003-Aal-‘Imraan

003-Aal-‘Imraan

Khamis

Next page 📄 3

 

 وَمَن يَبْتَغِ غَيْرَ الْإِسْلَامِ دِينًا فَلَن يُقْبَلَ مِنْهُ وَهُوَ فِي الْآخِرَةِ مِنَ الْخَاسِرِينَ ﴿٨٥﴾

85. Na yeyote anayetaka dini isiyokuwa ya Kiislamu basi haitokubaliwa kwake, naye katika Aakhirah atakuwa miongoni mwa waliokhasirika.[29]

 

 

كَيْفَ يَهْدِي اللَّـهُ قَوْمًا كَفَرُوا بَعْدَ إِيمَانِهِمْ وَشَهِدُوا أَنَّ الرَّسُولَ حَقٌّ وَجَاءَهُمُ الْبَيِّنَاتُ ۚ وَاللَّـهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ ﴿٨٦﴾ 

86. Vipi Allaah Atawaongoza watu waliokufuru baada ya kuamini kwao na wakashuhudia kwamba Rasuli ni haki na zikawajia hoja bayana? Na Allaah Hawahidi watu madhalimu.

 

 

 أُولَـٰئِكَ جَزَاؤُهُمْ أَنَّ عَلَيْهِمْ لَعْنَةَ اللَّـهِ وَالْمَلَائِكَةِ وَالنَّاسِ أَجْمَعِينَ ﴿٨٧﴾

87. Hao jazaa yao ni kwamba juu yao ipo Laana ya Allaah na ya Malaika na ya watu wote.

 

 

خَالِدِينَ فِيهَا لَا يُخَفَّفُ عَنْهُمُ الْعَذَابُ وَلَا هُمْ يُنظَرُونَ ﴿٨٨﴾

88. Wadumu humo, hawatopunguziwa adhabu wala hawatopewa muda wa kuakhirishwa adhabu.

 

 

إِلَّا الَّذِينَ تَابُوا مِن بَعْدِ ذَٰلِكَ وَأَصْلَحُوا فَإِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٨٩﴾

89. Isipokuwa wale waliotubu baada ya hayo na wakatengeneza, kwani hakika Allaah Ni Mwingi wa Kughufiria, Mwenye Kurehemu.

 

 

إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا بَعْدَ إِيمَانِهِمْ ثُمَّ ازْدَادُوا كُفْرًا لَّن تُقْبَلَ تَوْبَتُهُمْ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الضَّالُّونَ ﴿٩٠﴾ 

90. Hakika wale waliokufuru baada ya kuamini kwao kisha wakazidi kukufuru, haitokubaliwa tawbah yao, na hao ndio waliopotoka.

 

 

 إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا وَمَاتُوا وَهُمْ كُفَّارٌ فَلَن يُقْبَلَ مِنْ أَحَدِهِم مِّلْءُ الْأَرْضِ ذَهَبًا وَلَوِ افْتَدَىٰ بِهِ ۗ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ وَمَا لَهُم مِّن نَّاصِرِينَ ﴿٩١﴾

91. Hakika wale waliokufuru na wakafa nao wakiwa makafiri, basi kamwe haitakubaliwa kutoka kwa mmoja wao, dhahabu ya ujazo wa dunia nzima lau wakitaka kujifidia nayo. Hao watapata adhabu iumizayo na hawatopata watu wa kuwasaidia.

 

 

 لَن تَنَالُوا الْبِرَّ حَتَّىٰ تُنفِقُوا مِمَّا تُحِبُّونَ ۚ وَمَا تُنفِقُوا مِن شَيْءٍ فَإِنَّ اللَّـهَ بِهِ عَلِيمٌ ﴿٩٢﴾

92. Hamtoweza kuufikia wema kamili mpaka mtoe katika vile mnavyovipenda. Na kitu chochote mnachotoa basi hakika Allaah kwacho Ni Mjuzi.

 

 

 كُلُّ الطَّعَامِ كَانَ حِلًّا لِّبَنِي إِسْرَائِيلَ إِلَّا مَا حَرَّمَ إِسْرَائِيلُ عَلَىٰ نَفْسِهِ مِن قَبْلِ أَن تُنَزَّلَ التَّوْرَاةُ ۗ قُلْ فَأْتُوا بِالتَّوْرَاةِ فَاتْلُوهَا إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿٩٣﴾

93. Kila chakula kilikuwa halali kwa wana wa Israaiyl, isipokuwa kile alichojiharamishia Israaiyl[30] (Ya’quwb (عليه السّلام mwenyewe kabla ya kuteremshwa Tawraat. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Basi leteni Tawraat kisha muisome mkiwa wakweli.

 

 

 

فَمَنِ افْتَرَىٰ عَلَى اللَّـهِ الْكَذِبَ مِن بَعْدِ ذَٰلِكَ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ ﴿٩٤﴾

94. Na yeyote atakayemtungia Allaah uongo baada ya hayo, basi hao ndio madhalimu.

 

 

قُلْ صَدَقَ اللَّـهُ ۗ فَاتَّبِعُوا مِلَّةَ إِبْرَاهِيمَ حَنِيفًا وَمَا كَانَ مِنَ الْمُشْرِكِينَ ﴿٩٥﴾

95. Sema: Allaah Amesema kweli. Basi fuateni mila ya Ibraahiym aliyejiengua na upotofu akaelemea Dini ya haki na hakuwa miongoni mwa washirikina.[31]

 

 

إِنَّ أَوَّلَ بَيْتٍ وُضِعَ لِلنَّاسِ لَلَّذِي بِبَكَّةَ مُبَارَكًا وَهُدًى لِّلْعَالَمِينَ ﴿٩٦﴾ 

96. Hakika nyumba (Al-Ka’bah) ya awali iliyowekwa kwa ajili ya watu (kufanya ibaada) ni ile ambayo iko Bakkah (Makkah),[32] yenye barakah na mwongozo kwa walimwengu.

 

 

فِيهِ آيَاتٌ بَيِّنَاتٌ مَّقَامُ إِبْرَاهِيمَ ۖ وَمَن دَخَلَهُ كَانَ آمِنًا ۗ وَلِلَّـهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلًا ۚ وَمَن كَفَرَ فَإِنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ عَنِ الْعَالَمِينَ ﴿٩٧﴾ 

97. Ndani yake kuna Aayaat (Ishara na Dalili) zilizo wazi mahali aliposimama Ibraahiym (kujenga). Na mwenye kuingia humo anakuwa katika amani. Na kwa ajili ya Allaah imewajibika watu watekeleze Hajj katika nyumba (Al-Ka’bah) hiyo kwa mwenye uwezo. Na atakayekufuru, basi hakika Allaah Ni Mkwasi kwa walimwengu.

