An-Nisaa

An-Nisaa

 

  

 النِّسَاء

An-Nisaa: 4

Suwrah hii yote imeteremka Madiynah isipokuwa kauli ya Allaah: “Hakika Allaah Anakuamrisheni kurudisha amana kwa wenyewe” (58)

 

 

 بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

 

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اتَّقُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُم مِّن نَّفْسٍ وَاحِدَةٍ وَخَلَقَ مِنْهَا زَوْجَهَا وَبَثَّ مِنْهُمَا رِجَالًا كَثِيرًا وَنِسَاءً ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ الَّذِي تَسَاءَلُونَ بِهِ وَالْأَرْحَامَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلَيْكُمْ رَقِيبًا﴿١﴾ 

1. Enyi watu! Mcheni Rabb wenu Ambaye Amekuumbeni kutokana na nafsi moja (Aadam) na Akaumba kutoka humo mke wake (Hawwaa) na Akaeneza kutoka hao wawili wanaume na wanawake wengi. Na mcheni Allaah Ambaye Kwake mnaombana (haki zenu kwa kuunga) undugu. Hakika Allaah ni Mwenye kuwachunga daima.

 

 

وَآتُوا الْيَتَامَىٰ أَمْوَالَهُمْ ۖ وَلَا تَتَبَدَّلُوا الْخَبِيثَ بِالطَّيِّبِ ۖ وَلَا تَأْكُلُوا أَمْوَالَهُمْ إِلَىٰ أَمْوَالِكُمْ ۚ إِنَّهُ كَانَ حُوبًا كَبِيرًا﴿٢﴾ 

2. Na wapeni mayatima mali zao, na wala msibadilishe kibaya (chenu) kwa kizuri (chao). Na wala msile mali zao pamoja na mali zenu. Hakika hilo limekuwa ni dhambi kubwa.

 

 

 

وَإِنْ خِفْتُمْ أَلَّا تُقْسِطُوا فِي الْيَتَامَىٰ فَانكِحُوا مَا طَابَ لَكُم مِّنَ النِّسَاءِ مَثْنَىٰ وَثُلَاثَ وَرُبَاعَ ۖ فَإِنْ خِفْتُمْ أَلَّا تَعْدِلُوا فَوَاحِدَةً أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُكُمْ ۚذَٰلِكَ أَدْنَىٰ أَلَّا تَعُولُوا ﴿٣﴾

3. Na mkikhofu kuwa hamtoweza kufanya uadilifu kwa mayatima; basi oeni waliokupendezeni katika wanawake wengine; wawili au watatu au wanne. Lakini mkikhofu kuwa hamtoweza kufanya uadilifu, basi mmoja tu au ambao mikono yenu ya kulia imewamiliki. Hivyo ni karibu zaidi kwamba hamtoelemea kudhulumu.[1]

 

 

وَآتُوا النِّسَاءَ صَدُقَاتِهِنَّ نِحْلَةً ۚ فَإِن طِبْنَ لَكُمْ عَن شَيْءٍ مِّنْهُ نَفْسًا فَكُلُوهُ هَنِيئًا مَّرِيئًا ﴿٤﴾ 

4. Na wapeni wanawake mahari zao kwa maridhawa. Lakini wakitoa chochote wenyewe katika mahari yao kwa khiari zao, basi kuleni kwa kufurahia na kunufaika.

 

 

وَلَا تُؤْتُوا السُّفَهَاءَ أَمْوَالَكُمُ الَّتِي جَعَلَ اللَّـهُ لَكُمْ قِيَامًا وَارْزُقُوهُمْ فِيهَا وَاكْسُوهُمْ وَقُولُوا لَهُمْ قَوْلًا مَّعْرُوفًا﴿٥﴾ 

5. Wala msiwape wasiokomaa kiakili mali yenu ambayo Allaah Ameijaalia kuwa ni kisaidizi chenu cha maisha, na walisheni humo na wavisheni na waambieni maneno ya haki na kwa huruma.

 

 

وَابْتَلُوا الْيَتَامَىٰ حَتَّىٰ إِذَا بَلَغُوا النِّكَاحَ فَإِنْ آنَسْتُم مِّنْهُمْ رُشْدًا فَادْفَعُوا إِلَيْهِمْ أَمْوَالَهُمْ ۖ وَلَا تَأْكُلُوهَا إِسْرَافًا وَبِدَارًا أَن يَكْبَرُوا ۚ وَمَن كَانَ غَنِيًّا فَلْيَسْتَعْفِفْ ۖ وَمَن كَانَ فَقِيرًا فَلْيَأْكُلْ بِالْمَعْرُوفِ ۚ فَإِذَا دَفَعْتُمْ إِلَيْهِمْ أَمْوَالَهُمْ فَأَشْهِدُوا عَلَيْهِمْ ۚ وَكَفَىٰ بِاللَّـهِ حَسِيبًا ﴿٦﴾

6. Na wajaribuni mayatima (akili zao) mpaka wakifikia umri wa kuoa. Na mkihisi kupevuka kwao, basi wapeni mali zao. Wala msiile kwa israfu na pupa kwa kuwa watakuja kuwa watu wazima. Na aliyekuwa tajiri basi ajizuilie (kuchukua ujira); na aliyekuwa fakiri basi ale kwa kadiri ya kukubalika ki-shariy’ah. Mtapowapa mali zao washuhudizeni. Na Allaah Anatosheleza kuwa Mwenye kuhisabu.[2]

 

 

لِّلرِّجَالِ نَصِيبٌ مِّمَّا تَرَكَ الْوَالِدَانِ وَالْأَقْرَبُونَ وَلِلنِّسَاءِ نَصِيبٌ مِّمَّا تَرَكَ الْوَالِدَانِ وَالْأَقْرَبُونَ مِمَّا قَلَّ مِنْهُ أَوْ كَثُرَ ۚ نَصِيبًا مَّفْرُوضًا ﴿٧﴾

7. Wanaume wana fungu katika yale waliyoacha wazazi na jamaa wa karibu. Na wanawake wana fungu katika yale waliyoacha wazazi na jamaa wa karibu, ikiwa ni kidogo au kingi; ni mgao uliofaridhishwa.

 

 

 وَإِذَا حَضَرَ الْقِسْمَةَ أُولُو الْقُرْبَىٰ وَالْيَتَامَىٰ وَالْمَسَاكِينُ فَارْزُقُوهُم مِّنْهُ وَقُولُوا لَهُمْ قَوْلًا مَّعْرُوفًا ﴿٨﴾

8. Na wakati wa kugawa, wakihudhuria jamaa wa karibu na mayatima na masikini, basi wapeni kitu katika hayo na wasemezeni kauli ifaayo ya haki na kwa huruma.

 

 

وَلْيَخْشَ الَّذِينَ لَوْ تَرَكُوا مِنْ خَلْفِهِمْ ذُرِّيَّةً ضِعَافًا خَافُوا عَلَيْهِمْ فَلْيَتَّقُوا اللَّـهَ وَلْيَقُولُوا قَوْلًا سَدِيدًا ﴿٩﴾ 

9. Na waogope (wasimamizi kukhini) wale ambao lau nao wangeliacha nyuma yao dhuriya dhaifu wangeliwakhofia; basi wamche Allaah na waseme kauli iliyo sawa ya haki.

 

 

 إِنَّ الَّذِينَ يَأْكُلُونَ أَمْوَالَ الْيَتَامَىٰ ظُلْمًا إِنَّمَا يَأْكُلُونَ فِي بُطُونِهِمْ نَارًا ۖوَسَيَصْلَوْنَ سَعِيرًا ﴿١٠﴾

10. Hakika wale wanaokula mali ya mayatima kwa dhulma hapana shaka kwamba wanakula katika matumbo yao moto, na watauingia moto uliowashwa vikali mno.

