@Furqanbot
[1] Rejea fadhila za Suwratul-Baqarah kupata fadhila zinazoshirikiana.
[2] Rejea tanbihi (2: 234).
[3] Faida: Aayaat Muhkamaatun: Ambazo maana zake zinafahmika kiwepesi hazina mushkila wala utata na dalili zake ziko wazi. Mutashaabihaat: Ni Aayah ambazo ni ngumu kufahamika, zinawatatanisha baadhi ya watu wasio na ‘ilmu ya kutosha.
Mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) aliisoma Aayah hii: “YeyeNdiye Aliyeteremsha kwako Kitabu …” mpaka mwisho wa Aayah, kisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: Ee ‘Aaishah! Pindi utakapowaona wale ambao wanafuata zile Aayaat ambazo haziko wazi zaidi, basi fahamu kuwa hao ndio wale ambao Allaah Amewataja katika hii Aayah, basi tahadharini nao.” [Al-Bukhaariy na Muslim].
[4] Aayah hii tukufu inathibitisha kuwa mapenzi ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) hayawezi kutimia isipokuwa kwa kufuta Sunnah zake, na ni hoja ya wazi kwa wanaodai wanampenda Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) lakini wakafanya bid’ah katika Dini kama kusoma Mawlid, Khitmah, Talqiyn, Du’aa za uzushi n.k. na hali yeye mwenyewe Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ameonya katika Hadiyth aliyohadithia Mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها) kwamba: “Atakayetenda ‘amali isiyokuwa yetu (katika Dini yetu) basi kitarudishwa.” [Al-Bukhaariy].
[5] Neno Kun! (Kuwa) rejea Aayah namba (47) Suwrah hii.
[6] Sifa ya makri (njama) huthibitishwa kwa Allaah (سبحانه وتعالى) kwa njia ya muqaabalah; huthibitishwa kwa Allaah kwa maana inayoendana na Allaah (عزّ وجلّ), kwa hiyo, Allaah Anamfanyia makri (njama) yule anayestahiki na pia ambaye anayefanya makri kwa waja wake.
[7] Allaah (سبحانه وتعالى) Alimnyanyua Nabiy ‘Iysaa (عليه السلام) kuelekea mbinguni akiwa hai, na wala hakuuliwa kabla ya hapo. Na atakuja kuteremka duniani zama za mwisho, na atamuua Masiyh Ad-Dajjaal, na atawaua nguruwe wote, na atavunja misalaba yote na ataondosha kodi, na hatokubali ispokuwa Uislamu, na atahukumu kwa shariy’ah ya Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم). [Dalili katika Suwrat An-Nisaa (4: 156-158)].
Aayah hii tukufu ni dalili ya wazi kwa wanaodai kwamba neno la مُتَوَفِّيكَ lina maana “kukufisha kikamilifu.” Neno hilo hilo Amelitaja Allaah (سبحانه وتعالى) katika (Al-An’aam 6: 60, Az-Zumar 39: 42).
وَهُوَ الَّذِي يَتَوَفَّاكُم بِاللَّيْلِ وَيَعْلَمُ مَا جَرَحْتُم بِالنَّهَارِ ثُمَّ يَبْعَثُكُمْ فِيهِ لِيُقْضَىٰ أَجَلٌ مُّسَمًّى ۖ
60. Naye Ndiye Anayekufisheni usiku (mnapolala) na Anajua yale yote mnayoyafanya mchana, kisha Anakufufueni humo ili utimizwe muda maalumu uliokadiriwa.
اللَّـهُ يَتَوَفَّى الْأَنفُسَ حِينَ مَوْتِهَا وَالَّتِي لَمْ تَمُتْ فِي مَنَامِهَا ۖ فَيُمْسِكُ الَّتِي قَضَىٰ عَلَيْهَا الْمَوْتَ وَيُرْسِلُ الْأُخْرَىٰ إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى ۚ
42. Allaah Anafisha nafsi wakati wa mauti yake; na zile zisizokufa katika usingizi wake, basi Huzizuia ambazo Amezikidhia mauti, na Huzituma nyingine mpaka muda maalumu uliokadiriwa.