 

 

قُلْ يَا أَهْلَ الْكِتَابِ لِمَ تَكْفُرُونَ بِآيَاتِ اللَّـهِ وَاللَّـهُ شَهِيدٌ عَلَىٰ مَا تَعْمَلُونَ ﴿٩٨﴾ 

98. Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Kwa nini mnakanusha Aayaat (na Ishara, Miujiza, Dalili) za Allaah ilhali Allaah Ni Shahidi juu ya myatendayo?

 

 

قُلْ يَا أَهْلَ الْكِتَابِ لِمَ تَصُدُّونَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ مَنْ آمَنَ تَبْغُونَهَا عِوَجًا وَأَنتُمْ شُهَدَاءُ ۗ وَمَا اللَّـهُ بِغَافِلٍ عَمَّا تَعْمَلُونَ ﴿٩٩﴾ 

99. Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Kwa nini mnamzuilia aliyeamini Njia ya Allaah, mnaitafutia ionekane kombo na hali nyinyi ni mashahidi (juu ya haki)? Na Allaah Si Mwenye Kughafilika na hayo myatendayo.

 

 

 يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن تُطِيعُوا فَرِيقًا مِّنَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ يَرُدُّوكُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ كَافِرِينَ ﴿١٠٠﴾

100. Enyi walioamini! Mkilitii kundi la waliopewa Kitabu watakurudisheni baada ya nyinyi kuamini muwe makafiri.

 

 

وَكَيْفَ تَكْفُرُونَ وَأَنتُمْ تُتْلَىٰ عَلَيْكُمْ آيَاتُ اللَّـهِ وَفِيكُمْ رَسُولُهُ ۗ وَمَن يَعْتَصِم بِاللَّـهِ فَقَدْ هُدِيَ إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ ﴿١٠١﴾

101. Na vipi mkufuru na hali mnasomewa Aayaat za Allaah na Rasuli Wake yuko kati yenu? Na atakayeshikamana na Allaah basi kwa yakini ameongozwa kuelekea njia iliyonyooka.

 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ حَقَّ تُقَاتِهِ وَلَا تَمُوتُنَّ إِلَّا وَأَنتُم مُّسْلِمُونَ ﴿١٠٢﴾

102. Enyi walioamini! Mcheni Allaah kama ipasavyo kumcha na chungeni sana, angalieni msife isipokuwa nyinyi ni Waislamu.

 

 

وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّـهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا ۚ وَاذْكُرُوا نِعْمَتَ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ إِذْ كُنتُمْ أَعْدَاءً فَأَلَّفَ بَيْنَ قُلُوبِكُمْ فَأَصْبَحْتُم بِنِعْمَتِهِ إِخْوَانًا وَكُنتُمْ عَلَىٰ شَفَا حُفْرَةٍ مِّنَ النَّارِ فَأَنقَذَكُم مِّنْهَا ۗ كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّـهُ لَكُمْ آيَاتِهِ لَعَلَّكُمْ تَهْتَدُونَ ﴿١٠٣﴾ 

103. Na shikamaneni kwa Kamba ya Allaah nyote pamoja, wala msifarikiane.[33] Na kumbukeni Neema ya Allaah juu yenu, pale mlipokuwa maadui (kati yenu), kisha Akaunganisha nyoyo zenu, mkawa ndugu kwa Neema Yake, na mlikuwa ukingoni mwa shimo la moto Akakuokoeni humo. Hivyo ndivyo Allaah Anavyokubainishieni Aayaat (na Ishara) Zake mpate kuhidika.  

 

 

 

وَلْتَكُن مِّنكُمْ أُمَّةٌ يَدْعُونَ إِلَى الْخَيْرِ وَيَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ ۚ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفلِحُونَ ﴿١٠٤﴾

104. Na watokeze kutoka kwenu ummah wa watu unaolingania kheri, na unaoamrisha mema na unaokataza munkari. Na hao ndio waliofaulu.

 

 

وَلَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ تَفَرَّقُوا وَاخْتَلَفُوا مِن بَعْدِ مَا جَاءَهُمُ الْبَيِّنَاتُ ۚ وَأُولَـٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ ﴿١٠٥﴾

105. Na wala msiwe kama wale waliofarikiana na wakakhitilafiana[34]  baada ya kuwajia hoja bayana. Na hao watapata adhabu kuu kabisa.

 

 

 

يَوْمَ تَبْيَضُّ وُجُوهٌ وَتَسْوَدُّ وُجُوهٌ ۚ فَأَمَّا الَّذِينَ اسْوَدَّتْ وُجُوهُهُمْ أَكَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ فَذُوقُوا الْعَذَابَ بِمَا كُنتُمْ تَكْفُرُونَ ﴿١٠٦﴾ 

106. Siku nyuso zitakuwa nyeupe na nyuso (nyingine) zitakuwa nyeusi. Basi wale ambao nyuso zao zitakuwa nyeusi (wataambiwa): Je, mlikufuru baada ya kuamini kwenu?! Basi onjeni adhabu kwa sababu ya yale mliyokuwa mkiyakanusha.

 

 

 وَأَمَّا الَّذِينَ ابْيَضَّتْ وُجُوهُهُمْ فَفِي رَحْمَةِ اللَّـهِ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿١٠٧﴾

107. Na wale ambao nyuso zao zitakuwa nyeupe, basi watakuwa katika Rehma ya Allaah. Wao humo watadumu.

 

 

تِلْكَ آيَاتُ اللَّـهِ نَتْلُوهَا عَلَيْكَ بِالْحَقِّ ۗ وَمَا اللَّـهُ يُرِيدُ ظُلْمًا لِّلْعَالَمِينَ ﴿١٠٨﴾

108. Hizi ni Aayaat za Allaah Tunakusomea kwa haki (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم). Na Allaah Hataki dhulma kwa walimwengu.