 

 

يُوصِيكُمُ اللَّـهُ فِي أَوْلَادِكُمْ ۖ لِلذَّكَرِ مِثْلُ حَظِّ الْأُنثَيَيْنِ ۚ فَإِن كُنَّ نِسَاءً فَوْقَ اثْنَتَيْنِ فَلَهُنَّ ثُلُثَا مَا تَرَكَ ۖ وَإِن كَانَتْ وَاحِدَةً فَلَهَا النِّصْفُ ۚ وَلِأَبَوَيْهِ لِكُلِّ وَاحِدٍ مِّنْهُمَا السُّدُسُ مِمَّا تَرَكَ إِن كَانَ لَهُ وَلَدٌ ۚ فَإِن لَّمْ يَكُن لَّهُ وَلَدٌ وَوَرِثَهُ أَبَوَاهُ فَلِأُمِّهِ الثُّلُثُ ۚ فَإِن كَانَ لَهُ إِخْوَةٌ فَلِأُمِّهِ السُّدُسُ ۚ مِن بَعْدِ وَصِيَّةٍ يُوصِي بِهَا أَوْ دَيْنٍ ۗ آبَاؤُكُمْ وَأَبْنَاؤُكُمْ لَا تَدْرُونَ أَيُّهُمْ أَقْرَبُ لَكُمْ نَفْعًا ۚ فَرِيضَةً مِّنَ اللَّـهِ ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلِيمًا حَكِيمًا ﴿١١﴾ 

11. Allaah Anakuamrisheni kuhusu watoto wenu. Mwanamume atastahiki mfano wa fungu la wanawake wawili. Na ikiwa wanawake ni zaidi ya wawili basi watastahiki theluthi mbili za alichoacha (maiti). Lakini akiwa mtoto wa kike ni mmoja pekee basi atastahiki nusu, na wazazi wake wawili kila mmoja wao atastahiki sudusi katika alichoacha ikiwa anaye mtoto. Na ikiwa hakuwa na mtoto na wazazi wake wawili ndio warithi wake, basi mama yake atastahiki theluthi moja. Na ikiwa anao ndugu basi mama yake atastahiki sudusi, baada ya kutoa wasia aliousia (maiti) au kulipa deni. Baba zenu na watoto wenu hamjui ni yupi miongoni mwao aliye karibu zaidi kwenu kwa manufaa. Ni shariy’ah kutoka kwa Allaah. Hakika Allaah daima ni Mjuzi wa yote, Mwenye hikmah wa yote.[3]

 

 

وَلَكُمْ نِصْفُ مَا تَرَكَ أَزْوَاجُكُمْ إِن لَّمْ يَكُن لَّهُنَّ وَلَدٌ ۚ فَإِن كَانَ لَهُنَّ وَلَدٌ فَلَكُمُ الرُّبُعُ مِمَّا تَرَكْنَ ۚ مِن بَعْدِ وَصِيَّةٍ يُوصِينَ بِهَا أَوْ دَيْنٍ ۚ وَلَهُنَّ الرُّبُعُ مِمَّا تَرَكْتُمْ إِن لَّمْ يَكُن لَّكُمْ وَلَدٌ ۚ فَإِن كَانَ لَكُمْ وَلَدٌ فَلَهُنَّ الثُّمُنُ مِمَّا تَرَكْتُم ۚ مِّن بَعْدِ وَصِيَّةٍ تُوصُونَ بِهَا أَوْ دَيْنٍ ۗ وَإِن كَانَ رَجُلٌ يُورَثُ كَلَالَةً أَوِ امْرَأَةٌ وَلَهُ أَخٌ أَوْ أُخْتٌ فَلِكُلِّ وَاحِدٍ مِّنْهُمَا السُّدُسُ ۚ فَإِن كَانُوا أَكْثَرَ مِن ذَٰلِكَ فَهُمْ شُرَكَاءُ فِي الثُّلُثِ ۚ مِن بَعْدِ وَصِيَّةٍ يُوصَىٰ بِهَا أَوْ دَيْنٍ غَيْرَ مُضَارٍّ ۚوَصِيَّةً مِّنَ اللَّـهِ ۗ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَلِيمٌ﴿١٢﴾

12. Nanyi mtastahiki nusu katika walichoacha wake zenu ikiwa hawakuwa na mtoto. Na ikiwa wana mtoto, basi mtastahiki robo katika walichoacha, baada ya kutoa wasia waliyousia au kulipa deni. Nao wake zenu watastahiki robo katika mlichoacha ikiwa hamna mtoto. Na ikiwa mna mtoto basi watastahiki thumni katika mlichoacha, baada ya kutoa wasia mliousia au kulipa deni. Na ikiwa mwanamume au mwanamke anayerithiwa hana mtoto wala wazazi, lakini anaye kaka au dada, basi kila mmoja kati yao atastahiki sudusi. Na wakiwa ni wengi ya hivyo basi watashirikiana katika theluthi, baada ya kutoa wasia uliousiwa na kulipwa deni pasipo kuleta dhara. Huu ni wasia kutoka kwa Allaah, na Allaah ni Mjuzi wa yote, Mvumilivu.

 

 

تِلْكَ حُدُودُ اللَّـهِ ۚ وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ يُدْخِلْهُ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا ۚ وَذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ ﴿١٣﴾

13. Hiyo ni mipaka ya Allaah. Na yeyote atakayemtii Allaah na Rasuli Wake Atamuingiza Jannaat zipitazo chini yake mito, watadumu humo, na huko ndiko kufuzu kukubwa.

 

 

وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَيَتَعَدَّ حُدُودَهُ يُدْخِلْهُ نَارًا خَالِدًا فِيهَا وَلَهُ عَذَابٌ مُّهِينٌ ﴿١٤﴾

14. Na yeyote atakayemuasi Allaah na Rasuli Wake na akataadi mipaka Yake Atamuingiza motoni, ni mwenye kudumu humo na atapata adhabu ya kudhalilisha.

 

 

وَاللَّاتِي يَأْتِينَ الْفَاحِشَةَ مِن نِّسَائِكُمْ فَاسْتَشْهِدُوا عَلَيْهِنَّ أَرْبَعَةً مِّنكُمْ ۖ فَإِن شَهِدُوا فَأَمْسِكُوهُنَّ فِي الْبُيُوتِ حَتَّىٰ يَتَوَفَّاهُنَّ الْمَوْتُ أَوْ يَجْعَلَ اللَّـهُ لَهُنَّ سَبِيلًا ﴿١٥﴾

15. Na wale wanaofanya uchafu miongoni mwa wanawake wenu, basi washuhudisheni mashahidi wanne kati yenu. Na wakishuhudia basi wazuieni majumbani mpaka mauti yawafishe au Allaah Awajaalie njia (nyingine).[4]

 

 

وَاللَّذَانِ يَأْتِيَانِهَا مِنكُمْ فَآذُوهُمَا ۖ فَإِن تَابَا وَأَصْلَحَا فَأَعْرِضُوا عَنْهُمَا ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ تَوَّابًا رَّحِيمًا ﴿١٦﴾ 

16. Na wale wawili wanaofanya huo (uchafu) waadhibuni. Wakitubu na kutengenea basi waacheni. Hakika Allaah ni Mwingi wa kupokea tawbah, Mwenye kurehemu.

 

 

 إِنَّمَا التَّوْبَةُ عَلَى اللَّـهِ لِلَّذِينَ يَعْمَلُونَ السُّوءَ بِجَهَالَةٍ ثُمَّ يَتُوبُونَ مِن قَرِيبٍ فَأُولَـٰئِكَ يَتُوبُ اللَّـهُ عَلَيْهِمْ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ عَلِيمًا حَكِيمًا ﴿١٧﴾

17. Hakika tawbah inayokubaliwa na Allaah ni ya wale wanaofanya uovu kwa ujahili kisha wakatubia haraka, basi hao Allaah Anapokea tawbah yao. Na Allaah ni Mjuzi wa yote, Mwenye hikmah wa yote.

 

 

وَلَيْسَتِ التَّوْبَةُ لِلَّذِينَ يَعْمَلُونَ السَّيِّئَاتِ حَتَّىٰ إِذَا حَضَرَ أَحَدَهُمُ الْمَوْتُ قَالَ إِنِّي تُبْتُ الْآنَ وَلَا الَّذِينَ يَمُوتُونَ وَهُمْ كُفَّارٌ ۚ أُولَـٰئِكَ أَعْتَدْنَا لَهُمْ عَذَابًا أَلِيمًا ﴿١٨﴾ 

18. Lakini tawbah si kwa wale wanaofanya maovu mpaka mauti yanapohudhuria kwa mmoja wao husema: “Hakika mimi sasa nimetubu.” Na wala wale wanaokufa na hali wao ni makafiri. Hao Tumewaandalia adhabu iumizayo.