Hapo tunafahamu kwamba, mtu anapolala anachukuliwa au anafishwa usingizini na kurudishwa katika uhai kwa kuwa roho yake inachukuliwa na ndio inayojulikana kuwa niAl-Mawt As-Sughraa (mauti madogo). Kwa dalili pia kutoka katika mafunzo ya Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) katika nyiradi za kulala na kuamka tuwe tunasema:
بِاسْـمِكَ اللّهُـمَّ أَموتُ وَأَحْـيا
Kwa jina lako Ee Allaah ninakufa na ninakuwa hai.
الحَمْـدُ لِلّهِ الّذي أَحْـيانا بَعْـدَ ما أَماتَـنا وَإليه النُّـشور
Himdi Anastahiki Allaah Ambaye Ametupa uhai baada ya kutufisha na ni Kwake tu kufufuliwa.
[8] Mubaahalah: Kilugha ni kuomba kwa unyenyekevu na juhudi. Na katika istilahi ni kuomba laana ya Allaah imfikie mmoja kati ya watu wanaokhitilafiana katika jambo.
[9] Sababun-Nuzuwl: Aayah hii imeteremka kama alivyohadithia ’Abdullaah bin Mas’uwd(رضي الله عنه) kwamba: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alisema: ”Yeyote atakayeapa kiapo ili achukue mali ya Muislamu (bila ya haki) atakutana na Allaah Akiwa Amemghadhibikia.” Hapo Allaah Akateremsha kusadikisha kauli hii: ”Hakika wale wanaobadilisha ahadi ya Allaah na viapo vyao kwa thamani ndogo; hao hawana sehemu yoyote katika Aakhirah...” mpaka mwisho wa Aayah (3: 77). Akasema: Kisha akaingia Al-Ash’ath bin Qays akasema: Je, ’Abdur-Rahmaan anakuhadithieni nini? Tukasema: Kadhaa wa kadhaa. Akasema: Aayah hii imeteremshiwa kuhusu mimi; nilikuwa na kisima katika ardhi ya bin-’ammi yangu (lakini alikanusha kuwa similiki). Kisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akaniambia: ”Ima ulete ushahidi au yeye (bin-’ammi yako) atatoa kiapo (kuthibitisha madai yake).” Nikasema: Nina hakika atatoa kiapo (cha uongo) ee Rasuli wa Allaah. Kisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: ”Atakayeapa kwa ajili ya kuchukua ardhi ya Muislamu (bila haki) hali ya kuwa ni muongo katika kiapo chake, atakutana na Allaah Akiwa Amemghadhibikia.” [Al-Bukhaariy].
Na pia imeteremka kwa mtu mmoja ambaye aliisimamisha bidhaa yake sokoni kisha akaapa juu hiyo bidhaa kuwa amekwishapewa thamani kubwa kwenye hiyo bidhaa zaidi ya hiyo anayotaka kupewa, hali ya kuwa hajapewa thamani hiyo, na aliapa kiapo hicho ili amshawishi mmoja katika Waislamu ainunue hiyo bidhaa, hapo ikateremka hii Aayah [Amehadithia Ibn Abiy Awfaa (رضي الله عنه) ameipokea Al-Bukhaariy].
[10] Al-Hukma ni hukumu, mamlaka, ufakihi wa shariy’ah n.k.
[11] Aayah hii ni miongoni mwa dalili za kufariki kwa Khidhwr (عليه السلام) na kuwa yeye amekwishakufa na si kama wanavyodai Masufi kuwa Khidhwr yupo hai, na lau kama angelikuwa yupo hai basi angesimama kumnusuru Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa kauli na matendo.
