimethibiti kama ifuatayo:
Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Naapa kwa Yule Ambaye nafsi yangu iko Mikononi Mwake, hivi karibuni atateremka kwenu mwana wa Maryam ('Iysaa) akiwa ni kiongozi muadilifu na atavunja misalaba, na kuua nguruwe, na ataondosha jizyah (ushuru kutoka kwa wasio Waislamu ambao wamo katika himaya ya serikali ya Waislamu). Kisha kutakuwa na mali nyingi hadi itafikia kuwa hakuna mtu wa kupokea sadaka. Wakati huu sijda moja itakuwa ni bora kwao kuliko maisha haya na yote yaliyomo (katika dunia).” Kisha Abuu Huraryah akasema: Someni mkipenda: “Na hakuna yeyote katika Ahlil-Kitaabi ila atamwamini kabla ya kufa kwake. Na Siku ya Qiyaamah atakuwa shahidi juu yao.” (4: 159)[Al-Bukhaariy].
[38] Al-Asbaatw: Ni makabila yaliyotokana na wana kumi na mbili wa Nabiy Ya’quwb (عليه السلام) waliotoka Manabii.
[39] Faida: Allaah (سبحانه وتعالى) Alimsemesha Muwsaa (عليه السلام) Maneno kwa uhakika wake na si majazi kama wanavyosema watu wa bid’ah bali ni maneno yaliyojengeka kwa herufi na sauti na Swiffah ya Al-Kalaam (Maneno) ni Swiffah iliyothibiti kwa Allaah kwa uhakika wake bila kuifanyia Swiffah hiitamthiyl wala takyiyf na bila kuifanyia ta’twiylwala tahriyf na hii ndiyo kauli ya sawa ambayo wamepita kwayo Salaf na Maimaamu wa haki katika Uislamu katika Swifaat zote zilizokuja ndani ya Qur-aan na Sunnah zilizokuwa Swahiyh.
[40] Allaah (سبحانه وتعالى) Amewakataza Ahlul-Kitaab wasimfanye ‘Iysaa na Mama yake kuwa ni washirika wa Allaah bali hao ni waja wawili katika waja wema wa Allaah na si washirika Wake kama Anavyosema Allaah(سبحانه وتعالى) Akimzungumzia ‘Iysaa (عليه السلام)katika Suwrat Maryam (19: 30-36) Na pia katika Suwratul-Maaidah (5: 17, 72-76).
[41] Sababun-Nuzuwl: Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alipomtembelea Jaabir (رضي الله عنه) alipokuwa mgonjwa, Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alimkuta Jaabir akiwa amezimia kisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akatawadha na akamrashia maji ya wudhuu, Jaabir akazindukana, kisha Jaabir akamuuliza Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) namna gani ataigawa mali yake kwa sababu hali yake ni hali ya Al-Kalaalah (asiye watoto, wala wazazi. Au asiye na mrithi wa kwenda juu wala kwenda chini.),hapo ikateremka hii Aayah. [Amehadithia Jaabir (رضي الله عنه) ameipokea Al-Bukhaariy na Muslim]. Na katika riwaayah ya At-Tirmidhiy, Abuu Daawuwd: “Alikuwa na dada tisa.”