 

 

 يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا يَحِلُّ لَكُمْ أَن تَرِثُوا النِّسَاءَ كَرْهًا ۖ وَلَا تَعْضُلُوهُنَّ لِتَذْهَبُوا بِبَعْضِ مَا آتَيْتُمُوهُنَّ إِلَّا أَن يَأْتِينَ بِفَاحِشَةٍ مُّبَيِّنَةٍ ۚ وَعَاشِرُوهُنَّ بِالْمَعْرُوفِ ۚ فَإِن كَرِهْتُمُوهُنَّ فَعَسَىٰ أَن تَكْرَهُوا شَيْئًا وَيَجْعَلَ اللَّـهُ فِيهِ خَيْرًا كَثِيرًا ﴿١٩﴾

19. Enyi walioamini! Si halali kwenu kurithi wanawake kwa kuwakirihisha. Na wala msiwazuie kwa inda ili mpokonye baadhi ya vile mlivyowapa isipokuwa wakiwa wamefanya uchafu bayana. Na kaeni nao kwa wema. Na mkiwachukia, basi asaa ikiwa mnachukia jambo na Allaah Akalijaalia kuwa lenye khayr nyingi.[5]

 

 

وَإِنْ أَرَدتُّمُ اسْتِبْدَالَ زَوْجٍ مَّكَانَ زَوْجٍ وَآتَيْتُمْ إِحْدَاهُنَّ قِنطَارًا فَلَا تَأْخُذُوا مِنْهُ شَيْئًا ۚ أَتَأْخُذُونَهُ بُهْتَانًا وَإِثْمًا مُّبِينًا ﴿٢٠﴾

20. Na mkitaka kubadilisha mke mahali pa mke, na mmempa mmoja wao mirundi ya mali, basi msichukue humo chochote. Je, mnakichukua kwa dhulma na dhambi iliyo bayana?

 

 

وَكَيْفَ تَأْخُذُونَهُ وَقَدْ أَفْضَىٰ بَعْضُكُمْ إِلَىٰ بَعْضٍ وَأَخَذْنَ مِنكُم مِّيثَاقًا غَلِيظًا ﴿٢١﴾

21. Na mtachukuaje na hali nyinyi kwa nyinyi mmeingiliana, na wao wanawake wakapokea kwenu fungamano thabiti?

 

 

وَلَا تَنكِحُوا مَا نَكَحَ آبَاؤُكُم مِّنَ النِّسَاءِ إِلَّا مَا قَدْ سَلَفَ ۚ إِنَّهُ كَانَ فَاحِشَةً وَمَقْتًا وَسَاءَ سَبِيلًا ﴿٢٢﴾

22. Na wala msiwaoe wanawake waliowaoa baba zenu isipokuwa yaliyokwisha pita. Hakika hayo yalikuwa ni uchafu na chukizo na njia ovu.[6]

 

 

حُرِّمَتْ عَلَيْكُمْ أُمَّهَاتُكُمْ وَبَنَاتُكُمْ وَأَخَوَاتُكُمْ وَعَمَّاتُكُمْ وَخَالَاتُكُمْ وَبَنَاتُ الْأَخِ وَبَنَاتُ الْأُخْتِ وَأُمَّهَاتُكُمُ اللَّاتِي أَرْضَعْنَكُمْ وَأَخَوَاتُكُم مِّنَ الرَّضَاعَةِ وَأُمَّهَاتُ نِسَائِكُمْ وَرَبَائِبُكُمُ اللَّاتِي فِي حُجُورِكُم مِّن نِّسَائِكُمُ اللَّاتِي دَخَلْتُم بِهِنَّ فَإِن لَّمْ تَكُونُوا دَخَلْتُم بِهِنَّ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ وَحَلَائِلُ أَبْنَائِكُمُ الَّذِينَ مِنْ أَصْلَابِكُمْ وَأَن تَجْمَعُوا بَيْنَ الْأُخْتَيْنِ إِلَّا مَا قَدْ سَلَفَ ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿٢٣﴾

23. Mmeharamishiwa (kuwaoa) mama zenu, na mabinti zenu, na dada zenu, na shangazi zenu, na makhalati zenu (mama wakubwa na wadogo), na mabinti wa kaka, na mabinti wa dada, na mama zenu ambao wamekunyonyesheni, na ndugu zenu kwa kunyonya, na mama wa wake zenu, na watoto wenu wa kambo walio katika ulinzi wenu waliozaliwa na wake zenu ambao mmewaingilia. Lakini ikiwa hamkuwaingilia basi hakuna dhambi (kuwaoa). Na (mmeharamishwa) wake wa watoto wenu waliotoka katika migongo yenu, na kuwaoa dada wawili kwa wakati mmoja, isipokuwa yaliyokwisha pita. Hakika Allaah daima ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu.

 

 

 

وَالْمُحْصَنَاتُ مِنَ النِّسَاءِ إِلَّا مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُكُمْ ۖ كِتَابَ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ ۚ وَأُحِلَّ لَكُم مَّا وَرَاءَ ذَٰلِكُمْ أَن تَبْتَغُوا بِأَمْوَالِكُم مُّحْصِنِينَ غَيْرَ مُسَافِحِينَ ۚفَمَا اسْتَمْتَعْتُم بِهِ مِنْهُنَّ فَآتُوهُنَّ أُجُورَهُنَّ فَرِيضَةً ۚ وَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ فِيمَا تَرَاضَيْتُم بِهِ مِن بَعْدِ الْفَرِيضَةِ ۚإِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلِيمًا حَكِيمًا ﴿٢٤﴾

24. Na (Mmeharamishiwa pia) wanawake walio katika ndoa isipokuwa iliyowamiliki mikono yenu ya kuume. Ni shariy’ah ya Allaah kwenu. Na mmehalalishiwa wengineo wasiokuwa hao, mtafute (kuwaoa) kwa mali zenu mkijistahi pasi na kuzini. Basi mliostarehe nao, wapeni mahari yao kuwa ni waajib. Na wala si dhambi kwenu katika mliyoridhiana baada ya yaliyowajibika. Hakika Allaah daima ni Mjuzi wa yote, Mwenye hikmah wa yote.[7]

 

 

 

 

وَمَن لَّمْ يَسْتَطِعْ مِنكُمْ طَوْلًا أَن يَنكِحَ الْمُحْصَنَاتِ الْمُؤْمِنَاتِ فَمِن مَّا مَلَكَتْ أَيْمَانُكُم مِّن فَتَيَاتِكُمُ الْمُؤْمِنَاتِ ۚوَاللَّـهُ أَعْلَمُ بِإِيمَانِكُم ۚ بَعْضُكُم مِّن بَعْضٍ ۚ فَانكِحُوهُنَّ بِإِذْنِ أَهْلِهِنَّ وَآتُوهُنَّ أُجُورَهُنَّ بِالْمَعْرُوفِ مُحْصَنَاتٍ غَيْرَ مُسَافِحَاتٍ وَلَا مُتَّخِذَاتِ أَخْدَانٍ ۚ فَإِذَا أُحْصِنَّ فَإِنْ أَتَيْنَ بِفَاحِشَةٍ فَعَلَيْهِنَّ نِصْفُ مَا عَلَى الْمُحْصَنَاتِ مِنَ الْعَذَابِ ۚ ذَٰلِكَ لِمَنْ خَشِيَ الْعَنَتَ مِنكُمْ ۚ وَأَن تَصْبِرُوا خَيْرٌ لَّكُمْ ۗ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٢٥﴾

25. Na asiyeweza kati yenu kupata mali ya kuolea wanawake Waumini walio huru, basi (aoe) katika wale iliyomiliki mikono yenu ya kulia miongoni mwa wajakazi wenu Waumini. Na Allaah Anajua zaidi iymaan yenu. Nyinyi kwa nyinyi. Basi waoeni kwa idhini ya watu wao na wapeni mahari yao kwa ada inayokubalika, wawe wanawake wanaojistiri na machafu si makahaba na wala si wenye kuchukua hawara. Na watakapohifadhiwa katika ndoa, kisha wakafanya uchafu basi adhabu yao itakuwa ni nusu ya adhabu ya waliyowekewa wanawake walio huru (wasioolewa). Hayo ni kwa yule anayeogopa dhambi ya zinaa miongoni mwenu. Na mkisubiri ni khayr kwenu. Na Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu.