 

 

 

وَلِلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۚ وَإِلَى اللَّـهِ تُرْجَعُ الْأُمُورُ ﴿١٠٩﴾

109. Na ni vya Allaah vilivyomo katika mbingu na katika ardhi. Na kwa Allaah Pekee mambo (yote) yatarejeshwa.

 

 

 كُنتُمْ خَيْرَ أُمَّةٍ أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ تَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَتَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَتُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ ۗ وَلَوْ آمَنَ أَهْلُ الْكِتَابِ لَكَانَ خَيْرًا لَّهُم ۚ مِّنْهُمُ الْمُؤْمِنُونَ وَأَكْثَرُهُمُ الْفَاسِقُونَ ﴿١١٠﴾

110. Mmekuwa ummah bora[35] kabisa uliotolewa (mfano) kwa watu, mnaamrisha mema na mnakataza munkari na mnamwamini Allaah. Na lau wangeliamini Watu wa Kitabu, basi ingelikuwa ni bora kwao. Wako miongoni mwao wanaoamini lakini wengi wao ni mafasiki.

 

 

لَن يَضُرُّوكُمْ إِلَّا أَذًى ۖ وَإِن يُقَاتِلُوكُمْ يُوَلُّوكُمُ الْأَدْبَارَ ثُمَّ لَا يُنصَرُونَ ﴿١١١﴾

111. Hawatokudhuruni isipokuwa udhia tu, na wakikupigeni vita watakupeni migongo (wakimbie), kisha hawatonusuriwa.

 

 

ضُرِبَتْ عَلَيْهِمُ الذِّلَّةُ أَيْنَ مَا ثُقِفُوا إِلَّا بِحَبْلٍ مِّنَ اللَّـهِ وَحَبْلٍ مِّنَ النَّاسِ وَبَاءُوا بِغَضَبٍ مِّنَ اللَّـهِ وَضُرِبَتْ عَلَيْهِمُ الْمَسْكَنَةُ ۚ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ كَانُوا يَكْفُرُونَ بِآيَاتِ اللَّـهِ وَيَقْتُلُونَ الْأَنبِيَاءَ بِغَيْرِ حَقٍّ ۚ ذَٰلِكَ بِمَا عَصَوا وَّكَانُوا يَعْتَدُونَ ﴿١١٢﴾ 

112. Wamepigwa na udhalili popote wanapopatikana ila tu pale wanapolindwa na Ahadi ya Allaah na ahadi ya watu, na (pamoja na hayo) wamestahiki ghadhabu kutoka kwa Allaah, na wakapigwa na umasikini. Sababu ya hayo ni kuwa wao walikuwa wakikanusha Aayaat (na Ishara, Dalili) za Allaah na wakiua Manabii pasi na haki. Hayo (pia) ni kwa sababu ya kuasi kwao, na walikuwa wanataadi (kuvuka mipaka).

 

 

لَيْسُوا سَوَاءً ۗ مِّنْ أَهْلِ الْكِتَابِ أُمَّةٌ قَائِمَةٌ يَتْلُونَ آيَاتِ اللَّـهِ آنَاءَ اللَّيْلِ وَهُمْ يَسْجُدُونَ ﴿١١٣﴾

113. Hawako sawa sawa. Miongoni mwa Watu wa Kitabu wako watu wenye kusimama (kwa utiifu), wanasoma Aayaat za Allaah nyakati za usiku na wao wanasujudu (katika Swalaah).

 

 

يُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَيَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَيُسَارِعُونَ فِي الْخَيْرَاتِ وَأُولَـٰئِكَ مِنَ الصَّالِحِينَ ﴿١١٤﴾

114. Wanamwamini Allaah na Siku ya Mwisho, na wanaamrisha mema na wanakataza munkari[36]  na wanakimbilia katika mambo ya kheri, na hao ni miongoni mwa Swalihina.

 

 

وَمَا يَفْعَلُوا مِنْ خَيْرٍ فَلَن يُكْفَرُوهُ ۗ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ بِالْمُتَّقِينَ ﴿١١٥﴾

115. Na kheri yoyote waifanyayo basi hawatokanushiwa (thawabu zake). Na Allaah Anawajua vyema wenye taqwa.

 

 

 

إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا لَن تُغْنِيَ عَنْهُمْ أَمْوَالُهُمْ وَلَا أَوْلَادُهُم مِّنَ اللَّـهِ شَيْئًا ۖ وَأُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ ۚ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿١١٦﴾

116. Hakika wale waliokufuru hazitowafaa kitu mali zao wala watoto wao mbele ya Allaah. Hao ni watu wa motoni. Wao humo watadumu.

 

 

 

مَثَلُ مَا يُنفِقُونَ فِي هَـٰذِهِ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا كَمَثَلِ رِيحٍ فِيهَا صِرٌّ أَصَابَتْ حَرْثَ قَوْمٍ ظَلَمُوا أَنفُسَهُمْ فَأَهْلَكَتْهُ ۚ وَمَا ظَلَمَهُمُ اللَّـهُ وَلَـٰكِنْ أَنفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ ﴿١١٧﴾ 

117. Mfano wa vile wanavyovitoa katika uhai (wao) huu wa duniani ni kama mfano wa upepo ndani yake mna baridi ya barafu, ukasibu shamba lilolimwa la watu waliojidhulumu nafsi zao ukaliangamiza. Na Allaah Hakuwadhulumu lakini wamejidhulumu nafsi zao.

 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَتَّخِذُوا بِطَانَةً مِّن دُونِكُمْ لَا يَأْلُونَكُمْ خَبَالًا وَدُّوا مَا عَنِتُّمْ قَدْ بَدَتِ الْبَغْضَاءُ مِنْ أَفْوَاهِهِمْ وَمَا تُخْفِي صُدُورُهُمْ أَكْبَرُ ۚ قَدْ بَيَّنَّا لَكُمُ الْآيَاتِ ۖ إِن كُنتُمْ تَعْقِلُونَ ﴿١١٨﴾

118. Enyi walioamini! Msifanye rafiki mwandani na msiri (wenu) wasiokuwa nyinyi. Hawatoacha kukuharibieni. Wanatamani kama mngetaabika. Imekwishajitokeza bughudha kutoka midomoni mwao. Na yale yanayoficha vifua vyao ni makubwa zaidi. Tumekwisha kubainishieni Aayaat (Ishara, Dalili, Alama) [zao] mkiwa mtatia akilini.

 

 

هَا أَنتُمْ أُولَاءِ تُحِبُّونَهُمْ وَلَا يُحِبُّونَكُمْ وَتُؤْمِنُونَ بِالْكِتَابِ كُلِّهِ وَإِذَا لَقُوكُمْ قَالُوا آمَنَّا وَإِذَا خَلَوْا عَضُّوا عَلَيْكُمُ الْأَنَامِلَ مِنَ الْغَيْظِ ۚ قُلْ مُوتُوا بِغَيْظِكُمْ ۗ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ بِذَاتِ الصُّدُورِ ﴿١١٩﴾ 

119. Ha! Nyinyi ndio wale mnaowapenda na wala wao hawakupendeni, na mnaamini Kitabu chote, na wanapokukuteni husema: Tumeamini, na wanapokuwa peke yao wanakutafunieni ncha za vidole kutokana na chuki. Sema: Kufeni kwa chuki zenu! Hakika Allaah Anayajua vyema yaliyomo vifuani.