[12] Al-Asbaatw: Ni makabila yaliyotokana na wana kumi na mbili wa Nabiy Ya’quwb (عليه السلام) waliotoka Manabii.
[13] Rejea tanbihi (3: 20) katika Suwrah hii.
[14] Sababun-Nuzuwl: Aayah hizi (3: 86-89) ziliteremka kuhusu mtu mmoja katika Answaar ambaye alisilimu kisha akaritadi na akaingia katika shirki kisha akajuta kwa hilo tendo lake la kuritadi. Akatuma watu wake ili wamtumie ujimbe wa swali kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kuwa je, hivi anaweza kuleta tawbah kwa tendo lake hilo? Kisha baada ya swali hilo kuulizwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) zikateremka hizo Aayaat, akatumiwa, akasilimu [Amehadithia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) imepokelewa aathaar hii na Ibn Jariyr, na pia imesimuliwa na Ahmad, Ibn Hibbaan na wengineo na ameiwafiki Adh-Dhahabiy na Al-Albaaniy katika Asw-Swahiyhah (3066)].
[15] Sababun-Nuzuwl: Aayah hii imeteremshwa kuhusu watu waliosilimu kisha wakaritadi kisha wakasilimu tena kisha wakaritadi. Wakatuma watu wao kuuilizia kuhusu jambo hili wakamuuliza Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم), kisha hapo ikateremka Aayah hii: “Hakika wale waliokufuru baada ya kuamini kwao kisha wakazidi kukufuru; haitokubaliwa tawbah yao, na hao ndio waliopotoka.” (3: 90) [Amehadithia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما)ameipokea Al-Haafidhw Abuu Bakr Al-Bazzaar – Tafsiyr Ibn Kathiyr].
[16] An-Naasikh Wal-Mansuwkh: Aayah hii imefutwa hukmu yake kwa Aayah “Basi mcheni Allaah muwezavyo” [At-Taghaabun 64: 16].
[17] Hadiyth kadhaa zimetajwa fadhila za Ummah huu wa Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم), rejea tanbihi (2: 213).
[18] Sababun-Nuzuwl: Aayah hii imeteremka kama alivyohadithia Ibn Mas’uwd (رضي الله عنه) kwamba: (Siku moja) Rasuli (صلى الله عليه وآله وسلم) aliichelewesha Swalaah ya ‘Ishaa kisha akatoka kuja kuiswali Masjid akawakuta Maswahaba (رضي الله عنهم)vado wamemsubiri akasema: “Uhakika wa mambo ulivyo hakuna yoyote katika Watu wa Dini hizi anayemdhukuru Allaah katika wakati huu asiyekuwa nyinyi.” Hapo ikateremka Aayah:“Hawako sawa sawa; miongoni mwa Ahlil-Kitaabi…” mpaka mwisho wa Aayah 115.[Hadiyth ya Ibn Mas’uwd ameipokea Al-Imaam Ahmad].
[19] Sababun-Nuzuwl: Aayah hii imeteremka ikiwazungumzia Banuw Salamah na Banuw Haarithah kama alivyohadhithia Jaabir (رضي الله عنه) kwamba: Aayah hii imeteremshwa kuhusu sisi nasi tulikuwa ni makabila mawili; Banuw Haarithah na Banuw Salamah tusingelipenda (kama isingeteremshwa) na Sufyaan kasema: Tusingefurahi kama isingeteremshwa na hali Allaah Anasema: “Na Allaah ni Mlinzi na Msaidizi wao.”[Amehadithia Jaabir (رضي الله عنه) ameipokea Al-Bukhaariy na Muslim].
[20] Faida kuhusu Badr: Wametofautiana ‘Ulamaa katika maana ya jina hili ‘Badr’baadhi yao wamesema ni jina la mtu, na baadhi wamesema ni jina la kisima, na imeitwa kwa jina hilo sehemu hiyo baina ya Makkah na Madiynah na sehemu hiyo iko mbali na Madiynah kwa kilometa 150. Na Allaah ni Mjuzi zaidi.