 

 

 

يُرِيدُ اللَّـهُ لِيُبَيِّنَ لَكُمْ وَيَهْدِيَكُمْ سُنَنَ الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ وَيَتُوبَ عَلَيْكُمْ ۗوَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ ﴿٢٦﴾

26. Allaah Anataka kukubainishieni na kukuongozeni nyendo za wale walio kabla yenu, na Apokee tawbah kwenu. Na Allaah ni Mjuzi wa yote, Mwenyehikmah wa yote.

 

 

وَاللَّـهُ يُرِيدُ أَن يَتُوبَ عَلَيْكُمْ وَيُرِيدُ الَّذِينَ يَتَّبِعُونَ الشَّهَوَاتِ أَن تَمِيلُوا مَيْلًا عَظِيمًا ﴿٢٧﴾

27. Na Allaah Anataka kupokea tawbah kwenu; na wale wanaofuata matamanio wanataka mkengeuke, mkengeuko mkubwa mno.

 

 

يُرِيدُ اللَّـهُ أَن يُخَفِّفَ عَنكُمْ ۚ وَخُلِقَ الْإِنسَانُ ضَعِيفًا ﴿٢٨﴾

28. Allaah Anataka kukukhafifishieni (tabu zenu); kwani insani ameumbwa dhaifu. 

 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَأْكُلُوا أَمْوَالَكُم بَيْنَكُم بِالْبَاطِلِ إِلَّا أَن تَكُونَ تِجَارَةً عَن تَرَاضٍ مِّنكُمْ ۚ وَلَا تَقْتُلُوا أَنفُسَكُمْ ۚإِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِكُمْ رَحِيمًا ﴿٢٩﴾

29. Enyi walioamini! Msiliane mali zenu kwa ubatilifu, isipokuwa iwe biashara kwa kuridhiana baina yenu. Wala msijiue. Hakika Allaah ni Mwenye kuwarehemuni.

 

 

وَمَن يَفْعَلْ ذَٰلِكَ عُدْوَانًا وَظُلْمًا فَسَوْفَ نُصْلِيهِ نَارًا ۚ وَكَانَ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرًا ﴿٣٠﴾

30. Na atakayefanya hivyo kwa uadui na dhulma, basi Tutamuingiza motoni. Na hilo kwa Allaah ni mepesi. 

 

 

إِن تَجْتَنِبُوا كَبَائِرَ مَا تُنْهَوْنَ عَنْهُ نُكَفِّرْ عَنكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَنُدْخِلْكُم مُّدْخَلًا كَرِيمًا ﴿٣١﴾

31. Mkijiepusha na madhambi makubwa mnayokatazwa Tutakufutieni madhambi yenu madogo na Tutakuingizeni katika mahali patukufu.[8]

 

 

وَلَا تَتَمَنَّوْا مَا فَضَّلَ اللَّـهُ بِهِ بَعْضَكُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ ۚ لِّلرِّجَالِ نَصِيبٌ مِّمَّا اكْتَسَبُوا ۖ وَلِلنِّسَاءِ نَصِيبٌ مِّمَّا اكْتَسَبْنَ ۚ وَاسْأَلُوا اللَّـهَ مِن فَضْلِهِ ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمًا ﴿٣٢﴾

32. Wala msitamani ambayo Allaah Amewafadhilisha baadhi yenu kuliko wengine. Wanaume wanayo sehemu katika waliyoyachuma, na wanawake wana sehemu katika waliyoyachuma. Na muombeni Allaah fadhila Zake. Hakika Allaah daima ni Mjuzi wa kila kitu.

 

 

 

وَلِكُلٍّ جَعَلْنَا مَوَالِيَ مِمَّا تَرَكَ الْوَالِدَانِ وَالْأَقْرَبُونَ ۚ وَالَّذِينَ عَقَدَتْ أَيْمَانُكُمْ فَآتُوهُمْ نَصِيبَهُمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدًا ﴿٣٣﴾

33. Na kila mmoja Tumemuwekea warithi katika yale waliyoyaacha wazazi wawili na jamaa wa karibu. Na wale mliofungamana nao viapo (vya undugu) basi wapeni fungu lao. Hakika Allaah daima ni Shahidi juu ya kila kitu.[9]

 

 

الرِّجَالُ قَوَّامُونَ عَلَى النِّسَاءِ بِمَا فَضَّلَ اللَّـهُ بَعْضَهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ وَبِمَا أَنفَقُوا مِنْ أَمْوَالِهِمْ ۚ فَالصَّالِحَاتُ قَانِتَاتٌ حَافِظَاتٌ لِّلْغَيْبِ بِمَا حَفِظَ اللَّـهُ ۚ وَاللَّاتِي تَخَافُونَ نُشُوزَهُنَّ فَعِظُوهُنَّ وَاهْجُرُوهُنَّ فِي الْمَضَاجِعِ وَاضْرِبُوهُنَّ ۖ فَإِنْ أَطَعْنَكُمْ فَلَا تَبْغُوا عَلَيْهِنَّ سَبِيلًا ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلِيًّا كَبِيرًا ﴿٣٤﴾

34. Wanaume ni wasimamizi juu ya wanawake kwa kuwa Allaah Amefadhilisha baadhi yao kuliko wengine na pia kwa ambayo wanatoa katika mali zao. Basi wanawake wema ni wale watiifu wenye kujihifadhi katika hali ya kutokuweko waume zao kwa kuwa Allaah Ameamrisha wajihifadhi. Na wale ambao mnakhofu uasi wao wa ndoa, basi wanasihini na wahameni katika malazi na wapigeni (kipigo kisichodhuru). Wakikutiini, basi msitafute njia dhidi yao (ya kuwaudhi). Hakika Allaah daima ni Mwenye Uluwa, Mkubwa wa dhati, vitendo na sifa.[10]

 

 

وَإِنْ خِفْتُمْ شِقَاقَ بَيْنِهِمَا فَابْعَثُوا حَكَمًا مِّنْ أَهْلِهِ وَحَكَمًا مِّنْ أَهْلِهَا إِن يُرِيدَا إِصْلَاحًا يُوَفِّقِ اللَّـهُ بَيْنَهُمَا ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلِيمًا خَبِيرًا ﴿٣٥﴾

35. Na mkikhofu mafarikiano baina yao wawili, basi pelekeni mwamuzi kutoka watu wa mume na mwamuzi kutoka watu mke. Wakitaka sulhu Allaah Atawawafikisha baina yao. Hakika Allaah daima ni Mjuzi wa yote, Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika.

 

 

وَاعْبُدُوا اللَّـهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا ۖوَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا وَبِذِي الْقُرْبَىٰ وَالْيَتَامَىٰ وَالْمَسَاكِينِ وَالْجَارِ ذِي الْقُرْبَىٰ وَالْجَارِ الْجُنُبِ وَالصَّاحِبِ بِالْجَنبِ وَابْنِ السَّبِيلِ وَمَا مَلَكَتْ أَيْمَانُكُمْ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُحِبُّ مَن كَانَ مُخْتَالًا فَخُورًا ﴿٣٦﴾

36. Na mwabuduni Allaah na wala msimshirikishe na chochote. Na wafanyieni ihsaan wazazi wawili na jamaa wa karibu, na mayatima, na masikini na jirani mwenye ujamaa na jirani asiye na ujamaa na rafiki wa karibu, na msafiri aliyeishiwa masurufu, na wale iliyowamiliki mikono yenu ya kulia. Hakika Allaah Hapendi mwenye majivuno mwenyekujifakharisha.