 

 

إِن تَمْسَسْكُمْ حَسَنَةٌ تَسُؤْهُمْ وَإِن تُصِبْكُمْ سَيِّئَةٌ يَفْرَحُوا بِهَا ۖ وَإِن تَصْبِرُوا وَتَتَّقُوا لَا يَضُرُّكُمْ كَيْدُهُمْ شَيْئًا ۗ إِنَّ اللَّـهَ بِمَا يَعْمَلُونَ مُحِيطٌ ﴿١٢٠﴾

120. Ikikupateni kheri (nusura, ushindi) inawachukiza, na likikusibuni baya hulifurahia. Na kama mtasubiri na mkashikamana na taqwa, basi hila zao hazitakudhuruni kitu. Hakika Allaah Ni Mwenye Kuyazunguka wayatendayo. 

 

 

وَإِذْ غَدَوْتَ مِنْ أَهْلِكَ تُبَوِّئُ الْمُؤْمِنِينَ مَقَاعِدَ لِلْقِتَالِ ۗ وَاللَّـهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ ﴿١٢١﴾ 

121. Na pale ulipotoka asubuhi mapema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) ukaacha ahli zako ili uwapangie Waumini vituo vya kupigana (Vita vya Uhud).[37] Na Allaah Ni Mwenye Kusikia yote, Mjuzi wa yote.

 

 

 

إِذْ هَمَّت طَّائِفَتَانِ مِنكُمْ أَن تَفْشَلَا وَاللَّـهُ وَلِيُّهُمَا ۗ وَعَلَى اللَّـهِ فَلْيَتَوَكَّلِ الْمُؤْمِنُونَ ﴿١٢٢﴾

122. Pale makundi mawili miongoni mwenu walipofanya wasiwasi kwamba watashindwa nailhali Allaah Ndiye Rafiki Mlinzi wao. Basi kwa Allaah Pekee Waumini watawakali.

 

 

وَلَقَدْ نَصَرَكُمُ اللَّـهُ بِبَدْرٍ وَأَنتُمْ أَذِلَّةٌ ۖ فَاتَّقُوا اللَّـهَ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ ﴿١٢٣﴾

123. Kwa yakini Allaah Alikunusuruni katika Badr[38] na hali nyinyi ni wanyonge. Basi mcheni Allaah mpate kushukuru.

 

 

إِذْ تَقُولُ لِلْمُؤْمِنِينَ أَلَن يَكْفِيَكُمْ أَن يُمِدَّكُمْ رَبُّكُم بِثَلَاثَةِ آلَافٍ مِّنَ الْمَلَائِكَةِ مُنزَلِينَ ﴿١٢٤﴾

124. Pindi ulipowaambia Waumini: Je, haikutosheni ikiwa Rabb wenu Atakuongezeeni nguvu kwa Malaika elfu tatu walioteremshwa?

 

 

بَلَىٰ ۚ إِن تَصْبِرُوا وَتَتَّقُوا وَيَأْتُوكُم مِّن فَوْرِهِمْ هَـٰذَا يُمْدِدْكُمْ رَبُّكُم بِخَمْسَةِ آلَافٍ مِّنَ الْمَلَائِكَةِ مُسَوِّمِينَ ﴿١٢٥﴾ 

125. Bali, naam! Mkisubiri na mkashikamana na taqwa na hata wakikujieni kwa ghafla hivi (kukumalizeni), basi (mkitekeleza mawili hayo), Rabb wenu Atakuongezeeni nguvu kwa Malaika elfu tano waliojitia wenyewe na farasi wao alama maalum.

 

 

 وَمَا جَعَلَهُ اللَّـهُ إِلَّا بُشْرَىٰ لَكُمْ وَلِتَطْمَئِنَّ قُلُوبُكُم بِهِ ۗ وَمَا النَّصْرُ إِلَّا مِنْ عِندِ اللَّـهِ الْعَزِيزِ الْحَكِيمِ ﴿١٢٦﴾

126. Na Allaah Hakujaalia hayo isipokuwa ni bishara kwenu, na ili zitue nyoyo zenu kwayo. Na hakuna ushindi isipokuwa kutoka kwa Allaah Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote.

 

 

لِيَقْطَعَ طَرَفًا مِّنَ الَّذِينَ كَفَرُوا أَوْ يَكْبِتَهُمْ فَيَنقَلِبُوا خَائِبِينَ ﴿١٢٧﴾ 

127. Ili Akate sehemu ya waliokufuru au Awafedheheshe, warudi nyuma wakiwa wamekata tamaa.

 

 

 لَيْسَ لَكَ مِنَ الْأَمْرِ شَيْءٌ أَوْ يَتُوبَ عَلَيْهِمْ أَوْ يُعَذِّبَهُمْ فَإِنَّهُمْ ظَالِمُونَ ﴿١٢٨﴾

128. Jambo hili halikuhusu wewe, ima Apokee tawbah yao au Awaadhibu, kwani wao ni madhalimu.

 

 

وَلِلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۚ يَغْفِرُ لِمَن يَشَاءُ وَيُعَذِّبُ مَن يَشَاءُ ۚ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿١٢٩﴾

129. Ni vya Allaah Pekee vilivyomo katika mbingu na katika ardhi. Anamghufuria Amtakaye na Anamuadhibu Amtakaye. Na Allaah Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu.

 

 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَأْكُلُوا الرِّبَا أَضْعَافًا مُّضَاعَفَةً ۖ وَاتَّقُوا اللَّـهَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿١٣٠﴾

130. Enyi walioamini! Msile riba mkizidisha maradufu juu ya maradufu. Na mcheni Allaah mpate kufaulu.[39]

 

 

وَاتَّقُوا النَّارَ الَّتِي أُعِدَّتْ لِلْكَافِرِينَ ﴿١٣١﴾ 

131. Na uogopeni moto ambao umeandaliwa kwa makafiri.

 

 

وَأَطِيعُوا اللَّـهَ وَالرَّسُولَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ ﴿١٣٢﴾

132. Na mtiini Allaah na Rasuli mpate kurehemewa.

 

 

 

وَسَارِعُوا إِلَىٰ مَغْفِرَةٍ مِّن رَّبِّكُمْ وَجَنَّةٍ عَرْضُهَا السَّمَاوَاتُ وَالْأَرْضُ أُعِدَّتْ لِلْمُتَّقِينَ﴿١٣٣﴾ 

133. Na kimbilieni maghfirah kutoka kwa Rabb wenu, na Jannah upana wake ni wa mbingu na ardhi imeandaliwa kwa wenye taqwa.