[21] Sababun-Nuzuwl: Aayah hii imeteremka kama alivyohadithia Ibn ‘Umar (رضي الله عنه) kwamba: Alimsikia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alipoinua kichwa chake kutoka rukuu’ ya Swalaah ya Alfajir: “Allaahumma Rabbanaa Lakal-Hamdu fil-Aakhirah. Kisha akasema: “Allaahumma mlaani fulani na fulani.” Ikateremka: “Si juu yako katika jambo hili; ima Apokee tawbah yao au Awaadhibu, kwani wao ni madhalimu.”(3: 128) [Al-Bukhaariy na wengineo kwa riwayaah nyenginezo].
Na Anas bin Maalik (رضي الله عنه)amehadithia kwamba: Siku ya Uhud, jino la Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) lilivunjika na akachomwa mkuki begani mwake. Damu ikawa inamchirizika usoni mwake akawa anaifuta damu huku akisema: “Vipi watu watafaulu ikiwa wamerowanisha uso wa Nabiy wao kwa damu na hali yeye anawalingaia kwa Allaah?” Hapo ikateremka Aayah hii: “Si juu yako katika jambo hili; ima Apokee tawbah yao au Awaadhibu, kwani wao ni madhalimu.” (3: 128) [At-Tirmidhiy Hadiyth Hasan Swahiyh].
[22] Rejea tanbihi (2:275 – 279).
[23] Faida: Rejea tanbihi (4: 110).
[24] Sababun-Nuzuwl: Aayah hii imeteremka kama alivyohadithia Abuu Twalhah (رضي الله عنه): “Niliinua kichwa changu siku ya Uhud nikawa ninatazama sikuona yeyote katika wao siku hiyo isipokuwa kila mtu alikuwa amesinzia, kila mmoja ameinama chini ya silaha yake ya kujilinda na kujihami katika vita, na hiyo ndiyo kauli ya Allaah: “Kisha Akakuteremshieni amani baada ya dhiki; usingizi unaofunika kundi miongoni mwenu…” [At-Tirmidhiy].
Pia Az-Zubayr amehadithia kwamba: Nilikuwa pamoja na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) wakati khofu ilishadidi (katika vita vya Uhud) na Allaah Akutujaalia usingizi, basi hapakuweko mtu ila alikuwa akisinzia (isipokuwa wanafiki). Wa-Allaahi! Kama kwenye ndoto nilisikia maneno ya Mu’attib bin Qushayr akisema: “Lau tungelikuwa tuna amri yoyote katika jambo basi tusingeliuliwa hapa.” Basi nikayahifadhi, kisha Allaah (تعالى)Akateremsha: “Kisha Akakuteremshieni amani baada ya dhiki; usingizi unaofunika kundi miongoni mwenu…” mpaka kauli Yake:“tusingeliuliwa hapa.” Kutokana na kauli ya Mu’attib bin Qushayr. Akasema: “Lau mngelikuwa majumbani mwenu, bila shaka wangejitokeza wale walioandikiwa kuuwawa kwenye mahali pa kuangukia wafe…” mpaka kauli Yake: “Na Allaah ni Mjuzi kwa yaliyomo vifuani.” [Ameipokea Ibn Raahwayh katika Al-Matwaalib Al-‘Aaliyah, mj. 4, uk. 219].
[25] Fadhila na upole wa Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) umetajwa mare tele katika Qur-aan na Sunnah, na rejea Aayah (9: 128).
[26]Sababun-Nuzuwl: Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) amehadithia kwamba: “Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alituma jeshi, likarejeshewa bendera yake (yaani halikukubaliwa jeshi hilo ‘amali yake hiyo). Kisha akalituma tena likarejeshewa halikukubaliwa ‘amali yake kwa sababu ya khiyaana iliyofanyika ya dhahabu iliyokuwa kubwa mfano wa kichwa cha mbuzi. Ndipo ikateremka: “Na haikuwa (ni tabia) kwa Nabiy yeyote kukhini…” [Mu’jamu Atw-Twabaraaniy].