 

 

الَّذِينَ يَبْخَلُونَ وَيَأْمُرُونَ النَّاسَ بِالْبُخْلِ وَيَكْتُمُونَ مَا آتَاهُمُ اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ ۗ وَأَعْتَدْنَا لِلْكَافِرِينَ عَذَابًا مُّهِينًا﴿٣٧﴾

37. Wale wanaofanya ubakhili na wanawaamrisha watu ubakhili na wanaficha Aliyowapa Allaah katika fadhila Zake. Na Tumewaandalia makafiri adhabu ya kudhalilisha. 

 

 

وَالَّذِينَ يُنفِقُونَ أَمْوَالَهُمْ رِئَاءَ النَّاسِ وَلَا يُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَلَا بِالْيَوْمِ الْآخِرِ ۗوَمَن يَكُنِ الشَّيْطَانُ لَهُ قَرِينًا فَسَاءَ قَرِينًا ﴿٣٨﴾

38. Na wale wanaotoa mali zao kwa kujionyesha kwa watu na wala hawamwamini Allaah wala Siku ya Mwisho. Na yule ambaye shaytwaan amekuwa ni rafiki yake mwandani, basi mbaya alioje rafiki mwandani (huyo).

 

 

وَمَاذَا عَلَيْهِمْ لَوْ آمَنُوا بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَأَنفَقُوا مِمَّا رَزَقَهُمُ اللَّـهُ ۚ وَكَانَ اللَّـهُ بِهِمْ عَلِيمًا ﴿٣٩﴾

39. Na ingekuwa nini juu yao lau wangelimwamini Allaah na Siku ya Mwisho na wakatoa katika yale Aliyowaruzuku Allaah. Na Allaah ni Mwenye kuwajua vyema. 

 

 

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَظْلِمُ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ ۖ وَإِن تَكُ حَسَنَةً يُضَاعِفْهَا وَيُؤْتِ مِن لَّدُنْهُ أَجْرًا عَظِيمًا ﴿٤٠﴾

40. Hakika Allaah Hadhulumu hata uzito au chembe (au sisimizi). Na ikiwa ni ‘amali njema Huizidisha na Hutoa kutoka Kwake ujira adhimu. 

 

 

فَكَيْفَ إِذَا جِئْنَا مِن كُلِّ أُمَّةٍ بِشَهِيدٍ وَجِئْنَا بِكَ عَلَىٰ هَـٰؤُلَاءِ شَهِيدًا ﴿٤١﴾

41. Basi itakuwaje Tutakapoleta kutoka kila Ummah shahidi, na Tukakuleta (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kuwa shahidi juu ya hawa?

 

 

 

يَوْمَئِذٍ يَوَدُّ الَّذِينَ كَفَرُوا وَعَصَوُا الرَّسُولَ لَوْ تُسَوَّىٰ بِهِمُ الْأَرْضُ وَلَا يَكْتُمُونَ اللَّـهَ حَدِيثًا ﴿٤٢﴾

42. Siku hiyo wale waliokufuru na wakamuasi Rasuli watatamani lau ardhi isawazishwe juu yao. Na wala hawatoweza kumficha Allaah kauli hata moja. 

 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَقْرَبُوا الصَّلَاةَ وَأَنتُمْ سُكَارَىٰ حَتَّىٰ تَعْلَمُوا مَا تَقُولُونَ وَلَا جُنُبًا إِلَّا عَابِرِي سَبِيلٍ حَتَّىٰ تَغْتَسِلُوا ۚ وَإِن كُنتُم مَّرْضَىٰ أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ أَوْ جَاءَ أَحَدٌ مِّنكُم مِّنَ الْغَائِطِ أَوْ لَامَسْتُمُ النِّسَاءَ فَلَمْ تَجِدُوا مَاءً فَتَيَمَّمُوا صَعِيدًا طَيِّبًا فَامْسَحُوا بِوُجُوهِكُمْ وَأَيْدِيكُمْ ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَفُوًّا غَفُورًا ﴿٤٣﴾

43. Enyi walioamini! Msikaribie Swalaah na hali mmelewa mpaka mjue mnayoyasema, na wala mkiwa mna janaba isipokuwa mmo safarini mpaka muoge josho. Na mkiwa wagonjwa au safarini au mmoja wenu ametoka msalani au mmewagusa wanawake kisha hamkupata maji, basi mtayammam (ikusudieni) ardhi safi ya mchanga, pakeni nyuso zenu na mikono yenu. Hakika Allaah daima ni Mwingi wa kusamehe, Mwingi wa kughufuria.[11]

 

 

 

أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ أُوتُوا نَصِيبًا مِّنَ الْكِتَابِ يَشْتَرُونَ الضَّلَالَةَ وَيُرِيدُونَ أَن تَضِلُّوا السَّبِيلَ ﴿٤٤﴾

44. Je, huoni wale waliopewa sehemu ya Kitabu wanakhiari upotofu na wanataka mpotee njia?

 

 

وَاللَّـهُ أَعْلَمُ بِأَعْدَائِكُمْ ۚ وَكَفَىٰ بِاللَّـهِ وَلِيًّا وَكَفَىٰ بِاللَّـهِ نَصِيرًا ﴿٤٥﴾

45. Na Allaah Anawajua zaidi maadui zenu, na Allaah Anatosha kuwa Mlinzi Msimamizi na Allaah Anatosha kuwa Mwenye kunusuru. 

 

 

مِّنَ الَّذِينَ هَادُوا يُحَرِّفُونَ الْكَلِمَ عَن مَّوَاضِعِهِ وَيَقُولُونَ سَمِعْنَا وَعَصَيْنَا وَاسْمَعْ غَيْرَ مُسْمَعٍ وَرَاعِنَا لَيًّا بِأَلْسِنَتِهِمْ وَطَعْنًا فِي الدِّينِ ۚ وَلَوْ أَنَّهُمْ قَالُوا سَمِعْنَا وَأَطَعْنَا وَاسْمَعْ وَانظُرْنَا لَكَانَ خَيْرًا لَّهُمْ وَأَقْوَمَ وَلَـٰكِن لَّعَنَهُمُ اللَّـهُ بِكُفْرِهِمْ فَلَا يُؤْمِنُونَ إِلَّا قَلِيلًا﴿٤٦﴾

46. Katika Mayahudi wako wanaobadilisha maneno kuyatoa mahali pake, na husema: “Tumesikia” na “Tumeasi”; na (wanamwambia Rasuli): “Sikia bila ya kusikilizwa.” Na (husema): “Raa’inaa” kwa kuzipotoa ndimi zao na kutukana Dini. Na lau wangesema: “Tumesikia na tumetii na sikia na “undhwurnaa” ingelikuwa khayr kwao na yenye kufaa zaidi. Lakini Allaah Amewalaani kwa kufru yao; basi hawaamini isipokuwa wachache tu.[12]

 

 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ آمِنُوا بِمَا نَزَّلْنَا مُصَدِّقًا لِّمَا مَعَكُم مِّن قَبْلِ أَن نَّطْمِسَ وُجُوهًا فَنَرُدَّهَا عَلَىٰ أَدْبَارِهَا أَوْ نَلْعَنَهُمْ كَمَا لَعَنَّا أَصْحَابَ السَّبْتِ ۚوَكَانَ أَمْرُ اللَّـهِ مَفْعُولًا ﴿٤٧﴾

47. Enyi mliopewa Kitabu! Aminini yale Tuliyoyateremsha (kwa Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) yanayosadikisha yale mliyonayo, kabla hatujabadilisha nyuso Tukazirudisha kisogoni, auTukawalaani kama Tulivyowalaani watu wa As-Sabt. Na amri ya Allaah ni ya kufanyika tu.[13]

 

 

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدِ افْتَرَىٰ إِثْمًا عَظِيمًا ﴿٤٨﴾

48. Hakika Allaah Haghufurii kushirikishwa; lakini Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakae. Na yeyote atakayemshirikisha Allaah basi kwa yakini amezua dhambi kuu.