 

 

الَّذِينَ يُنفِقُونَ فِي السَّرَّاءِ وَالضَّرَّاءِ وَالْكَاظِمِينَ الْغَيْظَ وَالْعَافِينَ عَنِ النَّاسِ ۗ وَاللَّـهُ يُحِبُّ الْمُحْسِنِينَ ﴿١٣٤﴾ 

134. Ambao wanatoa (kwa ajili ya Allaah) katika hali ya wasaa na katika hali ya shida, na wanazuia ghadhabu, na wenye kusamehe watu. Na Allaah Anapenda wafanyao ihsaan.

 

 

وَالَّذِينَ إِذَا فَعَلُوا فَاحِشَةً أَوْ ظَلَمُوا أَنفُسَهُمْ ذَكَرُوا اللَّـهَ فَاسْتَغْفَرُوا لِذُنُوبِهِمْ وَمَن يَغْفِرُ الذُّنُوبَ إِلَّا اللَّـهُ وَلَمْ يُصِرُّوا عَلَىٰ مَا فَعَلُوا وَهُمْ يَعْلَمُونَ ﴿١٣٥﴾

135. Na ambao wanapofanya machafu au wakajidhulumu nafsi zao (kwa maasi), humdhukuru Allaah wakaomba maghfirah kwa madhambi yao. Na nani anayeghufuria madhambi isipokuwa Allaah. Na hawaendelei katika waliyoyafanya na hali wanajua.[40]

 

 

أُولَـٰئِكَ جَزَاؤُهُم مَّغْفِرَةٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَجَنَّاتٌ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا ۚ وَنِعْمَ أَجْرُ الْعَامِلِينَ ﴿١٣٦﴾

136. Hao jazaa yao ni maghfirah kutoka kwa Rabb wao na Jannaat zipitazo chini yake mito, wadumu humo. Ni uzuri ulioje ujira wa watendaji (wema).

 

 

قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِكُمْ سُنَنٌ فَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَانظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُكذِّبِينَ ﴿١٣٧﴾

137. Kwa hakika zimekwishapita kabla yenu nyendo nyingi (kama hali yenu), basi tembeeni katika ardhi kisha mtazame vipi ilikuwa hatima ya wenye kukadhibisha.[41]

 

 

 

هَـٰذَا بَيَانٌ لِّلنَّاسِ وَهُدًى وَمَوْعِظَةٌ لِّلْمُتَّقِينَ ﴿١٣٨﴾

138. Hii (Qur-aan) ni ubainisho kwa watu na mwongozo na mawaidha kwa wenye taqwa.

 

 

وَلَا تَهِنُوا وَلَا تَحْزَنُوا وَأَنتُمُ الْأَعْلَوْنَ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ ﴿١٣٩﴾ 

139. Na wala msilegee na wala msihuzunike ilhali nyinyi mko juu mkiwa ni Waumini.

 

 

 إِن يَمْسَسْكُمْ قَرْحٌ فَقَدْ مَسَّ الْقَوْمَ قَرْحٌ مِّثْلُهُ ۚ وَتِلْكَ الْأَيَّامُ نُدَاوِلُهَا بَيْنَ النَّاسِ وَلِيَعْلَمَ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا وَيَتَّخِذَ مِنكُمْ شُهَدَاءَ ۗ وَاللَّـهُ لَا يُحِبُّ الظَّالِمِينَ ﴿١٤٠﴾

140. Yakikupateni majeraha basi yamekwishawapata watu majeraha kama hayo. Na hizo ni siku Tunazizungusha zamu (za mabadiliko ya hali) baina ya watu, na ili Allaah Adhihirishe walioamini na Afanye miongoni mwenu Shuhadaa[42] (waliofariki katika vita vya Jihaad).  Na Allaah Hapendi madhalimu.

 

 

وَلِيُمَحِّصَ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا وَيَمْحَقَ الْكَافِرِينَ ﴿١٤١﴾ 

141. Na ili Allaah Awajaribu (au Awatakase) walioamini na Awafutilie mbali makafiri.

 

 

 أَمْ حَسِبْتُمْ أَن تَدْخُلُوا الْجَنَّةَ وَلَمَّا يَعْلَمِ اللَّـهُ الَّذِينَ جَاهَدُوا مِنكُمْ وَيَعْلَمَ الصَّابِرِينَ ﴿١٤٢﴾

142. Je, Mnadhani kwamba mtaingia Jannah na hali Allaah bado Hajawadhihirisha wale waliofanya Jihaad miongoni mwenu na Akadhihirisha wenye subira?

 

 

وَلَقَدْ كُنتُمْ تَمَنَّوْنَ الْمَوْتَ مِن قَبْلِ أَن تَلْقَوْهُ فَقَدْ رَأَيْتُمُوهُ وَأَنتُمْ تَنظُرُونَ ﴿١٤٣﴾

143. Na kwa yakini mlikuwa mnatamani mauti kabla hamjakutana nayo, basi mmekwishayaona na huku mnayatazama. 

 

 

وَمَا مُحَمَّدٌ إِلَّا رَسُولٌ قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِهِ الرُّسُلُ ۚ أَفَإِن مَّاتَ أَوْ قُتِلَ انقَلَبْتُمْ عَلَىٰ أَعْقَابِكُمْ ۚ وَمَن يَنقَلِبْ عَلَىٰ عَقِبَيْهِ فَلَن يَضُرَّ اللَّـهَ شَيْئًا ۗ وَسَيَجْزِي اللَّـهُ الشَّاكِرِينَ ﴿١٤٤﴾

144. Na Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) hakuwa isipokuwa ni Rasuli tu. Wamekwishapita kabla yake Rusuli. Je, akifa au akiuawa ndio mtageuka nyuma mrudi mlikotoka (ukafirini)? Na atakayegeuka nyuma akarudi alikotoka basi hatomdhuru Allaah kwa chochote. Na Allaah Atawalipa wenye kushukuru.