Pia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) amehadithia kwamba: Aayah hii: “Na haikuwa (ni tabia) kwa Nabiy yeyote kukhini…” imeteremshwa kuhusiana na mahameli jekundu lilopotea siku ya Badr, kisha baadhi ya watu wakasema ameichukua Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم), Wakazidi kuendelea kusema basi Allaah Akateremsha: “Na haikuwa (ni tabia) kwa Nabiy yeyote kukhini (ngawira). “Na yeyote atakayekhini atakuja na kile alichokikhini Siku ya Qiyaamah…” (3: 161) [Ameipokea Abuu Daawuwd, At-Tirmidhiy na akasema Hasan Ghariyb].
[27] Sababun-Nuzuwl: Aayah hii imeteremshwa kuhusu makafiri kutokana na wao kulipiza kisasi ya yale yaliyowasibu katika vita vya Badr. Wakauawa Waislamu sabini siku ya Uhud na yakavunjwa meno ya mbele ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na likavunjwa yai juu ya kichwa chake, na damu zikatirika juu ya uso wake, na hapo ikashuka kauli ya Allaah: “Ulipokusibuni msiba ingawa mliwasibu (maadui) mara mbili yake mlisema: “Umetoka wapi huu?” Sema:…” [Amehadithia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) amepokea Ahmad].
[28] Sababun-Nuzuwl: Jaabir bin ‘Abdillaah(رضي الله عنه) amehadithia kwamba: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikutana nami siku moja akaniambia: “Ee Jaabir! Unanini nakuona una huzuni?” Nikasema: Ee Rasuli wa Allaah! Baba yangu amekufa shahidi na ameacha nyuma madeni na watoto. Akasema: “Je, nikujulishe kuwa Allaah Hajapata kuongea na mtu yeyote sipokuwa nyuma ya pazia? Lakini Amemhuisha baba yako na akazungumza naye moja kwa moja. Akasema: Tamani (lolote) Nikupe! Akasema: Yaa Rabb! Nihuishe (nirudi duniani) ili niuliwe tena kwa ajili Yako! Akasema Rabb (تبارك وتعالى): Nimeshatanguliza kauli kwamba wao hawatorudi tena (maisha ya dunia). Akasema: Yaa Rabb! Basi nifikishie khabari kwa nilioawaacha nyuma. Kisha Allaah Akateremsha: “Na wala usiwadhanie kabisa wale waliouawa katika njia ya Allaah ni wafu, bali wahai, kwa Rabb wao wanaruzukiwa… (3: 169-171) [At-Tirmidhiy, Ibn Maajah, Swahiyh At-Targhiyb (2276), Swahiyh At-Targhiyb(1361)].
[29] Sababun-Nuzuwl: Aayah hii mpaka Aayah 174 (3: 172 – 174) zimeteremka pale Abuu Sufyaan aliporudi Makkah pamoja na washirikina kutoka Uhud wakafika (sehemu inayoitwa) Ar-Rawhaa, wakasema: Hamjamuua Muhammad wala hamkukusanya mateka wanawake. Ole wenu mliyoyatenda! Ikamfikia khabari hii Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akaamrisha jeshi la Waislamuwakatembea mpaka wakafikia Hamraa Al-Asad au Bi-ir Abiy ‘Uyaynah (Sehemu fulani) hapo Allaah (عزّ وجلّ) Akateremsha: “Wale waliomwitikia Allaah na Rasuli baada ya kuwasibu majeraha…” Na Abuu Sufyaan akamwambia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Agano lako msimu wa Badr pale mlipoua watu wetu, ama wale waoga walirejea na ama wale mashujaa walijiandaa kwa vita na biashara na wakaendea na hawakumkuta yeyote; wakafanya biashara. Kisha Allaah (عزّ وجلّ) Akateremsha: “Basi wakarudi na neema kutoka kwa Allaah na fadhila; halijawagusa ovu lolote;… (3: 174) [Atw-Twabaraaniy…].