 

 

أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ يُزَكُّونَ أَنفُسَهُم ۚ بَلِ اللَّـهُ يُزَكِّي مَن يَشَاءُ وَلَا يُظْلَمُونَ فَتِيلًا ﴿٤٩﴾

49. Je, hukuwaona wale wanaojitakasa nafsi zao? Bali Allaah Humtakasa Amtakaye; na wala hawatodhulumiwa hata kadiri ya uzi katika kokwa ya tende. 

 

 

انظُرْ كَيْفَ يَفْتَرُونَ عَلَى اللَّـهِ الْكَذِبَ ۖوَكَفَىٰ بِهِ إِثْمًا مُّبِينًا ﴿٥٠﴾

50. Tazama vipi wanavyomtungia uongo Allaah; na yatosha haya kuwa dhambi za dhahiri.

 

 

أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ أُوتُوا نَصِيبًا مِّنَ الْكِتَابِ يُؤْمِنُونَ بِالْجِبْتِ وَالطَّاغُوتِ وَيَقُولُونَ لِلَّذِينَ كَفَرُوا هَـٰؤُلَاءِ أَهْدَىٰ مِنَ الَّذِينَ آمَنُوا سَبِيلًا ﴿٥١﴾

51. Je, huwaoni wale waliopewa sehemu ya Kitabu wanaamini itikadi potofu na twaghuti na wanasema juu ya wale waliokufuru kuwa: “Hawa wameongoka zaidi katika njia kuliko wale walioamini.”[14]

 

 

أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ لَعَنَهُمُ اللَّـهُ ۖ وَمَن يَلْعَنِ اللَّـهُ فَلَن تَجِدَ لَهُ نَصِيرًا ﴿٥٢﴾

52. Hao ndio wale Allaah Aliowalaani. Na ambaye Allaah Amemlaani basi hatopata wa kumnusuru.

 

 

أَمْ لَهُمْ نَصِيبٌ مِّنَ الْمُلْكِ فَإِذًا لَّا يُؤْتُونَ النَّاسَ نَقِيرًا ﴿٥٣﴾

53. Au wanayo sehemu ya ufalme (wa Allaah?) basi hapo wasingeliwapa watu kadiri ya kitone cha kokwa ya tende.

 

 

أَمْ يَحْسُدُونَ النَّاسَ عَلَىٰ مَا آتَاهُمُ اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ ۖ فَقَدْ آتَيْنَا آلَ إِبْرَاهِيمَ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَآتَيْنَاهُم مُّلْكًا عَظِيمًا ﴿٥٤﴾

54. Au wanawahusudu watu (NabiyMuhammad صلى الله عليه وآله وسلم na Waumini) kwa yale Aliyowapa Allaah katika fadhila Zake? Basi kwa yakini Tuliwapa kizazi cha Ibraahiym; Kitabu na Hikmah na Tukawapa ufalme adhimu.

 

 

فَمِنْهُم مَّنْ آمَنَ بِهِ وَمِنْهُم مَّن صَدَّ عَنْهُ ۚ وَكَفَىٰ بِجَهَنَّمَ سَعِيرًا ﴿٥٥﴾

55. Basi miongoni mwao wako waliomuamini (Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) na miongoni mwao wako waliomkengeuka. Na Jahannam inatosheleza kuwa ni moto uliowashwa vikali mno.

 

 

إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا بِآيَاتِنَا سَوْفَ نُصْلِيهِمْ نَارًا كُلَّمَا نَضِجَتْ جُلُودُهُم بَدَّلْنَاهُمْ جُلُودًا غَيْرَهَا لِيَذُوقُوا الْعَذَابَ ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَزِيزًا حَكِيمًا﴿٥٦﴾

56. Hakika wale waliokanusha Aayaat (ishara) Zetu Tutawaingiza motoni. Kila ngozi zao zitakapobanikika zikaungua Tutawabadilishia ngozi nyingine ili waionje adhabu. Hakika Allaah daima ni Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote.

 

 

وَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ سَنُدْخِلُهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ۖ لَّهُمْ فِيهَا أَزْوَاجٌ مُّطَهَّرَةٌ ۖ وَنُدْخِلُهُمْ ظِلًّا ظَلِيلًا﴿٥٧﴾

57. Na wale walioamini na wakatenda mema Tutawaingiza Jannaat zipitazo chini yake mito, ni wenye kudumu humo abadi. Watapata humo wake waliotakasika na Tutawaingiza katika vivuli vya kina.

 

 

إِنَّ اللَّـهَ يَأْمُرُكُمْ أَن تُؤَدُّوا الْأَمَانَاتِ إِلَىٰ أَهْلِهَا وَإِذَا حَكَمْتُم بَيْنَ النَّاسِ أَن تَحْكُمُوا بِالْعَدْلِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ نِعِمَّا يَعِظُكُم بِهِ ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ سَمِيعًا بَصِيرًا ﴿٥٨﴾

58. Hakika Allaah Anakuamrisheni kurudisha amana kwa wenyewe. Na mtakapohukumu baina ya watu mhukumu kwa uadilifu. Hakika uzuri ulioje Anayokuwaidhini nayo Allaah; hakika Allaah daima ni Mwenye kusikia yote, Mwenye kuona yote.[15]

 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ ۖفَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا ﴿٥٩﴾

59. Enyi walioamini! Mtiini Allaah na mtiini Rasuli na wenye madaraka katika nyinyi. Mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Allaah na Rasuli mkiwa mnamwamini Allaah na Siku ya Mwisho. Hivyo ni bora na matokeo mazuri zaidi.[16]

 

 

 

أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ يَزْعُمُونَ أَنَّهُمْ آمَنُوا بِمَا أُنزِلَ إِلَيْكَ وَمَا أُنزِلَ مِن قَبْلِكَ يُرِيدُونَ أَن يَتَحَاكَمُوا إِلَى الطَّاغُوتِ وَقَدْ أُمِرُوا أَن يَكْفُرُوا بِهِ وَيُرِيدُ الشَّيْطَانُ أَن يُضِلَّهُمْ ضَلَالًا بَعِيدًا﴿٦٠﴾

60. Je, huoni wale wanaodai kwamba wao wameamini yaliyoteremshwa kwako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) na yale yaliyoteremshwa kabla yako; wanataka wahukumiane kwa twaghuti (ubatilifu) na hali wameamrishwa wakanushe hiyo. Na shaytwaan anataka awapoteze upotofu wa mbali.[17]

 

 

وَإِذَا قِيلَ لَهُمْ تَعَالَوْا إِلَىٰ مَا أَنزَلَ اللَّـهُ وَإِلَى الرَّسُولِ رَأَيْتَ الْمُنَافِقِينَ يَصُدُّونَ عَنكَ صُدُودًا ﴿٦١﴾

61. Na wanapoambiwa: “Njooni kwenye yale Aliyoyateremsha Allaah na kwa Rasuli; utawaona wanafiki wanakugeukilia mbali kwa mkengeuko.

 

 

فَكَيْفَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ بِمَا قَدَّمَتْ أَيْدِيهِمْ ثُمَّ جَاءُوكَ يَحْلِفُونَ بِاللَّـهِ إِنْ أَرَدْنَا إِلَّا إِحْسَانًا وَتَوْفِيقًا﴿٦٢﴾

62. Basi itakuwaje utakapowafika msiba kwa sababu ya yale iliyotanguliza mikono yao? Kisha wakakujia wakiapa “Wa-Allaahi hatukutaka ila mazuri na mapatano.” 

 

 

أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ يَعْلَمُ اللَّـهُ مَا فِي قُلُوبِهِمْ فَأَعْرِضْ عَنْهُمْ وَعِظْهُمْ وَقُل لَّهُمْ فِي أَنفُسِهِمْ قَوْلًا بَلِيغًا ﴿٦٣﴾ 

63. Hao ndio ambao Allaah Anayajua yaliyomo ndani ya nyoyo zao. Basi waachilie mbali na wape mawaidha na uwaambie maneno yatakayofikia kuathiri (nafsi zao). 