 

 

 

وَمَا كَانَ لِنَفْسٍ أَن تَمُوتَ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ كِتَابًا مُّؤَجَّلًا ۗ وَمَن يُرِدْ ثَوَابَ الدُّنْيَا نُؤْتِهِ مِنْهَا وَمَن يُرِدْ ثَوَابَ الْآخِرَةِ نُؤْتِهِ مِنْهَا ۚ وَسَنَجْزِي الشَّاكِرِينَ ﴿١٤٥﴾ 

145. Na haiwezekani nafsi yeyote kufa isipokuwa kwa Idhini ya Allaah, kwani imeandikiwa muda wake maalumu. Na yeyote anayetaka malipo ya dunia basi Tutampa sehemu tu ya hayo (Tuliyomkadiria). Na yeyote anayetaka thawabu za Aakhirah basi Tutampa sehemu ya hayo (bila mipaka) na Tutawalipa wenye kushukuru. 

 

 

وَكَأَيِّن مِّن نَّبِيٍّ قَاتَلَ مَعَهُ رِبِّيُّونَ كَثِيرٌ فَمَا وَهَنُوا لِمَا أَصَابَهُمْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَمَا ضَعُفُوا وَمَا اسْتَكَانُوا ۗ وَاللَّـهُ يُحِبُّ الصَّابِرِينَ ﴿١٤٦﴾

146. Na Manabii wangapi walipigana vita wakiwa pamoja nao Waumini wengi waliojaa imaan ya kikweli, basi hawakulegea kwa yaliyowasibu katika Njia ya Allaah, wala hawakudhoofika na wala hawakunyong’onyea. Na Allaah Anapenda wenye subira.

 

 

وَمَا كَانَ قَوْلَهُمْ إِلَّا أَن قَالُوا رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا ذُنُوبَنَا وَإِسْرَافَنَا فِي أَمْرِنَا وَثَبِّتْ أَقْدَامَنَا وَانصُرْنَا عَلَى الْقَوْمِ الْكَافِرِينَ ﴿١٤٧﴾

147. Na haikuwa kauli yao isipokuwa walisema: Rabb wetu! Tughufurie madhambi yetu na upindukaji wetu mipaka katika mambo yetu, na Ithibitishe miguu yetu na Tunusuru dhidi ya watu makafiri.

 

 

فَآتَاهُمُ اللَّـهُ ثَوَابَ الدُّنْيَا وَحُسْنَ ثَوَابِ الْآخِرَةِ ۗ وَاللَّـهُ يُحِبُّ الْمُحْسِنِينَ ﴿١٤٨﴾ 

148. Basi Allaah Akawalipa malipo ya dunia na thawabu nzuri za Aakhirah. Na Allaah Anapenda wafanyao ihsaan. 

 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن تُطِيعُوا الَّذِينَ كَفَرُوا يَرُدُّوكُمْ عَلَىٰ أَعْقَابِكُمْ فَتَنقَلِبُوا خَاسِرِينَ ﴿١٤٩﴾

149. Enyi walioamini! Mkiwatii wale waliokufuru watakurudisheni nyuma mlikotoka kisha mtageuka mkiwa wenye kukhasirika.

 

 

بَلِ اللَّـهُ مَوْلَاكُمْ ۖ وَهُوَ خَيْرُ النَّاصِرِينَ ﴿١٥٠﴾

150. Bali Allaah Ndio Rafiki Mlinzi wenu. Naye Ndiye Mbora kabisa kuliko wote wenye kusaidia.

 

 

سَنُلْقِي فِي قُلُوبِ الَّذِينَ كَفَرُوا الرُّعْبَ بِمَا أَشْرَكُوا بِاللَّـهِ مَا لَمْ يُنَزِّلْ بِهِ سُلْطَانًا ۖ وَمَأْوَاهُمُ النَّارُ ۚ وَبِئْسَ مَثْوَى الظَّالِمِينَ ﴿١٥١﴾

151. Tutatia hofu na woga katika nyoyo za waliokufuru kwa sababu ya kumshirikisha Allaah na (masanamu) ambayo Hakuyateremshia hoja wala dalili (kwamba yanastahiki kuabudiwa). Na makazi yao ni moto, na ubaya ulioje maskani ya madhalimu.

 

 

وَلَقَدْ صَدَقَكُمُ اللَّـهُ وَعْدَهُ إِذْ تَحُسُّونَهُم بِإِذْنِهِ ۖ حَتَّىٰ إِذَا فَشِلْتُمْ وَتَنَازَعْتُمْ فِي الْأَمْرِ وَعَصَيْتُم مِّن بَعْدِ مَا أَرَاكُم مَّا تُحِبُّونَ ۚ مِنكُم مَّن يُرِيدُ الدُّنْيَا وَمِنكُم مَّن يُرِيدُ الْآخِرَةَ ۚ ثُمَّ صَرَفَكُمْ عَنْهُمْ لِيَبْتَلِيَكُمْ ۖ وَلَقَدْ عَفَا عَنكُمْ ۗ وَاللَّـهُ ذُو فَضْلٍ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ ﴿١٥٢﴾

152. Na kwa yakini Allaah Amekwisha kusadikishieni Ahadi Yake mlipowaua vikali kwa Idhini Yake, mpaka mliposhindwa na mkazozana katika amri (aliyokupeni Rasuli) na mkaasi baada ya Yeye kukuonyesheni yale mnayoyapenda. Miongoni mwenu wako wenye kutaka dunia, na miongoni mwenu wako wenye kutaka Aakhirah. Kisha Akakugeuzeni nyuma mbali nao (hao maadui) ili Akujaribuni. Na kwa yakini Amekwisha kusameheni. Na Allaah Ni Mwenye Fadhila kwa Waumini.

 

 

إِذْ تُصْعِدُونَ وَلَا تَلْوُونَ عَلَىٰ أَحَدٍ وَالرَّسُولُ يَدْعُوكُمْ فِي أُخْرَاكُمْ فَأَثَابَكُمْ غَمًّا بِغَمٍّ لِّكَيْلَا تَحْزَنُوا عَلَىٰ مَا فَاتَكُمْ وَلَا مَا أَصَابَكُمْ ۗ وَاللَّـهُ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ ﴿١٥٣﴾

153. Pale mlipotimka kukimbia mbali wala hamgeuki nyuma kumtazama yeyote, na Rasuli anakuiteni nyuma yenu, kisha Allaah Akakulipizeni dhiki juu ya dhiki ili (kukufundisheni) msihuzunike kwa yaliyokupiteni na wala kwa yaliyokusibuni. Na Allaah Ni Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri kwa yale myatendayo.