[30] Sababun-Nuzuwl: Aayah hii imeteremka ikibainisha mabaya aliyokuwa akiyafanyaKa’b bin Al-Ashraf Myahudi alikuwa akimshambulia mno Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na anawashajiisha makafiri wa ki-Quraysh juu ya kumfanyia uadui Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) na walikuwa Mayahudi wakimuudhi Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na Maswahaba zake, kisha Allaah Akamuamrisha Nabiy Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) kusamehe na kuwapuuza hao Mayahudi ndio hapo ikateremka hii Aayah. [Ka’b Ibn Maalik (رضي الله عنه) ameipokea Abuu Daawuwd].
[31] Sababun-Nuzuwl: Aayah hii imeteremka kuhusu wanafiki kama alivyohadithia Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy (رضي الله عنه) kwamba: “Katika zama za Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم), pale alipokuwa anatoka Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kwenda vitani, wanafiki walimkhalifu na kubakia nyuma wasiende vitani, na wakifurahi kwa kubakia kwao nyuma kinyume na (alivyofanya) Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم). Kisha pale alipokuwa anarudi Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) walitoa nyudhuru kwake na wakiapa na wakipenda wasifiwe kwa hayo waliyoyafanya, hapo ikateremka (hii Aayah…)” [Amehadithia Abuu Sai’yd (رضي الله عنه), ameipokea Al-Bukhaariy na Muslim].
Pia, Marwaan alimwambia mlinzi wake, Rafiy’ aende kwa Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) kumwambia: “Ingekuwa kila mtu miongoni mwetu anafurahia kwa aliyoyafanya na kupenda kusifiwa kwa ambayo hakuyatenda, basi ataadhibiwa na sisi tutaadhibiwa.” Ibn ‘Abbaas akasema: Mna nini na Aayah hii? Hakika Aayah hii imeteremshwa kuhusu Ahlul-Kitaab. kisha akasoma Aayah (3: 187):“Na pindi Allaah Alipochukua fungamano la wale waliopewa Kitabu (Allaah Akawaambia): Bila shaka mtakibainisha kwa watu na wala hamtokificha…” (3: 187 Suwrah hii Aal-Imraan) kisha Ibn ‘Abbaas akasoma:“Usiwadhanie kabisa wale wanaofurahia kwa waliyopewa na wanapenda wasifiwe kwa wasiyoyatenda…” kisha akasema: “Waliuzwa jambo (waliokuwa na ujuzi nalo) na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) lakini walimficha ujuzi wake hilo jambo na wakamuambia kinyume cha uhalisia wa hilo jambo, kisha wakaondoka wakifurahia kuwa wamemuongopea wakataka wasifiwe kwa hayo waliyoyaficha.”[Muslim].
[32] Ni Sunnah kuzisoma Aayah kuanzia hiyo mpaka mwisho wa Suwrah anapoamka mtu usiku kuswali (tahajjud).
[33] Sababun-Nuzuwl: Aayah hii imeteremkaalipofariki An-Najaashiy kisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akaamrisha aswaliwe wakatoka katika jangwa wakamswalia. [Al-Bukhaariy na Muslim]. Na kwamba walipomswalia An-Najaashiy baadhi ya watu wakasema “Unamswalia mtumwa wa kihabeshi?” Hapo ikateremka hii Aayah. [Amehadithia Anas na Wahshiy na ‘Abdullaahi bin Az-Zubayr (رضي الله عنهم), imethibiti kwa irsaal kutoka kwa Hasan Al-Baswriy, Ahlul-‘Ilm wanasema kwamkusanyiko wa njia zake hizi inapanda daraja na kufanywa kuwa ni hoja].