 

 

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن رَّسُولٍ إِلَّا لِيُطَاعَ بِإِذْنِ اللَّـهِ ۚ وَلَوْ أَنَّهُمْ إِذ ظَّلَمُوا أَنفُسَهُمْ جَاءُوكَ فَاسْتَغْفَرُوا اللَّـهَ وَاسْتَغْفَرَ لَهُمُ الرَّسُولُ لَوَجَدُوا اللَّـهَ تَوَّابًا رَّحِيمًا﴿٦٤﴾

64. Na Hatukutuma Rasuli yeyote ila atiiwe kwa idhini ya Allaah. Na lau wao pale walipojidhulumu nafsi zao wangelikujia (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) wakamwomba Allaah maghfirah na Rasuli akawaombea maghfirah, basi wangelimkuta Allaah ni Mwingi wa kupokea tawbah, Mwenye kurehemu. 

 

 

 

فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لَا يَجِدُوا فِي أَنفُسِهِمْ حَرَجًا مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُوا تَسْلِيمًا ﴿٦٥﴾

65. Basi Naapa kwa Rabb wako, hawatoamini mpaka wakufanye wewe ni mwamuzi katika yale wanayozozana baina yao, kisha wasipate katika nyoyo zao karaha katika yale uliyohukumu na wajisalimishe, kwa kujisalimisha kikamilifu.[18]

 

 

وَلَوْ أَنَّا كَتَبْنَا عَلَيْهِمْ أَنِ اقْتُلُوا أَنفُسَكُمْ أَوِ اخْرُجُوا مِن دِيَارِكُم مَّا فَعَلُوهُ إِلَّا قَلِيلٌ مِّنْهُمْ ۖ وَلَوْ أَنَّهُمْ فَعَلُوا مَا يُوعَظُونَ بِهِ لَكَانَ خَيْرًا لَّهُمْ وَأَشَدَّ تَثْبِيتًا ﴿٦٦﴾

66. Na lau Tungeliwaandikia amri: “Jiueni nafsi zenu na tokeni katika majumba yenu”; wasingelifanya hayo ila wachache miongoni mwao. Na lau wangelifanya yale waliyowaidhiwa nayo ingelikuwa khayr kwao na uthibitisho wa nguvu zaidi (wa iymaan zao).

 

 

وَإِذًا لَّآتَيْنَاهُم مِّن لَّدُنَّا أَجْرًا عَظِيمًا﴿٦٧﴾

67. Na hapo Tungeliwapa kutoka Kwetu ujira adhimu.

 

 

وَلَهَدَيْنَاهُمْ صِرَاطًا مُّسْتَقِيمًا ﴿٦٨﴾

68. Na Tungewaongoza njia iliyonyooka. 

 

 

وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَالرَّسُولَ فَأُولَـٰئِكَ مَعَ الَّذِينَ أَنْعَمَ اللَّـهُ عَلَيْهِم مِّنَ النَّبِيِّينَ وَالصِّدِّيقِينَ وَالشُّهَدَاءِ وَالصَّالِحِينَ ۚوَحَسُنَ أُولَـٰئِكَ رَفِيقًا ﴿٦٩﴾

69. Na atakayemtii Allaah na Rasuli, basi hao watakuwa pamoja na wale Allaah Aliowaneemesha miongoni mwa Manabii na Swiddiqiyna na Mashuhadaa na Swalihina, na uzuri ulioje kuwa pamoja na hao.[19]

 

 

ذَٰلِكَ الْفَضْلُ مِنَ اللَّـهِ ۚ وَكَفَىٰ بِاللَّـهِ عَلِيمًا ﴿٧٠﴾

70. Hiyo ni fadhila kutoka kwa Allaah. Na inatosheleza Allaah kuwa ni Mjuzi wa yote. 

 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا خُذُوا حِذْرَكُمْ فَانفِرُوا ثُبَاتٍ أَوِ انفِرُوا جَمِيعًا ﴿٧١﴾

71. Enyi walioamini! Shikeni hadhari yenu; tokeni kwa vikosi vikosi au tokeni kwa pamoja. 

 

 

وَإِنَّ مِنكُمْ لَمَن لَّيُبَطِّئَنَّ فَإِنْ أَصَابَتْكُم مُّصِيبَةٌ قَالَ قَدْ أَنْعَمَ اللَّـهُ عَلَيَّ إِذْ لَمْ أَكُن مَّعَهُمْ شَهِيدًا ﴿٧٢﴾

72. Na hakika miongoni mwenu wako wanaobakia nyuma (wasiende vitani); inapokusibuni msiba husema: “Kwa yakini Allaah Amenineemesha nilivyokuwa sikuhudhuria pamoja nao.” 

 

 

وَلَئِنْ أَصَابَكُمْ فَضْلٌ مِّنَ اللَّـهِ لَيَقُولَنَّ كَأَن لَّمْ تَكُن بَيْنَكُمْ وَبَيْنَهُ مَوَدَّةٌ يَا لَيْتَنِي كُنتُ مَعَهُمْ فَأَفُوزَ فَوْزًا عَظِيمًا﴿٧٣﴾

73. Na ikikufikieni fadhila kutoka kwa Allaah husema; kama kwamba hakukuwa baina yenu na yake pendo (husema): “Laiti ningelikuwa pamoja nao nikapata kufuzu mafanikio adhimu.” 

 

 

فَلْيُقَاتِلْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ الَّذِينَ يَشْرُونَ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا بِالْآخِرَةِ ۚ وَمَن يُقَاتِلْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ فَيُقْتَلْ أَوْ يَغْلِبْ فَسَوْفَ نُؤْتِيهِ أَجْرًا عَظِيمًا﴿٧٤﴾

74. Basi wapigane katika njia ya Allaah wale wanaouza uhai (wao) wa dunia kwa Aakhirah. Na atakayepigana katika njia ya Allaah akauliwa au akashinda basi Tutampa ujira adhimu.

 

 

 

وَمَا لَكُمْ لَا تُقَاتِلُونَ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَالْمُسْتَضْعَفِينَ مِنَ الرِّجَالِ وَالنِّسَاءِ وَالْوِلْدَانِ الَّذِينَ يَقُولُونَ رَبَّنَا أَخْرِجْنَا مِنْ هَـٰذِهِ الْقَرْيَةِ الظَّالِمِ أَهْلُهَا وَاجْعَل لَّنَا مِن لَّدُنكَ وَلِيًّا وَاجْعَل لَّنَا مِن لَّدُنكَ نَصِيرًا ﴿٧٥﴾

75. Na mna nini hampigani katika njia ya Allaah, na walio wanyonge kati ya wanaume na wanawake na watoto ambao husema: “Rabb wetu Tutoe kutoka katika mji huu ambao watu wake ni dhalimu, na Tujaalie kutoka Kwako mlinzi na Tujaalie kutoka Kwako mwenye kunusuru. 

 

 

الَّذِينَ آمَنُوا يُقَاتِلُونَ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ ۖوَالَّذِينَ كَفَرُوا يُقَاتِلُونَ فِي سَبِيلِ الطَّاغُوتِ فَقَاتِلُوا أَوْلِيَاءَ الشَّيْطَانِ ۖإِنَّ كَيْدَ الشَّيْطَانِ كَانَ ضَعِيفًا ﴿٧٦﴾

76. Wale walioamini hupigana katika njia ya Allaah. Na wale waliokufuru hupigana katika njia ya twaghuti(kumtii shaytwaan) Basi wapigeni marafiki wandani wa shaytwaan. Hakika hila za shaytwaan daima ni dhaifu.