 

 

ثُمَّ أَنزَلَ عَلَيْكُم مِّن بَعْدِ الْغَمِّ أَمَنَةً نُّعَاسًا يَغْشَىٰ طَائِفَةً مِّنكُمْ ۖ وَطَائِفَةٌ قَدْ أَهَمَّتْهُمْ أَنفُسُهُمْ يَظُنُّونَ بِاللَّـهِ غَيْرَ الْحَقِّ ظَنَّ الْجَاهِلِيَّةِ ۖ يَقُولُونَ هَل لَّنَا مِنَ الْأَمْرِ مِن شَيْءٍ ۗ قُلْ إِنَّ الْأَمْرَ كُلَّهُ لِلَّـهِ ۗ يُخْفُونَ فِي أَنفُسِهِم مَّا لَا يُبْدُونَ لَكَ ۖ يَقُولُونَ لَوْ كَانَ لَنَا مِنَ الْأَمْرِ شَيْءٌ مَّا قُتِلْنَا هَاهُنَا ۗ قُل لَّوْ كُنتُمْ فِي بُيُوتِكُمْ لَبَرَزَ الَّذِينَ كُتِبَ عَلَيْهِمُ الْقَتْلُ إِلَىٰ مَضَاجِعِهِمْ ۖ وَلِيَبْتَلِيَ اللَّـهُ مَا فِي صُدُورِكُمْ وَلِيُمَحِّصَ مَا فِي قُلُوبِكُمْ ۗ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ بِذَاتِ الصُّدُورِ ﴿١٥٤﴾

154. Kisha Akakuteremshieni amani baada ya dhiki; usingizi unaofunika kundi miongoni mwenu na kundi likawashughulisha nafsi zao wakamdhania Allaah pasi na haki dhana ya kijahili, wanasema: Je, tuna amri yoyote sisi katika jambo hili? Sema: Hakika amri yote ni ya Allaah. Wanaficha katika nafsi zao yale wasiyokubainishia. Wanasema: Lau tungelikuwa tuna amri yoyote katika jambo basi tusingeliuliwa hapa. Sema: Lau mngelikuwa majumbani mwenu, bila shaka wangejitokeza wale walioandikiwa kuuawa kwenye mahali pa kuangukia wafe. Ili Allaah Ayajaribu yale yaliyomo katika vifua vyenu na Atakase yale yaliyomo katika nyoyo zenu. Na Allaah Anayajua vyema yaliyomo vifuani.

 

 

إِنَّ الَّذِينَ تَوَلَّوْا مِنكُمْ يَوْمَ الْتَقَى الْجَمْعَانِ إِنَّمَا اسْتَزَلَّهُمُ الشَّيْطَانُ بِبَعْضِ مَا كَسَبُوا ۖ وَلَقَدْ عَفَا اللَّـهُ عَنْهُمْ ۗ إِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ حَلِيمٌ ﴿١٥٥﴾ 

155. Hakika wale waliokengeuka miongoni mwenu siku yalipokutana makundi mawili (kwa mapambano), hakika hapana ila shaytwaan aliwatelezesha kutokana na baadhi ya waliyoyachuma. Na kwa yakini Allaah Aliwasamehe. Hakika Allaah Ni Mwingi wa Kughufuria, Mvumilivu.  

 

 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ كَفَرُوا وَقَالُوا لِإِخْوَانِهِمْ إِذَا ضَرَبُوا فِي الْأَرْضِ أَوْ كَانُوا غُزًّى لَّوْ كَانُوا عِندَنَا مَا مَاتُوا وَمَا قُتِلُوا لِيَجْعَلَ اللَّـهُ ذَٰلِكَ حَسْرَةً فِي قُلُوبِهِمْ ۗ وَاللَّـهُ يُحْيِي وَيُمِيتُ ۗ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ ﴿١٥٦﴾ 

156. Enyi walioamini! Msiwe kama wale waliokufuru na wakasema kuhusu ndugu zao waliposafiri katika ardhi au walipokuwa vitani: Lau wangelikuwa kwetu wasingelikufa na wala wasingeliuawa, ili Allaah Afanye hayo (yaliyoeleweka vibaya) kuwa majuto katika nyoyo zao. Na Allaah Anahuisha na Anafisha. Na Allaah Anayaona vyema myatendayo.

 

 

وَلَئِن قُتِلْتُمْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ أَوْ مُتُّمْ لَمَغْفِرَةٌ مِّنَ اللَّـهِ وَرَحْمَةٌ خَيْرٌ مِّمَّا يَجْمَعُونَ ﴿١٥٧﴾

157. Na kama mtauliwa katika Njia ya Allaah au mtakufa, basi bila shaka Maghfirah kutoka kwa Allaah na Rehma ni bora kuliko yale wanayoyakusanya.

 

 

وَلَئِن مُّتُّمْ أَوْ قُتِلْتُمْ لَإِلَى اللَّـهِ تُحْشَرُونَ ﴿١٥٨﴾

158. Na kama mtakufa au mtauliwa, bila shaka kwa Allaah mtakusanywa.

 

 

فَبِمَا رَحْمَةٍ مِّنَ اللَّـهِ لِنتَ لَهُمْ ۖ وَلَوْ كُنتَ فَظًّا غَلِيظَ الْقَلْبِ لَانفَضُّوا مِنْ حَوْلِكَ ۖ فَاعْفُ عَنْهُمْ وَاسْتَغْفِرْ لَهُمْ وَشَاوِرْهُمْ فِي الْأَمْرِ ۖ فَإِذَا عَزَمْتَ فَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ ۚإِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُتَوكِّلِينَ ﴿١٥٩﴾

159. Basi ni kwa sababu ya Rehma kutoka kwa Allaah ndio umekuwa mpole kwao (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم).[43] Na lau ungelikuwa mjeuri mwenye moyo mgumu, wangelitawanyika mbali nawe. Basi wasamehe na waombee maghfirah na washauri katika mambo. Na unapoazimia, basi tawakali kwa Allaah. Hakika Allaah Anapenda wanaotawakali.

 

 

 

إِن يَنصُرْكُمُ اللَّـهُ فَلَا غَالِبَ لَكُمْ ۖ وَإِن يَخْذُلْكُمْ فَمَن ذَا الَّذِي يَنصُرُكُم مِّن بَعْدِهِ ۗ وَعَلَى اللَّـهِ فَلْيَتَوَكَّلِ الْمُؤْمِنُونَ ﴿١٦٠﴾ 

160. Akikunusuruni Allaah, basi hakuna wa kukushindeni. Na Akikutelekezeni, basi nani atakunusuruni baada Yake? Na kwa Allaah Pekee watawakali Waumini.