 

 

أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ قِيلَ لَهُمْ كُفُّوا أَيْدِيَكُمْ وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ فَلَمَّا كُتِبَ عَلَيْهِمُ الْقِتَالُ إِذَا فَرِيقٌ مِّنْهُمْ يَخْشَوْنَ النَّاسَ كَخَشْيَةِ اللَّـهِ أَوْ أَشَدَّ خَشْيَةً ۚ وَقَالُوا رَبَّنَا لِمَ كَتَبْتَ عَلَيْنَا الْقِتَالَ لَوْلَا أَخَّرْتَنَا إِلَىٰ أَجَلٍ قَرِيبٍ ۗ قُلْ مَتَاعُ الدُّنْيَا قَلِيلٌ وَالْآخِرَةُ خَيْرٌ لِّمَنِ اتَّقَىٰ وَلَا تُظْلَمُونَ فَتِيلًا ﴿٧٧﴾

77. Je, huoni wale walioambiwa: “Zuieni mikono yenu (msipigane) na simamisheni Swalaah na toeni Zakaah.” Basi walipoandikiwa amri kupigana, mara kundi miongoni mwao linakhofu watu kama kumkhofu Allaah au khofu zaidi. Na husema: “Rabb wetu! Kwa nini Umetuamrisha kupigana? Lau Ungelituakhirishia hadi muda kidogo hivi!” Sema: “Starehe za dunia ni chache; na Aakhirah ni bora zaidi kwa mwenye kuwa na taqwa; wala hamtodhulumiwa kadiri ya uzi katika kokwa ya tende.”[20]

 

 

أَيْنَمَا تَكُونُوا يُدْرِككُّمُ الْمَوْتُ وَلَوْ كُنتُمْ فِي بُرُوجٍ مُّشَيَّدَةٍ ۗ وَإِن تُصِبْهُمْ حَسَنَةٌ يَقُولُوا هَـٰذِهِ مِنْ عِندِ اللَّـهِ ۖوَإِن تُصِبْهُمْ سَيِّئَةٌ يَقُولُوا هَـٰذِهِ مِنْ عِندِكَ ۚ قُلْ كُلٌّ مِّنْ عِندِ اللَّـهِ ۖ فَمَالِ هَـٰؤُلَاءِ الْقَوْمِ لَا يَكَادُونَ يَفْقَهُونَ حَدِيثًا ﴿٧٨﴾

78. Popote mtakapokuwa yatakufikieni mauti, japo mkiwa katika minara iliyojengwa kifakhari na madhubuti. Na likiwafikia jambo zuri husema: “Hili ni kutoka kwa Allaah.” Na likiwasibu ovu husema: “Hili kutoka kwako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم).” Sema: “Yote ni kutoka kwa Allaah.” Basi wana nini hawa watu hawakaribii kufahamu kauli?

 

 

 

مَّا أَصَابَكَ مِنْ حَسَنَةٍ فَمِنَ اللَّـهِ ۖ وَمَا أَصَابَكَ مِن سَيِّئَةٍ فَمِن نَّفْسِكَ ۚوَأَرْسَلْنَاكَ لِلنَّاسِ رَسُولًا ۚ وَكَفَىٰ بِاللَّـهِ شَهِيدًا ﴿٧٩﴾

79. Zuri lilokufikia ni kutoka kwa Allaah. Na ubaya uliokusibu (ee bin-Aadam) ni kutokana na nafsi yako. Na Tumekutuma (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kwa watu uwe Rasuli na inatosheleza Allaah kuwa ni Mwenye kushuhudia yote. 

 

 

 

مَّن يُطِعِ الرَّسُولَ فَقَدْ أَطَاعَ اللَّـهَ ۖوَمَن تَوَلَّىٰ فَمَا أَرْسَلْنَاكَ عَلَيْهِمْ حَفِيظًا ﴿٨٠﴾

80. Atakayemtii Rasuli basi kwa yakini amemtii Allaah. Na atakayekengeuka basi Hatukukutuma kuwa mlinzi juu yao.

 

 

وَيَقُولُونَ طَاعَةٌ فَإِذَا بَرَزُوا مِنْ عِندِكَ بَيَّتَ طَائِفَةٌ مِّنْهُمْ غَيْرَ الَّذِي تَقُولُ ۖوَاللَّـهُ يَكْتُبُ مَا يُبَيِّتُونَ ۖ فَأَعْرِضْ عَنْهُمْ وَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ ۚ وَكَفَىٰ بِاللَّـهِ وَكِيلًا ﴿٨١﴾

81. Na husema: “Tunatii.” Lakini wanapotoka kutoka kwako, kundi miongoni mwao hukesha kushauriana kinyume na unayoyasema. Na Allaah Anayaandika yale wanayokeshea. Basi waachilie mbali na tawakali kwa Allaah. Na inatosheleza Allaah kuwa Mdhamini Anayetegemewa kwa yote.

 

 

أَفَلَا يَتَدَبَّرُونَ الْقُرْآنَ ۚ وَلَوْ كَانَ مِنْ عِندِ غَيْرِ اللَّـهِ لَوَجَدُوا فِيهِ اخْتِلَافًا كَثِيرًا ﴿٨٢﴾

82. Je, hawaizingatii Qur-aan? Na lau ingelikuwa imetoka kwa asiyekuwa Allaah, bila shaka wangelikuta ndani yake khitilafu nyingi.[21]

 

 

وَإِذَا جَاءَهُمْ أَمْرٌ مِّنَ الْأَمْنِ أَوِ الْخَوْفِ أَذَاعُوا بِهِ ۖ وَلَوْ رَدُّوهُ إِلَى الرَّسُولِ وَإِلَىٰ أُولِي الْأَمْرِ مِنْهُمْ لَعَلِمَهُ الَّذِينَ يَسْتَنبِطُونَهُ مِنْهُمْ ۗ وَلَوْلَا فَضْلُ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَتُهُ لَاتَّبَعْتُمُ الشَّيْطَانَ إِلَّا قَلِيلًا ﴿٨٣﴾

83. Na linapowafikia jambo lolote la amani au la khofu hulitangaza. Na lau wangelirudisha kwa Rasuli na kwa wenye madaraka kati yao, wangelijua wale wanaotafiti wakabainisha ya sahihi miongoni mwao. Na lau si fadhila ya Allaah juu yenu na rahmahYake kwa yakini mngelimfuata shaytwaan ila wachache tu.[22] 

 

 

 

فَقَاتِلْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ لَا تُكَلَّفُ إِلَّا نَفْسَكَ ۚ وَحَرِّضِ الْمُؤْمِنِينَ ۖ عَسَى اللَّـهُ أَن يَكُفَّ بَأْسَ الَّذِينَ كَفَرُوا ۚوَاللَّـهُ أَشَدُّ بَأْسًا وَأَشَدُّ تَنكِيلًا ﴿٨٤﴾

84. Basi pigana (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) katika njia ya Allaah, hukalifishwi ila nafsi yako. Na wahimize Waumini (wakuunge). Asaa Allaah Akazuia mashambulizi ya nguvu ya waliokufuru. Na Allaah ni Mkali zaidi wa kushambulia na Mkali zaidi wa kuadhibu adhabu ya uzindusho. 

 

 

مَّن يَشْفَعْ شَفَاعَةً حَسَنَةً يَكُن لَّهُ نَصِيبٌ مِّنْهَا ۖ وَمَن يَشْفَعْ شَفَاعَةً سَيِّئَةً يَكُن لَّهُ كِفْلٌ مِّنْهَا ۗ وَكَانَ اللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ مُّقِيتًا ﴿٨٥﴾

85. Atakayeombea uombezi mzuri atapata fungu lake katika hayo. Na atakayeombea uombezi mbaya atapata sehemu yake katika hayo. Na Allaah daima ni Mwenye kudhibiti na Mwangalizi wa kila kitu. 

 

 

وَإِذَا حُيِّيتُم بِتَحِيَّةٍ فَحَيُّوا بِأَحْسَنَ مِنْهَا أَوْ رُدُّوهَا ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ حَسِيبًا ﴿٨٦﴾

86. Na mtapoamkiwa kwa maamkizi yoyote, basi itikieni kwa yaliyo mazuri zaidi kuliko hayo au yarudisheni hayo hayo. Hakika Allaah daima ni Mwenye kuhesabu kila kitu.

 

 

اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۚ لَيَجْمَعَنَّكُمْ إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ لَا رَيْبَ فِيهِ ۗ وَمَنْ أَصْدَقُ مِنَ اللَّـهِ حَدِيثًا ﴿٨٧﴾

87. Allaah; hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye. Bila ya shaka Atakukusanyeni Siku ya Qiyaamah haina shaka ndani yake. Na nani mkweli zaidi katika maneno kuliko Allaah?



Endelea Kusoma kwa Kugusa HAPA




Report Page