 

 

 وَمَا كَانَ لِنَبِيٍّ أَن يَغُلَّ ۚ وَمَن يَغْلُلْ يَأْتِ بِمَا غَلَّ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۚ ثُمَّ تُوَفَّىٰ كُلُّ نَفْسٍ مَّا كَسَبَتْ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ ﴿١٦١﴾

161. Na haikuwa (ni tabia) kwa Nabiy yeyote kukhini (ngawira). Na yeyote atakayekhini atakuja na kile alichokikhini Siku ya Qiyaamah. Kisha kila nafsi italipwa kamilifu yale iliyoyachuma, nao hawatodhulumiwa.

 

 

أَفَمَنِ اتَّبَعَ رِضْوَانَ اللَّـهِ كَمَن بَاءَ بِسَخَطٍ مِّنَ اللَّـهِ وَمَأْوَاهُ جَهَنَّمُ ۚ وَبِئْسَ الْمَصِيرُ ﴿١٦٢﴾ 

162. Je, aliyefuata Radhi za Allaah ni kama aliyestahiki ghadhabu kutoka kwa Allaah?! Na makazi yake ni Jahannam, na ubaya ulioje mahali pa kuishia!  

 

 

هُمْ دَرَجَاتٌ عِندَ اللَّـهِ ۗ وَاللَّـهُ بَصِيرٌ بِمَا يَعْمَلُونَ ﴿١٦٣﴾

163. Wao wana vyeo mbali mbali mbele ya Allaah. Na Allaah Anayaona vyema yale wayatendayo.

 

 

لَقَدْ مَنَّ اللَّـهُ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ إِذْ بَعَثَ فِيهِمْ رَسُولًا مِّنْ أَنفُسِهِمْ يَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِهِ وَيُزَكِّيهِمْ وَيُعَلِّمُهُمُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَإِن كَانُوا مِن قَبْلُ لَفِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ ﴿١٦٤﴾

164. Kwa yakini Allaah Amewafanyia fadhila Waumini pale Alipomtuma kwao Rasuli miongoni mwao wenyewe, anawasomea Aayaat Zake na anawatakasa na anawafunza Kitabu na Hikmah (Sunnah), japokuwa walikuwa kabla katika upotofu bayana.

 

 

أَوَلَمَّا أَصَابَتْكُم مُّصِيبَةٌ قَدْ أَصَبْتُم مِّثْلَيْهَا قُلْتُمْ أَنَّىٰ هَـٰذَا ۖ قُلْ هُوَ مِنْ عِندِ أَنفُسِكُمْ ۗ إِنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿١٦٥﴾

165. Ulipokusibuni msiba ingawa nyinyi mliwasibu (maadui) mara mbili yake mlisema: Umetoka wapi huu? Sema: Huo ni kutoka kwenu wenyewe. Hakika Allaah Ni Muweza juu ya kila kitu. 

 


 

وَمَا أَصَابَكُمْ يَوْمَ الْتَقَى الْجَمْعَانِ فَبِإِذْنِ اللَّـهِ وَلِيَعْلَمَ الْمُؤْمِنِينَ ﴿١٦٦﴾

166. Na yale yaliyokusibuni siku yalipokutana makundi mawili (katika Uhud), basi ni kwa Idhini ya Allaah na ili Adhihirishe Waumini.

 

 

وَلِيَعْلَمَ الَّذِينَ نَافَقُوا ۚ وَقِيلَ لَهُمْ تَعَالَوْا قَاتِلُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ أَوِ ادْفَعُوا ۖ قَالُوا لَوْ نَعْلَمُ قِتَالًا لَّاتَّبَعْنَاكُمْ ۗ هُمْ لِلْكُفْرِ يَوْمَئِذٍ أَقْرَبُ مِنْهُمْ لِلْإِيمَانِ ۚ يَقُولُونَ بِأَفْوَاهِهِم مَّا لَيْسَ فِي قُلُوبِهِمْ ۗ وَاللَّـهُ أَعْلَمُ بِمَا يَكْتُمُونَ ﴿١٦٧﴾

167. Na ili Adhihirishe wale waliofanya unafiki na wakaambiwa: Njooni mpigane katika Njia ya Allaah au (angalau) lindeni. Wakasema: Lau tungelijua kuwa kuna kupigana bila shaka tungelikufuateni. Wao siku hiyo walikuwa karibu zaidi na ukafiri kuliko imaan. Wanasema kwa midomo yao yasiyokuwemo ndani ya nyoyo zao. Na Allaah Anajua zaidi wanayoyaficha.

 

 

الَّذِينَ قَالُوا لِإِخْوَانِهِمْ وَقَعَدُوا لَوْ أَطَاعُونَا مَا قُتِلُوا ۗ قُلْ فَادْرَءُوا عَنْ أَنفُسِكُمُ الْمَوْتَ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿١٦٨﴾ 

168. Wale waliowaambia ndugu zao nao wakakaa (wasiende vitani): Lau wangelitutii basi wasingeliuawa. Sema: Basi ziondoleeni nafsi zenu mauti mkiwa ni wakweli.

 

 

وَلَا تَحْسَبَنَّ الَّذِينَ قُتِلُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ أَمْوَاتًا ۚ بَلْ أَحْيَاءٌ عِندَ رَبِّهِمْ يُرْزَقُونَ ﴿١٦٩﴾ 

169. Na wala usiwadhanie kabisa wale waliouawa katika Njia ya Allaah[44] kuwa ni wafu, bali wahai, wako kwa Rabb wao wanaruzukiwa.

 

 

فَرِحِينَ بِمَا آتَاهُمُ اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ وَيَسْتَبْشِرُونَ بِالَّذِينَ لَمْ يَلْحَقُوا بِهِم مِّنْ خَلْفِهِمْ أَلَّا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ ﴿١٧٠﴾ 

170. Wanafurahia kwa Aliyowapa Allaah kwa Fadhila Zake na wanawashangilia ambao bado hawajaungana nao, walio nyuma yao, kwamba: Hakuna khofu juu yao na wala hawatohuzunika.

 

 

 

يَسْتَبْشِرُونَ بِنِعْمَةٍ مِّنَ اللَّـهِ وَفَضْلٍ وَأَنَّ اللَّـهَ لَا يُضِيعُ أَجْرَ الْمُؤْمِنِينَ ﴿١٧١﴾

171. Wanashangilia Neema kutoka kwa Allaah na Fadhila na kwamba Allaah Hapotezi ujira wa Waumini.

 ☞ Ukurasa wa 3

 

Report Page